Malengo Yanavyoweza Kubadili Tabia ya Mtoto




Mwanangu wa miaka saba alikuwa na tatizo la kupenda sana kununua vitu vitamu. Kila siku alikuwa ombaomba wa chochote kinachomtosha kwenda dukani. Sikupenda tabia hii.

Mbali na kuharibu meno yake, kulikuwa na tatizo la kutokujizuia. Ilifika mahali tunagombana kwa sababu tu hajapata chochote kukidhi hamu yake ya kununua ‘ice cream’, ‘chocolate’ na vinavyofanana na hivyo. Jitihada za kubadili tabia hii ya kupenda vitu visivyo na faida kwake hazikuzaa matunda.

Nikaona nijaribu mbinu nyingine. Siku moja jioni nikamrushia swali:  ‘Ungekuwa na hela zako mwenyewe ungetaka kufanya nini mwezi wa 12 mwakani?’ Swali gumu. Aliomba ufafanuzi. Nikafafanua. Hatimaye akasema anachotaka. Nikaona ni lengo dogo. Nilitaka awe na lengo kubwa la kufanyia kazi. Katika umri wake, fahari ya kufikia malengo ni motisha tosha.

Nikamsaidia kuona zaidi: ‘Hivi unajua unaweza kabisa kujilipia ada ya shule ukiamua?’ Ikaonekana naongea ‘mazingaombwe.’ Baada ya maswali yake kadhaa tukafikia muafaka kuwa inawezekana.

Nikaamua kupanua lengo lake: ‘Ungependa kwenda wapi mwezi wa 12 wakati wa Chrismas ijayo?’ Macho yake yakachangamka kwa furaha. Nilikuwa nimegusa jambo muhimu kwake.

‘Sasa nataka nikupe mtihani utakaokuwezesha kufanya yote hayo kwa hela zako mwenyewe.’ Akasisimka. Nikamweleza mpango ulivyo: ‘Tunataka kuwa na kiasi kitakachokutosha kulipa ada yako, kwenda kufurahia Christmas kule ulikochagua na kununua mahitaji yako uliyonitajia.’

‘Nitakuwa nakupa kazi za kufanya na ukizikamilisha mwisho wa wiki nitakulipa.’ Naelewa hatari ya kutumia fedha kama motisha kwa mtoto. Hata hivyo, lengo langu lilikuwa kumfanya ajione anawajibika na kipato chake na wakati huo huo afikie malengo aliyojiwekea.

‘Hela utakazopata, utaziweka kwenye kibubu. Kila wiki utaweka kiasi cha fedha kinachoonekana kwenye karatasi hii ya mtihani.’ Nikamwonyesha katarasi iliyokuwa na utaratibu wa kuweka kiasi fulani cha akiba kwa wiki. Kiasi hicho kinaongezeka mara mbili kila wiki inayofuata.
‘Ukishaweka fedha yako kwenye kibubu, unatiki hapa.’ Nikamwonyesha kisanduku cha kutiki mbele ya tarakimu zinazoainisha kiasi cha fedha atakachoweka kila wiki.

‘Una swali lolote?’ Maswali mengi. Nikamwelewesha. Hatimaye akauliza swali la mwisho, ‘Tunaanza lini?’ Nikamwambia, ‘Utakapokuwa tayari aniambie tukatengeneze kibubu.’ Hapo nilikuwa napima uwezo wake wa kufuatilia mambo ya msingi.

Kesho yake sikusikia akiongea suala la kibubu. Wiki moja ikapita sisikii habari za kibubu. Nikapatwa na wasiwasi. Ikabidi nimwuulize kulikoni.
‘Baba nilikuwa bado nafikiria utakuwa unanipa kazi gani hizo mpaka unilipe?’ Nikaelewa hoja yake. Tukaliweka hilo vizuri.

Kesho yake akanikumbusha kibubu. Nikajua somo limeeleweka. Tukamwomba mama yake atutengenezee. Nikamkabidhi karatasi inayomwongoza kiasi cha kutumbukiza kwenye kibubu. Nikamwomba aeleze shughuli nzima itakavyokwenda. Nikagundua anaelewa. Kazi ikaanza.

Nilichokiona kimenifunza. Wiki ya 10 sasa mtoto haombi tena hela ya kwenda kununua ‘chocolate’ wala  ‘ice cream.’ Kila anachokipata, anakitumia kupunguza deni kwenye mtihani wake wa ‘kibubu.’ Inavyoonekana lengo lililokidhi mahitaji yake limebadili tabia yake.

Kilichonifurahisha zaidi, sasa hivi anaomba ‘kazi’ za kufanya ili apate fedha za kupunguza ‘deni’ lake la ‘kibubu.’ Uombaomba wa hela za kwenda kutumia, umepungua kwa asilimia kubwa. Binti yangu anaonekana kuhakikisha lengo lake limetimia. Kama kuna jambo umejifunza, bado hujachelewa. Kwa msaada wako, mwanao anaweza kusimamia malengo.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia

Uislamu ulianza lini?