Kwa nini Wazazi Huwapeleka Watoto Wadogo Shule za Bweni?

PICHA: The Citizen

Miaka kadhaa iliyopita, wakati huo nikiwa mwanafunzi, nilishangazwa kusikia mtoto wa ndugu yangu, wakati huo akiwa na miaka sita, alikuwa anasoma shule ya bweni. Sikufikiri jambo hilo lingewezekana.
                                                                                   
Nakumbuka mara yangu ya kwanza kwenda shule ya bweni nilikuwa na umri wa miaka 17 nikisoma kidato cha 5. Kwa kuwa haikuwa rahisi kwangu kuzoea maisha ya mbali na nyumbani, nilishindwa kuelewa inawezekanaje mzazi kumpeleka mtoto mdogo kiasi hicho kwenda shule ya bweni.

Huu ulikuwa mwanzo wa safari yangu ya kujaribu kulielewa jambo hili. Ingawa sikupata takwimu rasmi za idadi kamili ya shule za msingi za bweni kipindi hicho, niliamua kufanya uchunguzi mdogo jijini Dar es Salaam kuzitambua shule zinazotoa huduma ya bweni kwa watoto wadogo.

Idadi ilinishangaza kidogo. Kumbe kilichokuwa kigeni kwangu, kwa hakika hakikuwa ajabu kwa wazazi wengi jijini Dar es Salaam. Nilikuwa nimeachwa nyuma na maendeleo. Hapo ndipo nilipopata wazo la kufanya utafiti kama sehemu ya tunuku ya kitaaluma ya Shahada ya Umahiri ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 

Takwimu zinasemaje?

Takwimu rasmi ya idadi ya watoto wanaosoma shule za msingi za bweni hazipatikani. Hata hivyo, kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, mwaka 2012 jumla ya shule za msingi 684 zenye huduma ya bweni zilikuwa zinapatikana kwenye mikoa yote ya Tanzania bara isipokuwa Lindi. Mikoa inayoongoza kwa idadi kubwa ni Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro na Mwanza.

Kwa kuwaida shule hizi zinazofahamika kama English Medium, kwa maana ya shule zinazotumia Kiingereza kama lugha rasmi ya kufundishia, zina na makundi mawili ya watoto. Wapo wale wa kutwa wanaorudi nyumbani baada ya muda masomo. Kundi la pili ni wale wanaosoma kwa mfumo wa bweni.

Tunapozungumzia shule za msingi za bweni, kimsingi, tunazungumzia shule zinazopokea watoto wadogo kuanzia miaka mitatu, ambao hutengwa na familia zao kwa muda fulani kwa lengo la kuwapatia elimu inayokwenda sambamba na malezi.

Mtoto anayesoma kwenye shule za bweni, kwa kawaida, hukabidhiwa kwa mamlaka za shule husika na hukaa mbali na familia yake kwa muda unaoweza kufikia na hata kuzidi miezi saba kwa mwaka. Katika kipindi chote hiki, mtoto huishi na watoto wenzake shuleni chini ya uangalizi wa walezi na walimu. Wazazi na ndugu wanaotambuliwa na uongozi wa shule ya bweni huruhusiwa kumtembelea.

Nchi mbalimbali, ikiwemo Rwanda, zimepiga marufuku shule hizi. Hapa nchini, mwaka 2015, serikali kupitia Wizara ya Elimu iliwatahadharisha wazazijuu ya hatari ya kuwawahisha watoto kusoma kwenye shule za bweni. Hata baada ya tahadhari hiyo, bado wimbi la wazazi kuwapeleka watoto wao kusoma shule za bweni linaendelea kuwa kubwa. Je, kuna msukumo gani nyuma ya maamuzi hayo?

Matarajio ya wazazi

Charles Mwanri* mkazi wa Moshi anaamini shule ya bweni inamsaidia mwanae kupata muda wa kutosha kuzingatia masomo ya darasa la kwanza.
“Nilimpeleka boarding (bweni) kumwondolea usumbufu. Hapa nyumbani hakuwa anapata muda wa kutosha kutulia na kufuatilia masomo. Shuleni anazuiwa kuangalia televisheni, hakuna michezo kwa hiyo ni rahisi kufaulu kuliko akibaki hapa nyumbani.”

Nakumbuka juzi nilizungumza na jirani yangu hapa nyumbani ambaye naye amewapeleka watoto wake wote wawili wa kike kusoma shule msingi ya bweni. Maelezo yake hayatofautiani na hayo. Haoni uwezekano wa ‘watoto wa siku hizi’ kufanikiwa wakiachwa kwenye mazingira ya nyumbani ambayo, kwa maoni yake, hayamshawishi kujifunza.

“Huyu mkubwa (wa darasa la 4) alianza (bweni) akiwa darasa la pili. Amebadilika sana. Performance (ufaulu) yake imepanda na anafanya vizuri. Ukiangalia utaona [nyumbani] hakuwa anapata mazingira yanayomhamasisha kusoma.”

Changamoto za kifamilia

Robert Seuri* mwenye mtoto wa miaka 7 anayesoma nchini Kenya anataja sababu tofauti. “Sipendi kukaa mbali na mtoto. Nililazimika tu. Tulitofautiana na mke wangu na tukafikia kutengana. Sikutaka kabisa watoto wakae na mama yao awapandikizie mambo anayoyataka yeye. Ilibidi nifanye nisichotaka,” anaeleza.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake (WLAC), mwaka 2012 pekee kituo hicho kilipokea migogoro 6,780 na mingi ikihusisha matatizo ya ndoa katika maeneo ya Dar es Salaam, Kasulu na Muleba pekee. Katika mazingira kama haya, ya wazazi kutokuelewana, ni wazi kwamba wazazi wenye uwezo huamua kumlinda mtoto na mitafaruku isiyomhusu kwa kumpeleka shule ya bweni.

Sambamba na migogoro ya ndoa, yapo mazingira ya kazi yanayowafanya wazazi washindwe kuwa karibu na watoto wao kama anavyosimulia Elizabeth*:

“Mwanzo nilikuwa nakaa na housegirl (msichana wa kazi) amwangalie mtoto. Tulienda vizuri tu lakini baadae kazi zikawa nyingi nikawa situlii nyumbani kabisa. Ikawa nikisafiri muda mrefu kikazi nakosa amani na usalama wa mtoto. Baadae niliona nafuu mtoto aende bweni niwe na amani.’

Kiashiria cha maendeleo?

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Maria Margaret nje kidogo ya mji wa Moshi aliongeza sababu nyingine. “Tuna watoto wengi wazazi wao wanaishi maeneo ya jirani na hapa (Mabogini). Wengi mama zao hawana ajira za kusema hawakai nyumbani. Nafikiri ni kama fasheni…ukiwa na uwezo basi mtoto akisoma shule unayolipa ghali zaidi inakufanya uheshimike,” anaeleza.

“Nakubaliana kwa sehemu wapo wazazi hawana muda. Hapa huwa tukifunga shule wiki moja tu mzazi anaanza kupiga simu kuulizia shule inafunguliwa lini. Ukimwambia bado anaulizia kama kuna tuition (masomo ya ziada) amlete.”

Pamoja na sababu nyingine zaidi ya hizo, ni muhimu wazazi kujiuliza ikiwa shule za bweni zinaweza kuwawekea watoto mazingira ya kimalezi yanayowawezesha kukua na kujifunza bila kupata matatizo. Ili kuwasaidia wazazi kufanya maamuzi yanayoongozwa na uelewa, juma lijalo tutaangazia matokeo ya tafiti mbalimbali.


Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?