Namna ya kukopeshwa kirahisi na kuchangiwa michango ya harusi na marafiki

WALA usishangae hata kidogo. Umesoma vyema kabisa kichwa cha habari. Tunataka kujifunza namna bora kabisa za kuwapiga watu mizinga. Kukopa na kuchangiwa michango ya harusi. Vyote hivi vinafanana kimsingi kwa sababu vyote vinategemea hisani ya watu wanaoitwa ndugu, jamaa na marafiki.

Kwako usiyekopa, nikuambie mapema kabisa, hapa si mahali pako. Makala haya ni mahususi kwetu sisi wakopaji maarufu ambao (ni kama vile) haiwezekani kabisa kumalizia mwezi bila kuongezea na za watu. Sasa ili nieleweke nawalenga watu gani, niseme awali kabisa kwamba hatuzungumzii mikopo ya taasisi za fedha kwa ajili ya maendeleo. Nazungumzia mikopo kutoka kwa watu kwa ajili ya kusukuma siku, au misaada ya kufanikisha harusi.

Wazo la kuandika mikakati hii madhubuti ya kukopa, nimelipata jana baada ya kusoma taarifa ya google kuhusu kile hasa kilichotafutwa na watumiaji wa mtandao (netzens) kupitia kwenye google, kilichowaongoza na kujikuta wakiwa kwenye blogu yangu. Hapa nanukuu sentensi mbili nilizoziona:
             "Namna ya kumkopa rafiki"
             "Nawezaje kukopeshwa?" Sasa nikasikitika sana kwamba kwa vyovyote hawakupata walichokitarajia. 
Vile vile, pamekuwa na wasomaji wanaotafuta suluhu ya stress, "Kupunguza msongo wa mawazo". Nao, kama wale wanaotafuta namna bora za kukopa, sidhani kama wamekuwa wakipata mchango wa mawazo kupitia blogu hii.
Naelewa kabisa kuwa moja wapo ya sababu za msongo wa mawazo, ni pale unapojikuta una siku tano mbele kufikia tarehe ya mshahara, na akaunti yako benki ina Tsh. 1023.78. Usiombe kuwa katika mazingira hayo. Na wanaodhani tunatania, watuache zetu sisi tujadili namna ya kutatua stress zetu.

Sababu za kuishiwa na kulazimika kukopa

Si kila anayekopa ni mzembe. Asilimia kubwa ya wananchi wa Tanzania wanaishi kwa kipato kisichozidi 250,000 kwa mwezi, kwa siku thelathini. Utaelewa kwamba inahitajika akili ya ziada kumaliza mwezi, ikiwa ni pamoja na kukopa hapa na pale ili siku ziende. Kwa hiyo, sisi wa kundi hili huwa tunakopaji hela ndogo ndogo.

Vile vile, kuna ukweli kuwa kukopa kwaweza kabisa kuwa matokeo ya tabia ya matumizi. Uchunguzi wa kina unaonyesha kwamba wakopaji wengi hukopa kwa watu wanaopata kipato kinacholingana na chao au hata wenye kipato cha chini zaidi. Maana yake, kuna masuala ya mtindo wa maisha fulani wa maisha unaosababisha kipato siku zote kiwe chini ya matumizi. Hii nayo sio dhambi, ila inahusika sana stress za mara kwa mara. Wa kundi huwa tunakopa kiasi kinachoendana na mapato tarajiwa.

Lakini pia kuna tunaokopa mtaji, kwa matarajio ya kupanua au kuanzisha biashara. Si mara zote unapotaka kufanya kitu, waweza kuwa na fedha zinazokutosha. Na huenda benki nako hukopesheki. Si unajua benki hukopesha wenye fedha sio akina sisi? Basi vyovyote iwavyo, kuna tunaotarajia msaada wa mifuko ya watu kuliko taasisi rasmi za fedha. Mtuelewe.

Kanuni za kukopeshwa au kusaidiwa kirahisi

1. Jenga mahusiano/urafiki wa karibu na wakopeshaji wako watajiwa
Utakuwa mtu wa ajabu, na kweli wakopaji wenzako tutakushangaa kama unaanzisha mahusiano ya ghafla na mtu ili umkope siku hiyo hiyo. Ukishajijua wewe ni wa kukopa, mwezi hadi mwezi au unatarajia kutuma maombi ya kuchangiwa harusi, usikae mbali na watu. Ule mtindo wa kukaa na namba za watu uliosoma nao miaka mitano kumi iliyopita, bila kuwasiliana nao na kisha unakuja kuzifanyia matumizi wakati tu unapokuwa na shida, haufai.  Ustaarabu ni kuwa na mahusiano consistent na wakopeshaji wako watarajiwa.
Hali kadhalika, unapohusiana na watu, jitahidi kuwafagilia fagilia, wapambe kwa sifa hata kama hawanazo. Hii tunaiita ingratiation, na itakuongezea kukubalika na hivyo kuongeza urafiki wenu, raslimali muhimu kwa ajili ya malengo yako ya kukopa. Hi hi hi!

