Nilichojifunza katika maonyesho ya tatu ya wanasayansi chipukizi wiki hii

MAONYESHO ya wanasayansi chipukizi yaliyoandaliwa na Taasisi ya Young Scientists Tanzania yamefikia hatma yake wiki hii. Maonyesho haya ya siku mbili, yaliyofanyika kati ya tarehe 13 na 14 Agosti katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es salaam, yameacha mafunzo makubwa kadhaa.

Kwanza, yameweza kufanya ieleweke vizuri zaidi kwamba wanafunzi wanayo hamasa kubwa ya kufanya sayansi ikiwa watawezeshwa, kinyume kabisa na madai ya mara kwa mara kwamba sayansi haipendwi na wala haifanyiki mashuleni.
Washindi wa kwanza wakikabidhiwa zawadi na Dk Bilal. Picha: @bwaya
Katika muda wa siku mbili hizi, nimeshuhudia namna bongo za wanafunzi wa shule za sekondari, tena nyingi zikiwa zile za kata, zinavyochemka katika kujaribu kutatua changamoto zinazowakabili. Inasisimua kuwaona wanafunzi wakijaribu kutafuta mbinu za kupambana na vyanzo vya magonjwa, uharibifu wa mazingira na kutatua changamoto zinazowakabili watu wetu katika kujiletea maelendeleo kwa ujumla. Hilo limekuwa wazi kupitia maonyesho haya.



Pili, maonyesho haya yamethibitisha kuwa sayansi ni maisha na wala haihitaji vifaa vya gharama kubwa kuihimiza mashuleni. Katika maonyesho haya, wanafunzi wameonyesha namna walivyoweza kutumia vifaa vya kawaida kabisa, vinavyopatikana katika mazingira yetu, ili kuweza kuchunguza changamoto wanazoziona katika jamii na mazingira yao.

Ni kweli kwamba shule zetu zinakabiliwa na matatizo mengi yanayokwamisha ufundishaji kwa ujumla. Kuna ukosefu wa walimu wenye uwezo, vifaa vya maabara na kadhalika. Wimbo huo tumeuzoea. Lakini Young Scientists Tanzania imejaribu kuonyesha kwamba inawezekana kabisa kutumia vichache vilivyopo kupata majibu yanayotarajiwa.

Kwa mfano, katika mazingira ambapo vifaa fulani vinahitajika sana na havipo, Young Scientists Tanzania imekuwa ikiwashauri wanafunzi kutafuta msaada wa kimaabara katika taasisi za kiutafiti zilizo karibu nao. Hiyo si tu kujenga daraja kati ya watafiti waliobobea na wanafunzi, lakini pia huwasaidia wanafunzi kuona mazingira halisi ya kiutafiti hali inayotarajiwa kukuza hamasa.
Mfano mmoja wapo wa miradi iliyokuwa ikionyeshwa wiki hii. Picha: @bwaya

Itakumbukwa kwamba walimu wengi wa sayansi wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa vifaa kama kikwazo kikubwa cha kujenga utamaduni wa sayansi mashuleni. Lakini, maonyesho haya yamethibitisha kwamba penye nia ya dhati ya kukuza sayansi, vifaa haviwezi kuwa tatizo kubwa kiasi hicho. Huhitaji maabara ya viwango vya juu kuweza kufanya majaribio ya kisayansi. Kwa hiyo, kumbe basi inawezekana kabisa, walimu kuhalisisha sayansi kwa kutumia mazingira yao.

Jambo la tatu, tumeona namna wanafunzi wanavyoweza kuja na ugunduzi mpya kwa lengo la kurahisisha maisha ya kila siku na hata kupunguza umasikini kwa kutumia nadharia za kisayansi. Ungetarajia kwamba shughuli hii ingefanywa na wanasayansi wakubwa na maarufu. Lakini kupitia mradi wa maonyesho haya unaoratibiwa na Young Scientists Tanzania, tunafahamu sasa kwamba kuchunguza nadharia, kugundua teknolojia mpya na kuendeleza elimu kisayansi kwa njia ya utafiti na uvumbuzi kunawezakana kabisa tena kwa ngazi ya sekondari. 

