Zijue Ishara Tano Kuwa Mwajiri Amekuchoka




UMEWAHI kuhisi huhitajiki kazini? Umewahi kuona dalili kwamba pengine ni muda muafaka kwako kuchukua hatua kabla mambo hayajaharibika?
Mwandishi Speancer Johnson aliyeandika kitabu maarufu cha ‘Who Moved My Cheese” anasema ni muhimu kusoma alama za nyakati katika maeneo ya kazi. Unapofanya kazi bila kuelewa ishara za awali mambo yanapoanza kwenda mrama, unajiweka kwenye hatari ya kujikuta kwenye mazingira ya kufanya maamuzi kwa kuchelewa.

Wafanyakazi wengi huamini mwajiri akiwachoka atawaandikia barua ya kuwafuta kazi. Hawajisumbui kujua kusoma ishara mbaya kwa kuamini mwajiri hawezi kuwachoka na akabaki kimya.

Unaweza kujiuliza, kama kampuni haikuhitaji kwa nini hawakuambii? Ukweli ni kwamba, wakati mwingine mwajiri huona ni afadhali akuwekee mazingira ya wewe kuondoka mwenyewe kuliko kukuondoa.

Mwajiri anapokuondoa anajiweka kwenye mazingira yanayoweza kumletea usumbufu wa kisheria na wakati mwingine wafanyakazi wanaobaki hupatwa na tahayaruki.

Ili kuepuka kujiingiza kwenye mgogoro wa kisheria, waajiri wengine huweka mazingira ya wafanyakazi wasiohitajika kujiona hawawezi kuendelea na kazi. Ishara hizi tano zinaweza kukusaidia kusoma alama za nyakati.

Unaanza kukufuatiliwa kwa karibu

Ulizoea kuachwa ufanye majukumu yako bila kuingiliwa na wasimamizi wako. Wakubwa wako walikuacha ufanye kazi kwa uhuru fulani na kila ulipohitaji mrejesho, hapakuwa na urasimu. Ghafla, wakubwa hawa wanaanza kukufuatia kwa karibu sana mpaka unajiuliza maswali.

“Kama bosi wako ameanza kuwa na tabia ya kukufuatilia kwa karibu na kutaka mrejesho wa mara kwa mara isivyo kawaida, kuna uwezekano kuwa hali si shwari,” anaeleza Sayuni Nasari, mwanafunzi wa Shahada za Uzamivu (PhD) kwenye Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela jijini Arusha.

Hata hivyo, wakati mwingine kufuatiliwa kwa karibu inaweza kuwa ishara kuwa mkubwa wako wa kazi anataka uboreshe kazi yako. Muhimu ni mrejesho unaoupata. Ikiwa unakosolewa hata kwa mambo madogo, tena ukosoaji wenyewe wakati mwingine ni wa jumla na haulengi masuala mahususi, kuna uwezekano kuwa kuna jambo linaendelea nyuma ya pazia.

Unalazimika kuweka kila kitu kwenye maandishi

Inawezekana wakati unaanza kazi hapakuwa na haja yoyote ya kuweka kila kitu kwenye maandishi. Ruhusa ulipewa kwa mdomo, ulipokosea uliitwa faragha na kuonywa kwa maneno ya kirafiki, hata mrejesho wa kazi ulifanyika kwa maneno zaidi.

Sasa ghafla kila kitu kimeanza kuwekwa kwenye maandishi. Muda wa kuingia kazini, ruhusa, mrejesho wa kazi uliokuwa ukiupata kwa maneno sasa unaanza kufanyika kwa kujaza fomu.

Waajiri wengi huwa na utaratibu wa kuwawajibisha wafanyakazi wake. Utaratibu huu ni pamoja na kuweka kumbukumbu kwa maandishi. Lakini kama kampuni inataka uondoke, utaratibu huu unafanywa kuwa sehemu ya urasimu wa karibu kila unachokifanya. Mwajiri anayetaka kukuchosha atataka kutumia vielelezo vya maandishi kukutisha na kukufanya ujisikie hauko salama.