2.Jenga uaminifu kwa kuomba hela ndogo ndogo kwanza
Hakuna mtu anayependa kukopesha watu wasio waaminifu. Anzia hapo hapo rafiki yangu. Kama unajua utakuja kumkopa mtu 30,000 basi anzia na 5,000. Ukishakopa, ilipe. Hii inaitwa foot-in-the-door strategy. Ukiilipa kwa wakati, jamaa atakuamini. Ukija na mzinga wa 20,000 wala haitakuwa ngumu sana labda kama hana. Sasa tutakushangaa sana wenzako kama hata hiyo 5,000 uliyoanza nayo kama gia, utaingia nayo mitini. Litakuwa jambo la kusikitisha sana.

Kwa wewe wa harusi, cha kufanya ni kuanza kuwekeza kwa kuchangia wengine. Unawatia kwenye madeni bila wao kujua. Sasa usisahau kabisa kuwa na daftari la kuorodhesha wale uliowachangia na kiasi. Siku ukiibuka na meseji zako ya 'naomba mchango wa harusi', mtu wala hajiulizi. Dhamira inamshitaki.

3. Jenga mazingira kwa kuomba kisichowezekana
Hii ni kinyume cha mbinu namba tatu na inajulikana kisaikolojia kama door-in-the-face na inafaa kwa wote, wakopaji na waomba michango ya harusi. Kinachofanyika hapa, unamwomba mtu msaada ambao una uhakika hatakuwa nao. Kama ni hela, hakikisha hana. Kwa mfano, unamwomba mtu akusaidie milioni 1 na unajua kabisa hanayo. Lengo hapo ni kumtengenezea hali tunayoiita cognitive dissonance, ajisikie vibaya kwamba kashindwa kukusaidia. Hii inatokana na ukweli kwamba kwa kawaida, watu wanapenda kusaidia kama wana uwezo huo, kwa sababu kufanya hivyo kunawapandishia hadhi. Sasa inapotokea wameshindwa kukusaidia, kwa kweli wanajisikia vibaya.

Sasa hapo ndiko iliko siri yenyewe. Kule kujisikia vibaya ndio kutamfanya ahakikishe anaondoa hali yake hiyo ya kujisikia vibaya kwa kukusaida siku nyingine ukimfuata na hitaji dogo kama Tsh 30,000 unazozihitaji kumalizia mwezi. Umeelewa? Kukopa ni akili ujue! Nyongeza hapo, kumbuka kuonyesha uharaka. Hii tunaiita kwa kimombo, 'fast-approaching-deadline-technique'. Pressure fulani hivi, yenye lengo la kumweka mkopeshaji kwenye angle. 

4. Acha sifa, sema ukweli umepigika na unahitaji kuokolewa
Unajua kuna hii tabia ya mtu kuona haya ataonekanaje akisema kaishiwa. Acha hadithi za kujibaraguza, "Kuna cheque ya milioni tano naifuata Kigamboni....hebu nipe hapo 20,000 nikaichukue, ntakutoa nikirudi". Wenye akili wanakudharau hata wasipokwambia.

Mwingine utamsikia, "Naandaa program ya kufadhili mama ntilie, gharama zake ni kama milioni 10...na nimeshalipa...hapa kuna matangazo ya redio natakiwa kuyafanya kabla ya kesho...hebu nipe 50,000 hapo ntakurudishia program ikiisha." Kaka, hizo ni stress unajiongezea. Kuwa mkweli kwamba umepigika. Wakopaji wa kweli huwa hawapiganii ego/hadhi zao wakiwa katika hali kama yako. Nenda straight to the point kwamba, "Hali yangu si nzuri, naomba 20,000 nasubiri mshahara Ijumaa." Au kama that's too much, na utadhalilika basi, sema, "Tafadhali niazime 20,000 nitakurudishia Ijumaa."

Au kwako unayetaka michango ya watu, angalia sana maneno yako. Usiwe mtu wa kujigamba gamba bila sababu hali ukijua kuna siku hao hao unaojitutumua kwao leo, ndio utawafuata wakusaidie. Na unapoomba mchango, usionyeshe kuwa huhitaji sana mchango, wakati mambo hakiwa shingoni, huishi kutuma mfululizo wa meseji za kukumbushia. Sahamani najua hii inauma.

