Mpe Mtoto Wako Fursa ya Kujifunza Maisha Halisi

Katika mazingira yetu, si wazazi wengi wanaweza kuwa tayari kuona watoto hawawezi kufanya kazi za nyumbani kama kupika, kufua nguo, kusafisha vyombo na kutandika kitanda.

Lakini kutokuweza kufanya kazi hizi, wakati mwingine kunatokana na mitazamo ya wazazi kuwa kazi za ndani hufanywa na mama peke yake au msichana/kijana wa kazi na hivyo watoto hawaruhusiwi kushiriki kazi ‘zisizo zao’.

Utaratibu huu, hata hivyo, unaweza kuwa na athari kwa maisha ya mtoto pale atakapoondoka nyumbani na kuanza kuishi na watu wengine. Hata kama mtoto anaweza kuwa mwerevu na mchangamfu, bado huweza kuonekana kama mtu mvivu, tegemezi na asiyejua maisha.  

Ni kwa sababu hiyo, wazazi wanao wajibu muhimu wa kumfundisha mtoto kuwajibika na kufanya kazi za mikono kungali mapema.

Malezi ni kukuza uwezo wa kujimudu

Mbali na kutengeneza mazingira ya mtoto kukua kiakili, kimwili, kihisia na kimahusiano, lipo eneo muhimu la kimakuzi linalosahaulika. Nalo ni uwezo wa mtoto kufanya vitu bila msaada mkubwa wa watu wazima.

Uwezo huu humsaidia mtoto kukabiliana na changamoto za maisha na huimarika kadri mtoto anavyokuwa kiakili na kimwili. Mifano rahisi ya uwezo wa kujimudu anaozaliwa nao mtoto ni kukaa bila msaada, kusimama, kutembea mwenyewe na hata kutumia vifaa mbalimbali bila kuleta uharibifu.

Pia yapo maeneo ya kujimudu ambayo mtoto huhitaji kujifunza kama vile kulala bila kukojoa kitandani, kula mwenyewe, kujiogesha, kupiga mswaki, kufua nguo zake na kuvaa nguo.

Kadhalika, kujimudu huenda sambamba na kuwajibika, yaani kuwa tayari kufanya majukumu bila kuwasubiri wengine wafanye. Ni kinyume cha uvivu na kutegea. Faida yake ni kumwongezea mtoto uwezo wa kujiamini.

Tuangalie maeneo matatu muhimu yanayohitaji mkazo katika kukuza uwezo wa mtoto kujimudu na kujitegemea.

Kujimudu kimwili

Kama tulivyodokeza awali, mtoto huzaliwa na uwezo wa kujitegemea kimwili wakati mwingine bila msaada. Kwa mfano, mpaka anapotimiza miezi sita, mtoto humudu kiwiliwili chake na kuweza kunyanyua shingo na kichwa hata anapokuwa amelala kifudifudi.

Kati ya mwezi wa 8 na 9, huanza kusimama kwa msaada wa vitu, na hutembea mwenyewe ifikapo mwezi 10 hadi 15 tangu azaliwe.

Baada ya miezi 18, mengi anayoyafanya mtoto yanahitaji uongozi wa karibu wa mzazi. Mfano ili aweze kujua kushika vitu, kujilisha, kujisaidia kwa usafi, kufungua vifungo vya nguo na kuvaa nguo, ni lazima afundishwe.

Mzazi anahitaji kujua nini afanye ili mtoto aweze kujimudu kulingana na umri wake. Tuchukulie mfano wa kufundisha mtoto kujisaidia haja ndogo kwa muda maalum. Kwa mtoto asiye na matatizo ya kiafya, mzazi anahitaji kumzoeza mtoto kujisaidia kwa muda wa maalum.

Mbinu nyingine ni pamoja na kumpunguzia vimiminika nyakati za kulala pamoja na kutengeneza muda maalum wa kumwamsha kujisaidia nyakati za usiku ili aache mazoea ya kulowanisha kitanda anapokuwa usingizini.

Kumfundisha kujisafisha mwenyewe

Usafi ni eneo muhimu la kujimudu ambalo mzazi anahitaji kulikazia mapema. Kwa mfano, katika umri wa kati ya miezi 10 na 15 mtoto tayari ameota meno na anaweza kushika kitu vizuri kwa mikono yake hivyo unaweza kumfundisha kutumia mswaki.

Usafi ni pamoja na kujitawadha baada ya kujisaidia. Lazima mzazi ujenga ulazima wa mtoto kujisafisha mwenyewe hasa anapofikisha miaka mitatu. Mazoea haya yasipoanza mapema, mtoto anaweza kuwa mtu mzima asiyejua kama ni lazima kujisafisha.  

Vile vile, kati ya miaka minne na mitano, anza kumtaka alazimike kutandika kitanda na kusafisha chumba chake, kuoga, kufua nguo za ndani na soksi. Unaweza kumpa msaada pale unapohitajika lakini ikae akili mwake kuwa hakuna mtu anayewajibika kumfanyia kazi hizo. Kufanya hivi sio kumtesa mtoto, bali ni kumjengea tabia ya uwajibikaji.

Kumshirikisha majukumu ya ndani

Siku hizi wazazi wenye uwezo wanawategemea akina dada wa kazi kufanya kazi zote za ndani. Katika mazingira haya, mtoto anajikuta hajui kufanya chochote isipokuwa, kama ana bahati, kufanya usafi wake binafsi.


Mshirikishe mtoto kufanya kazi za usafi tangu akiwa mdogo

Hata hivyo, kwa kawaida, watoto huwa na shauku ya kushiriki kazi za ndani ikiwa watawekewa mazingira mazuri. Kwa nini basi mzazi usimpe nafasi mwanao kushiriki kuosha vyombo, kufagia, kudeki, kumwagilia maua?

Mpangie ratiba maalum ya kufanya kazi za nyumbani akishirikiana na watu wazima waliopo nyumbani. Kama mazingira yanaruhusu, mtume aende sokoni na dukani akifuatana na watu wazima. Lengo si kuishi maisha ya kimasikini bali kumpa nafasi ya kujifunza majukumu ya kila siku hapo nyumbani.

Kwa kufanya haya yote, tutakuwa tunawasaidia watoto kuwa watu wenye utimamu wa tabia wanaoweza kuishi na watu wengine pasipokuwa mzigo. Usimnyime mtoto fursa ya kujifunza maisha halisi.

Fuatilia jarida la Maarifa ndani ya gazeti la Mwananchi kila Jumanne kwa makala kama hizi.


Maoni

  1. AHSANTE SANA KWA DARASA HAKIKA NIMEAMINI ELIMU SIO KUNYIMANA INGAWA TAYARI NIMEKWISHA YAPITIA HAYO ....

    JibuFuta
  2. Asante sana dada Yasitha! Tuendelee kujadiliana :)

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo ya Kufanya Unapotafuta Kazi

Mbinu za Kumfundisha Mtoto Kusoma Akiwa Nyumbani

Kumsaidia Mtoto Kujifunza na Kumudu Lugha