Hakuna mipango ya muda mrefu ya kukuendeleza

Kukuza ujuzi wako ni sehemu ya wajibu wa mwajiri. Ingawa katika sekta binafsi utaratibu wa kumwendeleza mfanyakazi unategemea zaidi uwezo wa mwajiri na aina ya kazi unayofanya, bado ni lazima kuwe na utaratibu fulani wa kumwendeleza kiujuzi.

Si lazima kampuni ikupe ruhusa ya masomo ukasome shahada, lakini hata kupata mafunzo ya muda mfupi yanayolenga kuongeza thamani yako kazini ni sehemu ya mpango wa kukuendeleza.

Inapotokea unafanya kazi mahali kwa muda mrefu na huoni fursa yoyote ya kukuza kiujuzi, wakati huo huo unaona wenzako wanapelekwa kwenye mafunzo kwa msaada wa mwajiri, usichukulie kirahisi.

Ni kweli inawezekana uwezo wa mwajiri kifedha ni mdogo na anaelekeza rasilimali chache alizonazo kwenye maeneo ya kipaumbele. Lakini kama wenzako mnaolingana nao wanapelekwa kwenye mafunzo na wewe unaachwa usijue kinachoendelea, pengine ni wakati wa kujitafakari kwa kina.

Mambo mengi yanaanza kukupita

Mawasiliano ndio moyo wa utendaji wa kazi wa kitaasisi. Bila mawasiliano ni vigumu wafanyakazi kuoanisha malengo yao ya kiutandaji kwa lengo la kuongeza uzalishaji au huduma.

Kwa sababu hiyo kampuni huwa na utaratibu wa kuwa na vikao na mikutano ya mara kwa mara, mawasiliano ya simu na barua pepe ili kuwasaidia wafanyakazi kupata mtiririko wa taarifa za muhimu wanazozihitaji katika utendaji wao wa kila siku.

Inapotokea umewekwa pembeni kwenye mawasiliano haya, usichukulie kawaida —hasa kama wafanyakazi wenzako wanaendelea kupata taarifa hizi.
Chukulia sasa umeanza kupata taarifa muhimu kupitia mazungumzo ya ‘wakati wa chai’ na wenzako na hakuna anayekupatia taarifa hizi kwa kupitia utaratibu rasmi.  Hii inaweza kuwa na maana kuwa kuna watu wapya wamechukua nafasi yako.

Unaanza ‘kupunguziwa’ majukumu

Unapoona watu wanakubebesha majukumu mengi kazini, usijisikie vibaya. Mara nyingi hii ni dalili kuwa unaaminika. Lakini kama ulizoea kupewa majukumu mengi na sasa ghafla umeanza kuwekwa pembeni kwenye majukumu kwa madai kuwa umezidiwa una haki ya kuwa na wasiwasi.

Bosi wako anapoanza kukupunguzia majukumu uliyozoea kuyafanya—au yale anayojua unayapenda—bila maelezo ya msingi, tafsiri yake ni kwamba ni ama hawana kazi na wewe au hawakuamini tena.

Wakati mwingine inaweza kuwa kinyume. Unashangaa ghafla unapewa kazi ambazo mkubwa wako anajua fika huziwezi. Lengo mara nyingine huwa ni kuthibitisha kuwa huwezi kazi.

Ushauri

Mara nyingine ni vigumu sana kutafsiri dalili hizi tulizoziona. Ndio maana unahitaji kupata msaada wa wataalaam wa raslimali watu kujua hatua za kuchukua. Hata hivyo, unapoona unaanza kupatwa na wasiwasi na usalama wako kazini lazima kuna tatizo mahali.  Jitathimini uone umechangiaje hali hiyo na ujirekebishe. Ikiwa wasiwasi huo unaongezeka, pengine ni wakati muafaka kuanza kufikiria maisha mengine nje ya hapo ulipo.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia

Uislamu ulianza lini?