5. Ukikopeshwa, lipa deni na mshukuru mkopeshaji wako
Katika sababu za watu kusaidia, au hata kukopesha wengine, ni reward wanayopata kujisikia kuwa wamesaidia. Ile kujihisi wamekutoa kwenye matatizo yako, inawapa furaha. Inapandisha ego yao, of course ya kwako inadidimia. Sasa kuwa makini na hili. Mshukuru kwa dhati aliyekusaidia, ukiweza mwandikie na ki-note kabisa kuonyesha unavyo-acknowledge msaada wake. Atajisikia vizuri. Siku nyingine ukiwa na majanga yako ya kuishiwa, haitakuwa kazi kukusaidia. Unakuwa umemtengenezea ile cognitive dissonance tuliyoizungumza hapo juu, kwamba atajisikia vibaya kuharibu "picha ya kusaidia" aliyokujengea, kwa kukukatalia. Kama anayo, basi atajikuta akilazimika kukusaidia ili kuiendeleza picha hiyo aliyoijenga mwanzo ya 'rafiki asaidiaye'.

Kwa wewe unayekaribia kuanza kutuma meseji za mchango, kanuni ni ile ile. Epuka kuwekea watu viwango vya msaada wa kukupa. Tambua wanakupa mchango kwa hisani si kwa lazima. Mambo gani sasa ya kuomba mchango na unalazimisha upewe kiasi unachotaka wewe? Acha watu wakupe walichonacho, na ushukuru kwa hicho. Ukishukuru kwa kidogo, watakupa vingine usivyoomba. Vinginevyo, unajitafutia stress za bure halafu baadae uanze ku-google namna ya kusaidiwa.

6. Seriously, hivi kweli unahitaji kukopa kila mwezi? Ni kweli ni lazima uoe kwa harusi isiyolingana na uwezo wako?
Hayo yote niliyoyaandika kwenye hatua nne hapo juu, yalilenga kukuvuta ufike hapa. Nashukuru nimefanikiwa. Sasa nikuulize: Hivi kweli, ndugu mkopaji mwenzangu, ni lazima kuendeleza duara la mkopo kila mwezi? Kwamba unakopa, mshahara ukija, unalipa madeni, unakopa, unalipa, unakopa? Halafu cha ajabu huenda hata kipato unachokipata ni kikubwa!
Huu, huenda ukawa ni ukweli wa kukusaidia. Utafakari
Nakwambia, wakati mwingine unadhani huna fedha, lakini wapo watu wakilipwa hizo 500,000 unazoziona wewe hazikutoshi, huo kwao utakuwa ni muujiza na ndio watakuwa wameaga umasikini rasmi. This is serious. Ni kwamba huenda tatizo lako ni vipaumbele tu ila fedha unazo. Huna bajeti. Unatumia tu, mwishowe unakuta hazipo. Si ajabu huishiwi msongo wa mawazo. Tafadhali onana na washauri wa masuala ya fedha haraka sana.

Kupanga kuolewa kwa mbwembwe wakati uwezo wako unaujua, ni kujitafutia stress. Punguza matarajio kwa watu wanaokuzunguka. Wahurumie. Wana majukumu mengine mengi yasiyolingana na vipato vyao. Sasa isije ikawa unapunguza stress zako kwa kuzihamishia kwao. Usiwaongezee msongo wa mawazo kwa 'kuwadai' michango mikubwa isiyolingana na mahusiano yenu.Ngumu kabisa hii. Pole.

Kwa nini tabia ya kusaidiana imeanza kutoweka?

Nimalize kwa kuuliza, nini hasa kinachofanya tabia ya kusaidiana iwe adimu siku hizi? Kwa nini watu hawasaidiani kama ilivyokuwa zamani? Tumefika mahali, watu wanajadili namna ya kukataa kumsaidia rafiki yako! Utamaduni umebadilika. Ndio, kuna uzembe wakati mwingine. Ndio, kuna kutapeliwa. Ndio, kuna utegemezi. Lakini je, hiyo inamaanisha usimsaidie mwenye shida?
Kumbuka, shida ya mwenzako leo, kesho ya kwako. Ulioa kwa kusaidiwa, kwa nini hutaki kuwasaidia na wengine? Kweli unawaita wakopaji, 'mizigo?' Mbona wewe uliwahi kukopeshwa?

Tunu ya utamaduni wa Kiafrika ni kuishi kama ndugu. Ujamaa. Kushirikiana. Kusaidiana. Ni tunu, ni value. Tusiache kusaidiana, tusaidiane kupunguza stress za maisha magumu. Haipendezi wewe unajifunza namna ya kukataa maombi ya mkopo ya rafiki, wakati huo huo, rafiki yako ana-google mtandaoni kujua namna ya kukukopa! Vinginevyo, basi, siku hizi tunaishi na watu tunaofahamiana, na si marafiki. Ya leo kweli ngumu. Nilikuwa natania tu ndugu msomaji.

Maoni

  1. Mimi nina sherehe yangu ya unyago nimeamzisha group watu wanichangie nifanye ili nipate michango kilahisi?

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Mbinu za Kujenga Ujuzi wa Mwanafunzi