Waajiri wanajifunza nini kupitia Mradi wa ILO unaotambua na kukuza ujuzi usio rasmi?

Shirika la Kazi Duniani hapa nchini, ILO, kwa ushirikiano na wadau wengine wa kazi na ajira hapa nchini wameanzisha mafunzo ya aina yake yanayolenga kutambua na kukuza ujuzi usiorasmi hivyo kuchangia kutatua changamoto hiyo. Kupitia mafunzo maalum yanayoitwa uanagenzi (apprenticeship), ambayo kwa sehemu kubwa hutolewa mahali pa kazi, mwajiriwa mwenye ujuzi usiotambuliwa rasmi anawekewa mazingira rafiki yanayowezesha ujuzi wake kutambuliwa rasmi na inapobidi, kuwezeshwa kupata mafunzo yanayoimarisha ujuzi alionao ili kufanya kazi zenye staha na kwa ufanisi wakati huo huo akiendelea na kazi.
__________________________________________________________________________

TAKWIMU zinaonesha asilimia 64.2 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi hapa nchini, wameajiriwa au kujiajiri katika sekta binafsi. Kadhalika, tunaambiwa, watu wanaojiari au kuajiriwa kwenye sekta kama usafiri, ujenzi, hoteli,  ufundi, biashara ndogo na kadhalika, wameongeza  katika kipindi cha kati ya mwaka 2011 na 2012. Ongezeko hili lina maana kwamba sekta binafsi ni nguzo kubwa ya uchumi wa nchi hii.

Aidha, maeneo yanayoongoza kwa ukuaji wa sekta isiyo rasmi hapa nchini kwa mujibu wa Wizara ya Kazi na Ajira ni Dar es Salaam (asilimia 25.8), Morogoro (asilimia 6), Kilimanjaro (4.4) na Arusha (asilimia 4.2). Takwimu hizi ni kwa mwaka 2012 zilizotolewa na Idara ya Takwimu nchini.

Ujuzi usiorasmi na ujuzi usiokidhi mahitaji ya soko

Kwa sababu ya gharama za mafunzo rasmi, idadi kubwa ya wananchi wanaofanya kazi za kujiingizia kipato katika sekta binafsi na isiyo rasmi, hawapati fursa ya kuhudhuria mafunzo yanayowawezesha kupata ujuzi unaotambulika rasmi katika soko la ajira. Watu hawa wanajifunza na kupata ujuzi kupitia njia zisizo rasmi na kujikuta wakiwa na ujuzi unaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri lakini usiotambuliwa na mamlaka rasmi.

Bahati mbaya ni kwamba zipo kazi nyingi za kuajiriwa au hata za kujiajiri, ambazo watu hawa wenye ujuzi usiotambulika wanakosa sifa ya kuzipata, mfano tenda zinazotolewa na makampuni makubwa na ajira zenye staha. Matokeo yake ni kwamba watu wenye ujuzi mzuri tu usiothibitishwa na cheti, wanajikuta wakijihusisha na kazi zisizo na mazingira bora au zenye kipato kidogo. Kosa lao ni kuwa na ujuzi usiothibitishwa na mamlaka zinazotambuliwa.

Kadhalika, kwa upande mwingine, wapo wengi wanaopata fursa ya kuhudhuria mafunzo rasmi wenye ujuzi usio na tija inayotarajiwa katika soko la ajira ama kwa sababu ujuzi huo hauhitajiki au hawana uwezo wa kuoanisha maarifa ya darasani na hali halisi kwenye soko la ajira. Tunaambiwa, kwa mfano, waajiri wengi wanadai kuwa ufanisi kazini unategemea ujuzi mwepesi kwa zaidi ya asilimia 70, hiyo ikimaanisha kuwa mafunzo rasmi kabla ya kazi hayatoshi kumfanya mhitimu aweze kuajirika kama inavyotarajiwa.

Ndio kusema, ujuzi unaoingizwa katika soko la ajira haukidhi mahitaji halisi ya soko au hautambuliwi na soko lenyewe. Tuliwahi kujadili huko nyuma umuhimu wa waajiri kushirikiana na waajiriwa katika kutatua changamoto hii kwa pamoja.

