Malezi yanavyochochea ubabe katika jamii

Natamani tutafakari jambo hili kwa kina. Nyumbani tumemzoesha mtoto fujo —fimbo, makofi, matusi na aina nyingine za ubabe. Sisi wazazi tunaamini hatuwezi kulinda mamlaka yetu bila kumsababishia mtoto maumivu iwe kwenye mwili wake au hisia zake. Ukiangalia yanayoendelea nyumbani hakuna mazungumzo yenye upendo na mtoto. Tunaamini amani na utulivu kwenye ngazi ya familia ni pale tunapokuwa na watoto wasiofikiri, wasiouliza, wasiothubutu kutofautiana na wazazi ambao ndio mamlaka katika familia. 

 


Shuleni mtoto anakutana na mwalimu anayeamini njia pekee na ya uhakika kulinda heshima na mamlaka yake darasani ni vitisho, fimbo na kila aina ya ubabe kwa mwanafunzi. Ukiangalia mbinu za ufundishaji wake huoni wapi anaamini katika ushirikishwaji wa mwanafunzi. Tangu asubuhi mpaka jioni zoezi linalotawala ni wanafunzi kupokea maelekezo na kuyakariri. 

 

Mwalimu anaamini nidhamu ni pale amani na utulivu vinapotawala darasani. Hii, huenda ndio sababu shule zinahangaika na wapiga kelele zaidi kuliko kuchochea udadisi na fikra tunduizi. Mwanafunzi asiyepokea tu maelekezo bila kuuliza maswali magumu anaonekana kuwa jeuri, mkorofi na asipokuwa makini maisha yake yatatawaliwa na adhabu zinazolenga kumnyoosha aelewe mwalimu ni nani.

 

Mtoto huyu anamaliza shule anaenda kazini. Hali haiko tofauti. Mtoto anakutana na msimamizi, kwa jina jingine boss, asiyeamini mazungumzo yoyote ya wazi na usawa. Msimamizi anaamini katika kutoa amri, maelezo na kuwakumbusha wafanyakazi kuwa yeye ndiye mkubwa pale. Jukumu kubwa la mfanyakazi ni kusikiliza, kufuata na kutekeleza. Katika mazingira haya, kutoa maoni mbadala yanayolenga kuboresha jambo yanatafriwa kama ukosefu wa nidhamu. Hata vikao, kimsingi, ni matangazo yanayohitaji utekelezaji. 

 

Kijana huyu aliyekulia kwenye mfumo huu wa ubabe na fujo za wenye naffasi zao anaingia kwenye ndoa. Mule anakutana na mazingira yanayolinda mamlaka ya mume kwa vitisho, ubabe na unyanyasaji. Mume hasemi wazi lakini kimsingi haamini kabisa uwezekano wa kupanga jambo la maana na mke wake katika usawa na likaenda. Usiri na giza hugubika mfumo wa maisha yake na muda wote anaamini ni muhimu kukoroma, kufoka, kutisha na kunyamazisha sauti kinzani. 

 

Ukiangalia unaona utaratibu mzima wa malezi unaona tunavyoamini katika matumizi ya nguvu, vitisho na kuogopesha. Tunaamini madaraka hulindwa kwa ubabe na kuwafanyia fujo watu ambao wakati mwingine kwa unyonge wao hawana wanachoweza kufanya zaidi ya kuhitaji kusikika. Fujo na ubabe tunajifunza kupitia malezi mwanzo kabisa wa safari ya maisha yetu. Tunayowatendea watoto wetu yanakuwa itikadi inayoongoza sehemu kubwa ya maisha yao. 

 

Ukizungumza na wazazi wengi unaweza kuona wazi jinsi tunavyoamini kwa dhati katika bakora na adhabu kuliko malezi elekezi. Mwingine anakupa mpaka na vifungu vya biblia kabisa. “Usimnyime mtoto mapigo.” Mwingine anaamini ubabe a mabavu na kuumizana huo ndio utamaduni wetu. 

 

Tunachosahau wazazi ni kwamba unapoamini mtoto hawezi kuwa kufanya jambo bila kumwuumiza, kumtisha na kumpiga, maana yake unamwambia popote anapopata nafasi inayompa mamlaka juu ya wengine aitumie kuwatisha, kuwaonea, kuwaumiza na kuwanyamazisha wanaotofautiana naye, wasioamini katika kile anachoamini.

 

Unaposhabikia malezi ya kibabe—huoni uwezekano wa kumlea mtoto bila bakora, kumuumiza, kumtisha na kutweza utu wake—maana yake unashabikia maandalizi ya uongozi wa kibabe kazini kwako, mahusiano ya kibabe na mbaya zaidi siasa za kibabe ndani ya vyama vya siasa na hata siasa za ushindani katika nchi.

 

 

Ukiangalia matatizo mengi ya kitabia nyingi yanayotesa watu ukubwani —ikiwamo ubabe na kutokujali hisia za watu, kwa kiasi kikubwa, ni matokeo ya malezi ya kibabe, yasiyojali hisia za mtoto, yanayoamini zaidi katika kulinda mamlaka ya mzazi kwa kufoka, kuumiza, kutweza utu wa mtoto na hata ikibidi kupuuza. Watu wababe ukubwani, wasiojali hisia za mtu, ukichunguza, katika ukuaji wao walipuuzwa kihisia, walinyanyasika na pengine walipitia kwenye mazingira yanayowatia unyonge, walidharaulika kwa uwezo wao mdogo, na ukubwani wanakuwa na kazi ya kujaza ombwe la umuhimu walioukosa wakati wanakua. 

 

Kama kuna kitu cha maana unaweza kumpa mwanao ni kumfanya aamini yeye ni mtu muhimu kwako, anayestahili muda wako, sauti yake unaisikia, hisia zake unazielewa na wasiwasi wake unakuhusu. Mtu aliyelelewa hivyo hawezi kuwa mbabe anayeamini nguvu zake zinategemea unyonge wa wengine. Malezi bila fimbo yanawezekana. Malezi bila kutishana yanawezekana. Malezi yanayoheshimu hisia za mtoto yanawezekana. Malezi yanayoheshimu mtazamo wa mtoto yanawezekana. Tukilea bila kuumizana na kunyamazishana tutaongozana bila kuumizana. Tutaamini katika utatuzi wa matatizo kwa mazungumzo na kusikilizana bila matumizi ya nguvu na ubabe. Ninalenga kulieleza hili katika makala kadhaa zinazofuata.

 

 

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Uislamu ulianza lini?

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Jifunze Uhusiano wa Malezi na Vilema vya Haiba (Personality Disorders)

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)