Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia

Katika makala yaliyopita, tuliangalia matukio muhimu ya kimakuzi katika maeneo mawili makubwa ya ukuaji wa mtoto nayo ni 1) kimwili na 2) kiakili. Katika sehemu hii ya pili, tunasaili ukuaji wa kimahusiano na kihisia ili kutazama yabia zinazojitokeza pasipo kuathiriwa na malezi na haiba ya wazazi. Kwa lugha nyingine, haya ni matarajio ya mtoto yanayoendana na umri wake bila kuingiliwa na matarajio na yanayofanywa na mzazi kwake.


Tabia za kimahusiano

Kimahusiano, kwa ujumla tunaweza kusema mtoto wa umri pungufu ya miaka mitatu hufurahia uwepo wa watu wengine ingawa lengo ni kunufaika yeye. Hii ni kwa sababu kubwa mbili, 1) uwezo wake wa kutambua wanachokihitaji na kukiona wengine bado ni mdogo, hivyo 2) anatumia mahusiano kama njia ya kupata mahitaji yake. Ndio kusema tunapohusiana na mtoto huyu, kihalisia twapaswa kufikiri zaidi anachokihitaji yeye kuliko matarajio yetu kwake.

Tangu anapozaliwa, mtoto huonesha shauku ya mawasiliano na watu wanaomnufaisha. Uhusiano wa kwanza unaanza na mama yake kwa sababu ndiye anayemaliza njaa yake na ndiye anayemsikiliza zaidi ya watu wengine. Upo ushahidi wa kiutafiti unaothibitisha kwamba watoto huvutiwa zaidi na nyuso za watu kuliko vitu vingine. Maana yake ni kwamba tunazaliwa na hitaji la kuhusiana na watu kuliko vitu.

Mpaka anapofikisha miezi sita, mtoto huwa na uwezo wa kuhusiana na wanaomzunguka kwa kutabasamu, kucheka na vitendo. Akiwa na miezi minne tu, kwa mfano, mtoto huwa na uwezo wa kumtofautisha mama na watu wengine. Anaweza kucheka kama matokeo ya kuchekeshwa, kufurahishwa au hata kuiga wanaocheka.

Kwa kawaida, kabla ya miezi sita kuisha mtoto huwa hana aibu. Lakini anapofikisha mwaka mmoja, kwa kule kuanza kupambanua tofauti ya wenyeji na wageni, mtoto huanza kujenga hisia za aibu hasa kwa wageni. Wakati huo huo, huanza kujenga uwezo mzuri wa kusoma hisia za watu wengine na hivyo huwa na shauku kubwa ya kuonekana kwa watu wake wa muhimu.

Kuanzia mwezi wa 12 na 18, huanza kujitambua kwa kujitofautisha na wengine. Huelewa tofauti ya ‘mimi’ na ‘wewe’ na hunza kuitika akiitwa kwa jina lake. Anapojitazama kwenye kioo, hujigundua na kufurahia anachokiona. Hapa ndipo anapojifunza kumiliki kwa kuelewa maana halisi ya ‘yangu’, ‘vyangu’, ‘changu’. ‘mimi’ na ‘wewe’. Katika kipindi hiki, wazazi huweza kushindwa kuelewa kwa nini mtoto anaweza kuwa mgumu kumpa mwenzake kile alichonacho. Huu, hata hivyo, si uchoyo bali ni hatua ya kukua inayomsaidia kujua kumiliki vile anavyojua ni vyake.

Kadhalika, katika umri huu hawezi kucheza na watoto wengine kwa ushirikiano ingawa anaweza kucheza akiwa na watoto wengine. Sababu ni kwamba bado ana ‘ubinafsi’ wa kuyaona mambo kwa mtazamo wake mwenyewe na hawezi kuelewa mantiki ya kushirikiana na watu wengine. Lakini hata hivyo, huanza kupata tabu kutengana na mama/mlezi wake na hutamani kuambatana nae muda wote. Tunaambiwa ni shauri ya muunganiko wa karibu kabisa wa kihisia na mama yake, muunganiko ambao ndio huwa msingi wa namna anavyohusiana na watu wengine.  

Anapotimiza miaka miwili, anakuwa na uwezo wa kuanzisha michezo yake mwenyewe ingawa inabaki kuwa ile ile isiyobadilika.  Hana uwezo wa kushirikiana vizuri na wenzake katika michezo isipokuwa kama mazingira anayoishi yanamkutanisha na watoto wenzake. Kadhalika hana uwezo wa kusubiri na akitaka kitu anakitaka dakika hiyo hiyo. Uwezo wa kucheza na wenzake huonekana anapotimiza miaka mitatu na kwa ujumla ndipo huanza kuzoeana na watoto wengine mbali na familia yake. Katika kipindi hiki, anaweza kuelekezwa jambo jepesi na akalielewa.

