Kushinda Vikwazo vya Jitihada za Kumpa Mwenzi Anachostahili

KUYAELEWA mahitaji ya kihisia ya mwanamke ni suala moja, lakini kuuishi uelewa huo ni jambo jingine kabisa. Yapo mambo mengi tunayoyafahamu na tunajua kuyaelewa lakini hatuyaishi. Tujua kwa kina lakini hakuna tunalolitenda. Matokeo yake tunatenda tusiyoyajua na tunayoyajua hayatusaidii kubadili maisha yetu. Katika makala haya, ningependa kusimulia changamoto nilizokumbana nazo katika kupambana na utamaduni niliokulia wa kupuuza mahitaji ya msingi ya mwanamke.

Mwaka mmoja kabla ya kuoa, nilipata bahati ya kupata pre-marital counselling, nasaha za maisha ya ndoa kabla ya kuingia kwenye ndoa. Namshukuru sana mzee Kisinza na mkewe mama Kisinza kwa muda mwingi walioutumia kunipa elimu muhimu ya mahusiano. Kadhalika, niwashukuru wenzi wengine wengi niliobahatika kukutana nao miaka hiyo na kuchota mengi ya kuniandaa kuingia kwenye ndoa. Baade nilioa. Miaka kadhaa imepita sasa.
Nikiwa na mzee Kisinza na mke wake baada ya mazungumzo ya nasaha za maisha ya ndoa. Picha: Sayuni

Ingawa niliingia kwenye ndoa nikifahamu mengi yaliyonipasa kuyafanya  katika mahusiano shauri ya kiu kubwa ya kujifunza, hata hivyo, haikuwa kazi nyepesi kuyaishi niliyoyajua. Nilitamani kufanya nisichoweza. Na wakati mwingine nilifanya nisichokijua.

Malezi ya mfume dume

Nilikuja kutambua baadae kwamba utamaduni niliokulia ulikuwa kikwazo kikubwa cha mabadiliko yangu. Nilikuzwa katika utamaduni usioruhusu mwanaume kuonesha wazi ukaribu wa kirafiki na mwanamke. Si kwamba katika utamaduni wangu watu hawapendani, la hasha. Wanapendana lakini ni kwa namna ya kimya kimya fulani hivi.

Tena katika utamaduni wangu, japo mambo yameanza kubadilika kidogo siku hizi, wenzi wa ndoa hawakupaswa kulala nyumba moja. Mume alilala nyumba yake na watoto wa kiume, na mke naye alilala kwenye nyumba yake na watoto wa kike.

Si hivyo tu, hata kula, ilikuwa ni lazima baba na wanawe wa kiume wale kwanza, kisha kinachobaki kinapelekwa kwa mama na wanawe wa kike. Huu naweza kuuita mfumo dume halisi ambao haukuruhusu mawasiliano ya moja kwa moja kati ya baba na mama.

Na hata usingeweza kuona mume akifuatana na mkewe. Ilipobidi mume na mke kutoka pamoja, mke alitangulia mita kadhaa mbele akifuatwa na mume kwa nyuma. Hakuna ukaribu na wala hakuna ugomvi. Sasa unaweza kuona changamoto ya kubadilika kiutamaduni ilivyokuwa kubwa. Ilinibidi kubadili namna ninavyoyatazama mambo na kufanya tofauti ya kile nilichozoea. Haikuwa kazi nyepesi hata kidogo.

Lakini kwa sababu ya umuhimu wake, ilibidi kufanya bidii kubwa. Nikaanza kujizoeza kubadili mtazamo wangu kuhusiana na ule nilioamini ni wajibu wa mwanaume kwenye mahusiano na kuamua kuchukua hatua za makusudi kuwa karibu kihisia na mke wangu.

Kwa hiyo, nilianza kujifunza kufanya mambo yanayothibitisha upendo wangu kwa mke wangu hata kama nilijua anajua nampenda. Jitihada zangu za kufanya wajibu wangu kama mume zilimfanya mwenzi wangu naye kuitikia ipasavyo. Kadri nilivyoendelea kujitahidi kubadilika, ndivyo kazi ilivyoendelea kuwa nyepesi. Kumbe hata kubadili utamaduni mgumu inawezekana.
Mke wangu, wakati huo akiwa mchumba, siku ya nasaha za maisha ya ndoa. Picha: Sayuni

Mtazamo wa jamii kuhusu ndoa

Kikwazo kingine nilichokumbana nacho ni imani ya jumla ya wanaume wanaonizunguka. Karibu kila hatua niliyochukua ilikuwa kinyume na matarajio ya walionizunguka. Ukaribu nilioutaka na mke wangu ulikuwa kinyume na mazoea ya majirani, wafanyakazi, waumini na wengine wengi niliofahamiana nao. Kumbe sikuwa mwenyewe. Nilitambua kuwa ukaribu na mke si jambo jepesi kukubalika kwenye jamii nyingi. Ni mythos.

