Machapisho

Inaonyesha machapisho yenye lebo ya Lugha na kufikiri

Mbinu Sita za Kukumbuka Maarifa Unayojifunza

Picha
Mafanikio ya kitaaluma, kwa kiasi kikubwa, yanategemea namna unavyoweza kusoma na kukumbuka kile ulichokisoma. Kusoma kwa bidii na kuelewa unayoyasoma ni muhimu. Lakini kama huwezi kukumbuka ulichokielewa, itakuwa vigumu kufanikiwa. Mitihani, kwa mfano, hupima uwezo wako wa kukumbuka kile unachokijua. Hiyo, hata hivyo, haimaanishi uishie kukumbuka. Unahitaji kuelewa unayojifunza kwa kina lakini pia uwe na uwezo wa kukumbuka.

Jinsi ya Kukuza Umahiri wa Lugha kwa Mtoto

Picha
Tunahitaji lugha katika maisha yetu ya kila siku. Tunapofikiri mambo yaliyopita, yaliyopo na yajayo, tunatumia lugha. Tunapowasiliana na wengine, tunahitaji lugha. Lugha, katika mukhtadha huu, ni nyezo muhimu inayotuunganisha na watu wanaotuzunguka. Ingawa wataalam wa namna mtoto anavyojifunza lugha hawana jibu moja, ni wazi zipo kanuni za matumizi ya lugha ambazo mtoto huzaliwa nazo. Lakini pia mazingira anayokulia mtoto, nayo yana nafasi kubwa ya kujenga uwezo wake wa kutumia lugha. Ndio kusema, kama mzazi unahitaji kuelewa kuwa unao wajibu mkubwa wa kumsaidia mwanao kuwa mahiri katika lugha. Kujifunza lugha kunafuata hatua kadhaa.

Namna Michezo Inavyomsaidia Mtoto Kujifunza

Picha
Wazazi wengi wanaichukulia michezo ya watoto kama shughuli isiyo na maana. Kimsingi, ipo imani inajengeka kuwa kucheza ni kupoteza muda. Matokeo yake wazazi hujitahidi kuwazuia watoto wasicheze kwa matumaini ya kuwasaidia wapate muda wa kufanya mambo ya maana zaidi kama vile kusoma na kukamilisha kazi za shule. Pamoja na umuhimu wa kufanya hivyo, hata hivyo, michezo  inabaki kuwa shughuli yenye umuhimu mkubwa katika ukuaji wa jumla wa mtoto kimaarifa, kimahusiano, kimwili na kihisia.

Kumsaidia Mtoto Kujifunza na Kumudu Lugha

Picha
Lugha ni nyenzo muhimu sana tunayoihitaji katika maisha. Hatuwezi kufikiri vizuri, kuongea kwa ufasaha, kusikiliza, kueleza mambo tuliyokutana nayo na hata tunayoyatarajia siku zijazo bila kuhitaji lugha. Ni wazi tunalazimika kutumia maneno au ishara kuwasiliana na wanaotuzunguka. Mjadala wa namna gani mtoto hujifunza lugha ya mama una historia ndefu. Kwamba mtoto huzaliwa na asili ya lugha inayoongoza namna anavyojifunza lugha au ni mazingira anayokulia ndiyo yanayomwezesha kujifunza, ni vigumu kuhitimisha kwa hakika. Hata hivyo, kuna ukweli kwamba ili mtoto ajifunze lugha ipasavyo anahitaji kuwa na uwezo fulani anaozaliwa nao unaomwezesha kuelewa kanuni muhimu za lugha bila msaada mkubwa. Lakini pia mazingira, anayokulia mtoto, nayo yana nafasi kubwa ya kumwezesha kujifunza na kumudu lugha ya kwanza kirahisi.

Unauelezaje utamaduni wa kusainiwa kitabu na mwandishi?