Mafunzo ya uanagenzi yanavyojaribu kutatua changamoto hii

Shirika la Kazi Duniani, ILO, kwa ushirikiano na wadau wengine wa kazi na ajira hapa nchini wameanzisha mafunzo ya aina yake yanayolenga kutambua na kukuza ujuzi usiorasmi hivyo kuchangia kutatua changamoto hiyo.

Kupitia mafunzo maalum yanayoitwa uanagenzi (apprenticeship), ambayo kwa sehemu kubwa hutolewa mahali pa kazi, mwajiriwa mwenye ujuzi usiotambuliwa rasmi anawekewa mazingira rafiki yanayowezesha ujuzi wake kutambuliwa rasmi na inapobidi, kuwezeshwa kupata mafunzo yanayoimarisha ujuzi alionao ili kufanya kazi zenye staha na kwa ufanisi wakati huo huo akiendelea na kazi. Mafunzo hayo yalizinduliwa na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Septemba 19, 2014, Kunduchi Beach Hotel jijini Dar es Salaam.

Mratibu wa Ukuzaji wa Ujuzi wa ILO nchini, Bw. Albert Willian Okal katika uzinduzi wa mafunzo ya uanagenzi katika hoteli ya Kunduchi Beach, Dar es Salaam. Picha imetumiwa bila ruhusa.
Akizungumzia mafunzo hayo, Mratibu wa Ukuzaji wa Ujuzi wa Shirika la Kazi Duniani, ILO hapa nchini, Bw. Albert William Okal anasema mafunzo haya yanakusudiwa kujenga daraja linalounganisha moja kwa moja mafunzo ya kazi (training) na mazingira halisi ya kazi kwa kuwashirikisha waajiri, waajiriwa na wadau wengine wa kazi, lengo likiwa ni kumwezesha mwanagenzi (mwanafunzi mwajiriwa) kupata mafunzo yatakayowezesha kutambuliwa kwa ujuzi wake.

Bw. Okal anasema mradi huu unamsaidia mwanagenzi kupata ujuzi unaomfanya aajirike zaidi, katika mazingira bora zaidi, kwa maana ya kuwa na ujuzi unaowiana na mahitaji halisi ya soko katika mazingira ya kazi kuliko anapoyapata mafunzo hayo akiwa katika mazingira ya mafunzo pekee,  ambayo mara nyingi hushindwa kujibu kimahsusi mahitaji halisi kazi.

Mafunzo haya yanayoendeshwa kwa ushirikiano na Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA) hufanyika kwa makubaliano kati ya mnufaika (mwanagenzi) na mwajiri wake na hivyo kuhakikisha kwamba ujuzi wa mwanagenzi unakuzwa pasipo kuingilia majukumu yake ya kila siku. Na kwa kuwa mafunzo haya huratibiwa kwa karibu na wasimamizi wenye ujuzi walio kwenye mazingira hayo hayo ya kazi, baada ya kupatiwa mafunzo ya namna ya kufanya hivyo na mamlaka zinazohusika, kizuizi cha muda kwa waajiriwa wanaofanya kazi kwa masaa mengi, kinakuwa kimetatuliwa.

Kadhalika, mtu yeyote anayejitambua kuwa na ujuzi fulani, mathalan ufundi seremala, mwashi na kadhalika bila kujali ameupataje, huweza kutuma maombi ya kutaka ujuzi alionao utambuliwe bila kupata mafunzo, kisha afisa anayeratibu mradi huu kwa kutumia vigezo vilivyowekwa, atahakiki ujuzi huo kwa kutahini ushahidi wa kazi alizowahi kufanya kwa kutumia kumbukumbu ya picha au namna nyingine inayokubalika.

Mtahiniwa huyo akifanya vizuri, huweza kupatiwa cheti rasmi cha kumtambua bila kulazimika kupata mafunzo yoyote almuradi awe amewahi kujifunza ujuzi huo nje ya mfumo rasmi wa mafunzo kwa kipindi kisichozidi miaka mitatu.

Faida za kutambua ujuzi usio rasmi

Kuna faida gani hasa ya kutambua ujuzi uliopatikana kwa njia zisizo rasmi?  Faida kubwa, kwa mujibu wa Bw. Okal, ni kumwezesha fundi mwenye ari ya kujiendeleza kimasomo kutumia cheti atakachokipata kujiunga na mafunzo kwenye vyuo vinavyotambuliwa na serikali. Kwa kufanya hivyo, vijana ambao awali wasingeweza kuomba na kupata kazi zenye staha zaidi kwenye sekta rasmi, wanaweza sasa kuajiriwa katika mazingira bora zaidi ya kazi kama vile makampuni ya kigeni. 

