Mahusiano mazuri na watu hujengwa kwa kutambua na kuheshimu hadhi zao na sio kulinda hadhi yako

WATAFITI wa saikolojia ya jamii, wanakubaliana kuwa miongoni mwa sababu nyingi zinazosababisha hali ya mitafaruku katika mahusiano ya watu -iwe kazini, nyumbani, na kokote- ni kule kujisikia kushushiwa heshima. Kwa kawaida, binadamu hatupendi kushushiwa hadhi, ego, ambayo ndiyo hutufanya tupambane na yeyote anayetishia kuharibu namna tunavyojiona na pia tunavyoonwa na wengine.

Tunaambiwa, watu wenye kuamini kuwa hadhi zao haziko salama, insecure, wenye kujihisi kama watu wenye hitilafu fulani, huwa ni wepesi zaidi kuhisi hadhi zao zinachezewa na hivyo kuhitilafiana na watu kirahisi. Hawa ndio watu ambao, unaweza kuwakosea kwa bahati mbaya huhisi kudharauliwa. "Acha dharau dada!" Ndio kusema hawaamini hadhi zao.

Watu secure, wanaoamini kuwa hadhi zao hazitishiwi na wengine, si wepesi kukwaruzana na watu. Sababu ni kwamba hawaoni kirahisi threat ya heshima na hadhi zao, na vile vile wanao uwezo mzuri wa kulinda hadhi na heshima za watu wengine. Migongano ya kimahusiano kwa watu hawa, huwa ni jambo la nadra.

Kwa hiyo tunaweza kusema, kiujumla kuwa, ili kukuza mahusiano yetu na watu, jambo la msingi ni kuhakikisha tunajitahidi kulinda hadhi na heshima zao kwa kuwafanya wajisikie kuheshimiwa, kuthamaniwa na kadhalika. Kinyume na hapo, mahusiano yetu huwa katika hatari ya mitafaruku na misuguano. Na ili kufanikiwa kulinda ego za wengine, ni lazima kuanza kwa kushughulika na insecurities zetu kwanza. Kuhakikisha kwamba sisi wenyewe tuko salama kiasi kwamba, kwanza, hatutishiwi na hadhi za wengine, na hivyo hatulazimiki kupambana na wengine ili kushusha hadhi zao, kwa matarajio ya kupandisha hadhi zetu.

Namna ya kujenga mahusiano mazuri na watu wanaokuzunguka
Kanuni hizi ni matokeo ya tafiti nyingi, na zinazingatia nadharia ya mahusiano kwamba anayeona umuhimu kuhusiana vyema na watu, ndiye mwenye jukumu kuu la kuwajibika kutengeneza mahusiano hayo. Ndiye mwenye kulipa gharama za mahusiano hayo.

1. Onyesha kutambua uwezo wa mtu
Watu hupenda kutambulika. Ni hitaji la ego. Ukitambua na kuonyesha kutambua uwezo wa mtu yeyote, kwa kawaida, hujisikia vizuri kwa sababu ya hadhi yake hupanda na hivyo, uwezekano wa mahusiano kuimarika unaongezeka.

Katika familia kwa mfano, ni muhimu kutambua uwezo wa wanafamilia, waonyeshe kutambua vipaji na vipawa walivyo navyo. Wafanye wajue unaelewa uwezo wao kupitia mazungumzo na yale unayoyafanya kwao. Hata kama uwezo huo hauonekani kwa wepesi, jibidiishe kuutambua kupitia maisha ya kila siku. Kuutambua uwezo wa mwanao au mwenzi wako, na kuonyesha dhahiri kwamba unautambua, huongeza alama za kuwa rafiki yake. Vivyo hivyo, kazini. Kutambua uwezo wa wafanyakazi wenzako, kunajenga mahusiano yako na wao.

Kosa kubwa tunalofanya watu wengi, ni kuwa too insecure kiasi cha kushindwa kuonyesha kutambua uwezo wa watu wanaotuzunguka, kwa hofu ya kushusha hadhi zetu. Matokeo yake tunapuuza, na kufanya majaribio ya kuonyesha kuwa wengine hawawezi. Hakuna mahusiano ya kweli yanayojengwa katika mazingira ya namna hii.

2. Mpende mtu bila matarajio
Upendo una nguvu. Hakuna asiyependa kupendwa. Hata watu wanaojitangaza kutokujali kama wanapendwa ama la, mara nyingi wanachokifanya ni denial tu, lakini moyoni, wanajua wanahitaji kupendwa. Kwa kutambua hilo, kuwa jasiri kuwekeza katika kuwapenda watu kwa dhati. Dhihirisha hilo kupitia mazungumzo yako, mitazamo na matendo yako. Haitakugharimu kitu.

Penda watu kwa kuonyesha kuwa interested nao kwa kukumbuka majina yao, kuwaita kwa majina yao, kutabasamu unapozungumza nao, kuwashukuru wanapokupa huduma au msaada na kadhalika. Upendo wa dhati usiotarajia malipo ya namna yoyote, unconditional love, una nguvu ya kumvuta mtu yeyote.

Upendo huu hauathiriwi na makosa ya anayependwa. Hautolewi kama zawadi ya kufikia matarajio. Ni upendo unatolewa kwa sababu ya upendo. Basi. Kwa mfano, katika familia, mzazi anayejenga mahusiano na mwanae, hasiti kuonyesha upendo hata anapokuwa kakosewa. Haonyeshi hasira zisizokuwa na kiasi, chuki, au nia ya kuadhibu, kama gharama anayopaswa kulipa mtoto kwa kosa alilofanya. Upendo si malipo ya tabia njema, bali hali ya kuwakubali watu jinsi walivyo.

Tunapowapenda watu hata wakati wanapojua hatukupaswa kuwapenda, huwajengea mazingira ya kuhusiana vyema na sisi. Hutuamini.

3. Onyesha kuelewa hisia halisi na mazingira alionayo mtu

Mara nyingine kwa kushindwa kuvaa viatu vya rafiki zetu, tunajikuta katika mazingira ya kulaumu na kuona makosa. Lakini pengine, kama tungekuwa katika mazingira yao, huenda tungefanya yale yale. Mtu secure ni mwepesi kuelewa mazingira ya mwingine na kuhusisha upungufu na mambo yaliyo nje ya uwezo wa mhusika. Tofauti na watu insecure, ambao kwa sababu mara zote hupenda kupandisha ego zao kwa gharama ya wengine, ni wepesi sana kuhusisha udhaifu na tabia halisi za mtu.

Unaelewa hisia za mwenzako? Picha:pattworld.wordpress.com
Faida ya kujenga mazoea ya kuelewa mazingira ya mtu, na kuonyesha kuelewa mazingira hayo, ni kujenga naye mahusiano mazuri. Hata hivyo, hatusemi, mara zote hutaona kosa kwa watu. Hapana. Lakini jifunze kuelewa kwa nini kosa limefanyika.

Chukulia mfano mwanao ameharibu kitu chako cha thamani. Mzazi asiye na uwezo wa kuelewa mazingira ya mwanae, anaona kulaumu na adhabu ndiyo jibu. Lakini hayo yote yatamfanya mtoto ajisikie kulipa gharama ya makosa yake, hali inayoongeza ufa kati ya mzazi na mtoto. Lakini mzazi mwenye uwezo wa kuelewa mazingira ya mwanae, atajitahidi kuelewa kuwa hata yeye, angekuwa katika nafasi ya mwanae, angeweza kukosea vivyo hivyo. Badala ya kulaumu na kumfanya mtoto ajisikie hatia, atachukua hatua chanya cha kukabiliana na kilichotokea, na hivyo kujenga mahusiano mema.

4. Kuwa halisi na mwaminifu, na aminika
Uaminifu ni sifa muhimu katika mahusiano. Watu wanapenda watu wanaoaminika, hata kama wao wenyewe hawaaminiki. Uaminifu hufikiwa pale mtu mwingine anapofikia mahali pa kuamini kuwa unavyoonekana ndivyo ulivyo, na unachokisema na kukifanya unakimaanisha kwa dhati. Ni kule kubashirika na kutabirika tabia yako. Predictability. Mtu anapokuwa na hakika kwamba katika mazingira fulani utakuwa katika hali fulani, atakuamini zaidi.

Mfano,  mtu aweze kujua kwa hakika kwamba ukiahidi kufika mahali saa 3:30 utakuwa mahali hapo wakati huo. Asiwe na mashaka kwamba unaweza kuchelewa kwa makusudi. Kwamba ukipewa kazi, aliyekupa kazi hiyo aweze kutarajia pasipo shaka kwamba kazi hiyo utaikabidhi sawa na mlivyokubaliana. Huo ndio uaminifu unajenga misingi ya mahusiano ya kweli kati ya watu.