Picha
Profesa Mbele anaeleza vizuri kuhusu utamaduni wa kusainiwa vitabu katika blogu yake:  "...Suala hili la kusaini au kusainiwa vitabu linastahili  kutafakariwa. Naamini lina vipengele kadhaa muhimu, kama vile kiutamaduni, kisoshiolojia, kisaikolojia, na kifalsafa. Hata katika maduka ya vitabu hapa Marekani, aghalabu utaona vimepangwa vitabu vya mwandishi vikiwa na ujumbe "Signed copy." Jambo hili linaisukuma akili yangu kutaka kulielewa zaidi. Ningependa kujifunza zaidi kuhusu suala hili, kwa kusoma maandishi mbali mbali na kufanya tafakari mwenyewe..."  Msomaji wa kitabu cha Profesa Mbele, akifurahia nakala ya kitabu. Picha: @hapakwetu Unaweza kusoma zaidi kwenye blogu yake hapa . Kama mmoja wa wasomaji waliowahi kupata bahati ya kusainiwa kitabu na mwandishi mwenyewe, mmoja wapo akiwa Profesa Mbele, mwandishi wa kitabu kizuri cha " Africans and Americans Embracing Cultural Differences ", nikiri kabisa kwamba suala hili lina muujiza wa aina...

Je, ni kweli lugha huathiri namna tunavyofikiri?

Picha
MJADALA wa nafasi ya lugha katika namna tunavyofikiri na kuyaelewa mazingira yetu una historia ndefu. Kwa ujumla kumekuwepo na pande mbili kuu. Upande wa kwanza unashikilia kuwa lugha, ama mawasiliano ayafanyayo mtu na wengine, iwe kwa maneno, ishara, alama au vitendo haina uhusiano wowote na namna mtu anavyofikiri. Ushahidi wa madai haya ni namna watoto wadogo wanavyoweza kufikiri uzuri bila hata kujua lugha. Na ni kweli pia kwamba kwa mtoto fikra au uelewa hutangulia uwezo wa lugha. Kwamba hawezi kusema wala kuonyesha kusikia kinachosemwa, hiyo haimaanishi kuwa mtoto hafikiri. Na ndio maana wakati anajifunza lugha, mtoto huweza kutumia neno moja kumaanisha mambo mengi. Anaelewa kuliko anavyotumia lugha. Vile vile, inasemekana, watu wenye ulemavu wa kutumia maneno kuwasiliana na wenzao, bubu kama tunavyowaita, wana uwezo mzuri wa kufikiri kama watu wengine. Kwamba watu hawa hawana tatizo la kuyatambua na kuyaelewa mazingira yao kwa ufanisi ule ule tunaouona kwa watu wasio na ulemavu...

CHANGAMOTO Insha za Jamii - Prof. Mbele

Picha
Natamani sana kukisoma kitabu hiki. Ninakitafuta kwa bidii. Unajua kinakopatikana? Mwandishi Profesa Mbele anasema kakiandika kusahihisha majungu kuhusu Mwalimu Nyerere. Msome hapa halafu uone kama unaweza kujishindia Dola 100! Waweza pia kusoma majadiliano katika Jamii Forums yanayodurusu ikiwa wanaomkosoa Mwalimu Nyerere wana hoja.

Je, tunafikiri kwa kutumia lugha?

Kuna changamoto zimejitokeza kwenye ule mjadala wa tasnifu ya msomi wetu ambayo kwa maoni yaliyotolewa huenda ingekuwa bora kama ingekuwa katika kiswahili. Changamoto kubwa zaidi ni ile iliyoletwa na msomaji Godwin Habib Meghji akihoji ikiwa mwanadamu hufikiri kwa kutumia lugha. Hapa anasema: "Mimi sina uhakika kama binadamu anafikiria kwa kutumia lugha fulani. Viziwi na bubu pia hufikiri". Hii ni changamoto nyingine. Una maoni gani katika hili? Je, tunawezaje kufikiri? Fikra zinauhusiano wowote na lugha? Je, bubu ama kiziwi hana lugha kwa sababu tu hawezi kutamka ama kusikia?

