Je, Kazi yako Inakuza au Inadumaza Wito Wako?
Inawezekana unafanya kazi ambayo hukuwahi kufikiri kama siku moja ungeifanya. Labda unadhani hukuchagua vizuri kipi cha kufanya, au pengine mazingira yalikulazimisha kushika kilichokuwa kinapatikana. Kwa upande mwingine, inawezekana pamoja na kuipenda kazi yako, unahisi kuna namna fulani ya udumavu. Hupati fursa za kupanda ngazi kiutendaji na umeanza kujihisi unapoteza wito wako. Vyovyote iwavyo, bado kuna tumaini. Unaweza kabisa kufanya kazi unayojua fika haiendani na wewe, lakini hatua kwa hatua, ikakutengenezea jukwaa zuri la kuumba vizuri wito wako. Hapa ninakuletea uzoefu utakaokusaidia kujitathmini na pengine kuchukua hatua muhimu katika kuchochea ule uwezo wa pekee ambao Mungu ameuhifadhi ndani yako. Unafanya kazi yenye staha? Mratibu wa Ukuuzaji wa Ujuzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Dar es Salaam, Bw. Albert William Okal anaeleza namna gani mazingira yako ya kazi yanavyoweza kukuza wito wako: “Hakuna kitu kama uchaguzi mbaya wa kazi. Kila kaz...