Kipimo cha Uadilifu Wetu ni Namna Tunavyopambana na Mimba za Utotoni
PICHA: Huffington Post |
NINGEPENDA kuamini, katika mjadala unaoendelea kuhusu
mimba za utotoni, kila mchangiaji bila kujali mapendekezo yake, anatamani kuona
tunamaliza tatizo hili. Hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kutetea watoto
wa kike kupata ujauzito katika umri mdogo.
Lakini pia, mbali na kupoteza fursa ya kuendelea
na masomo, watoto hawa wanaopata mimba shuleni wanajikuta katika mazingira
magumu linapokuja suala la mahusiano ya kudumu. Wanaume wengi wanaowapa mimba
huukwepa mkono wa sheria kwa kuwakataa. Kitendo cha kukataliwa na mtu aliyemwamini
kinaweza kujenga chuki ya kudumu na watu wanaomzunguka.
Hata wanapokuwa watu wazima, wengi wa wasichana
hawa hupata tabu kuingia na kudumu kwenye ndoa.
Sababu kubwa inaweza kuwa ni chuki wanayokuwa nayo dhidi ya wanaume au
mtazamo hasi walionao wanaume dhidi ya wanawake wenye watoto tayari. Matokeo
yake ni kumdidimiza mtoto kwenye maisha ya upweke, kukataa tamaa na ufukara.
Kama jamii iliyostaarabika, hatuwezi kuacha hali hii
iendelee. Kwanza, tunao wajibu wa kimaadili wa kufikiria namna ya kuwasaidia
wasichana wanaojikuta katika mazingira kama haya. Kuwaita wahuni na malaya
hakutusaidii sisi wala hakuwasaidii wao. Tunahitaji kutafakari kwa kina namna
tunavyoweza kuwaepusha watoto wetu na madhila haya ambayo kimsingi wanajifunza
kwetu. Kama tulivyosema katika makala iliyopita, hatuwezi kuwabebesha lawama zote
wasichana hawa kwa sababu wanayoyafanya yanafanywa na jamii inayowazunguka.
Katika makala haya tunapendekeza namna nne zinazoweza
kutumika kutatua tatizo la mimba za utotoni. Kwanza kabisa, tunahitaji
kuelekeza nguvu nyingi katika elimu ya malezi. Tunafahamu kwamba wazazi wengi
tumesahau wajibu wetu. Tunapambana na maisha na kuwaacha watoto bila mtu wa
karibu anayeweza kujua kinachoendelea katika maisha yao. Tunatumia muda mwingi
kazini na hatukumbuki kupata muda mfupi kuzungumza na watoto. Tunahitaji
kubadilika.
Wazazi tutambue wajibu wetu. Tujisikie kuwajibika
kuwa karibu na watoto tangu wanapokuwa wadogo. Ukaribu huu na watoto utasaidia
kujenga mawasiliano mazuri yatakayowafanya wawe na imani na sisi. Imani hii ndiyo
msingi wa kupata upenyo wa kushirikishwa mambo ya siri yanayowasibu watoto. Bila
kuaminika, mzazi hawezi kuwa kimbilio la kwanza mtoto anapokuwa na maswali
yanayohitaji majibu.
Kadhalika, tunahitaji kujenga utamaduni wa uwazi
zaidi tunapozungumza na watoto. Kuendelea kuyafanya mazungumzo yanayohusu
ujinsia na ngono kuwa siri hakuwezi kutusaidia. Mambo yamebadilika. Watoto
wanaishi kwenye dunia ambayo taarifa zenye vionjo vya ngono ziko waziwazi.
Uholela huu wa taarifa unawafanya wawe na udadisi mwingi. Fahamu zao zinatafuta
majibu ya mambo mengi wanayoyaona. Tukitaka kufanikiwa lazima tuwe tayari
kubadilika na kuweka nguvu nyingi kwenye elimu ya afya ya uzazi.
Tunalo tatizo kubwa la watoto wengi kutokujitambua.
Wengi wao wanakutana na balehe bila maandalizi yoyote. Hakuna mtu mzima
anayethubutu kuzungumza nao. Matokeo yake wanajikuta wakiamini taarifa potofu
wanazoziokoteza mtaani na kuzifanyia majiribio. Bahati mbaya, hata hivyo, wanaopozifanyia
kazi taarifa hizo, wanajikuta wakijifunza tabia zilizo kinyume na maadili.
Tuwasaidie watoto kujitambua mapema. Mtoto
anapoanza kupevuka mwili, asiachwe akanong’onezwe na wenzake kujua
kinachoendelea kwenye mwili wake. Tujenge utaratibu rasmi wa kuwapa elimu inayohusu
miili yao. Mifumo yetu ya elimu isiishie kutoa elimu ya afya na uzazi kama
nadharia za kukariri kwa ajili ya mitihani. Tuwawezeshe walimu wetu kufundisha
masuala haya kwa ufanisi zaidi yasaidie kujenga uwezo wa mtoto kujielewa.
Pamoja na yote hayo, elimu kwa umma ni muhimu.
Hivi sasa tunasikia kelele za watu wanaohubiri maadili lakini wao wenyewe
wameshindwa kuyaishi maadili hayo. Tunakemea ngono kwa watoto wadogo wakati
sisi wenyewe tunawashawishi watoto wadogo kujiingiza kwenye vitendo hivyo. Hatuwezi
kuwafundisha watoto maadili wakati sisi wenyewe hatuna maadili. Ikiwa kweli tunamaanisha
kukomesha tatizo la mimba za utotoni, tunahitaji kubadilika. Kila mmoja asaidie
kuelimisha jamii kwa nafasi yake. Tujisikie kuwajibika kuonesha mfano mwema kwa
watoto na wadogo zetu badala ya kuwahukumu na kuwanyooshea vidole kwa makosa
ambayo kimsingi tumeyasababisha sisi wenyewe.
Ndio kusema, jamii iliyobadilika na yenye
maadili, haiwezi kutumia muda mwingi kuwahukumu walikosea. Jamii inayojitambua haimbebeshi
lawama mkosefu na kujitenga na wajibu wa kutafuta ufumbuzi. Hatuwezi kuwa jamii
yenye maadili na tukawa tayari kuwakejeli na kuwadhihaki watoto waliopata mimba
utotoni. Lawama na kejeli kwa wenye makosa ni ukosefu wa maadili. Kipimo cha
maadili yetu na ukomavu wetu kama jamii kiwe namna tunavyofikiria kuwasaidia
hata wale ambao tayari wamekosea.
Maadili hayo lazima yatafsiriwe katika sera zetu.
Tujiulize, kwa mfano, namna gani sera zetu zinamlinda mtoto na hatari ya kukosa
maadili? Namna gani sera zetu zinampa nafasi mtoto aliyekosea kurekebisha
makosa yake? Je, sisi kama jamii yenye maadili tunaweza kuwa tayari kuvumilia
vitendo vya ngono miongoni mwa wanafunzi wa kiume lakini tukiwafukuza watoto wa
kike wanaopata mimba? Je, sisi kama jamii yenye watu waadilifu, tunaweza
kuwaadhibu watoto wajawazito bila kufikiria namna ya kuwasaidia?
Maoni
Chapisha Maoni