Mambo Sita Mwanao Anayohitaji Kuyasikia

PICHA: houstonpress.com



Watoto wadogo ni watu kamili wenye hisia kama sisi watu wazima. Hata kama wakati mwingine hawawezi kusema wazi wazi, ukweli ni kwamba akili zao ni kama dodoki linalonyonya kimya kimya yale wanayoona tukiyasema na kuyatenda.

Unaweza, kwa mfano, kusema jambo dogo kwa mtoto tena bila kumaanisha lakini jambo hilo likawa sumu itakayoharibu kabisa maisha ya mwanao. Unaweza kuwa na nia njema ya kumlazimisha kufanya kitu fulani sahihi kabisa, lakini kwa sababu hujaweza kuelewa na kujali hisia zake, jambo hilo likakosa nafasi kwenye moyo wa mtoto. 

Jukumu letu kama wazazi ni kuwasaidia watoto kujenga mtazamo sahihi wa maisha utakaowasaidia kuwa na mtazamo chanya na maisha, kujiamini na hata kuwa na nguvu ya kufanya mambo makubwa katika maisha kadri wanavyokuwa.

Katika makala haya, nimechagua mambo sita ninayoamini mtoto akiyasikia kwa mzazi wake anajenga mtazamo chanya na maisha yake. 

‘Ninakupenda’

Unaweza kumpa mtoto vitu vingi, lakini kamwe huwezi kumpa mtoto upendo utakamzidi. Unapokuwa na tabia ya kumwambia mwanao mara kwa mara kuwa unampenda unamfanya ajione anathaminika. Kuthaminika ni hitaji la msingi la kila mwanadamu.

Mwambie mtoto mara kwa mara kwamba unampenda. Mtoto akishaamini wewe mzazi wake unampenda atakuwa mtu mwenye ujasiri na furaha. Moyo wake utachangamka na atakuwa na utulivu. Bila kuwa na uhakika na upendo wako wewe mzazi wake, mtoto hukosa utulivu wa nafsi. Moyo wake utakuwa na ombwe. Hatajiamini.

Achana na yale mawazo kuwa ukimpenda sana mtoto unamdekeza. Unaweza kumpenda mtoto na bado ukawa na msimamo kuhakikisha anafanya kile anachotakiwa kukifanya.

‘Wewe ni fahari yangu’

Watoto, kwa kawaida, wanapenda kuwa na uhakika kuwa wao ni watu wa maana. Ndio maana mara nyingi wanafanya vitu kwa lengo la kusifiwa na wazazi wao. Huo sio udhaifu bali hitaji la msingi la nafsi. Mtoto anayeamini wazazi wake wanajisikia fahari na yeye mara nyingi anakuwa na mtazamo chanya na nafsi yake. Moyo wake unashiba na tabia zake zinatulia.

Hata kama hukubaliani na mengi wanayoyafanya, wajibu wako ni kuonesha unatambua juhudi wanazozifanya kufikia malengo fulani. Usiwe na matarajio makubwa mno kiasi kwamba mtoto anajikuta muda wote yuko kwenye shinikizo.

Kama ni kwenye masomo, usisubiri awe wa kwanza ili umtambue. Mpongeze kwa kila hatua anayopiga kwenye uelekeo sahihi. Kama ni tabia fulani, usisubiri awe mkamilifu ili umtambue. Tambua kila badiliko dogo jema analolionesha.

‘Nisamehe nimekosea’

Wakati mwingine sisi kama wazazi hatupendi kuonekana huwa tunakosea. Ingawa tunapenda watoto wajifunze kuomba msamaha pale wanapokesea, hatuwi tayari kuwa mfano wa kukiri makosa na kuomba msamaha.

Mtoto anahitaji kusikia ukikiri makosa yako. Hupotezi mamlaka yako kwa kumwambia mtoto kweli umekosea. Unapokubali kuwa umekosea, unapanda mbegu njema ya kuomba msamaha. Ukimwambia mwanao nisamehe, unamwonesha kuwa na wewe ni binadamu unayeweza kukosea na atakuamini zaidi.