Niliamua kupuuza fikra za jumla zinazotukuza ubabe wa kiume katika mahusiano. Kama ambavyo huwezi kuwa mfanyabiashara bila kuhusiana kwa karibu na wafanyabiashara,  nami niliamua kujitenga kimsimamo na wanaume wababe wanaojisifia umbali na wake zao, wanaojisifia nyumba ndogo bila haya, wanaobeza jitihada za mwanaume kumpenda mkewe, wanaodhani ndoa si kipaumbele, na mitizamo mingine inayofanana na hiyo.

Badala yake niliamua kwa makusudi kuwa karibu zaidi na wanaume waliobadili fikra zao wawe mfano wangu. Niliwatafuta wanaume wanaoona fahari kutumia muda mzuri na familia zao. Wanaoamini katika uaminifu wa ndoa. Watu wanaojisikia vibaya kutafuta na kutimiza mahitaji yao ya kihisia kwenye michepuko. Matokeo yake yakawa chanya: mbali na mtazamo wangu kubadilika, lakini nilijikuta nikianza kutenda na kuyaishi niliyoyafahamu, hatua kwa hatua.

Kutokutaka kujifunza, muscularly arrogance 

Pamoja na kujifunza kwa wenzi nilioamini ni mfano bora wa ndoa, naam, hata kwa ndoa zilizokuwa njikani au zilizovunjika, pia nilijisomea yaliyooandikwa kwenye vitabu. Sikumbuki idadi ya vitabu nilivyosoma katika jitihada ya kubadilisha fikra na mtazamo wangu. Wengine walibeza jitihada za kujifunza kwenye maandishi. Kwao, mahusiano bora huja automatic bila kulazimika kujifunza, jambo ambalo si kweli. Hivyo, sikujali. 

Niliamua kwa makusudi kukivunja kiambaza hicho na kuazimia kujenga mahusiano yangu kwa jitihada za makusudi. Iwe kupitia kwa wenye uzoefu chanya na hasi, masimulizi, vitabu na kadhalika, niliamua kuwekeza kwenye maarifa.

Matokeo yake yalikuwa chanya. Wakati urafiki wangu na mke wangu ukiimarika, wale wababe, wasiotaka kujifunza, arrogant, wanaoona haya kusoma vitabu vya mahusiano, sikuwaona wakifurahia mahusiano yao. Ni kweli kwamba wakati mwingine walifanya bidii ya kuficha hali halisi, lakini miparaganyiko katika mahusiano yao haikujificha. Niliwaogopa awali, walibeza jitihada zangu, lakini hatimaye walipata cha kujifunza.

Changamoto ya kulipa gharama

Wakati mwingine nilijikuta katika mazingira magumu ya kazi yaliyonitaka kutanguliza kazi dhidi ya familia. Niliazimia kuchagua kuweka mbele familia yangu. Kwamba kama nilipaswa kuchagua kati ya kazi na ndoa, niliamua kuchagua ndoa, tena kwa furaha. Hili ni jepesi kulisema, lakini si katika hali halisi. Niliamua kulipa gharama ya kuweka mbele familia.

Wakati mwingine nilipaswa kuchagua upande kati ya rafiki au ndugu wa karibu na mke wangu. Nilichagua mke na akatambua hivyo. Maamuzi hayo yaligeuka kuwa salio lililokuza mahusiano yetu hatua kwa hatua.

Insecurity, 'kiburi cha uanaume'

Msingi mkuu niliojifunza katika kumfanya mwanamke ajisikie kupendwa, ni kushughulika na kile kiburi cha uanaume kinachokufanya uone una haki ya kutendewa kuliko kutenda. Kufaidi, kuliko unavyofaidisha. Kiburi kinachokufanya uone huwezi kushuka na kujitoa kwa dhati ili uweze kumfurahisha mwenzako. Ile hali ya kuona ni jukumu la mke kukutii na kukuheshimu wakati hutaki kuwekeza kwenye uhusiano huo.

