Tumia Mitandao ya Kijamii Kuboresha Utendaji wa Taasisi, Kampuni Yako

PICHA: kairalinewsonline.com



Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufikia Novemba 2017, Tanzania ilikuwa na jumla ya watumiaji wa mtandao wa intaneti wapatao 22,995,109. 

Moja wapo ya kichocheo kikubwa cha matumizi haya makubwa ya mtandao ni ongezeko la watu wanaotumia simu za viganjani zinazowezesha kuunganishwa na mtandao bila kulazimika kuwa na kompyuta zenye gharama kubwa. Hivi sasa, kwa mfano, takribani  line za simu za kiganjani zinazotumika zinafikia 40,080,954.

Uzoefu unaonyesha kuwa wengi wa watumiaji wa mtandao wa intaneti wanatumia zaidi mitandao kama vile WhatsApp, Facebook, Twitter, Instagram na YouTube.

Nguvu ya mitandao ya kijamii

Nguvu ya mitandao ya kijamii, kwa kiasi kikubwa, inategemea tabia ya watumiaji wake. Inakadiriwa kuwa mtumiaji mzuri wa mitandao hii, huchungulia kinachoendelea mtandaoni zaidi ya mara 20 kwa siku.

Makampuni makubwa ya habari kama Mwananchi Communications yanaonekana kuelewa fursa hii. Kwa mfano, wakati nikiandika makala haya, ukurasa wake wa Facebook ulikuwa na wafuasi 1,401,176  wakati ukurasa wake wa Twitter ulikuwa na wafuasi 267,179.

Hata hivyo, utafiti mdogo unaonyesha kuwa taasisi nyingi hazijaweza kuitumia vyema fursa hii. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa mfano, hakina ukurasa kwenye mtandao wa Twitter na kina wafuasi 9,558 kwenye mtandao wa Facebook.

Chuo Kikuu cha Mzumbe, kina wafuasi wasiofika 1000 Twitter na kina wafuasi 8,534 Facebook. Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kina wafuasi 6,070 Facebook na wafuasi 900 kwenye mtandao wa Twitter. Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kina wafuasi 4,768 Facebook na hakina ukurasa kwenye mtandao wa Twitter.

Bahiya Abdi, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU) anafikiri tatizo ni aina ya taarifa zinazohitajika na watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Anasema, “Kwamba taasisi za elimu ya juu zinapatikana kwenye mitandao ya kijamii lakini hazina wafuasi, tatizo linaweza kuwa watumiaji wenyewe wa mitandao. Kuna habari wanazozifuata na labda hazipatikani kwenye kurasa za taasisi hizi. Ndio maana unaweza kuona kurasa, kwa mfano, zinazojadili tetesi za watu maarufu ndizo zinazofuatiliwa zaidi.”

Maranya Mayengo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma anasema, “Kuwa na wafuasi wachache pia inasababishwa, pamoja na mambo mengine, kutokutangaza ukurasa wa mtandao wa kijamii angalau hata kupitia tovuti […] Kuna taarifa nyingi ambazo wateja wao wangehitaji kujua. Badala ya kutegemea tovuti pekee, mitandao ya kijamii ingewasaidia kuwafikia kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.”

Kwa kuwa ni ukweli uliodhahiri kuwa mitandao hii imekuwa ushawishi mkubwa katika jamii, kuna ulazima wa taasisi na makampuni kuangalia namna yanavyoweza kuwekeza katika mitandao hii. Katika makala haya, tunaangazia maeneo manne makubwa.

Kujenga taswira chanya ya taasisi

Moja wapo ya malengo ya kila taasisi au kampuni ni kujenga taswira chanya mbele ya macho ya jamii. Mitandao ya kijamii inaweza kuwa namna bora zaidi ya kufikia malengo hayo kama  anavyoeleza Maranya Mayengo:
 “Mitandao ya kijamii inasaidia kampuni au taasisi kupeleka taarifa kwa wateja wake watarajiwa kuhusu jambo lolote ambalo kampuni ingetamani kutangazia umma.”

Kama nilivyogusia awali, idadi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii ni kubwa kuliko watazamaji wa televisheni na wasomaji wa magazeti. Fedha nyingi zinazotumika kulipia matangazo kwenye vyombo vikuu vya habari  zinaweza pia kuelekezwa kwenye majukwaa haya ambayo ni rahisi kuwafikia watu.

Kuwafikia wateja wako kirahisi

Faida moja wapo ya mitandao ya kijamii ni kusaidia kutangaza huduma au biashara yako. Ukiweza kuwa na ufuasi wa kutosha kwenye mitandao ya kijamii, ni rahisi kujua wateja wako wanataka nini na ufanye nini kukidhi mahitaji yao.

Tafiti zinaonyesha kuwa unapokuwa na namna ambayo unafanya mawasiliano ya moja kwa moja na mteja wako, mteja huyu hujisikia kuthaminika na hivyo inakuwa rahisi kwake kufuata bidhaa au huduma unazotoa pale atakapokuwa na uhitaji.

Sayuni Nasari, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMMUCO) anasema, “Kumbuka mtumiaji wa mitandao ya kijamii huwa na mtandao wake wa watu wanaomwamini. Ukiweza kumpata mteja mmoja mwaminifu kwa huduma zako, unatengeneza mnyororo wa matangazo kupitia maoni anayoyatoa na hata picha anazoweka kuwaeleza marafiki zake mahali alipo na nini amekipata.”

Kupata mrejesho wa huduma na bidhaa zako

Taarifa kuhusu huduma zako zinapopatikana mtandaoni zinasaidia kuwafikia watu ambao kwa namna moja au nyingine ungehitaji fedha nyingi kuwafikia.
Ingawa taasisi nyingi hupenda kutumia tovuti kutangaza huduma zake, changamoto yake ni watumiaji kukosa fursa ya kuleta mrejesho kwa sababu hawana namna ya kuweka maoni yao.

Maranya Mayengo, ambaye pia ni mwanafuzni wa shahada ya uzamivu (PhD) anasema mitandao ya kijamii inatoa suluhisho:
“Watu wanapokuja kupokea huduma kwako wanakuwa hawajajiandaa kuandika maoni. Hata kama sanduku la maoni lipo lakini wanaweza wasiwe na kalamu na karatasi. Kwa msingi huo, mitandao ya kijamii ni namna ya kurahisisha upokeaji wa maoni juu ya huduma au bidhaa za kampuni husika.”

Kuwafahamu wafanyakazi wako

Kama mwajiri makini unahitaji kuwafahamu wafanyakazi wako. Kwa kuwa ni vigumu kupata uhalisia wa mfanyakazi wako katika mazingira ya kazi, unaweza kufuatilia shughuli zake katika mitandao ya kijamii.

Kwa mfano, kwa kutumia makundi ya WhatsApp ni rahisi kujua mfanyakazi yupi hutumia muda mwingi kupiga soga mitandaoni wakati wa saa za kazi na hivyo kumsaidia kudhibiti matumizi ya muda wake.

Lakini pia, shughuli za mfanyakazi wako mtandaoni zinaweza kukusaidia kujua aina ya maudhui anayopenda kuyafuatilia na hivyo kujua mitazamo yake kwa ujumla. Hili pia husaidia katika mchakato wa kuajiri wafanyakazi wapya.

Angalizo

Ipo hatari ya wahalifu kutumia vibaya jina la kampuni au taasisi kufanya shughuli zao mitandaoni. Hakikisha kurasa zako kwenye mitandao ya kijamii zimethibitishwa.

Kadhalika, unahitaji timu ya watu makini wanaoweza kujibu kero, dukuduku na maoni yanayotolewa mtandaoni bila kuharibu taswira ya taasisi au kampuni yako.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia

Uislamu ulianza lini?