Dhana ya 'mapenzi' kwa mtazamo wa kisaikolojia

Makala haya yanasaili namna mtazamo wa awali wa watu wanaoamua kuingia katika uhusiano wa kimapenzi unavyoweza kuathiri kwa kiasi kikubwa namna wawili hao watakavyohusiana. Na tunaonesha namna kiwango cha mapenzi kati yao kinatengemea masuala matatu makuu; Ukaribu wa kihisia, tamaa ya mwili na maamuzi yao.
TULIJARIBU kuonyesha tofauti ya mwanaume na mwanamke katika namna wanavyoyatazama mahusiano kihisia.  Kwa ujumla, tuliona kuwa wakati mwanamke anatarajia kujisikia ana usalama wa kihisia kwa kupendwa, mwanaume anatarajia kujisikia yu na usalama wa kimamlaka katika kudhibiti mahusiano. Na kadri kila mmoja anavyoweza kuyaelewa na kuyajibu mahitaji ya mwenzake kwa usahihi, ndivyo mawasiliano kati ya wawili hao yanavyoimarika, na hivyo kuboresha mahusiano yao. 

Katika sehemu zinazofuata tutajaribu kusaili masuala kadhaa yanayochangia kujenga mahusiano yanayowaridhisha wenzi wawili wenye mahitaji tofauti kama tulivyoona na kisha tutatazama namna hali hiyo ya kuridhika inavyoweza kuondoka na kusababisha matatizo.

Lakini kabla hatujafika huko, kwa sababu aghalabu kila anayeingia kwenye mahusiano, hutarajia mapenzi, nimeona ni vyema katika makala haya tuangalie kwa ufupi dhana ya mapenzi kwa mtazamo wa kisaikolojia ili kuelewa sababu zinazoweza kusababisha ama mahusiano yawe bora au kinyume chake.

Nadharia ya mapenzi ya Stenberg

Kwa kutumia nadharia ya Robert Stenberg, mapenzi imara kati ya watu wawili wanaotaka kuwa pamoja kimahusiano, au walio kwenye mahusiano ni lazima yawe na pande tatu muhimu zinazotegemeana ili kuendeleza mahusiano hayo
1) Hisia za mvuto wa kimapenzi ambapo wawili husisimkiana kimwili;
2) ukaribu wa kirafiki ambapo wawili hao hutaka kuwa pamoja muda mwingi na wakati mwingine wakijitenga na wengine; na
3) maamuzi ya kuendeleza uhusiano wao ambapo wawili hao huwekeana ahadi ya kuwa pamoja.

Matatu hayo yakiwepo, kwa mujibu wa Stenberg, basi uwezekano wa uhusiano huo kudumu hali ukiwa imara huongezeka ingawa katika hali ya kawaida matatu hayo yote huweza kupungua hapa na pale kutegemea na mazingira ya kimahusiano, haiba na wakati. Tutarejea hapa baadae.

Kwa kawaida, kinapokosekana kimoja wapo kati ya hivyo vitatu, mahusiano hayo huchukua sura tofauti tatu kama mchoro unavyoonyesha; mahusiano ya muda mfupi (msisimko wa kifilamu), mahusiano ya siri yasiyo wazi, na kisha mahusiano yanayodumu.

Msingi wa mahusiano ni hisia, ukaribu na maamuzi Picha: @bwaya
Maana yake ni kwamba, zikiwepo hisia za kimapenzi na ukaribu wa kirafiki lakini yakakosekana maamuzi ya kuendelea kuwa pamoja, Stenberg anasema uhusiano huo utakuwa wa muda mfupi ambao unaweza kuishia kwenye kukutana kimwili. Uhusiano wa namna hii ni vigumu kudumu.

Lakini katika mazingira yenye hisia za kimapenzi na maamuzi ya kuwa pamoja, lakini bila kujisikia kuwa karibu, Stenberg anasema mahusiano yatakuwa ya siri yasiyo na uhuru unaotarajiwa. Ingawa yanaweza kudumu, lakini kukosekana kwa ukaribu kunaweza kupunguza msisimko wa mahusiano.

Kwa upande mwingine, Stenberg anasema, inapotokea wawili wakawa na urafiki, kwa maana ya kuwa karibu, na kisha wakawa na maamuzi ya kuendeleza urafiki wao, wasipokuwa na hisia za kimapenzi au tamaa, basi, kinachobaki hapo ni maamuzi yasiyo na mapenzi yanayoeleweka. Ilivyo ni kwamba wenzi wanaoanza mahusiano kwa uelekeo huu, wanakuwa na uwezo wa kudumisha uhusiano wao kwa muda mrefu, na kisha kuoana. Lakini katika ndoa, hali hii ya kukosa hisia za humaanisha kuchokana, na huweza kutafsiriwa kuwa hatua ya kuelekea kwenye matatizo ya kimahusiano. Tutaona zaidi mbeleni.

Au ni hatua za mahusiano ya kimapenzi?

Ukifikiri vizuri zaidi pande hizo tatu, yaani, hisia, urafiki na maamuzi, unaweza kuona zinaweza kuelezea hatua kuu za watu kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi. Kwamba, mapenzi huanza kwa mmoja kuvutiwa kimapenzi na mtu mwingine, hali inayosababisha hatua ya kuanza kujenga ukaribu na huyo unayevutiwa naye. Ikiwa hivyo, hatua hizi mbili hujenga mahusiano ya karibu yenye msisimko mkubwa ambao hata hivyo hudumu kwa muda mfupi. Huu ndio msisimko unaofikiriwa na wengi wanapoanza mahusiano.

Msisimko huo huweza kuwapelekea wawili hao kufanya maamuzi ya kuendeleza uhusiano wao. Lakini kadri mahusiano yanavyoendelea kuimarika katika hatua hiyo, ukijumlisha na changamoto za maisha ambazo tutazijadili hapo mbeleni, basi hutokea hisia zikapungua na hata kutokomea kusikojulikana na hivyo wawili hao kubaki kuwa marafiki wa kawaida walio kwenye uhusiano wa kudumu usio na msisimko wa kihisia za kimapenzi.

Vile vile, inaweza kutokea ukaribu wenyewe (intimacy) ukatoweka, na hivyo wawili hao kujikuta katika mazingira ya kuwa wapenzi walioamua kuwa pamoja tena wenye msisimko wa kimapenzi lakini wasio na mahusiano ya karibu. Hali hii, unaweza kuiita mahusiano yanayoegemezwa na ahadi pekee na woga wa kuvunja maamuzi yaliyokwisha fanyika awali.

Ikitokea, na msisimko nao ukatoweka, kinachobaki hapo ni ahadi, au maamuzi, ambayo kwa mazingira hayo huendelea kukosa nguvu na hatimaye, hatua za haraka zisipochukuliwa, huelekea kwenye matatizo ya kutengana na kadhalika. Tutarejea hoja hii huko mbeleni.

Tunachojifunza...

Kwanza, mtazamo wa awali wa watu wanaoamua kuingia katika uhusiano wa kimapenzi unaweza kabisa kuathiri kwa kiasi kikubwa namna wawili hao watakavyohusiana. Na kiwango cha mapenzi kati yao kinatengemea sura hizo tatu za mapenzi.

Kwa mfano, wapenzi wanaoanzisha mahusiano yao kwa msingi wa ukaribu wa kirafiki wenye msisimko wa kimapenzi, bila kuwa na maamuzi ya kuendelea kuwa pamoja, wanakabiliwa na hatari ya kujikuta wanawakiana tamaa za kimwili, ambazo zinaweza zisiwafikishe mbali kimahusiano.

Ni vizuri basi kuhakikisha kwamba mwanaume na mwanamke, wote kwa pamoja, wanao uelewa unaoshahibiana katika suala la matarajio yao ya jumla pale wanapofikiri kuingia kwenye mahusiano na kwamba wanaelewa kwa hakika ni kona ipi wanaitumia kuingilia kwenye mahusiano yao.

Kadhalika, tunajifunza kwamba mahusiano yetu huathiriwa kwa kiasi kikubwa na kuwepo au kupotea kwa kimoja wapo kati ya hivyo vitatu, yaani hisia, ukaribu na uamuzi. Hisia za kimwili pekee yake, hazitoshi kudumisha mahusiano, ingawa zinaweza kusaidia kuanzisha mahusiano. Ukaribu unapoungana na hisia unaweza kuwapeleka watu wawili kwenye hatua ya mahusiano ya kudumu, ingawa hatari yake yaweza kubaki kuwa mahusiano ya juu juu, lakini yenye msisimko mkubwa.

Kupotea kwa kimoja wapo kati ya hisia na ukaribu, ni hatua mbaya kwa watu walio kwenye mahusiano ya kudumu, ambao, kwa kufumba na kufumbua wanaweza kujikuta katika mazingira ya kuparaganyika na hivyo kuongeza takwimu za kuachana tulizoziona hapa.

Katika makala yanayofuata tutaangalia kwa nini msisimko wa awali, kwa maana ya hisia na ukaribu hupungua hatua kwa hatua na kuwafanya wenzi wakijikuta wakibaki na maamuzi yasiyo na nguvu ya kihisia.

Twitter: @bwaya

Maoni

  1. Kaka mi Naitwa Semio Sonyo ni Mtangazaji wa Radio 5,nimejaribu kupitia Makala na Masomo yako kuna kitu naamini naweza kukipata kutoka kwako tafadhali naomba mawasiliano yako.

    JibuFuta
  2. Tuwasiliane mkuu. Naona nikupata notification kwa wakati

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Pay $900? I quit blogging

Fumbo mfumbie mwerevu