Uhusiano wa haiba ya mzazi na malezi ya watoto – 1

Katika mfululizo huu tunatarajia kujadili mahitaji ya kimahusiano ya mtoto mwenye umri usiozidi miaka 20 kwa vipengele kadhaa. Katika kufanya hivyo, tunajikita kwenye uhusiano wa moja kwa moja ulipo kati ya haiba ya wazazi na namna haiba hiyo inavyoweza kuathiri vile tunavyolea watoto wetu. Tutaona namna malezi hayo yanavyoathiri tabia na mwenendo wa watoto tangu wanavyozaliwa mpaka wanapofikia umri wa kujitegemea. Tutaonesha kwamba kwa kiasi kikubwa tabia tunazoziona kwetu si za kuzaliwa na wala hazitokei kwa bahati mbaya. Ni matokeo ya haiba na mahusiano yenu na wazazi waliotulea.

Haya si mambo mepesi yanayofurahisha sana nafsi ya msomaji anayependa kuwa ‘inspired’. Katika kusoma maandishi haya unaweza kujikuta ukijisikia hatia hapa na pale lakini habari njema ni kwamba hatia hiyo, hata hivyo, inakusudiwa kuwa kichocheo cha tafakuri ya kuboresha mahusiano na watoto. 

Watoto kutengwa na wazazi
Tafiti za uhusiano wa wazazi na tabia za watoto zilianza kufanyika katika kipindi cha vita ya pili ya dunia. Wataalam wa malezi na makuzi ya mtoto walitafuta kuchunguza athari za kitabia zilizowakumba watoto waliokuwa wametengwa na wazazi wao kwa miaka kadhaa katika kipindi cha vita. Hawa ni watoto waliojulikana kama ‘mayatima wa vita’ kwa sababu walikuwa na wazazi ambao hata hivyo hawakuwepo karibu kwa kipindi fulani. 

Matokeo yake yalionesha kwamba watoto hawa waliotengwa na wazazi shauri ya vita walianza kuonekana kuwa na matatizo kadha wa kadha ya kihaiba/kitabia ambayo kwa kweli yalihusishwa na uchungu wa  ‘kupoteza’ wazazi mapema. Kadhalika, matatizo haya ya kihaiba yaliathiri uelewa wao pamoja na hali ya afya. Ikawa wazi kwamba mahusiano na wazazi ndio msingi mkuu wa makuzi ya mtoto.
Furaha ya watoto hutegemea uhusiano wazazi wao. Picha: ruthostrow.com

Baadae tafiti ziliendelea kupanuka na kuchunguza watoto wengine wanaotengwa na wazazi wao kwa sababu nyinginezo zaidi ya vita. Hapa tunazungumzia mzazi kuwa mbali na mtoto kwa sababu nyingine kama kazi, kuhama na kulazimika kumwacha mtoto mahali pengine zaidi ya kule aliko yeye. Hatimaye ikaanza kuwa wazi kwamba watoto wadogo wanaotengwa na wazazi wao kwa sababu yoyote ile hujikuta wakipitia misukosuko mikubwa ya kihaiba inayotokana na hofu ya kupoteza upendo wa wazazi. 


Ikafahamika kwamba watoto hawa baada ya kuchoshwa na maombolezo kwa kipindi fulani ambayo hayakufanikiwa kumrejesha mzazi wanayemhitaji, walianza kukabiliana na hali ya kukata tamaa kwa kujifariji na kujilinda binafsi.  Kwa hivyo, watoto wakajenga hali tunayoweza kuiita ‘kumpotezea’ mzazi husika kwa kuvunja mahusiano kisaikolojia. Hapa tuna maana ya mtoto kumwondoa mzazi kichwani ili isiwe tabu. Na ilipotokea mzazi huyo alirejea na kukutana na mtoto huyo ambaye tayari alishakamilisha zoezi la kumfuta mzazi kichwani mwake, mtoto alionesha hasira kwa kulia, kumkataa mzazi, kugoma kukuhusiana tena au kumganda mzazi kwa hofu ya kuachwa.

