Kumsaidia Mtoto Kujifunza, Kumudu Lugha -2

Makala yaliyopita yalipendekeza njia nne za kumsaidia mtoto mdogo kujua kuongea. Kadhalika, tuliona hatua kuu anazopitia mtoto katika kujifunza lugha. Katika makala haya, tunamtazama mtoto anayejua kuongea na tunaangalia mapendekezo kadhaa ya kumsaidia kuwa mtumiaji mahiri wa lugha katika mawasiliano yake ya kila siku.

Mazingira yahamasishe lugha

Ni muhimu kuweka mazingira yanayompa mtoto nafasi ya kukuza uwezo wake wa lugha. Mazingira hayo ni pamoja na kumruhusu kucheza na wenzake kwa muda maalum. Kucheza ni fursa nzuri ya mtoto kuwasiliana na wengine kuhusu kanuni za michezo husika, kujadiliana pale wanapohitalifiana na kadhalika, na hivyo kukuza uwezo wake wa kujieleza.

Vile vile, kadri hali inavyoruhusu, ni vizuri kumtafutia mtoto CD za katuni (mfano Ubongo Kids), nyimbo na mafundisho mengine na ikibidi kumruhusu mtoto kutazama vipindi vya televisheni vyenye maudhui yanayoweza kumpanua uelewa wake. Vyote hivi, mbali ya kupanua uelewa wa mambo ya kawaida, humsaidia kukuza msamiati wake na hata kujifunza mambo mengi asiyoyasikia katika mazungumzo na watu wengine nyumbani.

Anapoanza kujifunza kusoma, vitabu vyenye picha zinazomvutia kujifunza zaidi vina nafasi kubwa ya kumsaidia kuelewa mambo mbalimbali yanayoendana na umri wake. Hivyo, ni vyema kuhakikisha mazingira ya nyumbani yanampa nafasi mtoto kujifunza lugha.

Ongea nae

Mazungumzo ya kirafiki na mtoto pia yanamhamasisha kujifunza matumizi sahihi ya lugha. Kuongea naye, kunampa nafasi ya kuiga na kujifunza maneno ya kiutu uzima. Maneno haya yanamwongezea mtoto msamiati mpya wenye kubeba mawazo mapana zaidi ambayo kwa hali ya kawaida pengine asingeisikia kwa watoto wa umri wake.

Unapoongea nae, hata hivyo, ni muhimu kuhakikisha lugha inakuwa rahisi, wazi na ya moja kwa moja. Lugha ngumu isiyoeleweka kirahisi haimsaidii kujifunza.
Mawasiliano ya karibu kama haya yanasaidia watoto kujifunza lugha kwa urahisi. Picha: Mitandao

Mwulize maswali yanayofikirisha

Maswali yanayohitaji kufiria kwa kina yanamsaidia kukuza uwezo wake wa lugha. Badala ya kumwuliza maswali yanayohitaji majibu ya ndio na hapana, au yale yenye majibu mafupi, mwuulize maswali yanaitaji maelezo marefu kidogo. Kwa mfano, maswali kama ‘kwa nini unafikiri hivyo?’ yanamfanya afikirie zaidi kile ambacho angeweza kukijibu kirahisi kwa jibu la ndio au hapana.

Kadhalika, maswali yenye kumwuuliza njia aliyoitumia kufanya mambo fulani, maswali yanayomfanya afikirie zaidi ya alichokifanya yanamsaidia kujifunza kutumia maneno anayoyafahamu tayari katika kujieleza vizuri zaidi.

Mpe nafasi ya kukusimulia

Vile vile, kumpa nafasi ya kukusimulia mambo anayokutana nayo kunamsaidia kujenga uwezo wake wa kujieleza. Imethibitika kwamba watoto wanaopata fursa ya kusimuliza mambo yao kwa wengine, wanakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuijua lugha zaidi ya wale wasiopata fursa hiyo. Mtoto anapolazimika kueleza mambo yake kwa maneno yake, hujifunza kuelewa namna ya kuelezea hisia zake kwa kutumia maneno sahihi na kwa wakati sahihi.

Kwa mfano; unaweza kumwomba kusimulia anayoyaona kwenye televisheni, michezo aliyocheza mchana, mambo mazuri aliyojifunza shuleni/kanisani/madrasat, nani alimfanya afurahie siku yake na mambo kama hayo. Kusimulia mambo haya hukuza uwezo wake wa kuelezea mambo.


Kwa ujumla, ukaribu wa mzazi na mtoto ndio msingi mkuu wa mtoto kumudu lugha. Kadri unavyokuwa nae karibu, ndivyo anavyopata usaidizi wa kukuza uwezo wake wa kujieleza na kuwa mtumiaji mahiri wa lugha.

Fuatilia safu ya Uwanja wa Wazazi kwenye gazeti la Mtanzania kila Alhamis kwa makala kama hizi. Barua pepe: bwaya@mwecau.ac.tz 

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia