Wajibu wa pamoja wa mwajiriwa na mwajiri katika kuziba pengo la ujuzi unaotakiwa kazini

Katika makala yaliyopita tulisaili kwa uchache kile hasa ambacho waajiri wengi wanahitaji kukiona kwa watu waombao ajira. Kwa kifupi tuliona kwamba pamoja na uwezo wa kutumia nadharia za darasani katika mazingira ya kazi, waajiri wanatafuta kuona ujuzi tuliouita 'rahisi', au kwa kiingereza soft skills. Huu ni ujuzi usiosomewa lakini ndio huwa mithili ya mafuta yalainishayo ngozi iliyofubaa, kwa maana ya kuongeza ufanisi wa ujuzi rasmi wa kazi.

Kama tulivyoona, kutokuoana (mismatch) kwa mahitaji ya mwajiri na sifa za mtafuta kazi ni moja wapo ya changamoto kubwa katika ulimwengu wa sasa wa ajira. Kwamba wapo watu wengi wenye kutafuta ajira kwa kuamini kuwa wanazo sifa za kuajiriwa, lakini waajiri wanaotazamiwa kuwapokea watu hao wakiwatilia shaka kuwa hawana uwezo wa kujaza nafasi walizonazo.

Ni tatizo la elimu au mtazamo?

Wapo wanaoamini kwamba tatizo ni elimu. Kwamba tunawajaza wanafunzi maarifa ya kinadharia ambayo kwa hali halisi hayahitajiki kwenye soko la ajira. Kwamba wanafunzi wanajifunza kwa lengo la kujibu na kufaulu mitihani, pasipokujengewa uwezo wa kukabiliana na changamoto halisi kwenye mazingira ya kazi.

Mhitimu afanyaje kumudu ushindani wa soko la ajira? Picha: @bwaya
Hata hivyo, utafiti unaonesha kwamba bado, katika elimu hiyo hiyo inayolalamikiwa, wapo wanafunzi wanaokuwa na uwezo unaohitajika na waajiri. Tanzania, kwa mfano, inasemekana kuwa na asilimia 39 ya wahitimu wa chuo kikuu wenye ujuzi na weledi unaohitajika kwa waajiri. Hiyo ikiwa na maana kadhaa. Moja kabisa, kwamba wapo wanaotokana na elimu hii hii wanaokubalika katika soko la ajira, maana yake, si mara zote tutalamika kuishutumu elimu kuwa chanzo cha matatizo. Lakini pili, inawezekana kuwa ingawa zipo programu za kitaaluma zinazotolewa vyuoni ambazo kimsingi hazina tija kwenye soko la ajira, bado kuna uwezekano wa kuwa na programu zenye kukidhi matakwa ya soko la ajira.

Swali la msingi ni je, elimu yapaswa kukidhi mahitaji ya soko la ajira, kwa maana ya kuwaandaa wahitimu waliotimia katika maeneo yote ya ujuzi na weledi, au ni kazi ya wahitimu kutumia kinachopatikana madarasani ili kuwafanya walibadili soko la ajira likidhi matakwa ya ujuzi wao kwa njia ya ujasiriamali?  Kipi hasa chapaswa kuwa mbele ya mwenzake, mahitaji ya wahitimu au ni soko ya ajira? Nini nafasi ya elimu katika kukidhi mahitaji mahsusi ya wahitimu na hivyo kukidhi mahitaji ya soko? Je, haiwezekani soko la ajira kubadilika kukidhi mahitaji ya wahitimu wanaofikiri kujiajiri kulingana na ujuzi, maarifa na weledi walionao?

Hata hivyo, bado tunaweza kukubaliana kwamba, pamoja na changamoto zinazoukabili mfumo wa elimu, bado tunalo tatizo la kimtazamo kwa upande wa wahitimu wenyewe kwa maana ya kuweka matumaini yote katika elimu. Kwamba mhitimu anaamini kuwa ni wajibu kamili wa elimu na mwalimu kumlisha kila anachokihitaji kukidhi matakwa ya soko la ajira.

