Je, Shule za Bweni Zinafaa kwa Malezi ya Watoto Wadogo?
PICHA: SOS Schools |
Ongezeko kubwa la shule za
bweni kwa watoto wadogo ni kiashiria kimoja wapo cha mabadiliko ya kijamii
yanayoendelea kuathiri desturi za malezi. Pamoja na changamoto zake, mzazi
anapofanya maamuzi ya kumpeleka mwanae shule ya bweni huamini anafanya hivyo
kwa faida ya mtoto.
Mazingira ya nyumbani yanaposhindwa
kufikia matarajio aliyonayo mzazi kwa mwanae, kitaaluma kwa mfano, mzazi hutafuta ufumbuzi
kupitia shule ya bweni.
Pia, wakati mwingine
shule ya bweni huwa ni jitihada za mzazi kumlinda mtoto na changamoto za kifamilia. Wazazi wanapokosa muda wa
kutosha kumwangalia mtoto au hata pale wanapokuwa na mgogoro wanaofikiri unaweza
kumwathiri mtoto, wanaweza kufikiri kumpeleka mtoto bweni kwa lengo la kumnusuru.
Hata hivyo, wapo pia wazazi wanaoamua kuwapeleka
watoto shule za bweni kwa kuwa wamechoka na kile wanachokiita ‘usumbufu’ wa
watoto kuwa nyumbani. Shule ya bweni, kwa maana hiyo, ni jitihada za kupunguza
makelele nyumbani.
Lakini je, watoto wadogo
wanaowahishwa kupata huduma za bweni wanapata malezi yanayolingana na mazingira
ya nyumbani? Je, mazingira ya bweni yanawasaidia kujifunza vizuri zaidi kuliko
nyumbani?
Dhana ya ujifunzaji
Jamii imekuwa ikiamini kuwa kujifunza kwa mtoto
kunaanzia pale mtoto anapofundishwa maarifa yanayoweza kupimwa kwa mitihani. Tunayachukulia
maarifa hayo kwa uzito kwa imani kwamba maisha ya mtoto yanategemea eneo moja
la ufahamu wa mambo. Dhana hii, hata hivyo, si sahihi. Ukuaji na maisha ya
mtoto kwa ujumla yanategemea maarifa yote anayoyafyonza mtoto kutoka kwenye
mazingira yake.
Ili maarifa hayo yawe na msaada kwa mtoto, ni lazima
yaweze kugusa maeneo yote muhimu ya maisha ya mtoto. Kwa mfano, mtoto lazima
afundishwe maadili, mahusiano yake na watu, masuala ya kiroho/kiimani na stadi
za maisha. Mtoto anayejengwa katika haya kwa pamoja, anakuwa na utu ndani yake
unaoweza kumwongoza kuwa mtu timamu anayejiheshimu na kuwaheshimu watu wengine.
Mtoto anayewekewa msisitizo kwenye eneo moja la ukuaji, hawezi kuwa binadamu
timamu.
Nafasi ya ukaribu wa kifamilia
Ukuaji wa jumla wa mtoto unategemeana na mfungamano
wa kimahusiano anaoujenga na watu wake wa karibu. Familia ndiyo mahali pekee
ambapo mtoto anaweza kupata watu wanaoweza kumwelewa na kujali maendeleo yake
kuliko mahali kwingine kokote.
Ukaribu unaopatikana katika familia unamjengea mtoto
utulivu wa nafsi. Kule kujua anazungukwa na watu wanaoaminika, kunamjengea hali
ya kujiamini. Katika mazingira haya, ya ukaribu wa familia, mtoto anakuwa
kwenye nafasi nzuri ya kuiga tunu za maisha kupitia maisha wanayoishi wazazi
wake.
Mtoto anaponyang’anywa fursa hii ya kujifunza maisha
katika familia yake mwenyewe, anakosa msingi muhimu wa maisha. Kumlazimisha
mtoto kujitegemea kabla ya wakati wake, ni kumfungulia milango mingi ya watu
wengine kuwekeza mambo ambayo wakati mwingine yanakinzana na matarajio ya mzazi
mwenyewe.
Hali ya malezi shuleni
Mwaka 2014 nilitembelea
shule kadhaa za msingi za bweni hapa nchini. Lengo lilikuwa kuchunguza ikiwa
mazingira ya kimalezi katika shule hizi yanaweza kulinganishwa na malezi
yanayopatikana katika familia. Vigezo vya malezi nilivyovitazama vilikuwa ni
pamoja na ukaribu baina ya watu wazima na watoto, uangalizi na kiwango cha
udhibiti kwa watoto, kutaja kwa uchache.
Katika shule kadhaa,
watoto walinipa ushuhuda wa kusikitisha. Wengi wao walionekana wazi kukosa
fursa ya kuwasiliana na walezi wao. Nakumbuka mtoto mmoja wa miaka sita alilalamika,
“Sijaonana na mama tangu amenileta shule. Nipelekee kwa mama!” Hakuwa peke
yake. Watoto wengi hasa wa darasa la kwanza walionekana kuwa wanyonge
nilipowauliza mambo yanayowakumbusha nyumbani.
Walezi nao walinisimulia
namna wanavyopata shida kuwatuliza watoto hasa mwanzoni mwa muhula. Mmoja wao
aliniambia, “Kipindi cha mwanzo wanapoletwa hapa, huwa inasikitisha sana. Usiku
hawalali wanalia kurudi nyumbani. Kuna wengine wanafungashaga mizigo yao usiku wakidai kurudi nyumbani. Inasikitisha sana kwa
kweli. Lakini baada ya muda huwa wanazoea na kuchangamka kama wenzao wakubwa.”
Wastani wa uwiano wa
mlezi na watoto ulikuwa mlezi mmoja anayeangalia watoto kati ya 50 na 100. Hii
ni idadi kubwa. Nilimwuliza mlezi mmoja anawezaje kuwahudumia watoto wote hao?
“Ni changamoto kubwa. Jioni wengi wao wanakuwa wanadeka na kulia lia. Kila
mmoja anataka nimsikilize. Ninachofanya naanza na wale wadogo wenye shida
kubwa. Wengine inabidi wanasubiri.”
Ukaribu kati ya mlezi na
mtoto ni hitaji la msingi. Ukaribu huu unapokosekana unamfanya mtoto ajisikie
kutengwa. Mtoto anayehisi mlezi anampuuza hupoteza hali ya kujiamini. Hata
hivyo, mtoto anayekosa kujiamini wakati mwingine hujenga tabia fulani za
kujihami kama alivyoniambia mtoto mmoja wa darasa la pili:
“Kukaa na baba na mama
ni mambo ya kitoto,” anacheka na kuendelea, “Ukishakuwa mkubwa kama mimi unaachana
na wazazi unatafuta maisha yako.” Lugha kama hii ni mfano mzuri wa kujihami.
Mtoto huyu amepoteza thamani ya mahusiano na familia yake. Ufahamu wake umeamua
kuwapotezea wazazi ili kupooza maumivu ya kuishi mbali na nyumbani.
Uangalizi hafifu
Nilitaka kujua namna
watoto wa bweni wanavyolala. “Tunawachanganya kwa umri,” aliniambia mlezi mmoja
na kuendelea, “Wale wa darasa la kwanza tunawachanganya na wale wakubwa ili
waangaliane.”
Pamoja na nia njema ya
kufanya hivyo, utaratibu huu unaibua changamoto nyingine. Watoto wadogo
huwachukulia wale wakubwa kama mfano wa namna ya kuishi. Inapotokea wale
wakubwa wametoka kwenye familia zenye desturi tofauti, inakuwa rahisi kwa wale
wadogo kuiga tabia zisizofaa.
Pia, katika baadhi ya shule yapo matukio ya
wanafunzi wakubwa kuwafanyia wadogo zao vitendo viovu. Wanatumia ukubwa wao
kuwanyanyasa watoto wadogo wasio na ubavu wa kuwakatalia.
Nilizungumza na mzazi
mmoja kujua kama kuna tabia zozote mwanae anayesoma bweni anazionesha. “Huyu wa
kwangu kwa kweli yuko vizuri. Sijaona shida kubwa. Lakini kuna hii tabia ya
matusi. Wakati anaondoka kwenda shule hakuwa na kawaida ya kutukana. Nimeona
akirudi anatukana wenzake.”
Uwezekano wa mtoto
kujifunza tabia mbaya zaidi ya hizi anazozitaja mzazi huyu ni mkubwa. Watoto wadogo
wanaotoka kwenye familia tofauti wanapochanganywa hujikuta hawana namna
nyingine zaidi ya kufundishana chochote kwa sababu hakuna mtu mzima anayefuatilia
kinachoendelea.
INAENDELEA
Thanks Nakuelewa sana KWA makala zako uzidi Kutumika kwa Jamii na Mungu akupe nguvu zaidi@stephen Mligo
JibuFutaThanks Nakuelewa sana KWA makala zako uzidi Kutumika kwa Jamii na Mungu akupe nguvu zaidi@stephen Mligo
JibuFutaBinafsi naona wazazi tunakwepa majukumu watoto wanatakiwa kulelewa na wazazi hadi walau wamalize darasa la 7 ndipo wajiunge na shule za bweni. Hapo kidogo mtoto anajielewa shule nyingi za bweni hazina uwezo wa kuwafuatilia watoto kwa karibu hasa pale wanapougua hata kugundulika ni kazi.
JibuFutaAsante sana kwa maoni mazuri. Shukrani kwa kuwa wadau muhimu wa blogu yetu.
JibuFuta