Jumanne, Septemba 27, 2016

Jenga Fikra Chanya, Uwe na Furaha

Kuwa na furaha ni uamuzi wako mwenyewe. Furaha ni matokeo ya namna ulivyoamua kufikiri. Kadhalika, kukata tamaa na kukosa amani mara nyingi ni matokeo ya kufikiri mambo yanayokatisha tamaa na wakati mwingine tusiyo na majibu yake. Tunatafsiri vibaya mambo tunayokutana nayo na ndiyo sababu tunapatwa na msongo wa mawazo.

Jumatatu, Septemba 26, 2016

Kumfundisha Mtoto Kuwajibika, Kufanya Kazi

Kumjengea mtoto uwezo wa kuwajibika ni wajibu muhimu sana wa wazazi. Bila kuweka mkazo mapema katika kukuza uwezo huu, mtoto anaweza kuwa mtu mzima asiyefahamu kufanya majukumu mengi ya msingi na ya kawaida. Mtoto aliyefundishwa kuwajibika hujiona ana wajibu wa kushiriki shughuli za ndani bila kujali jinsia yake. 

Katika makala haya, tunaangalia namna unavyoweza kumsaidia mtoto wako kujifunza kuwajibika angali mdogo na hivyo kujenga uwezo wa kumudu majukumu ya msingi kadri anavyoendelea kukua.

Jumamosi, Septemba 24, 2016

Kujenga Uwezo wa Kufanya Maamuzi kwa Mtoto

Unajisikiaje mzazi unapogundua mtoto ameanza kujifunza tabia zisizofaa? Inaumiza, kwa mfano, kuona mtoto anaanza kujifunza wizi, kudanganya na hata kutokuwa na uwezo wa kujisimamia mwenyewe bila uangalizi wa karibu.   

Ijumaa, Septemba 23, 2016

Kumsaidia Mtoto Kujifunza, Kumudu Lugha -2

Makala yaliyopita yalipendekeza njia nne za kumsaidia mtoto mdogo kujua kuongea. Kadhalika, tuliona hatua kuu anazopitia mtoto katika kujifunza lugha. Katika makala haya, tunamtazama mtoto anayejua kuongea na tunaangalia mapendekezo kadhaa ya kumsaidia kuwa mtumiaji mahiri wa lugha katika mawasiliano yake ya kila siku.

Alhamisi, Septemba 22, 2016

Tunavyoweza Kuacha Tabia ya Kuhukumu Wengine

Majuzi nikiwa kwenye mgahawa mmoja mjini, waliingia watu wawili wanaume waliokuwa wamevalia mavazi yanayoashiria imani yao ya kidini. Wote wawili walipamba vichwa vyao kwa vilemba nadhifu, mmoja wao akibeba mfuko mdogo mweusi. Nyuso zao, kwa hakika zilipambwa na tabasamu pana la kirafiki lililofanya ndevu zao ndefu ziwe na mwonekano wa kupendeza. Miguu yao ilivaa viatu vya wazi na juu yake zilining’inia suruali fupi mithili ya kaptula ndefu zilizojitokeza ndani ya kanzu fupi nadhifu.

Jumanne, Septemba 13, 2016

Kwa Nini Tunapenda Kusikia Habari Mbaya?

Umewahi kujiuliza kwa nini habari tunazofuatilia kwenye vyombo vya habari mara nyingi ni matukio mabaya? Kwamba ili iwe habari yenye kuvutia watu wengi mara nyingi hulazimu iwe habari ya jambo lisilotarajiwa. Kwa mfano, habari za mbunge kulala wakati kikao cha bunge kikiendelea inaweza kuwa na mvuto kuliko habari ya namna mbunge huyo huyo alivyotekeleza wajibu wake kabla ya ‘kupitiwa na usingizi.’


Jumatano, Septemba 07, 2016

Kumsaidia Mtoto Kujifunza na Kumudu Lugha

Lugha ni nyenzo muhimu sana tunayoihitaji katika maisha. Hatuwezi kufikiri vizuri, kuongea kwa ufasaha, kusikiliza, kueleza mambo tuliyokutana nayo na hata tunayoyatarajia siku zijazo bila kuhitaji lugha. Ni wazi tunalazimika kutumia maneno au ishara kuwasiliana na wanaotuzunguka.

Mjadala wa namna gani mtoto hujifunza lugha ya mama una historia ndefu. Kwamba mtoto huzaliwa na asili ya lugha inayoongoza namna anavyojifunza lugha au ni mazingira anayokulia ndiyo yanayomwezesha kujifunza, ni vigumu kuhitimisha kwa hakika.

Hata hivyo, kuna ukweli kwamba ili mtoto ajifunze lugha ipasavyo anahitaji kuwa na uwezo fulani anaozaliwa nao unaomwezesha kuelewa kanuni muhimu za lugha bila msaada mkubwa. Lakini pia mazingira, anayokulia mtoto, nayo yana nafasi kubwa ya kumwezesha kujifunza na kumudu lugha ya kwanza kirahisi.

Jumanne, Agosti 30, 2016

Kuanzisha na Kuimarisha Urafiki wa Karibu

Katika zama hizi za maendeleo ya kidijitali, ni rahisi sana kufahamiana na watu wengi ambao, hata hivyo, wanaweza wasiwe marafiki. Unaweza, kwa mfano, kuwa na ‘marafiki’ elfu tano kwenye mitandao ya kijamii, lakini usiwe na rafiki hata mmoja katika maisha halisi.

Marafiki wa kweli na wa karibu ni moja wapo ya mahitaji muhimu katika maisha. Tunaweza kuwa na sababu nyingi kuhalalisha kwa nini hatuna (haja na) marafiki wa karibu.  Hata hivyo, zipo nyakati  hufika tukajikuta katika maisha yenye kujaa upweke  na msongo wa mawazo kwa sababu hatukutumia muda wetu kutengeneza urafiki wa karibu na watu tunaofahamiana nao.

Jumatatu, Agosti 29, 2016

Kujenga Tabia ya Kusoma kwa Watoto Wadogo

Kusoma si tabia nyepesi kuijenga katika mazingira ambayo masimulizi na mazungumzo ni vyanzo vikuu vya maarifa kuliko maandishi. Tumelelewa katika utamaduni usiosisitiza sana umuhimu wa kusoma. Lakini, hata hivyo, hatuwezi kukwepa kusoma katika ulimwengu huu unaotulazimisha kuyasaka maarifa kwa njia ya maandishi.

Ijumaa, Agosti 26, 2016

Umuhimu wa Kujenga Tabia ya Kujitolea

Kujitolea ni kutoa sehemu ya muda wako, ujuzi na maarifa uliyonayo na wakati mwingine nguvu zako kufanya kazi ya watu wengine bila kupata malipo ya moja kwa moja. Kazi unayoifanya kwa kujitolea mara nyingi ungeweza kuifanya kwa kudai ujira lakini unaamua kuifanya bure.  Mathalani, mwajiriwa anayetamani kuleta mabadiliko nje ya ajira yake, anapotumia ujuzi wake kufanya kazi za jamii bila kudai malipo, anakuwa amejitolea. Tuangalie kwa mhutasari kwa nini ni muhimu kujenga tabia ya kujitolea.

Jumanne, Agosti 23, 2016

Kipimo cha Kujitambua ni Tunavyowatendea Tusiowajua, Wasioheshimika

Mjema anaandika ripoti inayohitajiwa na mkuu wake wa kazi. Wakati muda wa kukabidhi ripoti hiyo ukikaribia, anapigiwa simu na mtu asiyemfahamu. Mjema hajui ni nani hasa anayemtafuta muda huo hivyo anaamua kupokea simu. Bahati mbaya aliyempigia simu hasikiki vyema. Mjema anahisi labda ni tatizo la mtandao, anaamua kuikata mara moja.

Jumamosi, Agosti 20, 2016

Kujitambua ni Kushinda Ubinafsi, Kujali Mahitaji ya Wengine?

Tulianza kudodosa suala la kujielewa katika makala yaliyopita. Kama tulivyodokeza, kujielewa kunakwenda sambamba na kuelewa msukumo ulio nyuma ya yale tuyatendayo kila siku. Katika sehemu hii, tutaangalia kwa ufupi kwa nini kujitambua ni zaidi ya ule ‘ubinafsi’ unaoishi ndani yetu.

Alhamisi, Agosti 18, 2016

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia

Ingawa ni kweli tunazaliwa na sehemu ya tabia tulizonazo, upo ukweli wa kiutafiti unaothibitisha kwamba mazingira ya kimalezi yana nafasi kubwa katika kujenga tabia za mtu. Ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili, mathalani, unatawaliwa zaidi na uasili ambao kwa kiasi kubwa hatuna mamlaka nao. Hata hivyo, ukuaji wa kihisia na kimahusiano unatawaliwa zaidi na mazingira ya kimalezi ambayo tayari tuliyaona kwenye makala iliyopita.