 Vile vile, tunalo tatizo hilo hilo la kimtazamo kwa upande wa mwajiri. Kwamba mwajiri anaamini kuwa mhitimu ataingia kwenye soko la ajira akiwa mkamilifu mwenye ujuzi unaotakikana pasipo kasoro, nalo ni sehemu ya tatizo. Haihalisiki kutaka elimu ikutane moja kwa moja na kila hitaji la soko.

Mwanafunzi afanyeje katika mazingira haya?

Pasipo kuubebesha lawama za moja kwa moja mfumo wa elimu, ni vyema tukitazama namna ambavyo mwanafunzi anayepikwa katika elimu hii hii inayolalamikiwa anavyoweza kujijengea uwezo ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira atakalokutana nalo baada ya masomo. Ndo kusema, badala ya kulaumu dude liitwalo 'mfumo', tuchukue hatua za kukabiliana na changamoto tulizozitaja.

Mosi kabisa, ni muhimu kwa mwanafunzi kujihakikishia kwamba programu anayoisoma inahusiana kwa namna moja au nyingine na vipaji alivyo navyo na malengo yake halisi ya mbeleni na si vinginevyo. Naelewa kuwa yapo mazingira ambayo huweza kutufanya tujikute tukitumia muda wetu mwingi kusoma mambo tusiyoyapenda wala kuyahitaji. Hata hivyo, bado, ni jambo la msingi kujikagua tunapokuwa katika mazingira hayo, ambayo, mara nyingi husababisha tusijifunze kwa kina yale tunayopaswa kujifunza. Programu za kitaaluma zinazokidhi mahitaji ya jumla ya mhitimu ni sehemu ya suluhu ya changamoto.

Aidha, ni wajibu wa moja kwa moja kwa mwanafunzi kujinoa kibinafsi, kwa jitihada zake mwenyewe, kuhakikisha kwamba anakwenda mbele zaidi ya lengo la kufaulu mtihani. Wanafunzi wengi tuna tabia ya kusoma ndani ya matakwa ya programu, kwa lengo ya kukidhi haja ya mitihani. Na si ajabu wengine tunamaliza vyuo, na hatujawahi kusoma vitabu halisi zaidi ya vikaratasi vinavyotolewa na walimu. Na wala hatujishughulishi kuhudhuria maktaba kupanua uelewa wa yale tuyasomayo. Katika mazingira haya, ni vigumu kuwa na uelewa mpana wa kitaaluma, na matokeo yake, tunaweza kujikuta tukikabiliwa na changamoto kubwa katika kuyahalisisha katika mazingira ya kazi.

Kadhalika, ni wajibu kamili wa mwanafunzi kujihusisha kikamilifu na shughuli zilizo nje ya matakwa ya darasa kwa lengo la kuoanisha nadharia na mambo mengine yasiyo ya kitaaluma kwa mfano, kushiriki vilabu vya kitaaluma na shughuli za kujitolea sambamba na masomo. Shughuli hizi ambazo mara nyingi hazina faida ya moja kwa moja kitaaluma wala kiuchumi kwa wakati huo, zinaweza kukusaidia kujijengea uwezo wa maarifa ambayo kwa kawaida hayapatikani moja kwa moja darasani.

Maana yake kila inapowezekana, ni busara kutumia muda wa ziada kufanya kazi zinazohusiana na nadharia unazozisoma. Ni jambo la kushangaza kwamba wanafunzi wengi huwa na muda wa kutosha sana kufanya mambo yasiyo na maana ya moja kwa moja, lakini wakijihurumia linapokuja suala la kubadili matumizi ya muda huo unaoteketea kwa mambo yasiyo na maana.

Kwa mfano, inawezekana kutumia muda wa ziada mathalani likizo, ili kufanya kazi hata ikibidi bila malipo kwa lengo la kujinoa. Faida ya kuyafanya haya, ni kujitengenezea uzoefu ambao hapo baadae unaweza kumshawishi vizuri mwajiri kuwa unaweza kukabiliana na changamoto za kazi.

 Mwajiri anawezaje kuziba pengo hili?

Kwa upande wa mwajiri, mtazamo kwamba mwanafunzi ni lazima awe na ujuzi na weledi unaooana moja kwa moja na majukumu ya kazi, na kwamba ataingia kwenye soko la ajira akiwa ametimia kwa asilimia zinazohitajika, unahitaji kusahihishwa.

Kwanza, ni muhimu kwa waajiri kuwa na programu maalumu zinatengeneza daraja kati ya darasa na kazi. Haiwezekani vyuo vikaweza kukidhi kwa asilimia mia moja mahitaji ya soko la ajira. Na mara nyingine, kwa lugha ya ujasiria mali, ni soko ndilo hubadilika kukidhi matakwa ya wahitimu wanaotokana na mfumo ule ule wa elimu. Hivyo, ndio kusema kwamba kutarajia kwamba mhitimu anakuwa na weledi uliotimia kukidhi matakwa ya mwajiri, ni kuwa too ambitious. Darasa libaki na wajibu wake wa kutoa maarifa ya jumla ambayo, mhitimu naye, anajibidiisha kuyahalisisha kama tulivyoona hapo juu. Mwajiri kwa upande wake, asaidie kuoanisha malengo ya kazi zake na nadharia wakati anapofikiri kuajiri.

Kadhalika, ni muhimu mwajiri kupunguza matarajio yake kwa kudai uzoefu na ujuzi usio halisi kwa mwajiriwa mpya. Ni kweli kwamba uzoefu ni hitaji la msingi katika kujihakikishia kuwa mwajiriwa ataweza kukabiliana na majukumu fulani fulani. Hata hivyo, kuna uwezekano wa kudai uzoefu ulio halisi kwa kazi zisizohitaji ujuzi wa hali ya juu. Mfano kuna haja gani ya kudai uzoefu wa miaka mitatu kwa kazi inayoweza kufanywa na mhitimu yeyote mwenye uelewa mzuri bila uzoefu?

Vile vile, mwajiri atakuwa msaada muhimu kwa mwajiriwa mpya anapobeba wajibu wa kiulezi (mentor) ili kumsaidia kukua na kuboresha kazi hatua kwa hatua. Hakuna kosa, na kweli ni sahihi kuvumilia makosa na udhaifu wa mwajiriwa mgeni. Mfano, ikiwa mwajiriwa mpya hawezi kuandika taarifa ya kazi kama ilivyotarajiwa, si kosa kumjenga mazingira ya kujifunza kwa wazoefu waliopo kazini. Kushindwa, kusichukuliwe kuwa ni udhaifu. Kuchukuliwe kuwa sehemu ya mafunzo ya awali katika mazingira halisi.

Kwa kufanya hivyo, mhitimu anayetarajia kuingia kwenye soko la ajira atakuwa ametimiza wajibu wake wa kujiandaa kutafsiri malengo mapana ya kitaaluma kuwa ufanisi kazini, na wakati huo huo mwajiri naye kwa upande wake atakuwa ametimiza wajibu wake kuweka mazingira saidizi yasijenga ukuta, na hivyo kurahisisha 'mpito' huo anaokabiliana nao mhitimu aliyetoka kwenye nadharia kuja kwenye mazingira halisi na mageni ya kazi.

Mambo mengine ya kimfumo kama elimu, wakati mwingine, hayatatuliki kiwepesi kwa kushutumiana na kuviziana. Kuyasema mara kwa mara, na kuyafanya yaoenekane kuwa ndiyo tatizo kuu la msingi, huwa haisaidii, na kwa hakika huwa ni aina ya kutafuta mbuzi wa kafara kwa mambo tunayoweza kuyashughulikia kirafiki, tena hatua kwa hatua.

Twitter: @bwaya

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Pay $900? I quit blogging

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini