Je, Walimu na Wazazi Wanazungumza Lugha Moja Kujenga Maadili ya Watoto?
PICHA: Godot13 |
SUALA la maadili limezua mjadala mrefu katika
siku za hivi karibuni hasa baada ya wanasiasa kupinga wasichana wajawazitokuendelea na masomo yao kwa sababu ya ujauzito. Kauli hizo zilipingwa vikali na
wanaharakati wenye msimamo wa kuwatetea watoto wa kike. Hoja yao ni kwamba
kumnyima msichana fursa ya kupata elimu kwa kosa la kuwa mhanga wa mfumo holela
usiomjenga msichana kimaadili ni kutokuyatazama mambo katika upana wake.
Tunapozungumzia maadili ya wanafunzi, kimsingi
hatukwepi kusaili ushirikiano wa karibu kati ya wazazi, walimu, wanasiasa na
jamii kwa ujumla. Jitihada za kujenga maadili katika ngazi ya familia, kwa
mfano, lazima zioane na jitihada kama hizo katika eneo la shule. Ikiwa tunataka
kweli kujenga kizazi cha watoto wenye maadili, lazima kuhakikisha juhudi za
wazazi zinakwenda sambamba na juhudi zinazofanywa na walimu. Panapotokea
mazingira ambayo wazazi na walimu wanapishana mbinu, ni vigumu kujenga kizazi
cha watoto wenye maadili.
Utafiti uliofanywa na Dk Daniel Mngarah wa ChuoKikuu cha Dodoma na kuchapishwa na Jarida la “Global Journal of Human Social Sciences” Toleo la 17, Na.4 la 2017
unaweza kutupa picha halisi ya ushirikiano uliopo kati ya wazazi na walimu. Kwa
mujibu wa Dk. Mngarah, ushirikiano baina ya wazazi na uongozi wa shule
umekuwepo kwa muda mrefu ingawa lengo limekuwa ni taaluma ya wanafunzi. Kamati
za shule zinapoitishwa, kwa mfano, hoja kuu imekuwa ni ‘namna ya kuinua ufaulu
wa wanafunzi.’ Suala la maadili ni kama halijapewa kipaumbele katika mipango na
sera za elimu.
Hata hivyo, tafiti mbalimbali zinaonesha kwamba
maadili yana nafasi kubwa katika safari ya kujifunza aliyonayo mwanafunzi. Ni
dhahiri mwanafunzi mwenye nidhamu na usikivu, anakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi
ya kujifunza.
Katika utafiti huo, pamoja na mambo mengine, Dk
Mngarah alilenga kuchunguza ikiwa walimu na wazazi wana mtazamo unaofanana
katika kujenga maadili ya wanafunzi na athari ya mitazamo hiyo katika
kushughulikia nidhamu ya wanafunzi. Matokeo ya utafiti huo muhimu yanaonesha
hali ya kushangaza kidogo. Kwanza, walimu wakuu walidai hapakuwa na ushirikiano
unaoeleweka baina ya shule na wazazi. Wazazi, kwa mfano, walidaiwa kupinga
juhudi kubwa zilizokuwa zikifanywa na uongozi wa shule katika kujenga nidhamu
ya watoto. Adhabu zilipotolewa, wazazi walikuja juu na kuzitafsiri kama kisasi
kati ya walimu na wanafunzi wanaoadhibiwa.
Mkuu mmoja wa Shule anatoa mfano wa mzazi
aliyefika shuleni hapo kumshtaki mwalimu aliyekuwa amemwadhibu mwanafunzi kwa
utovu wa nidhamu. Inavyoonekana, mwanafunzi alikuwa ameadhibiwa kwa tabia yake
ya kutoroka shule na kwenda kuonana na rafiki yake wa kiume pale kijijini.
Mwanafunzi huyu alipoadhibiwa, alikwenda kushitaki kwa mzazi kwamba walimu wana
chuki naye. Mzazi alipofika shuleni, ilibidi mwalimu na mwanafunzi husika
waitwe. Kwa kuwa mwalimu alikuwa ana hakika na kile alichokuwa anakisema,
aliomba begi la mwanafunzi lipekuliwe. Begi lilipopekuliwa, zilikutwa nguo ‘za
nyumbani’ zilizokuwa zinavaliwa muda wa kutoroka unapowadia. Baadae ilifahamika
kwamba mwanafunzi huyo alikuwa mjamzito.
Walimu, kwa upande wao, walionekana kutilia mkazo
zaidi kwenye ufaulu wa wanafunzi kuliko tabia na mienendo yao. Mwalimu mmoja
ananukuliwa akisema, “Nimeajiriwa kufundisha. Hiyo ndiyo kazi yangu. Sioni
sababu ya walimu kuhangaika na masuala ya maadili wa wanafunzi. Wazazi wenyewe
ndio hawa na wakuu wa elimu wanataka matokeo makubwa.” (Tafsiri ni yangu).
Walimu
hawakuonekana kushughulika sana na masuala ya maadili isipokuwa kwa utashi wa
mwalimu mmoja moja. Kwa upande wao, wazazi walionekana kulichukulia suala la
maadili kama wajibu wa akina mama zaidi kuliko wa familia. Wanaume waliamini
kazi yao ya msingi ni kuhakikisha familia inapata mahitaji ya kila siku. Suala
la malezi liliachwa mikononi mwa akina mama.
Utafiti huu unatusaidia kuelewa changamoto
inayotukabili kama jamii. Kwanza, mfumo wetu wa elimu unaonekana kusahau kumjenga
mtoto katika maeneo yote ya kimaisha. Lakini pili, inaonekana hakuna uelewa wa
pamoja baina ya wazazi na walimu linapokuja suala la maadili kwa watoto. Shule
zinasisitiza kufaulu masomo, na wazazi nao wanaendelea na shughuli wanazofikiri
ni muhimu. Hali hii ni kikwazo cha jitihda za kujenga maadili.
Umefika wakati
elimu ya maadili si tu iwe sehemu ya mfumo wa elimu bali isisitize mabadiliko
ya tabia kuliko uelewa pekee. Kadhalika, jamii nzima ishirikishwe katika juhudi
za kuwalea watoto kimaadili badala ya kusubiri kutoa matamko matatizo
yanapotokea.
Maoni
Chapisha Maoni