Machapisho

Inaonyesha machapisho yenye lebo ya Malezi na Makuzi ya watoto

Malezi yanapokuwa ‘rasha rasha’ tuilaumu teknonojia?

Picha
PICHA: businessday.ng Kama ambavyo imeanza kuwa vigumu wengi wetu kumaliza siku bila usaidizi wa zana za teknolojia, ndivyo malezi nayo yanavyoanza kuchukua uelekeo wa kuhitaji usaidizi wa teknolojia. Saa nyingine mzazi usingependa watoto waangalie katuni muda mrefu. Lakini unafanyaje sasa kama wewe mwenyewe hata unapokuwepo nyumbani huna mengi ya kufanya na watoto? Ombwe, kwa kawaida, huwa ni muhimu lizibwe. Lakini pamoja na kusaidia kujaza ombwe la sisi wazazi kutokuwepo kwenye maisha ya watoto, bado teknolojia inayo mengi yenye manufaa. Kubwa zaidi ni kuwachangamsha watoto kiakili.  Nitumie mfano wa mwanangu. Hajakamilisha miaka mitatu. Ukikaa naye anayo mengi ya kukusimulia. Uwezo tu wa kusimulia jambo na likaeleweka katika umri wa miaka miwili sikuuona kwa dada yake waliozidiana karibu muongo mzima. Ingawa bado ni mapema mno kumpeleka darasani, anatambua herufi na tarakimu zote, ana uelewa wa awali wa kuhesabu, anafahamu majina ya rangi nyingi, anawafahamu majina na tabia ...

Jinsi ya kumlinda mtoto na tofauti zenu

Picha
Simulizi la Renee limenikutanisha na wadau wa ushunuzi mjini Moshi. Tunapata kahawa jioni baada ya shughuli za siku. Hatujaonana muda. Tunasalimiana na kisha mada inageuka ghafla. Rebert anarejea mfano wa Renee, “Suala la mgogoro wa wazazi kumuathiri mtoto hilo halina mjadala.” Robert ‘anavuta’ kahawa kidogo kama mtu anayesikilizia ladha ya kinywaji cha moto sana na kisha anaendelea.   “Ukimsoma huyu dada ni dhahiri migogoro ya kifamilia ilikuwa na nguvu ya kuchora mwelekeo wa maisha yake ya kimahusiano.” Robert anasita. Wajumbe wamepotelea kwenye vioo vya simu zao. Kajihisi anaongea mwenyewe. Natingisha kichwa kumwitikia.   “Inasikitisha sana namna maamuzi yetu kama wazazi yanavyoweza kumnyanyasa mtoto kwa kiasi kile. Sitamani niwe mzazi nitakayemfanya mtoto awe na kazi kubwa ya kurekebisha tabia alizojifunza kwangu,” anajitahidi kujieleza Robert lakini kakatishwa tamaa. Wanaume hawamsikilizi wanacheka na simu zao. Hata mimi pia ninahisi huenda ninamsikiliza mwenyewe...

Usiyempenda anaweza kuwa baba wa mwanao?

Picha
  Watoto wanahitaji uwepo wa mzazi. Simulizi la Slaquara lilitukumbusha hakuna muujiza kwenye malezi. Mzazi unavuna ulichopanda. Renee anakazia funzo hilo. “Umeongelea athari za umbali kati ya mzazi na mwanae. Nayajua maumivu yake,” anasita na kufafanua, “Sikumbuki lini niliongea na mama yangu. Siwezi kusema ni adui yangu lakini sio mtu naweza kumtegemea kwa lolote.”   “Mara ya mwisho kuonana naye ni miaka miwili iliyopita alipokuja kusuluhisha mgogoro wangu na mzazi mwenzangu,” leso anayoitumia kujifutia inalowa machozi. Renee anaikunjua na kuigeuza kutafuta penye ukavu. “Nilimpa nafasi ya pili akaitumia vibaya. Badala ya kusikiliza upande wangu anielewe, aling’ang’ania kuwa upande wa yule mwanaume akinilazimisha kuishi naye. Hakutaka kabisa kuelewa kwa nini nilichagua abaki kuwa mzazi mwenzangu na si zaidi ya hapo.”   Mgororo huu mkubwa wa mzazi na mwanae umeanzia wapi? Renee anasimulia, “Nimekuzwa kama mtoto yatima. Nasimuliwa baba alipofariki nikiwa mdogo sana...

Mbinu za Kumfundisha Mtoto Kusoma Akiwa Nyumbani

Picha
Katika utafiti uliofanywa na program ya Uwezo iliyochini ya Shirika la Twaweza, zaidi ya nusu ya watoto wa darasa la nne na tano katika nchi za Afrika Mashariki hawana uwezo wa kusoma na kuandika. Nilimwuuliza Bahiya Abdi, mhadhiri wa masuala ya mitalaa, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, maana ya kutokujua kusoma na kuandika. Anasema: “Kuna mambo kadhaa ya kuangalia tunapozungumzia uwezo wa mtoto kusoma. Mbali na mtoto kutambua herufi, lazima awe na uwezo wa kusoma kwa haraka.” “Lakini pia, uwezo wa kusoma unapimwa kwa kiwango cha kuelewa kile anakisoma. Kama mtoto anaweza kusoma tu lakini hawezi kupata ujumbe vizuri, hapo tunaweza kusema uwezo wake uko chini ya kiwango.” Kwa mujibu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) mtoto wa darasa la kwanza na la pili anatarajiwa kutambua na kusoma kwa ufasaha maneno 50 yenye maana kwa dakika na maneno 40 yasiyo na maana kwa dakika. Kadhalika, anatarajiwa kuandika kwa ufasaha herufi kubwa na ndogo, na kufanya hesabu za kujumlisha na k...

Unaweza Kumruhusu Mtoto Afuate Dini Apendayo?

Picha
PICHA: Pixabay Ipo nafasi muhimu ya imani/dini katika malezi ya watoto. Imani si tu inamsaidia mtoto kujitambua, lakini pia ina nafasi ya kumtengenezea mtoto sauti kutoka ndani yake inayomsaidia kupambanua lililo jema na baya. Sauti hii inaitwa dhamira. Utakuwa shahidi kuwa kuna mambo wakati mwingine unatamani kuyafanya lakini unajisikia hatia kuyafanya. Unaweza, kwa mfano, kuwa na uhuru wa kutaka kufanya chochote, lakini kuna sauti ndani yako ikakunyima ujasiri wa kukifanya. Hakuna anayekuona, hakuna anayekuhukumu, lakini kuna kengele ndani yako inakwambia kuwa unachotaka kukifanya sio sahihi. Mwanasaikolojia wa kale anayeitwa Sigmund Freud aliita kengele hiyo ‘Superego’ kumaanisha mkusanyiko wa maelekezo tunayoyapata kwa watu wanaotuzunguka. Kwa kawaida, sauti na maelekezo hayo inayoumbika ndani yetu ndiyo inayoamua namna gani tunadhibiti matamanio yetu ya asili kama hasira na tamaa za mwili. Imani, tafiti zinasema, ina kazi kubwa ya kujenga dhamira. Mtu mwenye ...

Malengo Yanavyoweza Kubadili Tabia ya Mtoto

Picha
Mwanangu wa miaka saba alikuwa na tatizo la kupenda sana kununua vitu vitamu. Kila siku alikuwa ombaomba wa chochote kinachomtosha kwenda dukani. Sikupenda tabia hii. Mbali na kuharibu meno yake, kulikuwa na tatizo la kutokujizuia. Ilifika mahali tunagombana kwa sababu tu hajapata chochote kukidhi hamu yake ya kununua ‘ice cream’, ‘chocolate’ na vinavyofanana na hivyo. Jitihada za kubadili tabia hii ya kupenda vitu visivyo na faida kwake hazikuzaa matunda.

Mambo Sita Mwanao Anayohitaji Kuyasikia

Picha
PICHA: houstonpress.com Watoto wadogo ni watu kamili wenye hisia kama sisi watu wazima. Hata kama wakati mwingine hawawezi kusema wazi wazi, ukweli ni kwamba akili zao ni kama dodoki linalonyonya kimya kimya yale wanayoona tukiyasema na kuyatenda. Unaweza, kwa mfano, kusema jambo dogo kwa mtoto tena bila kumaanisha lakini jambo hilo likawa sumu itakayoharibu kabisa maisha ya mwanao. Unaweza kuwa na nia njema ya kumlazimisha kufanya kitu fulani sahihi kabisa, lakini kwa sababu hujaweza kuelewa na kujali hisia zake, jambo hilo likakosa nafasi kwenye moyo wa mtoto. 

Umuhimu wa Kumpunguzia Mtoto Shinikizo la Kufaulu

Picha
PICHA: Stressed Out Students Ufaulu wa mitihani umepewa nafasi ya pekee katika mfumo wetu wa elimu. Shule zetu, kwa hakika, hazina namna nyingine ya kumwelimisha mtoto zaidi ya kumtaka akusanye, akumbuke na kutumia maarifa aliyonayo kujibu maswali ya mtihani. Ingawa ustawi wa jumla wa mwanadamu hautegemei eneo hilo moja la ukusanyaji na utumiaji wa maarifa, shule zetu zinaonekana kuamini pasipo mtu kuwa na maarifa mengi hawezi kufanikiwa.

Ufanyeje Kijana Chipukizi 'Anapokata' Mawasiliano na Wewe?

Picha
PICHA:  Parent Pump Radio Kama nilivyoeleza kwenye makala yaliyopita, tofauti za kimtazamo kati ya mzazi na kijana anayechipukia ni hali zinazotarajiwa. Wakati mwingine tofauti hizi zinaweza kuonekana kama mambo madogo yasiyo na msingi. Lakini tofauti hizi zinazoonekana kuwa ndogo zisiposhughulikiwa zinaweza kukomaa na hatimaye kusababisha matatizo makubwa. Wazazi, mara nyingi, hatupendi kuzipa uzito tofauti hizi mara zinazopoanza kujitokeza. Kijana wako anaweza kuanza kuwa mkimya bila sababu za msingi, anaanza kukukwepa na hata kupunguza mawasiliano na wewe, lakini ukachukulia ‘kawaida.’

‘Homework’ Zinavyodumaza Ukuaji wa Watoto Wadogo

Picha
PICHA:  PhillyVoice Ukiwauliza wazazi kitu gani wanafikiri kikisitizwa mapema zaidi kwa watoto kitawasaidia kufanikiwa, wengi  watakwambia elimu. Kwa sababu hiyo, wazazi hasa wasomi wanaharakisha kuwapeleka shule watoto wenye umri mdogo. Ninawafahamu watoto wengi wa miaka minne wanaosoma darasa la kwanza. Wazazi wa watoto hawa wanafanya hivyo wakiamini mtoto akisoma mapema, maana yake uwezekano wa kufanikiwa maishani unakuwa mkubwa.

Nafasi ya Mzazi Katika Kukuza Vipaji vya Watoto

Picha
Jioni moja, mwanzoni mwa miaka ya tisini, nikiwa darasa la tatu, mama alikuja nyumbani na barua aliyoniambia ilikuwa yangu. Barua hiyo fupi iliyoanza na maneno, ‘Mpendwa mwanangu Christian,’ ilikuwa ndani ya bahasha yenye barua ya mama kutoka kwa baba yangu, ambaye kwa wakati huo alikuwa masomoni.

Unamsaidiaje Mtoto Asiyefanya Vyema Kimasomo?

Picha
PICHA: BBC News Kwa mzazi mwenye mtoto anayesoma shule, ni rahisi kuelewa inakuwaje pale unapokuwa na uhakika mwanao ana uwezo mzuri lakini matokeo anayoyapata shuleni hayalingani na uwezo wake. Kama mzazi unayejali unajaribu kufanya wajibu wako, unamsaidia kazi za shule, unamwekea mazingira mazuri yanayomhamasisha kujisomea akiwa nyumbani, unashirikiana na walimu wake, lakini bado matokeo yanakuwa kinyume.

Madhara ya Kumpeleka Mtoto Shule ya Bweni

Picha
PICHA: Daily Maverick Moja wapo ya sababu nyingi zinazowasukuma wazazi kuwapeleka watoto wadogo kusoma shule za bweni ni mafanikio ya taaluma. Mazingira ya shule yanaaminiwa kuwa bora zaidi katika kuwasaidia watoto kufanya vizuri zaidi kuliko wanapokuwa nyumbani.

Kitabu Kipya cha Malezi na Makuzi

Picha
Malezi ya sasa yamekumbwa na changamoto nyingi na kusababisha watu kushindwa kuwasaidia watoto na vijana wao ili kufanikiwa. Mmomonyoko wa maadili umekuwa chanzo kikubwa cha matatizo yanayomkumba kijana na jamii kwa ujumla. Matatizo hayo ni kama vile ukosefu wa ajira, kushindwa kufikia ndoto za maisha, migogoro katika familia, pamoja na watu kushindwa kuwa na utulivu na amani.

Je, Shule za Bweni Zinafaa kwa Malezi ya Watoto Wadogo?

Picha
PICHA: SOS Schools Ongezeko kubwa la shule za bweni kwa watoto wadogo ni kiashiria kimoja wapo cha mabadiliko ya kijamii yanayoendelea kuathiri desturi za malezi. Pamoja na changamoto zake, mzazi anapofanya maamuzi ya kumpeleka mwanae shule ya bweni huamini anafanya hivyo kwa faida ya mtoto.

Kwa nini Wazazi Huwapeleka Watoto Wadogo Shule za Bweni?

Picha
PICHA: The Citizen Miaka kadhaa iliyopita, wakati huo nikiwa mwanafunzi, nilishangazwa kusikia mtoto wa ndugu yangu, wakati huo akiwa na miaka sita, alikuwa anasoma shule ya bweni. Sikufikiri jambo hilo lingewezekana.                                                                                     Nakumbuka mara yangu ya kwanza kwenda shule ya bweni nilikuwa na umri wa miaka 17 nikisoma kidato cha 5. Kwa kuwa haikuwa rahisi kwangu kuzoea maisha ya mbali na nyumbani, nilishindwa kuelewa inawezekanaje mzazi kumpeleka mtoto mdogo kiasi hicho kwenda shule ya bweni.

Upendeleo wa Wazazi Unavyoweza Kuchochea Uadui kwa Watoto

Picha
PICHA: Aim Lower Journal KUNA kisa kimoja kwenye biblia kinachoweza kutufundisha jambo muhimu kama wazazi. Kisa chenyewe ni kile cha Yusufu, mtoto wa mzee Yakobo, aliyejikuta kwenye mtafaruku mkubwa  na ndugu zake. Ugomvi wa Yusufu na kaka zake ulikuwa mkubwa kiasi kwamba kaka zake waliazimia kwa pamoja kumwuuza Misri kama adhabu. Jambo la kuzingatia ni kwamba ugomvi huu wa Yusufu na ndugu zake haukutokea kwa bahati mbaya. Chanzo cha yote hayo ni upendeleo.

Kipimo cha Uadilifu Wetu ni Namna Tunavyopambana na Mimba za Utotoni

Picha
PICHA:  Huffington Post NINGEPENDA kuamini, katika mjadala unaoendelea kuhusu mimba za utotoni, kila mchangiaji bila kujali mapendekezo yake, anatamani kuona tunamaliza tatizo hili. Hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kutetea watoto wa kike kupata ujauzito katika umri mdogo.

Tunavyoweza Kuboresha Vituo vya Malezi

Picha
PICHA: John-Paul Iwuoha MALEZI katika vituo vya kulelea watoto hayakwepeki. Katika mazingira ambayo wazazi wanafanya shughuli zao mbali na nyumbani kituo cha malezi kinakuwa msaada. Tafiti za malezi zimekuwa zikijaribu kuangalia namna gani huduma hizi zinavyoweza kuboreshwa. Moja wapo ya mashirika maarufu katika eneo hili ni   Taasisi ya Marekani ya Mtandao wa Afya ya Mtoto na Maendeleo ya Utafiti wa Malezi ya Watoto (NICHD) .

Unayopaswa Kuzingatia Unapompeleka Mtoto Wako Katika Vituo vya Malezi -1

Picha
PICHA: Hope for Bukasa UTARATIBU wa wazazi kuwapeleka watoto kwenye vituo vya malezi umeanza kuwa maarufu hapa nchini. Karibu kila mji mdogo katika mikoa yote vipo vituo kadhaa mahususi kwa ajili ya kuwatunza watoto wakati wazazi wao wakiwa kazini. Kinachofanya huduma ya malezi ya vituoni kuwa maarufu ni changamoto za akina dada wa kazi, ambao mara nyingi, huwa ni wadogo kiumri na hawana uwezo wala ari ya kuwalea watoto vizuri.