Soma 'tasnifu' ya msomi wa Chuo Kikuu

Mjadala wa lugha gani itumike katika mfumo wetu wa elimu, ni suala la kutia aibu kuliko hata aibu yenyewe. Inadhalilisha sana unaposikia watu wazima hajui tutumie lugha gani kufundishia. Eti tunabishana kipi bora Kiswahili ama Kiingereza, kweli? Fedheha hii inatokana na ukweli kwamba lugha ya kiingereza inayolazimishiwa hivi sasa ni miongoni mwa maajabu saba ya dunia kwa wanafunzi wengi. Leo nimekuja na ushahidi wa karibu kabisa unaonyesha sura halisi ya tatizo. Nimepata bahati ya kupata karabrasha la 'utafiti' uliofanywa na mwanafunzi mmoja wa Chuo Kikuu aliyekuwa anajiandaa kuitetea Digrii yake kwa kuandika 'tasnifu'. Baada ya kusoma vipande vichache vya karabrasha hili naomba uamue mwenyewe kuwa Digrii iliyomwezesha kuandika andiko hili ni halali ama ni feki. Halafu fikiri nani wa kumlaumu: yeye mwenyewe asiyejua lugha ambayo ni ya wakoloni na haitumii kuwasiliana na jamii yake au ni serikali yake isiyoelewa makosa ya kugenisha hadi lugha? Inawezekana kabisa ku...

Viziwi wanaosikia tusivyovisikia...

Singida kwema. Nimekuwa na wakati mzuri na marafiki tulioachana kwa kipindi kirefu. Nimekuwa kiguu na njia utadhani kuku mfungwa aliyeachiwa kwa makosa. Jana nilipata fursa ya kutembelea shule ya viziwi na wasioona, Huruma. Nilikutana na walimu waliojitoa kuwasaidia watu hawa kwa moyo. Ilisisimua kuona viziwi wakipiga soga kwa lugha ya ishara. Walikuwa wenye furaha, kiasi kwamba hakuna kilichoonekana kuwapungukia. Nikajifunza. Kumbe furaha ni vile unavyoamua uwe. Huna haja ya kuwa na vyote ili kuipata. Nilimwona kijana asiyeona wala kusikia, lakini mwenye kusema! Ili kuwasiliana nae, unaandika mkononi mwake, anaelewa, halafu anajibu kwa mdomo! Naye huwezi amini kwa jinsi alivyojaa furaha! Nikaonana na wasioona wenye matumaini. Wasioona, wenye kuona tusivyoviona. Wenye furaha bila kutegemea vionekanavyo. Nikaondoka nikiwa na mawazo tele. Upofu na uziwi ni zaidi ya huu wa mwilini!

Kama sio utumwa ni nini hiki?

Habari za siku ndugu msomaji. Binafsi sijambo. Nafurahi kurejea kibarazani baada ya heka heka za huko na huko. Itoshe kuhusu mimi, nikukaribishe tena humu ndani. Leo ningependa kukusimulia kisa kimoja. Nikuase kwanza, kwamba usilazimike kunielewa vibaya. Sijawa na tabia ya kuona makosa zaidi niwapo mahali ama nikutanapo na watu. Maana siamini kwamba binadamu ana kazi ya kushabikia makosa kuliko jema moja. Nisijitetee sana. Jumapili hii nilipata fursa ya kuhudhuria ibada kwenye kanisa la 'kisomi'. Washirika wa kanisa hili, wengi wao ni wale ambao umande haukuwazuia kuhudhuria shule. Wamesoma. Pamoja na ukweli kwamba wote walikuwa weusi kama mimi, lakini ilikuwa bayana kwamba kiingereza kilikuwa 'nguzo' ya ibada hiyo. Hilo halikuwa tatizo kwangu. Maana inaeleweka kwa wengi wetu kwamba, kusoma kunathibitishwa na umahiri wa kusema kiingereza. Nshazoea hili. Pamoja na ukweli kwamba kiuhalisia kiswahili ndicho kinachotawala madarasani lakini watu hatutaki kuukubali ukweli...

Uhuru huu ni kwa ajili ya nani?