Kwa mfano, mwaka huu, wapo wanafunzi kadhaa waliobuni teknolojia kadhaa kama vile, mfumo wa kupiga kura kwa njia ya kuandika ujumbe mfupi wa maneno (SMS), kuarifiwa dharura inayotokea nyumbani kwa kutumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS) na kadhalika. Kwa jinsi hii tunaona namna wanafunzi wanavyoweza kutumia nadharia na ubunifu kutafuta majibu ya matatizo yetu ya kila siku.

Mhe Zitto Kabwe akiwasikiliza wanasayansi. Picha: @Zitto
Vile vile, mwamko wa washikadau wa sayansi katika kuhakikisha kuwa fikra, tabia na utamaduni wa sayansi unaanza kujengwa mapema, umeonekana bayana. Mbali na mkono wa serikali ambao tunauhitaji sana katika kujenga mazingira, makampuni na mashirika makubwa kama BG Tanzania yameona umuhimu wa kuwekeza wajibu wao wa kijamii kwenye sayansi. Na dalili zinaonyesha kwamba uwekezaji huo ni endelevu. Si upepo wa kupita. Hili ni jambo jema la kuigwa na makampuni mengine yanayotaka kurudisha faida kwa jamii.

Ushiriki wa wanasiasa katika mambo haya, unaweza kuwa hamasa kwa vijana kuona umuhimu wa sayansi. Mwaka jana, akiwa mgeni rasmi katika sherehe za utoaji wa zawadi, Mhe Januari Makamba, Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasialino aliwahakikishia wanafunzi kwamba serikali imeanza utaratibu wa kuheshimu tafiti za kisayansi na kufanya maamuzi kwa mujibu wa matokeo ya tafiti. Kauli hiyo ilijenga hamasa kubwa.

Mwaka huu, mbunge maarufu aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Mhe Zitto Ruyagwa Kabwe, alipata nafasi ya kutembelea maonyesho hayo na kuwasikiliza watafiti hawa chipukizi. Ujio wake, kama mwanasiasa maarufu, ulikuwa kivutio kikubwa kwa vijana.

Washindi wa pili, wakipewa zawadi na Balozi wa Ireland nchini. Picha: @bwaya
Hatimaye, alasiri hiyo hiyo, Makamu wa Rais, Mhe Dk Mohamed Gharib Bilal, akiwa mgeni rasmi wa sherehe za kutoa zawadi, akifuatana na Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, Mhe Profesa Makame Mbarawa, aliwahakikishia vijana walioshiriki maonesho hayo kwamba serikali itandelea kuwa bega kwa bega na Young Scientists Tanzania, ili kuhakikisha kwamba mradi huu muhimu unakuwa endelevu.

Andiko la kiutafiti lililoshika nafasi ya kwanza mwaka huu liliandikwa na Dhariha Amour Ali na Salma Khalfan Omar kutoka Skuli ya Lumumba 'nchini' Zanzibar na lilionyesha namna ya kupambana na mbu na wadudu wengine kwa kutumia mazingira ya kawaida ya ki-Zanzibar  na mbinu nyepesi za kisayansi. Pamoja na zawadi nyingine, washindi hao watahudhuria maonyesho kama haya nchini Ireland, yaitwayo BT Young Scientist & Technology Exhibition mwezi Januari 2015.

Washindi wa pili, walikuwa Upendo Mwanuo na Josephine Chomya kutoka Shule ya Sekondari St. Christina, na andiko lao lilihusu matumizi ya mtindo wa ulaji wa Wamasai katika kudhibiti magonjwa.

Twitter: @bwaya

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?