Machapisho

Inaonyesha machapisho kuanzia Agosti, 2009

Je! Yesu ni Mungu?

Haya ni maoni ya mdau asiyependa jina lake lijulikane. Nimeyatundika hapa kwa sababu ya uzito wa anachokisema. Tafadhali soma na kama unaweza changia maoni yako tuelimike. Nimshukuru sana kwa kutumia muda wake kuandika maoni yake na hapa namnukuu: MAKANISA ya Kikristo yanafunza ya kuwa Yesu Kristo si kama kuwa ni Mwana wa Mungu tu, bali hakika ni Mungu khasa. Baba, Mwana na Roho Mtakatifu ni mmoja. Watatu katika mmoja, na mmoja katika watatu. Wote ni wa milele, wote ni sawa. Yesu ni Mungu, na Mungu ni Yesu. Hiyo ni imani ya Kikristo, ambayo inaaminiwa na karibu Wakristo wote. Hebu tuifunue Biblia tutazame inasema nini katika jambo hili? Mt Paulo katika barua yake ya kwanza kuwapelekea Wakorintho aliandika: Naam, na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi. 1 Wakorintho 15.15 Juu ya kuwa Paulo anaambiwa ya kuwa akiamini kuwa Masihi (yaani Kristo) na Mwenyezi Mungu ni ki

Dini: Matamanio ya kinadharia

Dini hunadi matamanio na taraji za kinadharia, zisizo halisi. Dini zinatangaza hukumu kwa mambo ya kimaumbile (nature) zikilenga kuwafanya watu kuishi maisha ya kimaigizo, yasiyoyao. Kwa mfano, zipo dini zinalazimisha 'makada' wake wenye damu kama sisi kutokuoa, ama kuolewa. Ilani hii ya useja, hata ikiwa nzuri vipi, inabaki kuwa mapendekezo mazuri yasiyotekelezeka. Huwezi kupambana na maumbile na ukanikiwa. Huwezi kuusukuma mwamba na kweli ukasogea ukiona. Kwa hiyo, matokeo yake unakuta wenye dini wanabaki kuzungumza kitu wasichokifanyia kazi. Hadharani wanazuia watu kuoa, gizani wanayatenda yayo hayo wanayoyazuia. Hadharani wana uwezo usioelezeka, sirini ni dhaifu kama wadhaifu wengine. Nini maana yake? Je, ni kweli dini i zaidi ya uhalisi? Je, miujiza inayonadiwa na dini, ni jambo lililo halisi? Je, dini si jumla ya matamanio hafifu yenye mipaka ya kibinadamu?

Dini na maoni ya wadau

Ninazo nyaraka kadhaa zilizotumwa kwangu na wadau wa ule mjadala wa dini. Zinafikia kumi. Wengine hawachelewi. Wamekuja na tuhuma nzima nzima kwa watu, ama vikundi vya watu. Ninatafakari namna muafaka ya kuwasilisha maoni yao bila upendeleo. Hata hivyo, ningependa kuwashauri wadau wa dini, kuzungumza mambo ambayo wana hakika nayo, yenye hoja, ambayo hataibua ugomvi usio na tija katika kutuelimisha. Kwa wale wasioridhika bila kutukana, ujumbe wangu kwao: Dini isipoweza kukusaidia kuitetea kwa lugha rahisi, hiyo haiwezi kuwa pungufu ya ubatili mtupu.

Viziwi wanaosikia tusivyovisikia...

Singida kwema. Nimekuwa na wakati mzuri na marafiki tulioachana kwa kipindi kirefu. Nimekuwa kiguu na njia utadhani kuku mfungwa aliyeachiwa kwa makosa. Jana nilipata fursa ya kutembelea shule ya viziwi na wasioona, Huruma. Nilikutana na walimu waliojitoa kuwasaidia watu hawa kwa moyo. Ilisisimua kuona viziwi wakipiga soga kwa lugha ya ishara. Walikuwa wenye furaha, kiasi kwamba hakuna kilichoonekana kuwapungukia. Nikajifunza. Kumbe furaha ni vile unavyoamua uwe. Huna haja ya kuwa na vyote ili kuipata. Nilimwona kijana asiyeona wala kusikia, lakini mwenye kusema! Ili kuwasiliana nae, unaandika mkononi mwake, anaelewa, halafu anajibu kwa mdomo! Naye huwezi amini kwa jinsi alivyojaa furaha! Nikaonana na wasioona wenye matumaini. Wasioona, wenye kuona tusivyoviona. Wenye furaha bila kutegemea vionekanavyo. Nikaondoka nikiwa na mawazo tele. Upofu na uziwi ni zaidi ya huu wa mwilini!

Shuzi la mwenye nyumba halinuki?

Kwa wale wenye uzoefu huu, tusaidiane kufikiri. Baba akichafua hewa (ashakumu si matusi akijamba) mbele ya wageni na wanae, nani hasa huwajibikia tendo hilo? Yeye, ama wanae? Manake mara nyingi hukosi kusikia mzee akijiwahi: ' Nyie watoto, sipendi kabisa hiyo tabia yenu...nendeni mkacheze nje.' Watoto pamoja na kuujua ukweli kwamba mtumiwa halisi ni baba yao, ambaye anawasingizia wao, huenda nje wakilalamika '...baba sio mimi...mi'shijajamba labda Mangi...!' Je, kuna ulazima wowote wa baba kukiri kuuwajibikia uchafuzi wake huo wa hewa badala ya kuwabebeshea wanawe?

Operesheni ya kilimo cha barabara

Nimerejea tena baada ya kumalizana na Kaizari. Nimepita Moshi kwa ufupi Jumamosi, kisha nikaja Singida, kupitia Arusha. Njiani nilishuhudia 'maendeleo' ya kilimo cha barabara. Barabara ya Minjingu-Babati inaparurwa kwa kasi. Ile ya Babati - Katesh - Singida nayo haiko nyuma, mkandarasi yuko 'saiti.' Nakumbuka tukiwa Magugu, abiria mmoja niliyebahatika kukaa naye, mtu wa makamo akaniambia; 'Kijana hivi unajua kwa nini barabara hii inajengwa kwa kasi hivi?' Nikamjibu; '...mzee sina hakika kama najua' Akafunga gazeti alilokuwa analisoma, akanitazama akisema: '...hii ni operesheni pumbaza kuelekea uchaguzi.' akaendelea; '...Nchi hii haitawaliwi kwa mipango ya muda mrefu. Kila kinachofanywa kina nia ya miaka isiyozidi mitano..' Barabara hii italimwa wee mpaka kampeni zifike, waitumie kama mradi wa kuvunia kura, na usishangae mambo yakiishia hapo hapo...' Niko Singida mpaka mwezi wa tisa.