Mambo ya Kutafakari Unapoanzisha Uhusiano wa Kimapenzi Kazini
PICHA: Shalinii Choudhary |
Sehemu
kubwa ya maisha yako kama mfanyakazi unaitumia kwenye eneo la kazi. Ingawa
inategemea na aina ya kazi unayoifanya, ni wazi muda mrefu kwa siku unaoutumia kutekeleza
majukumu yako unakuweka karibu zaidi na wafanyakazi wenzako kuliko hata familia
na marafiki. Mazingira haya ya ukaribu wa kikazi, wakati mwingine,
yanatengeneza uwezekano wa uhusiano wa kimapenzi baina ya wafanyakazi.
Kwa
kawaida, unapokuwa na mtu mnayefanya naye kitu kinachofanana kwa muda mwingi,
ni rahisi kuanza kuvutiwa naye. Kadri mnavyoonana mara kwa mara ndivyo mnavyozidi
kufahamiana kwa karibu. Hisia za mapenzi zinaweza kuzaliwa kama tahadhari
hazitachukuliwa.
Msomaji
mmoja ambaye hakujitambulisha jina lake aliniandikia
ujumbe mfupi wa maneno, ‘Mazingira yanayoweza kuanzisha mapenzi kazini, Da.
Nimeyasoma vizuri sana. Nahisi kama hayaepukiki hivi. Tatizo ni muda mwingi
watu wanakuwa pamoja katika kufanya kazi… Issue (suala) ya mapenzi katika
mazingira ya kazi haiepukiki. Hayo ndio mambo yetu sie vijana.’ Kwa vijana wengi wanaoanza
kazi, eneo la kazi linaweza kuwakutanisha na watu wanaoweza kuwa wapenzi wao.
Ni
dhahiri ofisi zinakutanisha watu wenye uelewa usiotofautiana sana, wenye mtindo
wa maisha usiotofautiana sana na hivyo kuongeza uwezekano wa mahusiano ya
karibu. Kukaa pamoja kwa muda mrefu pia inaweza kuwa fursa ya kumfahamu mtu
anayeweza kuwa mpenzi wako bila yeye kufahamu kama Mage (27) anavyofafanua.
‘Ukisema
nikwepe mapenzi kazini saa nyingine haiwezekani. Mimi karibu kila siku naondoka
nyumbani saa 12 asubuhi narudi usiku saa 2. Nitaonana wapi na watu wengine?’
Kwa
wafanyakazi wasiopata muda wa kukutana na watu wengine nje ya eneo la kazi kama
Mage, ofisi inaweza kuwa fursa ya mahusiano ya kudumu.
Ukaribu unaowatenga na wengine
Upo uwezekano
mkubwa wa ofisini kuwa eneo la ‘michepuko.’ Wanandoa wenye matatizo nyumbani
wanaweza kutumia ukaribu wa ofisi kujiliwaza kama anavyosimulia Khalid, ‘Kazi
zinawezesha michepuko. Unakuta mtu ana mafrustration (matatizo) yake nyumbani. Hapa
kazini anakutana na watu wajanja wanaomjali na kumsikiliza kuliko mke wake
nyumbani, kuchepuka ni dakika.’
Vyovyote
iwavyo, unapokuwa na mpenzi kwenye eneo la kazi, ni vigumu kuficha. Ingawa
inategemea na ukomavu wenu, ni suala la muda tu kabla hamjaanza kuonekana karibu
kuliko ilivyo kawaida. Tetesi zitakapoanza kuenea kwamba ‘mnatoka’ hamtazifurahia
na zinaweza kutengeneza ufa baina yenu na wafanyakazi wenzenu.
Pia, wafanyakazi
wenzenu kwa kutambua mapenzi yenu wanaweza kuanza kuwapa nafasi ya kuwa na
faragha yenu wenyewe. Hali hii mtaitafsiri kama kutengwa na kuonewa wivu. Katika mazingira kama haya, ni rahisi uhusiano wenu na wafanyakazi wengine
kuzorota.