Ninaomba msamaha kama hutanielewa. Ila ninadhani jambo hili ni muhimu ukalitafakari kwa kina wakati ukisherehekea “uhuru” wa nchi yako iliyo masikini kuliko zote kusini mwa jangwa la Sahara. Hivi kweli nchi yetu ina haki ya kusherehekea hicho kilichopewa jina la “uhuru”? Uhuru maana yake ni nini? Ni kwa kiasi gani twaweza kujikagua kuona ikiwa tu huru kweli? Kama uhuru una maana ya mambo kuwa hivi yalivyo, vipi utumwa? Ni kwa kiasi gani uchumi wa nchi hii unathibitisha kuwa kweli tu “huru”? Ni kwa kiasi gani utamaduni wetu unathibitisha hicho kinachoitwa “uhuru”? Ni kwa kiasi gani? Ni kwa vipi tunaweza kujiridhisha kwamba elimu yetu inakubaliana na kelele zetu za “uhuru”? Hivi mababu zetu walipokuwa wakiusaka uhuru lengo hasa lilikuwa nini? Leo hii tunasoma Vyuo Vikuu kwa vitisho kutoka kwa wenzetu wanaofafana na sisi. Haturuhusiwi kufikiri. Elimu yenyewe imekaa mkao wa kitumwa. Tunafundishwa akademia ituondoayo katika wigo wa kuyaelewa matatizo yetu ya kila siku. Inatuondoa k...

Matokeo ya utafiti wa Mwaipopo

Mwaipopo, mwanablogu wa Sauti ya baragumu ameonyesha mfano wa namna wanablogu tunavyoweza kuyachunguza mambo na kisha kupata michango yenye uzito unaovutia. Mfano huu ni wa kuigwa na kila mpenda mijadala. Nataraji kwamba wasomaji watakumbuka lile swali la lugha nililokuwa nimeliuliza kuonyesha ugumu uliopo katika kulitafsiri kwenda kwenye kiingereza ambacho hakitapoteza maana. Tulipata majibu mengi. Ndipo Mwaipopo kwa msukumo wa kupenda utafiti, akafanya uchunguzi na haya ndiyo majibu yake: " Jamani sikuishia hapo. Nilikuwa nafanya kautafiti kadogo ili nije tena...Swali hili liliponitoa jasho nikaona nimuulize rafiki yangu mzungu. Nae kaiona shida. Bahati njema anajuajua kidogo Kiswahili cha kuendea kariakoo. Kama mjuavyo mimi ni linguist. Niliwahi kusoma translation course. Hili ni tatizo miongoni mwa matatizo ya fasili - maneno ama miundo yenye kuegemea katika utamaduni wa lugha husika. hata hivyo panapo nia ya kutafsiri lazima njia itafutwe. hasa ni kwa nia ya kujif...

Kwa mabingwa wa Tafsiri fasaha

Kwa wanaopenda kiingereza.Tafadhali naomba tafsiri ya maneno haya kwa kiingereza ambacho hakitabadili maana iliyopo katika kiswahili hiki: "MAMA, HIVI MIMI NI MWANAO WA NGAPI KUZALIWA?" Ukipata tushirikishane.

Kukosoa, kutafuta makosa, si tabia njema

Siamini kwamba ukosoaji ni asili ya mwanadamu. Kufikiria kinyume (negative). Kwamba watu wote wanakosea isipokuwa wewe. Kwamba watu wote wamepotea isipokuwa wewe. Kwamba watu wote wanahitaji msaada isipokuwa wewe. Kufikiria ubaya zaidi wa jambo kuliko uzuri wake. Kufikiria udhaifu kuliko ubora wake. Kufikiria uharibifu zaidi kuliko uboreshaji. Kwamba unaweza kusoma kitabu cha mwandishi fulani, si kwa sababu unataka kujifunza, bali kupekua wapi kakosea. Kwamba unaweza kuzungumza habari za mtu, si kwa nia ya kujenga, bali kwa nia ya kumtafutia makosa yake. Kwamba watu wanaweza kukwambia jambo zuri na la manufaa, lakini wewe ukalichukulia kwa mtazamo hasi. Ukakosoa. Kwa nini iwe rahisi zaidi kufikiria udhaifu/ubaya wa mtu/suala kuliko kufikiria uzuri wake? Hivi mwanadamu anavutiwa na nini kutafuta kasoro? Je, kutafuta/kupekua kasoro ni asili ya mwanadamu ama ni tabia inayojiotea kulingana na mazingira ya mhusika?