Kitabu Kipya cha Malezi na Makuzi
Malezi ya
sasa yamekumbwa na changamoto nyingi na kusababisha watu kushindwa kuwasaidia
watoto na vijana wao ili kufanikiwa. Mmomonyoko wa maadili umekuwa chanzo
kikubwa cha matatizo yanayomkumba kijana na jamii kwa ujumla. Matatizo hayo ni
kama vile ukosefu wa ajira, kushindwa kufikia ndoto za maisha, migogoro katika
familia, pamoja na watu kushindwa kuwa na utulivu na amani.
Kwa bahati
mbaya, masuala haya hayajapewa nafasi katika mijadala yetu. Na hata pale
yanapojadiliwa, uchambuzi wake umekuwa wa kijuu juu usiojaribu kutazama kiini
cha matatizo. Kadhalika, pamekuwa na uhaba wa maandishi yanayoweza kuchochea
mijadala inayolenga kutafuta ufumbuzi wa masuala haya mazito.
Mwalimu Joseph
Chikaka ameandika kitabu kinachoitwa “Watoto na Ndoto za Maisha.” Katika kitabu
hiki, mwandishi anachambua kwa kina malezi na makuzi ya mtoto yanayosababisha
tupate vijana, familia zilizo imara, na hatimaye, taifa lenye furaha. Anakupa
mbinu na ushauri wa kimalezi na kimakuzi zitazokuwezesha kupata jamii bora
yenye usawazo kiroho, kiakili (kimtazamo), kimwili (afya) na kijamii (mahusiano).
Pia, kitabu
hiki kinatoa mbinu na ushauri wa masuala ya msingi ya mzazi, mlezi na mwalimu
ya kuzingatia; ili kumsaidia mtoto, kijana na mtu yeyote kuweza kutimiza ndoto
zake. Jinsi gani mtu anaweza kutimiza ndoto zake kupitia watu wengine, jinsi gani
anadumu ama kupotea kwa njia ya kuelekea katika ndoto.
Mwandishi
anachambua kwa kina, jinsi ambavyo watoto huzaliwa na kukua kwenye familia
nyingi wakiwa na ndoto nyingi katika maisha yao ya baadae. Ndoto hizo huweza
kutimizwa au kushindwa kutokana na jinsi gani wazazi, walezi na serikali
zinaweza kusaidia. Aghalabu, wanakuwa na ndoto za kuwa wahandisi, wasanii,
walimu, kasisi/ mchungaji, wanasiasa, madaktari, wakulima wa kisasa au kuwa
fundi sanifu.
Kwa bahati
mbaya, ndoto hizi hazitimii watu wanapofikia umri wa ujana na utu uzima. Sababu
kubwa ni changamoto za maisha na ukosefu wa malezi na makuzi bora; ambazo
mwandishi ametoa suluhu yake kwa kina.
Vile vile,
amethibitisha kwamba, mafanikio ya mtu hayaji kwa bahati mbaya, bali
huandaliwa; na mafanikio ya kijana wa leo ni matokeo ya malezi na makuzi ya
utotoni.
Mwandishi ni
mwalimu mwandamizi katika shule ya Awali na Msingi ya Ignatius, Dodoma. Pia, amefundisha
shule mbalimbali hapa nchini. Ni mbobezi katika uandishi wa vitabu, makala,
ujasiriamali, unasihi na saikolojia. Pia, ni mtaalamu wa kuendesha mafunzo,
semina, kongamano na matamasha ya kitaaluma, michezo na stadi za maisha.
Kitabu hiki kinapatikana
kwenye duka la vitabu lililo karibu nawe kwa bei nafuu ya Tsh 15,000. Pia, unaweza
kupiga simu namba 0755 423 258, 0658 423 258 kwa mawasiliano zaidi.
Maoni
Chapisha Maoni