Tabia za Mamlaka kwa Wanyonge Zinavyoweza Kuzalisha Uovu
Umewahi kujiuliza kwa nini watu huweza kupokea na kutekeleza amri hata zile wanazoamini ni kinyume cha maadili, utu na dhamiri zao? Kwa nini mtu anaweza kuambiwa ‘fanya kitu cha kikatili’ na akatii hata kama amri hiyo inamaanisha mtu kuumia na hata kufa?
Mwanzoni mwa miaka ya 1960, Stanley Milgram wa Chuo Kikuu cha Yale alifanya utafiti maarufu kwa jina la #TheMilgramExperiment. Milgram alitaka kuangalia nini hasa kinachangia mtu kutii mamlaka hata katika mazingira ambayo utii huo unaweza kusababisha madhara kwa binadamu mwenzake.
Kwa lugha nyingine, nini hasa kilifanya watu kama Hitler waliofahamika wazi ni wakatili wawe na wafuasi waaminifu wanaotekeleza maagizo yao kuumiza watu, kutesa na hata kuwaua?
Utafiti ulivyofanyika
Washiriki wa utafiti huo waliaminishwa wanashiriki utafiti wa kuangalia uhusiajo wa kumbukumbu na ujifunzaji na wao wanashiriki kama ‘walimu.’ Jukumu lao lilikuwa ni kusoma swali na kufanya maamuzi ya kumuadhibu mwanafunzi papo kwa hapo ikiwa jibu analotoa si sahihi. Wanafunzi hawa, kwa upande mwingine, walikuwa wandani wa mtafiti na walijua siri ya utafiti.
Adhabu waliyotakiwa kutoa hawa ‘walimu’ ni kubonyeza kitufe kinachoachia shoti ya umeme kwa mwanafunzi. Kadri kosa linavyofanyika, mwalimu alipewa maelekezo ya kuongeza kiwango cha shoti kutoka volt 15 mpaka 450 kulingana na idadi ya makosa yanayofanywa. Ikumbukwe volt 450 ingeweza kutoa uhai wa mwanafunzi —ingawa katika mazingira halisi, hapakuwa na madhara yoyote kwa mwanafunzi.
Kilichokuwa muhimu hapa ni mamlaka ya mtafiti. Kwa hivyo, mtafiti aliwekewa mazingira ya ‘power’, kwa kuvaa koti la maabara, akionekana kuwa msomi, na ndiye aliyekuwa anatoa amri kwa mshiriki —mwalimu, kuendelea na zoezi hasa pale alipoonekana kusita.
Mwanafunzi, anayejua lengo la utafiti, alikaa chumba kingine na mara nyingi alitoa majibu yasiyo sahihi (ili aadhibiwe) na ikiwa mwalimu alibonyeza kitufe cha shoti, mwanafunzi alitoa sauti ya kuugulia maumivu makali akimsihi mwalimu kuacha kumwuumiza. Kama mwalimu alisita kuadhibu, mtafiti hakuonekana kujali na aliamuru zoezi liendelee. Kilichoangaliwa hapa ni utayari wa mwalimu kufuata maelezo na kuyatii bila kujali matokeo yake kwa binadamu mwenzake.
Matokeo
Washiriki wawili kati ya watatu (65%) ‘walitii sheria bila shurti’, wakitoa adhabu ya shoti hadi kufikia volti 450 ambayo walijua ingeweza kumwuua mwanafunzi. Ingawa wakati mwingine walifanya hivyo kwa masikitiko makubwa, uwepo wa jamaa mwenye madaraka pale uliwafanya wakawa hawana namna nyingine zaidi ya kutii na kutekeleza amri wanayojua inaweza kuleta madhara kwa binadamu mwenzao.
Stanley Milgram aligundua utii wa mwalimu uliongezeka zaidi mamlaka ya mtoa amri yalipoongezwa (namna alivyojitambulisha na kuvalia) lakini pia ukaribu uliokuwepo kati yakr na mwanafunzi (mfano mwalimu kuona mateso anayoyapata mwanafunzi wake badala ya kusikia sauti pekee).
Tafsiri
Milgram alitafsiri matokeo hayo kwa jicho la hatari ya madaraka katika kugeuza tabia za watu na kuwaingiza kwenye migogoro mikubwa ya kimaadili. Unapomuweka mtu wa kawaida kabisa kwenye mazingira yenye power, kwa mfano, unampa shinikizo la kuhalalisha mamlaka iliyo juu yake badala kuheshimu dhamira, miiko binafsi na misingi ya utu.
Hii ina maana kwamba kuna mazingira yanaweza kuchochea tabia ya ukatili kwa mtu na kumsukuma kufanya kitendo cha kikatili usiofikirika. Mazingira haya, kwa kiasi kubwa, yana uhusiano mkubwa na kuhalalisha mamlaka na madaraka ya watu fulani fulani na uwezo wao wa kusema kitu na kikatekelezeka.
Kwa mara nyingine, Milgram anatuonesha madhara yanayotokana na madaraka hasa yanapotumiwa kutoa amri zisizoongozwa na misingi ya utu wala maadili. Katika mazingira haya ya kulinda mamlaka, mtu mwema ayekuzwa katika mazingira ya utu, anaweza kabisa kutumika na kugeuka kuwa mtu katili asiye na chembe ya utu na akajitetea kuwa hakuwa na uchaguzi mwingine zaidi ya kutekeleza alichoamrishwa kutekeleza.
Tunachojifunza
Ingawa utafiti huu ulishambuliwa vikali kwa kuwadanganya washiriki, kutweza hisia zao na kuwafanya wajione ni watu wakatili, bado tunaweza kuutumia kuelewa uhusiano baina ya wenye mamlaka/madaraka na vibaraka wao. Unaweza kuelewa, kwa mfano, hatari ya kuwa na mtu mbabe kwenye mifumo ya siasa, makazini na kwingineko mwenye mamlaka ya kuagiza jambo ovu maslahi yake.
Hata hivyo, ni vigumu kutumia utafiti huu kuhalalisha ushiriki wa watu ‘wema’ kwenye maovu yanayofanywa kitaasisi. Je, ni kweli amri inatosha kukusukuma kumwuumiza binadamu mwenzako? Je, unaweza kusema nilidhihaki maumivu ya binadamu mwenzangu kwa sababu tu nilijua wakubwa zangu wanaamini katika mabavu, ubabe na ukatili? Wakati upi dhamiri ya mtu inaweza kumchochea kupingana na amri batili anazojua zinakwenda kinyume na misingi anayoiamini? Milgram hana majibu na anakosolewa vikali.
Mshunuzi Ginna Perry, kwa mfano, anafikiri wingi wa watu waliotii amri hiyo ya kikatili (wawili kati ya watatu) huenda ulitokana na ukweli kuwa walishtukia zile shoti za Milgram hazikuwa za kweli na ndio maana hawakuona shida kubonyeza mpaka kitufe cha mwisho kumaanisha walijua hakuna mtu anakufa pale. Hata hivyo, bado marudio mengine mengi ya utafiti kama huo yanaonesha kuwa kiwango cha utii kilikuwa kikubwa ingawa asimilia zinatofautiana.
Maoni
Chapisha Maoni