Tabia za kihisia

Kimsingi, mahusiano yake na wanaomzunguka yanategemea sana ukuaji wake wa hisia.  Kadri anavyoweza kutambua na kumudu hisia zake sambamba na kuzisoma hisia za wengine ndivyo anavyokuwa na uwezo wa kuhusiana na watu wengine. Kwa ujumla, katika kipindi cha miaka mitatu ya mwanzo, lugha kuu ya kuonesha hisia zake ni kulia. Analia kusema ana njaa, ana maumivu, haridhiki, ameona kitu kisicho cha kawaida na kadhalika. Hiyo ni kusema kwamba kulia si lazima kuwa na maana ya uchungu na hasira bali namna bora zaidi ya kuwasiliana na wanaomzunguka.

Tangu anapozaliwa, hisia zozote anazokuwa nazo mtoto ni matokeo ya anachokifanya mama au mlezi wake wa karibu.  Kwa mfano, katika mwaka wa kwanza, ingawa mtoto huwa na uwezo wa asili wa kusoma hisia za wengine tangu anapozaliwa, bado kutabasamu, kulia, wasiwasi, na hata kucheka hutegemea kwa kiasi kikubwa mwitikio wa mzazi kwa mahitaji yake. Sababu ni kwamba bado mtoto huwa hana uwezo wa kumudu hisia zake yeye mwenyewe pasipo msaada wa wengine.

Anapoelekea mwezi wa 18, mtoto huanza kuelewa mahitaji ya wengine na kuanza kujaribu kuwapa wengine vile anavyofikiri ni mali yake. Hata hivyo, hiyo hutegemea yale anayoyaona kwa wanaomzunguka. Kwa sababu ya kushindwa kuelewa wengine wanataka nini, hupenda kuwa huru na kujitegemea na ndio maana katika umri pungufu ya miaka miwili hawezi bado kufuata maelekezo rasmi yanayotolewa na watu wazima ingawa ni kweli anaanza kuelewa hisia zao.

Shauri ya shauku ya kutaka kufanya mambo hushika kasi anapofikia mwaka wa pili. Anatamani kufanya yanayofanywa na watu wazima wanaomzunguka.  Hukasirika sana hususani pale anaposhindwa kufanya anachotaka kukifanya. Huanza kutumia lugha kama namna moja wapo ya kudhibiti hisia zake na hivyo kulia-lia huanza kupungua. Lugha humpunguzia udhaifu wa kuwasiliana kwa kulia zaidi.

Baada ya kutimiza miaka miwili, mtoto huanza kuelewa matokeo ya tabia fulani fulani anazozifanya yeye au wanazozifanya wengine, uwezo ambao huimarika anapoelekea mwaka wa watu. Mathalani, huweza kuelewa kwa vipi alichokifanya kimemfanya mama akasirike au afurahi. Kinachomsaidia kujua matokeo ya tabia yake ni matokeo. Kusifiwa, kuzawadiwa, kufurahiwa, humaanisha kilichofanywa ni sahihi. Kukemewa, uso wa hasira, kunyimwa anachokihitaji na adhabu nyingine zina maana ya kilichofanywa hakikuwa sahihi.

Hitaji lake kuu anapofikia miaka mitatu ni kuwaridhisha wazazi wake ingawa lengo hasa ni kupata fursa ya kusifiwa na kuonewa huruma. Katika kipindi hiki, kwa ujumla, mtoto huanza kuwa na uwezo wa kujisikia aibu, fedheha na fahari kwa kupima mwitikio wa matarajio ya wazazi na wengine kwa kile alichokifanya.

Katika kuhitimisha, tunaweza kusema, mtoto wa umri wa kati ya siku moja na miaka mitatu, anao uwezo mkubwa kama mtu mwingine yeyote ingawa uwezo huo unamsaidia kutambua mambo kwa namna tofauti na watu wenye umri mkubwa. Kwa mfano, kama tulivyoona, katika umri wa miaka mitatu, kiakili mtoto anafikiri kwa kutegemea anayoyaona kwenye mazingira yake na hana uwezo mzuri wa kuelewa mambo ya kufikirika. Kihisia, anatumia hisia zake kuwasiliana na wengine ingawa hajaweza kuzimudu bado. Hali hii humfanya ashindwe kuelewa wengine wanafikiri nini na wanahisia gani. Kimahusiano, watu wa maana ni wale wanaomnufaisha kwa namna yoyote ile iwe kwa kumsifia, kumlinda na kadhalika.

Katika makala inayofuata, tutajadili namna malezi ya mtoto huyu tuliyemwona hapa yanavyoweza kuathiri haiba yake.

Inaendelea

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Pay $900? I quit blogging

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini