Uhusiano wa haiba ya mzazi na malezi ya watoto – 2

Wakati tunajiandaa kuangalia kwa kina malezi ya watoto wenye umri wa miaka 0 – 3 kama tulivyoahidi, na kuona namna watoto hawa wanavyoweza kuathiriwa na malezi wanayoyapata, ni vizuri tutazame japo kwa ufupi haiba kuu nne za wazazi zinazoweza kuathiri sana malezi ya watoto.

Haiba hizi ni mkusanyiko wa matokeo ya watafiti wengi wa mahusiano ya watoto na wazazi. Ingawa zimegawanywa katika makundi manne ya kitabia na kihulka, kiuhalisia kila kundi lina pande mbili, chanya na hasi na hivyo kufanya katika mazingira halisi ziwepo haiba nane. Chanya zina matokeo mazuri kwa mtoto, wakati mkusanyiko wa hasi una matokeo mabaya katika mahusiano ya mtoto na mzazi wake. Wingi wa hasi unamaanisha ukubwa wa tatizo kama tutakavyogusia kwenye aya tatu za mwisho.

Kwa muhtasari kabisa, haiba chanya nne zinalenga kumchangamsha na kumsisimua mtoto na hivyo kumfanya ajisikie kuwa karibu na mzazi na watu wengine wanaomzunguka. Kwa upande mwingine, mchanganyiko wowote wa tabia hasi matokeo yake ni kumfanya mtoto ajenge tabia za kujihami na maumivu ya kujisikia kupuuzwa kama tutakavyoona kadri tunavyooendelea.
 
Kutambua/kutokutambua mahitaji mahsusi ya mtoto
Hapa tunazungumzia uwezo/utashi wa ‘kuyasoma’ na kuyaelewa yale anayoyahitaji mtoto na kuyajibu ipasavyo. Ni ule umakini wa kujua mtoto anataka nini na kwa wakati gani. Mfano kutofautisha ni wakati gani mtoto hulia shauri ya njaa, maumivu, hasira au kusikilizwa.

Mzazi mwenye uwezo huu anatofautisha ishara zinazomaanisha furaha, kujisikia vibaya, wasi wasi, mashaka na kadhalika. Hata pale mtoto anapoonesha ‘ishara mbaya’ kama kulia, mzazi 'mtambuzi' hapuuzi wala kukasirika bali huvutwa kwenda kwa mtoto ili kujua yanayomsibu. Hali hii hujenga mahusiano imara kwani mtoto hujenga tumaini lake kwa mzazi anayevutika kwake kwa mazingira yoyote.

Kutambua anachokihitaji mtoto kina athari kubwa moja. Humfanya mtoto aamini anaweza kuashiria jambo na jambo na likatokea hivyo hujiona ana uwezo fulani wa kusababisha mambo yafanyike. Huanza kujiona anaweza kusababisha mambo kadhaa kwenye mahusiano yake na watu wa karibu na kuanza kujiona kuwa sehemu ya maisha ya familia na sauti yake inasikika.

Kinyume chake ni kutokutambua anachokihitaji mtoto kwa kushindwa ‘kusoma’ ishara zake au kuzipuuza. Mfano mtoto anaweza kulia kudai kusikilizwa, lakini mama akashindwa kuelewa maana yake na hata akielewa anatafsiri kuwa usubumbufu na hivyo kilio cha mtoto kinakosa mtu wa kukisikiliza.

Kadhalika, kutokutambua mahitaji ya mtoto yaweza kuwa ni kushughulika na mahitaji mengine ambayo kimsingi si yale anayoyahitaji mtoto mwenyewe. Ni pale mzazi anapofanya bidii kumhudumia mtoto kwa kutumia anachokifikiri yeye na sio anachokihitaji mtoto. Mfano ni kutaka kukaa na mtoto wakati ambao mtoto anahitaji kucheza na wenzake. Mzazi anaona kutumia muda na mwanae ni hitaji la mtoto, lakini kihalisia, si hitaji la mtoto kwa wakati huo maana anachokihitaji mtoto ni kuruka ruka na wenzake nje.

Matokeo ya kushindwa kutambua anachokihitaji mtoto humfanya akose imani na wanaomzunguka  kwa sababu wakati mwingi anachodai mtoto sicho kinachopatikana. Hisia za kujiona hana uwezo wa kuathiri vinavyomzunguka na kusababisha mambo yatokee huanza kujitokeza na kumnyong’onyeza.

Utayari wa kumpokea mtoto alivyo/kushindwa kumpokea mtoto
Ujio wa mtoto kwa kiasi kikubwa hubadilisha mtindo wa maisha wa mzazi. Kuanzia utaratibu wa kila siku, mwonekano na umbile la mwili (kwa mama), saa za kulala na kuamka, na hata tabia. Haya yote ni sehemu ya gharama za kukubali wajibu wa kuwa mzazi ambao huchukuliwa na watafiti wa malezi kama utayari wa mzazi wa kumpokea mtoto.

Kukubali kwamba sasa mambo yanaweza kubadilika kwa sababu ya ujio wa mtoto ndio kumpokea mtoto kwenyewe. Kuona kwamba mtoto ni wa thamani kuliko utaratibu wa maisha ya ujana bila kujali 'hasara' zinazotokana na kuwa mzazi. Vile vile, kumpokea mtoto kuna maana ya mtoto kupokelewa vile alivyo, bila kujali ikiwa ana jinsia isiyotarajiwa, rangi isiyo tarajiwa, tabia isiyotarajiwa na kadhalika. Kwamba hata kama mzazi alitarajia kuwa na mtoto wa kike, bado ajisikie vizuri inapotokea kuwa ana mtoto wa kiume kinyume na shauku yake. Kwamba hata mtoto anapoonesha tabia zisizotarajiwa, bado haoneshwi kukataliwa hata kama zipo jitihada za kumsaidia kubadilika.

Kinyume chake ni kukataa kubadilika shauri ya kuweka mbele mahitaji binafsi, mipango binafsi na mambo mengine binafsi yasiyo na uhusiano wa moja kwa moja na malezi. Kwa mfano, kuacha kumnyonyesha mtoto kwa muda unaoshauriwa na wataalam bila sababu yoyote ya msingi isipokuwa tu mama kuogopa kupoteza umbile la ubinti, ni kushindwa kukubali na kulipokea jukumu la uzazi. Matokeo yake huenda mbele zaidi ya kumnyima mtoto haki ya kukubaliwa kama tutakavyoona.

Kutokuwa tayari kumpokea mtoto ni pamoja na kuweka mahitaji yako kama mzazi mbele ya yale ya mtoto kwa kudhani unachokifikiri wewe ndicho sahihi hata kama hakijibu hitaji halisi la mtoto. Mfano mtoto anapoonesha wasiwasi katika mazingira fulani, mzazi asiyemkubali mtoto humlazimisha kukanusha hali halisi akidhani hiyo itamsaidia mtoto kupambana na wasiwasi alionao.
Kadhalika, kushindwa kumpokea mtoto ni pamoja na kuchoshwa na kile kinachoonekana kuwa msaada/madai ‘yanayopita kiasi’ aliyonayo mtoto  kiasi cha hata kukasirika na kulalamika kuhusu ‘kutokuridhika’ kwake. Mzazi anayemkataa mtoto, haishi kulalamika namna majukumu ya uzazi yalivyo magumu na ‘…namna watoto wa siku hizi wanavyosumbua …’

Utayari wa kushirikiana na mtoto/kukosa uvumilivu na kumwingilia mambo yake
Kwa asili, watoto huzaliwa wakipenda  kuwa na sauti inayosikika na kusababisha mambo yafanyike. Tangu anapozaliwa, mtoto huonekana akihitaji kuwasiliana na kuweka mazingira ya kuwaalika watu wanaomzunguka kuhusiana/kushirikiana/kumsikiliza. Hutumia ishara nyingi za mwili kama kichocheo cha kukaribisha mahusiano. Sababu ni kwamba mtoto angependa sana kushirikiana na wengine. Tunazaliwa tukiwa na hitaji la kushirikiana na wengine. Mazingira ndiyo hutufanya tuwe wabinafsi kama tutakavyoona.

