Uhuru huu ni kwa ajili ya nani?

Ninaomba msamaha kama hutanielewa. Ila ninadhani jambo hili ni muhimu ukalitafakari kwa kina wakati ukisherehekea “uhuru” wa nchi yako iliyo masikini kuliko zote kusini mwa jangwa la Sahara.

Hivi kweli nchi yetu ina haki ya kusherehekea hicho kilichopewa jina la “uhuru”? Uhuru maana yake ni nini? Ni kwa kiasi gani twaweza kujikagua kuona ikiwa tu huru kweli? Kama uhuru una maana ya mambo kuwa hivi yalivyo, vipi utumwa?

Ni kwa kiasi gani uchumi wa nchi hii unathibitisha kuwa kweli tu “huru”? Ni kwa kiasi gani utamaduni wetu unathibitisha hicho kinachoitwa “uhuru”? Ni kwa kiasi gani? Ni kwa vipi tunaweza kujiridhisha kwamba elimu yetu inakubaliana na kelele zetu za “uhuru”?

Hivi mababu zetu walipokuwa wakiusaka uhuru lengo hasa lilikuwa nini?

Leo hii tunasoma Vyuo Vikuu kwa vitisho kutoka kwa wenzetu wanaofafana na sisi. Haturuhusiwi kufikiri. Elimu yenyewe imekaa mkao wa kitumwa. Tunafundishwa akademia ituondoayo katika wigo wa kuyaelewa matatizo yetu ya kila siku. Inatuondoa kwenye wigo wa kuwatumikia watu wetu. Tunafundishwa kubadilisha tamaduni zetu zifanane fanane na hao “wanaotutawala”. Eti tunajidai kuwa huru? Kama si kichekesho ni nini hiki basi?

Ni sisi wenye “uhuru” huu, tunaodharau hata lugha yetu adhimu. Eti tunasoma vya kwao kwa lugha yao, na bado tunajiona tuna uhuru! Kweli tuko huru?

Uhuru unamaanisha nini kama si usawa katika jamii? Je, tu sawa? Leo hii masikini kama mimi nabinywa mbavu kwa kulazimishwa kulipa asilimia arobaini nisiyoweza kuilipa, wakati huo huo watoto wa hao wanaofurahia matunda ya“uhuru” wetu wanalipiwa asilimia mia moja na bodi ya mikopo ya elimu ya juu!

Nikijidanganya niko huru, na hivyo nidai haki ya “kula matunda ya uhuru” natimuliwa kwa muda usiojulikana. Eti tuko huru? Kweli? Au uhuru maana yake ni nini basi? Na “uhuru” huu unapimwaje-pimwaje? “Uhuru” huu ni kwa faida ya nani? Isijefikia mahala napaswa kuwa na shati la kijani ili kuelewa maana hasa ya uhuru.

Nakutakia maadhimisho mema ya “uhuru” wa wenzio.

Maoni

  1. Mkuu unanikumbusha AYA za Ndesanjo kwenye ile makala yake ya MAUAJI YA HALAIKI AFRIKA itafute. unachokisema ni kweri tunatakiwa kudurusu mwenendo wetu, tunapswa kuweka tafakuri juu ya hili jambo. lakini kuna kasoro nazioa toka enzi za waliopigani uhuru{nimejaribu kuziandika katika gazeti la RAI, alhamisi hii nadhani itakuwa mtaani ikiwa ni shemu ya kwanza} haya mambo ya uhuru yanachefua wakti mwingine. lakino kosa lingine nakubalian na Samson Mwigamba (Tanzania daima, kila jumatao) kwamba tulifanya kosa kumwachia Nyerere kila kitu, yaani afikirie kwa naiba yetu. lakini kwangu nafikiria sana maana ya uhuru, kani kumefanyika mktano hivi karibu pale Movenpick na mama mmoja wa Kimarekani aliilaumu vikali CHINA kwamba haichezi mchezo bali inadili mchezo. Jiulize mchezo gani? alibanwa na kukazuka mtafaruku aeleze nini maana yake, lakini alinywea kwahiyo kafichua siri kwamba hawataki AFRIKA iendeleee. kwetu kama uhuru nini maana yake maana bado kuna mkanganyiko hapo, uhuru wetu kwa maana ya bendera au? uhuru wa miaka 47 halafu tunasema nchi changa? kivipi iwe changa wakati Singapore, Indonesia wanatupiku kwa maendeleo ya kiuchumi? je wao wana maligahfi kuliko sisi??
    Mkuu ngoja niishie hapo tuwape wengine nafasi nina maswali ambayo hakuna kiongozi anaweza kutoa jawabu sahihi simuoni kabisa nchini

    JibuFuta
  2. Kaka. Hapa tutakuwa na maswali mengi saana maana nadhani tafsiri ya UHURU wetu itatokana na "maslahi" ya msemaji. Si geni katika nchi na kiswahili. Ni kama mtu anapokwambia "haraka haraka haina baraka" kisha akiwa anataka uwahi anakwambia "chelewa chelewa utakuja mwana si wako". Ama "Pole pole ndio mwendo" kisha "ujanja kuwahi" Kwa hiyo tusikilizapo tafsiri za UHURU wetu tuangalie twazipata toka kwa nani.
    Blessings

    JibuFuta
  3. Mzee wa changamoto umemaliza kila kitu. Uhuru ni kwa maslahi ya wao wanaodhani wapo juu ya sheria.
    Ni hayo tu.

    JibuFuta
  4. Walioko huru nyumba zao zimezungushiwa kuta na vibao Mbwa Mkali na walinzi wawalindao wasio huru. Si wako huru ndio maana geti kali?

    JibuFuta
  5. Kama uhuru wenyewe ndio huu wa kujengeana matabaka, kazi ipo. Na kazi yenyewe ndiyo hiyo ya hao wanaojidhania huru wanajiimarishia mageti ya nyumba zao. Haki ya nani itafika wakati tutaanza kutwangana humu. Ohooooo! na sio sio nyingi. tutatafuta uhuru wa kweli

    JibuFuta
  6. nimeipenda ya kitururu. kunatofauti gani kati ya kuishi jela na kuishi geti kali?

    JibuFuta
  7. Michango yenu imenipa changamoto. Asante sana kwa kubonyeza kisanduku cha maoni.

    JibuFuta
  8. kwaheriiii kwa leo nimepita tu nilikuwa namsaba jamaa mmoja hivi kanishtua jambo hapa nyumbani

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Pay $900? I quit blogging