Kumsaidia Mtoto Kujifunza na Kumudu Lugha

Lugha ni nyenzo muhimu sana tunayoihitaji katika maisha. Hatuwezi kufikiri vizuri, kuongea kwa ufasaha, kusikiliza, kueleza mambo tuliyokutana nayo na hata tunayoyatarajia siku zijazo bila kuhitaji lugha. Ni wazi tunalazimika kutumia maneno au ishara kuwasiliana na wanaotuzunguka.

Mjadala wa namna gani mtoto hujifunza lugha ya mama una historia ndefu. Kwamba mtoto huzaliwa na asili ya lugha inayoongoza namna anavyojifunza lugha au ni mazingira anayokulia ndiyo yanayomwezesha kujifunza, ni vigumu kuhitimisha kwa hakika.

Hata hivyo, kuna ukweli kwamba ili mtoto ajifunze lugha ipasavyo anahitaji kuwa na uwezo fulani anaozaliwa nao unaomwezesha kuelewa kanuni muhimu za lugha bila msaada mkubwa. Lakini pia mazingira, anayokulia mtoto, nayo yana nafasi kubwa ya kumwezesha kujifunza na kumudu lugha ya kwanza kirahisi.


Hatua za mtoto kujifunza lugha

Tangu mtoto anazaliwa hujaribu kuwasiliana na wanaomzunguka. Kulia ni lugha ya kwanza anayoitumia mtoto kuwasiliana na wengine. Hulia kuonesha kutokuridhishwa, wasiwasi, maumivu au hata kutafuta kusikilizwa. Lakini kadri mtoto anavyozidi kukua, mbinu ya kulia kama namna ya kuwasiliana hupungua na mtoto huanza kujifunza kuwasilisha hisia zake kwa kutumia sauti zisizoeleweka.

Mama akimsaidia mtoto kujifunza  PICHA: readingrockets.org
Ni kawaida kwa watoto wa miezi miwili hadi sita kucheza kwa kutoa sauti kama Brrrr-brrrrr! Da-da-da-da! zinazoonesha furaha na sisi wazazi wakati mwingine huziigiza sauti hizo kama namna ya kuonesha furaha yetu tunapokuwa nao.

Mpaka anapofikia umri wa miezi sita, mtoto huanza kujifunza lugha ya mama yake hatua kwa hatua. Kwa mazingira yetu kuna maneno ya awali kama ‘mama’, ‘dada’ ambayo kwa kawaida mtoto huanza kuyatamka kama ishara ya kuanza kuongea.

Kadri anavyoendelea kusikia maneno kwa watu wanaomzunguka, ndiyo anavyoongeza maneno anayoweza kuyatamka siku kwa siku. Katika umri wa miaka mitatu na minne mtoto huiga maneno mengi zaidi hasa yale anayoyasikia yakitamkwa mara kwa mara katika mazingira yake.

Wakati mwingine neno moja kwa mtoto humaanisha zaidi ya jambo moja. Mfano neno ‘mma’ laweza kuwa na maana ya ‘mama’, ‘maji’, ‘njaa’ na kadhalika. Ni kama vile mtoto huonekana kuelewa vitu vingi zaidi ya vile anavyoweza kuvitamka kwa maneno yake.

Katika umri wa miaka mitano na sita mtoto huanza kumudu lugha na huwa mwongeaji. Hupenda kusimulia yale anayokutana nayo na kuuliza maswali mengi. Kadri anavyopata msaada kwa wanaomzunguka, mtoto hujifunza msamiati zaidi. Baada ya miaka sita, mtoto huwa bingwa wa lugha na huweza kuitumia kwa ufasaha katika kufikiri asiyoyaona.

Kumsaidia mtoto kujifunza kuongea

Njia ya kwanza iliyozoeleka ni kuongea na mtoto mchanga kwa lugha ya kitoto. Hii ni lugha yenye kutumia maneno rahisi yanayotamkwa kwa sauti ya juu kuliko kawaida. Lengo la lugha hii ni kumhamasisha mtoto kuvutiwa kuongea. Kadri tunavyojibidiisha kuongea naye kitoto tunampa hamasa ya kujifunza.

Kadhalika, kurudia kutamka kwa usahihi maneno na sentensi anazojaribu kuzitamka mtoto humsaidia kuiga utamkaji bora zaidi wa maneno. Mfano, anaposema, ‘mma’ tunaweza kurudia kwa marekebisho, ‘Unataka maji? Chukua m-to-to!’ Kurudia maneno yake hukuza uwezo wake wa kuongea bila kuchelewa.

Vile vile, kuongezea maana ya kile anachokisema mtoto humsaidia kujifunza matumizi sahihi ya lugha. Kwa mfano, anaposema, ‘baba kuja’, tunaweza kumsaidia kutengeneza sentensi fupi na sahihi zaidi kama, ‘Ndio! Baba anakuja!’ Kufanya hivi humharakishia mtoto kuelewa namna ya kujieleza kwa kutumia sentensi rahisi.

Sambamba na hiyo, tunaweza kumsaidia mtoto kuoanisha majina ya vitu anavyovitumia mara kwa mara na maneno husika. Mfano, anapokuwa ameshika gauni lake tunaweza kumsaidia kutamka neno ‘gauni’ ili aweze kuhusisha neno ‘gauni’ na kile anachokiona. Kwa kufanya hivyo, tunamwekea mazingira ya kuongeza zaidi msamiati wake.

Pamoja na ukweli kwamba si kila anachokifahamu mtoto anakuwa amefundishwa, bado kuna uwezekano mkubwa kuwa mtoto anayeishi kwenye mazingira yanayomtia moyo kujifunza lugha anaweza kumudu lugha kirahisi zaidi.

Inaendelea

Fuatilia safu ya Uwanja wa Wazazi katika gazeti ya Mtanzania kila Alhamisi kwa mada kama hizi.Maoni

 1. PROMO DELIMA
  poker online terpercaya | poker online | Agen Domino | Agen Poker | Kumpulan Poker | bandar poker | Judi Poker | Judi online terpercaya | bandar qiu | situs judi online

  Ayo segera daftarkan diri anda dan bergabunglah bersama kami !!
  Delimapoker.com Situs Agen Poker Online Terpercaya di Indonesia akan melayani Anda dengan profesional, memproses depo/wd dgn cepat. Come join and be a winer with us !!

  Untuk info selanjutnya silakan chat ke :
  Livechat_____: delimapoker
  BBM__________: 7B960959
  Facebook_____: delimapoker
  Phone number_: +85595678845
  pendaftaran___

  JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3