Mgongano wa maslahi
Unapokuwa
na uhusiano na mfanyakazi mwenzako, unajiweka kwenye mitihani ya kiutendaji. Fikiria,
kwa mfano, mazingira ambayo mmoja wenu kati ya ninyi mlio wapenzi anawajibika
kwa mwenzake kikazi. Kibinadamu ni vigumu kuacha kukupendelea. Katika mazingira
ambayo wafanyakazi wengine wanashuhudia hilo likiendelea, sifa na maslahi ambayo
pengine mmoja wenu angestahili kwa haki, yanaweza kuibua maneno yatakayowaudhi.
Kwa
upande mwingine, aliye chini ya mwenzake naye anaweza kuanza kuwa mzembe kazini
akiamini mpenzi wake ambaye ndiye bosi atamlinda. Hali kama hii inaweza kuibua
changamoto kubwa ya kiutendaji. Mkubwa ataanza kujisikia kudharaulika, na aliye
chini ataanza kujisikia hatendewi haki pale atakapokosa kile anachokihitaji.
Inapotokea mmeachana
Tunajua mapenzi
yana nyakati zake ngumu pia. Si mara zote unapoanzisha uhusiano na mtu basi
maana yake mnaweza kuendelea kuwa wapenzi kwa muda mrefu. Inawezekana
mkashindwa kuelewana kwa sababu moja au nyingine na mkaamua kuachana.
Ugomvi wa
mapenzi mara nyingi hufanya watu waliokuwa wapenzi wasiendelee kuwa marafiki.
Fikiria namna utakavyoendelea kufanya kazi katika mazingira kama haya.
Unapofanya kazi na mtu ambaye alikufahamu kwa karibu sana na baadae mkaachana
vibaya huwezi kuwa na ujasiri.
Hali hii
inaweza kusababisha kuzorota kwa kazi zako, utoro kazini na hata kuchukia kazi
bila sababu za msingi. Kinachosababisha yote haya ni kuanza kuyahusisha
mazingira ya kazi na mazingira ya ugomvi wenu wa kimapenzi. Katika mazingira
kama haya, ni rahisi kupoteza utoshelevu kazini.
Unaweza
kupoteza kazi
Mbali na
kuathiri mawasiliano yako na wafanyakazi wenzako, mapenzi kazini yanaweza
kukuingiza kwenye matatizo. Kumbuka kwamba maisha ya ofisini hayatoshi kumfahamu
mtu. Unayefikiri anatafuta mwenza inawezekana ameacha familia nyumbani. Uhusiano
wa namna hii unaweza usiwe na mwisho mzuri.
Janeth
Urio, Mhadhiri wa Sheria Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge anaonya mazingira
hatarishi yanayoweza kugharimu mtu kazi. ‘Mahusiano ya kimapenzi kazini
yanaweza kuwa na athari kwa mwajiriwa pale atakaposhindwa kutekeleza majukumu
yake ipasavyo. Katika mazingira ya namna hiyo, kwa mujibu wa Sheria ya
Mahusiano Kazini namba 6 ya 2004, mwajiriwa anaweza kujikuta akipoteza kazi kwa
sababu ya utendaji usioridhisha.’
Chukua
tahadhari
Mkurugenzi
wa Raslimali Watu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Fr. Adalbert Donge
anatoa tahadhari. ‘Eneo la
kazi linapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa. Mahusiano ya kimapenzi kazini si
mahali pake. Mahusiano yanayoruhusiwa kazini ni yale ya kuheshimiana na
kusaidiana ili kuboresha utendaji kazi,’ anasema na kisha kutoa ushauri kwa
waajiri.
‘Mahusiano mengi ya muda mrefu
ikiwemo maisha ya ndoa msingi wake unaweza kuwa maeneo ya kazi. Ili kuwa na tahadhari
na heshima katika suala la mapenzi kazini waajiri wanashauriwa kuwa na miongozo
ili kulinda heshima ya ajira na malengo yake.’
Mapenzi
ofisini yanaweza kuzaa uhusiano wa kudumu ikiwa hayataharibu kazi na tahadhari
za msingi zikichukuliwa. Kupima faida na hasara kabla haujaanzisha uhusiano wa
kimapenzi ofisini ni jambo la busara.
Maoni
Chapisha Maoni