Kadhalika, hata kwa wale wanaopenda kujiajiri wenyewe, mpango huu wa kuwatambua rasmi kwa kuwatunuku vyeti unawawezesha kuwapanua fursa zaidi za kiujasiriamali. Kwa mfano, tenda nyingi za makampuni makubwa hutolewa kwa watu wenye ujuzi unaoeleweka. Kwa hiyo wajasiriamali wasio na vyeti vinavyothibitisha ujuzi wao, hujikuta wakikosa fursa ya kupata tenda hizo. 

Mradi huu pia unawasaidia kuwafanya wajiamini zaidi na hivyo kuheshimika zaidi katika kazi zao.  Kwa namna hii, kila mmoja katika jamii yetu, bila kujali alikoupata ujuzi huo, anakuwa na fursa ya kutambuliwa ujuzi wake. 

Kwa upande wa waajiri, kutambua ujuzi usio rasmi kunawaidia kuongeza tija ya bidhaa au huduma zao kwa sababu ya kutumia watu wenye ujuzi uliothibitishwa na mamlaka zinazotambulika.

Mradi umeanza na fani zipi kwa sasa?

Mradi huu umeanza hatua kwa hatua kwa kuandaa mwongozo/mtaala unaoendana na mazingira halisi ya soko la ajira kuainisha namna ya kutambua vigezo vya kiujuzi katika sekta zilizochanguliwa. Kwa sasa, sekta tano zimeingia kwenye mpango huu 1) Utengenezaji wa vyakula 2) Utoaji wa huduma kwenye migahawa na mahoteli 3) Ufundi seremala 4) Ufundi uashi na 5) Ufundi wa magari. 

Mradi mmoja wapo kati ya hiyo ulizinduliwa Septemba 5, 2014 katika Hoteli ya Holidays Inn na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhe Maimuma Tarishi. Katika mafunzo hayo ya miaka miwili, walengwa wakiwa ni watoa huduma wa mahoteli mwanagenzi wenye umri wa kati ya miaka 17 na 25, hujengewa uwezo na ujuzi wa kufanya kazi vizuri katika mahoteli makubwa ya kitalii na hivyo kuongeza ufanisi wa huduma katika sekta ya utalii.
Uzinduzi wa uanagenzi wa wahudumu wa hotel, Holiday Inn. Picha: bila ruhusa
Asilimia 60 ya mafunzo inatolewa katika mazingira halisi ya kazi na asilimia 40 iliyobaki hutolewa kwa mfumo wa kawaida wa darasani katika Chuo cha Taifa cha Utalii na hatimaye baada ya kufuzu, mwanagenzi atakabidhiwa cheti kinachotambuliwa na Baraza la Ufundi la Taifa (NACTE) na hivyo kuwawezesha kujiendeleza katika vyuo vingine kadri watakavyopenda wenyewe. Tayari Baraza la Ufundi la Taifa limeshatoa idhitabi ya mafunzo hayo.

Mafunzo haya husimamiwa na wajuzi wasimamizi wanaopatiwa mafunzo na kutambuliwa na Chuo cha Taifa cha Utalii, katika namna inayowawezesha kuendelea na majukumu ya ajira zao. Kwa jinsi hiyo, mradi huu unajenga mtandao wa mafunzo unaounganisha mafunzo na ajira. Kwa kuanzia mradi unafanyikia Dar es Salaam na Arusha.

Huu, kwa hakika, ni mfano bora wa namna mafunzo ya darasani yanavyoweza kufungamanishwa kwa karibu na mazingira ya kazi na hivyo kupunguza ama kuondoa kabisa tatizo la kutowianisha kinachofundishwa darasani na kinachohitajika kwenye soko.

Bila shaka, waajiri na wadau wengine wa ajira na kazi wanaweza kupata somo muhimu kupitia mradi huu unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Kazi Duniani kupitia Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Msaada wa Maendeleo (UNDAP), Wizara ya Kazi na Ajira, Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka nyingine za Elimu na Mafunzo hapa nchini. Ni imani yetu kuwa mradi huu utakuwa endelevu.

Twitter: @bwaya

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Pay $900? I quit blogging

Uislamu ulianza lini?