Sambamba na kumwomba msamaha, unahitaji kujenga tabia ya kumsamehe. Mtoto anapokukosea, onesha mfano wa kuachilia. Kosa lisiwe sababu ya kuvunja uhusiano wako na mwanao.

‘Ninakusikiliza’

Binadamu tunapenda kusikilizwa. Unapoongea na mtu asiye na tabia ya kukusikiliza unajisikia vibaya. Unajiona huna thamani kwake. Hali hii inapoendelea kwa muda mrefu, inaweza kufanya ukawa na wasiwasi na vile ulivyo. Unaanza kujidharau.

Ndivyo ilivyo hata kwa watoto wetu. Pamoja na udogo wao, wanapenda sana kujua kuwa wanasikilizwa. Kumsikiliza mtoto kunagusa moyo wake kwa sababu anajisikia unajali na kumheshimu kama binadamu timamu.

Kusikiliza maana yake ni kumpa muda na masikio yako na kumpa usikivu. Pia kumsikiliza mtoto ni pamoja na kuvumilia mawazo yake. Badala ya kutoa maelekezo ya nini afanye muda wote, unaweza kumpa nafasi ya kusema mawazo yake hata kama unadhani hayana mantiki.

Ikiwa kuna haja ya kumrekebisha na kumwelekeza, fanya hivyo kwa upendo baada ya kuwa umemsikiliza. Mtoto anayelelewa kwenye mazingira kama haya hujenga tabia ya kuwa mkweli, kujiamini na kufanya maamuzi.

‘Unawajibika’

Umewahi kukutana na watu wanaopenda kubebesha wengine lawama hata kwa makosa yao wenyewe? Wapo pia wavivu lakini wenye tabia ya kuwalalamikia na kuwakosoa wale wanaojaribu kufanya kitu. Watu hawa hawajajifunza kuwajibika.

Mtu mwajibikaji, kwa kawaida, anajua kile anachotakiwa kukifanya. Unapokuwa mwajibikaji hutegemei watu wengine wafanye badala yako; hutafuti mtu wa kumlaumu mambo yanapokwenda mrama; huogopi kufanya maamuzi na kuwajibikia maamuzi yako.

Mfundishe mtoto uwajibikaji kwa kujenga tabia ya kuongozwa na malengo anapofanya majukumu uliyompa. Pale anaposhindwa kufikia malengo, au hata pale anapokosea, mwajibishe na aone matokeo ya kutokufikia malengo aliyonayo.

Pia, mpe mtoto fursa ya kufanya maamuzi yanayomhusu. Usimfanye awe mtu anayesubiri kuambiwa nini cha kufanya kila wakati. Pale anapohitaji mawazo, msaidie bila kummnyang’anya uhuru wake.

‘Ukiwa na bidii utafanikiwa’

Nimeshakutana na watu wengi wanaoamini mafanikio huja kwa muujiza. Wanafikiri kufanikiwa ni bahati na ‘kismati’ hivyo ili ufanikiwe lazima uombewe au basi upate msaada wa ‘nguvu za giza.’ Mawazo kama haya yamefanya watu wengi watumie muda mwingi kudanganyika kuliko kufanya kazi.

Nimefuatilia maisha ya watu wengi waliofanikiwa. Jambo moja liko wazi. Wanafanya kazi kwa bidii na kujituma. Hawasubiri kusaidiwa, hawasubiri muujiza utokee. Muujiza wanaoujua wao ni kujifunza mambo mapya na kuchukua hatua.

Tunahitaji kuingiza mawazo haya kwa watoto wetu. Hakuna mafanikio yanayopatikana kwa njia za mkato. Mtoto ajue bila kufanya kazi kwa juhudi na maarifa hawezi kufanikiwa.

Kadhalika, ni vyema mtoto ajue kuwa Mungu amempa kila anachokihitaji kupata mafanikio kulingana na uwezo wake. Kilicho muhimu na cha maana ni yeye kuelewa ulipo uwezo wake na aufanyie kazi. Mtoto akiwa na nidhamu ya maisha itakuwa rahisi kwake kupata mafanikio anayoyahitaji sasa na baadae.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia

Uislamu ulianza lini?