Kuwepo kimwili au kihisia?
Kwa hiyo ikawa wazi kwamba hitaji la kwanza na la msingi la mtoto tangu anapozaliwa ni uwepo wa mzazi. Uwepo huu ndio unaojenga msingi wa haiba/tabia mtoto ambayo huongoza namna anavyohusiana na wazazi wake na watu wengine wote. Mpaka hapa ikaanza kuwa wazi kwamba ili mtoto awe na mahusiano mazuri na wazazi wake, kwa kweli anahitaji uhusiano wa karibu sana na endelevu na wazazi hao tangu anapozaliwa.

Aidha, yalianza kujitokeza maswali kuhoji ikiwa kuwepo kimwili kwa mzazi kunatosha kumfanya mtoto ajisikie salama. Tafiti zaidi zikaonesha kuwa si kweli kwamba uwepo wa mzazi kimwili unatosha. Ikaonekana mtoto anahitaji uwepo wa mzazi kihisia na huu ndio uwepo halisi ambao lengo lake ni kutambua na kujibu mahitaji ya mtoto kwa wakati. Hiyo ikiwa na maana kuwepo kwa mzazi asiyejibu matakwa ya mtoto kuna madhara sawa sawa na mtoto mwenye mzazi asiyekuwepo kimwili kama tutakavyoona hatua kwa hatua.

Ikumbukwe kuwa uwepo huu unahitajika katika kipindi cha mwanzo kabisa cha maisha ya mtoto ambacho ndicho kinachojenga tarijiba ya sura ya maisha ya mtoto huko mbeleni. Ndicho kipindi ambacho tafiti zinasisitiza kwamba mazingira ya nyumbani yanamsadia kuamini kuwa mzazi/mlezi yupo kimwili na kisaikolojia na kwamba anaweza kutegemewa. Kutegemewa hapa ndio msingi mkuu wa uwekezaji katika malezi. Mafanikio ya kutegemewa huko ni mtoto kufikia kuaamini kwamba mzazi anaweza kukosekana kwa muda, lakini bado uwepo wake ukahisiwa akili mwa mtoto. Mzazi halazimiki kuwepo muda wote ili kumfanya mtoto amwamini. 

Mzazi kama msingi wa tabia ya mtoto
Tafiti hizi zilizochunguza matokeo/athari za mazingira ya kimalezi katika ukuaji wa mtoto ndizo zilizokuja kujenga nadharia zilizoeleza asili ya haiba na mienendo ya mtoto kama matokeo ya mahusiano yake na mzazi/mlezi. Hizo ndizo tutakazozieleza katika makala hizi.

Kwa ufupi, tunaweza kusema mambo mawili kwa kutumia matokeo ya tafiti hizo. Kwanza, mahusiano ya mzazi na mtoto ndiyo yanayoamua mahusiano ya mtoto na watu wengine. Mahusiano na mzazi ndiyo yanayoamua namna mtoto huyu atakavyojitazama yeye mwenyewe na atakavyowatazama watu wengine akiwamo mzazi wake kadri anavyokua.

Jambo la pili ni matokeo ya umbali -kimwili na kihisia- unaotokea katika kipindi cha awali kabisa cha maisha ya mtoto, unaoweza kujenga hitilafu za kitabia kwa mtoto ambazo kimsingi ndizo zinazomsaidia mtoto kujihami na kujisikia vibaya. Kwa lugha nyingine, matatizo ya kitabia yanayokuja kujitokeza kadri mtoto anavyokuwa, ni jitihada anazofanya mtoto -bila yeye kujua- ili kukabiliana na umbali wa kihisia unaotengenezwa na mzazi.

Kwa kutambua matokeo ya tafiti nyingi yanayoonesha nafasi kubwa ya mahusiano ya mzazi na mtoto katika kujenga uelewa wa mtoto na afya ya mwili, makala hizi zitajikita katika kubainisha namna mahusiano hayo yanavyoathiriwa na haiba ya mzazi kuanzia dakika ya kwanza mtoto anavyozaliwa. Katika makala inayofuata, tutajadili malezi ya mtoto katika umri wa kuanzia anapozaliwa, mpaka miaka mitatu.

Inaendelea

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Pay $900? I quit blogging

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini