Upendeleo wa Wazazi Unavyoweza Kuchochea Uadui kwa Watoto
PICHA: Aim Lower Journal |
KUNA kisa kimoja kwenye
biblia kinachoweza kutufundisha jambo muhimu kama wazazi. Kisa chenyewe ni kile
cha Yusufu, mtoto wa mzee Yakobo, aliyejikuta kwenye mtafaruku mkubwa na ndugu zake. Ugomvi wa Yusufu na kaka zake
ulikuwa mkubwa kiasi kwamba kaka zake waliazimia kwa pamoja kumwuuza Misri kama
adhabu. Jambo la kuzingatia ni kwamba ugomvi huu wa Yusufu na ndugu zake
haukutokea kwa bahati mbaya. Chanzo cha yote hayo ni upendeleo.
Mzee Yakobo aliyekuwa na
watoto 12 alimpenda zaidi Yusufu na kuonesha kumpendelea waziwazi. Kwa mfano,
tunaambiwa Yakobo alimshonea kanzu nzuri kijana wake huyo Yusufu. Pia, wakati
wenzake wakiungua jua wakichunga porini, Yusufu alitulia nyumbani na wazazi. Huu
ulikuwa ni upendeleo wa wazi.
Inawezekana mzee Yakobo
alikuwa na nia njema na hakukusudia kuchochea ghasia kwenye familia. Lakini matokeo
ya nia hiyo njema yalikuwa ni kujenga ufa mkubwa kati ya Yusufu kipenzi chake na
kaka zake waliojiona hawana nafasi kwenye familia hiyo. Upendo wa mzee
ulimgharimu Yusufu na alichukiwa vikali na kaka zake. Chuki ilifanya iwe vigumu kwa Yusufu
kuzungumza na kaka zake. Mwisho wake, tunaambiwa, ilipojitokeza fursa ya
kulipiza kisasi, ndugu zake wakawa tayari kumwuua.
Hali kama hii hutokea
hata leo. Wapo wazazi, ambao bila kujua, wana tabia ya kuonesha upendeleo kwa
watoto. Kwa sababu tu mtoto fulani anafanya vizuri na kukidhi matarajio ya
mzazi, basi anapendwa kuliko wengine. Kwa wazazi wengi wa siku hizi, ni wazi
mtoto anayefaulu darasani, asiyemsumbua mzazi, ndiye anayegeuka kuwa kipendi
cha wazazi. Ndivyo ilivyokuwa kwa Yakobo. Ingawa sababu kubwa ya kumpenda Yusufu
inayotajwa ni kuwa mtoto wa mke mdogo aliyependwa zaidi, pengine hata ndoto zake
kubwa, kuonekana anajitambua kuliko wenzake, ilimfanya mzee akampenda.
Wakati mtoto mwema
akipendwa na kila mmoja kwenye familia akishuhudia, anakuwepo mtoto anayekosea
na kushindwa kufikia matarajio ya wazazi, ambaye naye, anajikuta matatani. Wazazi
wanamchukia, wanaonesha dhahiri kwamba hawana muda naye, na wamemkatia tamaa. Wazazi
ndani yao wanafikiri kufanya hivi ni kumfundisha adabu huyu anayekosea ili
ajifunze kuwa mtoto mzuri.
Lakini matokeo yake huwa
ni kinyume. Mtoto asiyependwa na anayetengwa anajenga chuki na visasi vya ndani
kwa ndani dhidi ya wazazi wenyewe na mwenzake anayeonekana kuwa chaguo la
wazazi. Hali hii hutengeneza ufa mkubwa katika familia. Hapawezi kuwa na
ushirikiano na maelewano katika mazingira kama haya.
Visa kama hivi visiposhughulikiwa
mapema, huweza kuhamia kwenye vizazi vinavyofuata miaka mingi baada ya wazazi
kuondoka duniani. Kwa kutumia mfano wa Yakobo, tunaambiwa, naye pia alitokea
kwenye familia iliyokuwa na matatizo kama hayo. Baba yake aliyeitwa Isaka, alikuwa
na tatizo la ubaguzi kwenye familia yake. Alimpenda Esau na akawa tayari
kumbariki na kumtamkia maneno mazuri Esau kuliko Yakobo ambaye naye tunaambiwa alipendwa na mama
yake.
Hali hii, ilijenga ufa
mkubwa kwenye familia hiyo. Mbali na Yakobo kulazimika kutoroka familia baada
ya kufanya udanganyifu na kumzidi ujanja Esau, hatuoni ushahidi wowote wa
mawasiliano kati ya ndugu hawa wa tumbo moja. Miaka mingi baadae, ilibidi
ifanyike kazi kubwa kuhakikisha mahusiano yanarudi. Pamoja na hayo, tunaona, hata yeye Yakobo alipopata
familia yake, alirudia kufanya yale yale aliyoyaona yakifanywa na wazazi wake.
Tunajifunza hatari ya
kupalilia ubaguzi katika familia. Familia inayopalilia ubaguzi wa wazi wazi au
kificho huwa haikosi misuguano. Kwa kawaida, kunakuwa na makundi yasiyoaminiana
katika familia. Katika mazingira haya ya kutokuaminiana, ni vigumu wanafamilia kuwa
na ushirikiano na upendo kati yao.
Kuepusha matatizo kama
haya wazazi tunahitaji kujenga mazingira ya watoto kujisikia kutendewa kwa
usawa. Asiwepo mtoto anayejisikia kunyang’anywa haki yake na kupewa mwingine. Tunapowatendea
kwa haki na kuwafanya wajione kuwa sawa machoni pa wazazi wao, tunawafanya wawe
tayari kushirikiana.
Pengine unajiuliza,
nitajuaje kama familia yangu ina ushirikiano na kwamba hakuna mtoto
anayejisikia kutengwa na kutokutendewa haki? Hapa vipo viashiria kadhaa za familia yenye uhai. Moja,
ni hali ya watu kuaminiana. Kuaminiana maana yake kila mmoja anakuwa hana
wasiwasi na kile kinachosemwa au kufanywa na mwanafamilia mwingine. Wazazi wana
kazi ya kuhakikisha si tu wanatenda haki, lakini pia wanaaminika kwa maneno yao.
Lakini pili ni kuheshimiana.
Unaposema unamheshimu mtu maana yake unajali utu wake kama ambavyo nawe
ungependa watu wengine wakujali. Mzazi
asiyemheshimu mtoto, kwa mfano, ni mwepesi kumvunjia heshima pale anapokuwa ametenda
kinyume na matarajio yake. Unapomtolea mtoto maneno makali kwa sababu ya makosa
aliyoyafanya, unamfanya ajisikie kuvunjiwa heshima kama binadamu. Hali hii
huongeza ufa kati yako na mtoto.
Pia, kuwa na desturi ya
kufanya mambo kwa ushirikiano kunakuza uhai baina ya wanafamilia. Kwamba hakuna
anayejisikia kubaguliwa wala kukosewa heshima, inamfanya kila mmoja ajione
anawajibika kwa mwenzake. Kinyume chake ni ubinafsi wa kila mwanafamilia.
Familia yenye watu wanaofanya mambo bila kushirikiana haiwezi kuwa na uhai.
Kama wazazi tunaotambua
umuhimu wa familia kuwa pamoja, tuna kila sababu ya kuhakikisha tunawawekea
watoto mazingira ya kushirikiana kufanya mambo. Tuwape watoto kazi
zinazowalazimisha kusaidiana kufikia malengo ya pamoja. Kwa kufanya hivyo, tunajengea
kizazi kinachothamini ushirikiano katika kufanya mambo yake.
Chapisho hili limeondolewa na msimamizi wa blogu.
JibuFuta