Vile vile, mtu mwaminifu huwa halisi na mwenye ujasiri wa kushusha matarajio ya watu kwake, huku akifanya bidii kuyazidi matarajio hayo. Hili ni jepesi kusemwa kuliko kulitekeleza, shauri ya kutojiamini, na hivyo kujikuta tukitafuta kukubalika kirahisi kwa kuahidi zaidi kuliko wanavyoweza kutekeleza. Hasara yake ni kujikuta tukipandisha mno matarajio ya watu kwetu, ili kuwavuta watu kwetu, lakini matokeo yake, tunaishia kuwakatisha tamaa kwa kufanya chini ya kilichotarajiwa. Kwa namna hii mahusiano yanakuwa kwenye matatizo.

Kuwa halisi ni sehemu ya uaminifu. Uhalisi hata usiopendeza unajenga mahusiano ya kuaminika. Kile unachodhani hukiwezi, huonyeshi unakiweza. Unapokasirika, huonyeshi umefurahi. Unapokosewa, huigilizi kwamba hujakosewa. Haya yote hukufanya uaminike. Uwe predictable kiasi cha watu kukuamini, na matokeo yake, mahusiano yako na watu yataimarika.

5. Pongeza na kukweza wengine kuliko unavyokosoa na kujikweza
Usalama wa moyo wako, hudhihirishwa na namna unavyo-react kwa yale yanayofanywa na wenzako. Unapojihisi salama, ni rahisi sana kuona mema ya wenzako, hata wasio rafiki zako, na kuyafurahia. Hutasita kuonyesha wazi wazi kuwa umeyaona mema yao na utapongeza panapostahili pongezi. Bahati njema ni kwamba hakuna mtu asiyependa pongezi. Lazima upate maksi.

Lakini ni ukweli kuwa si rahisi kumpongeza mtu kama wewe mwenyewe unahitaji lililopindukia la kupongezwa. Si kazi nyepesi ikiwa unadhani kwa kumpongeza mwenzako utakuwa unahatarisha hadhi yako. Chukulia mfano mfanyakazi mwenzako amefanya vyema, pengine kuliko wewe. Mnapokuwa katika kikao cha wafanyakazi, unaweza kabisa ushindwe kumpongeza mwenzio aliyefanya vizuri, kwa sababu unahisi kufanya hivyo kutatishia heshima yako. Anakuwa threat na rival (mshindani). Hizi ni dalili za mtu anayeumwa insecurity.

Na kwa kweli, mtu wa namna hii huwa na kazi kubwa ya kukosoa na kujikweza kuliko kupongeza. Atakosoa anaowafahamu na hata anaowaona kwenye televisheni.  Maana kukosoa kunampa kuridhika fulani hivi kwamba hadhi ya wengine ikishuka, basi ya kwake itapanda. Ndio hawa wanaotumia muda mwingi kujisema wao, na kujigamba. Matokeo yake, watu hawa hudharaulika, na inakuwa vigumu kujenga mahusiano mema na wengine.

Ingawa ni kazi ngumu, iizoeze kufurahia kupongeza wenzako.  Jisikie fahari kuwakweza wenzako. Kama huwezi kumfanya mwenzako awe juu yako, basi, mfanye awe sawa na wewe kwa kufanya naye kazi. Team work. Isiwe mimi, mimi, na hadhi yangu. Iwe sisi, sisi, na hadhi yetu.

Kama ni mzazi, pongeza wanao. Kama ni mwanandoa, pongeza mwenzi wako kwa dhati. Epuka kukosoa na kuona mapungufu pekee kuliko mazuri machache yanayoonekana. Kuona mapungufu pekee na kupuuzia mazuri ya wengine ni dalili za ugonjwa wa insecurity. Ni dalili za watu wasiojiamini na kuamini uwezo wao.

Matano hayo, kwa pamoja, yatakuongezea uwezekano wa kujenga mahusiano bora na wanaokuzunguka. Maana, mahusiano na watu huboreshwa kwa gharama ya kuwatanguliza wengine na sio kujitanguliza mwenyewe na hadhi yako, na heshima yako, na mahitaji yako. Lipa gharama ya ego yako kwa kuwafanya wajisikie vizuri kama binadamu, heshima yako itajengwa vyema zaidi, kwa mahusiano yatakayozaliwa kwa kufanya hivyo. Unapowatanguliza wengine, hayo yote unayoyahitaji, iwe hadhi, heshima na mahitaji yako, utayapata bila kuyadai kwa nguvu. Utayapewa bure. Na utafurahi.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?