Chuki Unakuumiza Wewe Kuliko Unayemchukia
PICHA: PM Notes |
MIAKA kadhaa iliyopita nilikosana na
mtu ambaye awali tulikuwa karibu kikazi. Nilimwamini kama rafiki tuliyefanya
kazi pamoja. Sikufikiri angeweza kujitafutia sifa binafsi kwa kunihujumu. Kilichoniumiza si tu kutendewa osa la makusudi, bali kuona mtu niliyemheshimu akijaribu kufikia
malengo yake kwa kujaribu kuniharibia kazi yangu.
Nakumbuka baadae tulizungumza na nikafikiri
nimemsamehe. Hata hivyo, ninapotazama nyuma, ninagundua kwamba sikuwahi kumsamehe
kwa karibu miaka miwili baadae. Uhusiano wetu ulizorota na haukuweza kurudi
kama ilivyokuwa hapo kabla. Ingawa tuliendelea kuzungumza lakini ule urafiki wa dhati unaoanzia
moyoni haukuwepo tena.
Sikuwa na imani naye. Sikuamini
aliyoyasema na kuyafanya. Kila nilipokumbuka namna alivyonihujumu, hisia za
usaliti zilinirudia. Ingawa nilijiaminisha kwamba nimemsamehe, lakini katika
maisha halisi sikuwa nimemsamehe. Kwanza, wakati wote nilikumbuka yale
aliyonitendea. Akili yangu ‘ilisamehe’ kwa maneno lakini haikusahau kwa
vitendo. Mara kadhaa moyo wangu ulijaa huzuni na ghadhabu. Kwamba sikuwa nimesahau kosa lake maana yake bado nilikuwa nahesabu
kosa lake.
Lakini pili, sikuwa natamani kusikia akipatwa
na mema. Kama ningesikia akisifiwa kwa jambo zuri alilolitenda, moyoni nilijisikia
vibaya. Mafanikio yake yaliniudhi. Sifa na jitihada zake njema zilikuwa kero kwangu. Moyoni
nilitamani kusikia akipata mshahara wa mabaya aliyonitendea. Wahindi wanaita
‘karma’.
Nakumbuka siku moja alipatwa na
changamoto fulani kazini. Niliposikia kilichotokea moyo uliruka ruka kwa furaha hata kama
sikusema. Niliamini ‘mungu’ hatimaye amemlipa kwa mabaya aliyonitendea. Nilifurahia
kwamba sasa amekula matunda ya matendo yake mwenyewe. Sasa nafahamu hiki
kilikuwa ni kisasi cha kificho ndani yangu. Huyu bwana aliishi moyoni mwangu hata kama kwa nje niliamini nimemsamehe.
Hali hii ya kutokusamehe ilipanda ngazi
na kugeuka kuwa chuki. Ungeniuliza kwa nini nilimchukia, pengine ungeungana na mimi. Nilikuwa na kila sababu sahihi ya 'kuachana naye.' Sikutamani kuwa karibu naye tena. Chuki iliyokuwa
inanitafuna moyoni ilinifanya nikawa mwepesi kuamini tetesi za mapungufu yake. Nilijikabidhi kuwa mtumwa wake.
Unapomchukia mtu, kwa hakika,
unajibebesha mzigo mzito kihisia kama ilivyokuwa kwangu. Unakuwa na kazi na
kupambana na mtu ambaye pengine hana habari na wewe. Wakati wewe ukijiumiza kwa
kutamani aharibikiwe, mwenzako ndio kwanza anafanikiwa. Chuki, katika mazingira
haya, inakuwa na kazi ya kukuumiza wewe kuliko inavyomwumiza unayemchukia.
Hatimaye nilijifunza kusamehe. Nikagundua
unapomsamehe mtu maana yake si tu unaachilia kile alichokufanyia, bali unarejesha
uhusiano uliokuwepo kabla ya kosa. Kiashiria kimojawapo kwamba umerejesha
uhusiano ni pale unapoanza kufurahia mafanikio yake na kusikitika unaposikia
amepatwa na mabaya. Hiki ndicho kipimo cha msamaha wa kweli. Kinyume na hapo ni
chuki inayoishi ndani yako.
Inawezekana unaposoma hapa unakumbuka
watu waliokukosea. Pengine ni mume wako au mke wako. Pengine ni mwanao. Pengine
ni ndugu yako wa karibu, mfanyakazi mwenzako au mshirika wako wa kibiashara.
Unapokumbuka aliyokufanyia unajikisia uchungu. Unajiapiza hutakaa usamehe. Huo
ndio utumwa ambao chuki inaweza kukutengenezea.
Kuushinda utumwa huu ni kuwaruhusu watu
kukukosea. Nilipojifunza kujiondoa kwenye hadhi ya kuwa mtu maalumu asiyepaswa
kuguswa na mwingine, ilikuwa rahisi kuanza ukurasa mpya. Nilianza kuachana na
gereza la ‘karma’ la kufikiri kwa kuwa mtu amenikosea, lazima na yeye apatwe na
mabaya.
Unaweza kufanya hivyo pia. Msamehe
yeyote aliyekutendea mabaya. Hufanyi hivyo kumsaidia yeye kwa sababu pengine
anafurahia kukuona unateseka. Unasamehe kwa faida yako mwenyewe. Badala ya
kujifungia kwenye gereza la kulipiza kisasi, unajiwekea mazingira ya kuushinda
ubaya kwa wema.
Ikiwa ni lazima kulipiza kisasi ili
ujisikie ahueni moyoni mwako, kisasi sahihi zaidi ni upendo. Mpende mchumba
aliyekuacha. Mpende rafiki aliyekusaliti. Mpende mfanyakazi aliyekuhujumu. Kwa
kufanya hivyo, unajiweka huru wewe mwenyewe na kujifungulia milango ya kusonga
mbele na maisha.
Maoni
Chapisha Maoni