Mbinu Sita za Kukumbuka Maarifa Unayojifunza

Mafanikio ya kitaaluma, kwa kiasi kikubwa, yanategemea namna unavyoweza kusoma na kukumbuka kile ulichokisoma. Kusoma kwa bidii na kuelewa unayoyasoma ni muhimu. Lakini kama huwezi kukumbuka ulichokielewa, itakuwa vigumu kufanikiwa.
Mitihani, kwa mfano, hupima uwezo wako wa kukumbuka kile unachokijua. Hiyo, hata hivyo, haimaanishi uishie kukumbuka. Unahitaji kuelewa unayojifunza kwa kina lakini pia uwe na uwezo wa kukumbuka.
Kukumbuka ni uwezo wa kuzipata taarifa ulizozihifadhi akilini ili uweze kuzitumia pale unapozihitaji. Kwa mfano unapokutana na mtu uliyekutana naye miaka kumi iliyopita na kuweza kupata jina lake katika fahamu zako na ukamwita kwa jina lake, hapo umekumbuka. 
Kwa kawaida, akili ya mwanadamu haikumbuki kila taarifa. Huchagua kipi cha kusahaulika na kipi cha kukumbuka. Ndio maana tunaona mengi lakini tunakumbuka yale machache ambayo akili inayapa uzito.
Ingawa kusahau kuna faida zake, wewe kama mwanafunzi ungependa kukumbuka mambo unayoyasoma.  Uzoefu unaonesha kuwa hata kama tunapenda kukumbuka, wakati mwingine tunasahau yale tunayotamani kuyakumbuka.
Makala haya, kwa kutumia uchambuzi wa tafiti mbalimbali za elimu ya kujifunza, yanapendekeza mbinu sita kukuwezesha kukumbuka.


Furahia unachotaka kukikumbuka

Maya Angelou aliwahi kusema, watu huweza kusahau yale uliyowaambia, lakini hawawezi kusahau ulivyowafanya wajisikie. Kisayansi jambo hili ni kweli. Tunakumbuka kwa urahisi zaidi mambo yanayogusa mioyo yetu kuliko fahamu zetu.

Unapoudhiwa na mtu, kwa mfano, ni rahisi kukumbuka. Unapofurahishwa na jambo, hulazimiki kukariri ili ukumbuke. Ndio kusema, hisia zako zinapokuwa zimeguswa moja kwa moja ni rahisi kukumbuka kilichokugusa. Tumia kanuni hiyo unaposoma.

Jitahidi kufurahia kile unachojifunza. Penda masomo yako. Kama unasoma Hisabati, anza kwa kuipenda. Unapopenda kile unachokisoma, unaongeza uwezekano wa kukikumbuka. Usipopenda masomo, itakuwa rahisi kusahau.

Fahamu wazo kuu kabla ya undani

Kwa kawaida, akili haipendi kuhangaika. Hutafuta namna rahisi ya kuelewa jambo. Kama unataka kuiongezea uwezo wa kukumbuka jambo unalokusudia kulikumbuka, isaidie akili yako kuingiza vitu kichwani hatua kwa hatua. Usisome kwa mkupuko. Soma kwa awamu.

Anza kwa kuelewa wazo kuu la kile unachojifunza kabla hujaweka nguvu kuelewa undani wake. Unapoelewa maarifa ya jumla kwanza, unajenga msingi wa hatua ya pili ya kuingiza taarifa za kina kujazia kile ambacho tayari akili yako inakijua.

Ndio kusema, unahitaji kusoma kwa utaratibu bila papara. Soma mara ya kwanza kupata wazo kuu linalobeba uelewa wa jumla kwanza. Ukishaelewa, tafuta muda wa kuongeza taarifa za undani wa kile unachokijua.

Tafuta mfanano na utofauti wa dhana

Kuelewa unachokisoma kunategemea ni kwa kiasi gani hicho unachokisoma kinaoana na kile unachokifahamu. Akili ina kawaida ya kupangilia maarifa kwa kuhusianisha kile kinachoingia akili na kile kilichopo tayari.

Unapoingiza taarifa isiyofanana na kile unachofahamu, utatumia nguvu nyingi bila sababu. Kwa hivyo unashauriwa kusoma kidogo kidogo kwa kuhusianisha kile unachokisoma na kile unachokifahamu ili kurahisisha kazi ya akili kupangilia mambo kukuwezesha kuelewa.

Hata hivyo, ili uweze kukumbuka baadae, lazima ujue namna gani hicho unachokiingiza akili kinatofautiana na kile unachokijua tayari. Ni vizuri unaposoma ujiulize, ‘hiki ninachokisoma kinatofautianaje na ninachokifahamu?’

Oanisha unachokisoma na maisha halisi

Akili, kama tulivyoona, ina kawaida ya kukumbuka mambo inayoyachukulia kuwa ya muhimu. Mambo yasiyo na umuhimu akili huachana nayo na kuyasahau. Sambamba na hilo, ni rahisi kukumbuka maarifa yanayoendana na maisha halisi kuliko maarifa yasiyo na uhusiano na maisha yetu.

Unapopita barabarani, kwa mfano, unakutana na watu wengi ambao kimsingi huwezi kuwakumbuka. Lakini unapokutana na mtu anayehusiana na maisha yako, ni rahisi kumkumbuka.

Jaribu kuhusianisha maarifa unayojifunza na maisha yako ya kila siku. Kama huwezi kuona namna gani hayo unayoyasoma yanahusiana na maisha yako ya kila siku, lazima utasahau.

Tumia maarifa unayojifunza

Wataalamu wa elimu wanasema hatua ya juu kabisa ya kujifunza ni kutumia kile unachokijua. Uelewa usiotumika hakuna maana. Ndio maana walimu wazuri husisitiza mwanafunzi afanye kitu kama matokeo ya kujifunza.

Mwalimu atakupa kazi ya kusoma mwenyewe, atakufanya ujadili na wenzako, lengo likiwa kukushughulisha utumie maarifa unayojaribu kujifunza kwa wakati huo kwa kuyaongelea, kuyaandika na namna nyingine za kuyatumia.

Jenga tabia ya kutumia maarifa yako. Andika kila unaposoma. Fundisha wenzako. Jadili na wenzako. Fanya maswali mara kwa mara. Kufanya hivyo, kunakusaidia kuyamiliki maarifa uliyonayo na hivyo kurahisisha kazi ya kukumbuka.

Inapobidi, kariri

Pamoja na umuhimu wa kuelewa taarifa tunazojaribu kuzikumbuka, bado wakati mwingine tunakutana na taarifa zisizohusiana na yale tunayoyafahamu. Tunapotaka kukumbuka namba za simu, kwa mfano, tunalazimika kukariri. Hatuwezi kusema tunazielewa tarakimu kumi zinazotambulisha namba ya simu.

Katika mazingira kama haya unahitaji kukariri. Ingawa watu wengi hubeza neno ‘kukariri’ na kulihusianisha na kutokuelewa, lakini ukweli ni kwamba kukariri ni sehemu ya maarifa tuliyonayo.

Jifunze mbinu za kukariri kwa urahisi. Rudia rudia kile unachotaka kukikumbuka. Unaporudia rudia jambo hata kama hulielewi, unaongeza nafasi ya kulikumbuka. Unaweza pia kutumia herufi za mwanzo za orodha ya hoja unazotaka kuzikumbuka kutengeneza maneno unayoweza kuyakumbuka kirahisi.


Fuatilia Jarida la Maarifa ndani ya gazeti la Mwananchi kwa makala kama hizi.

Maoni

  1. Nmependa na ningependa npate ushauli mwingi wa namna ya kukalili na kufulah kile ktu. Unachokikalili

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mbinu za Kujenga Ujuzi wa Mwanafunzi

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?