Nilikuja kugundua kwamba ugumu nilioupata awali ulikuwa shauri ya kiburi changu cha uanaume. Kwamba nilikuwa mtupu wa nafsi kiasi kwamba nilijiaminisha kwamba ni mke wangu ndiye mwenye jukumu la kunitendea mimi, na sio mimi kumtendelea yeye. Kwamba ni yeye ndiye anapaswa kujua mahitaji yangu au aniambie mahitaji yake, lakini si mimi niliyepaswa kujua mahitaji yake. Kwa maneno mengine, utupu ule ulinifanya nione kama kujibidiisha kuwekeza kwenye mahusiano ni kama kushusha hadhi yangu hivi, hivyo nilitegemea yeye ndiye wa kuwekeza kwenye mahusiano na sio mimi.

Niliposhughulika na kiburi changu, ikawa nyepesi kidogo kuwa tayari kufanya jitihada za kuwekeza kwa kumfanya mke wangu ajisikie kupendwa na kuthaminiwa. Nikayaelewa vizuri zaidi mahitaji yake na kujishughulisha kuyajibu.

Kiu ya kuendelea kujifunza

Hata hivyo, sisemi kwamba nina uhusiano uliokamilika kwa asilimia mia. Hapana. We have our rough times too. Tunapishana wakati mwingine. Naichukulia hali hiyo kuwa afya ya mahusiano hasa katika kipindi cha mwanzo wa uhusiano wa karibu kama ndoa. Wakati mwingine ninakuwa stressed na kazi na majukumu mengine, na kwa hivyo tunapishana.

Wakati mwingine naweza kuwa nyumbani akili yangu ikiwaza namna ninavyoweza kumaliza viporo vya kazi zinazonisubiri. Wakati mwingine naweza kujisahau na kuzamia kwenye mitandao nikihudumia wasomaji wa blogu yangu niwapo nyumbani wakati ambao mwenzi wangu angetamani tuzungumze. Ninakosea. Na bado ninakosea. Lakini kuna uwepesi fulani kwenye namna tunavyotazama kupishana kwetu na vile vile namna tunavyotatua changamoto zetu kwa sababu sote tunatambua kwamba ustawi wa familia ni kipaumbele chetu.

Nikisema tumefika, ninadanganya. Ndio kwanza tumeanza, lakini angalau tumeifahamu njia inayoweza kutupelekea huko tunakokutaka. Jambo moja nina hakika nalo nalo ni kwamba kumbe inawezekana kabisa kuishi maisha yenye ukaribu na familia kuliko watu wengine wowote. Kuweka mbele familia kwa gharama ya kuahirisha mambo mengine ya muhimu kunawezekana.


Twitter: @bwaya

Maoni

  1. Be blessed. ..mfumo dume kikwazo kikubwa...i will make it...thnks ma lecture

    JibuFuta
  2. Maisha yangu Maajabu yanashangaza ushuhuda, Jinsi nimepata kisanduku chenye nguvu sana ambacho sasa ni pesa yangu mara mbili kutoka mia hadi elfu ya pesa ndani ya masaa 24, na pia jinsi nimerudisha mpenzi wangu wa zamani, sababu kuu niliwasiliana na Dk Lomi kwa msaada mimi kumrudisha mpenzi wangu wa zamani, basi ananisaidia ni nguvu kubwa ya kumrudisha mpenzi wangu wa zamani, na ananipenda na ananithamini sasa, basi mimi na Dr Lomi tukawa marafiki, baada ya mazungumzo kadhaa namuuliza ikiwa kuna njia anaweza kuniganga ili nipate pesa, hapo ndipo aliponiambia juu ya sanduku hili la uchawi, akaniambia kuna aina na saizi tofauti ya sanduku, aliniambia aina zote za sanduku, ningeweza kumudu ndogo tu ya sanduku, baada ya maombi muhimu anayofanya kwenye sanduku, ananipeleka kupitia huduma ya kujifungua, aliniambia niweke pesa ndani, niliweka ndani ya sanduku 100 euro baada ya masaa 24 nikagundua ilikuwa elfu 10 euro ndani, na nimekuwa nikitumia sanduku kwa miezi 7 sasa, mimi na mchumba wangu tunaishi maisha bora, ikiwa unahitaji b ack mpenzi wako au pesa spell wasiliana na Dr Lomi kwa barua pepe: lomiultimatetemple@gmail.com au WhatsApp namba +2349034287285 unaweza pia kumwandikia kupitia Jina la Mtumiaji la Snapchat: drlomi20 atakusaidia nje, asante kwa kusoma

    Kwaheri Gerd Ulrich

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Pay $900? I quit blogging

Fumbo mfumbie mwerevu