Nini kimemsibu? Malezi au asili? Picha: worldnotobaccodayafrica.org/
Mzazi mwenye ushirikiano na mwanae, hutambua na kumpa nafasi mtoto kujitegemea kulingana na umri wake. Hapa hatumaanishi kumwaacha mtoto atende apendavyo, bali kumpa fursa ya kujisikia anaaminiwa na kuonesha uwezo wake bila kuingiliwa sana. 

Utayari wa kushirikiana na mtoto maana yake ni kutambua kuwa naye anayo mambo anayoyapenda kama binadamu mdogo na kwamba wajibu wa mzazi ni kumhakikisha usalama na kumwondolea uwezekano wa madhara. Kuaminiwa huku humsaidia sana kujiamini na kuwaamini wengine wanaomzunguka akianzia na wazazi wake.

Kinyume cha utayari wa kushirikiana naye ni tabia ya kushindwa kuvumilia uhuru wa mtoto kwa kumwingilia kupita kiasi na hivyo kumfanya ajione hana uwezo wa kufanya lolote yeye mwenyewe pasipo msaada wa mtu mwingine. Kumfanya mtoto ajione yeye ni mtekelezaji tu wa matakwa ya mzazi anayehakikisha kwamba kila anachokitaka yeye kinatendeka kwa mazingira yoyote ndio kukosa uvumilivu kwenyewe. Tabia hii ya kutaka kudhibiti maisha ya mtoto inaambatana sana na kukosekana kwa uwezo wa kutambua matakwa salama ya mtoto. Matokeo yake ni kunyong'onyeza uwezo wa kujiamini kwa mtoto.

Kupatikana anapohitajika/kumpuuza anapotuhitaji
Kama tulivyoona kwenye utangulizi, mtoto anahitaji sana mzazi apatikane kimwili na kihisia. Kupatikana maana yake ni kuwepo kwenye maisha ya mtoto. Ni kuwa na muda wa kutosha na mtoto ili kupata fursa ya kutambua uwezo wake, changamoto anazokabiliana nazo na mengineyo yanayomhusu. Haya yanawezekana tu pale mzazi anapokuwa na uwezo wa kuahirisha 'mambo mengine muhimu' kwa sababu ya malezi. Tunazungumzia kuyapa malezi kipaumbele.

Mzazi anapoacha majukumu ya kazi ili awahi nyumbani kumwona mtoto; mzazi anayeamua kufuta mpango wa kwenda masomoni mbali na nyumbani kwa sababu tu ana kichanga kinachohitaji uangalizi wa karibu; au hata kuamua kuacha kazi kwa muda kwa lengo la kupata nafasi ya kutosha kuwa karibu na mtoto; maana yake ni kuamua kupatikana katika maisha ya mtoto kunakokwenda sambamba na kupatikana kihisia kama tulivyoona kwenye utangulizi.

Kinyume chake, ni kuweka mbele shughuli nyingine kwa gharama ya malezi; kuchukulia malezi kirahisi rahisi kwa kudhani watu wengine kama babu na bibi wanaweza kutusaidia kubeba jukumu la malezi ili sisi tuweze kujikita kwenye 'mambo mengine ya maana' katika maisha. Ni kule kuamini mtoto anaweza kukua bila gharama ya kuahirisha mambo mengine yanayoonekana kuwa ya msingi. Huku ndio kupuuza wajibu.

Hata hivyo, inaeleweka kuwa maisha yana mengi. Wakati mwingine inalazimika kuwa mbali na mtoto tena kwa kipindi kirefu. Lakini pamoja na hayo, hilo linapotokea katika umri mdogo, yatupasa kupima ikiwa ni lazima kumwacha mtoto au kuacha mengineyo ili kumlinda mtoto na madhara yasiyokwepeka.

Ndio kusema, kuzamia kwenye harakati za maisha na kuacha suala la malezi mikononi mwa watu wengine ni sawa na kupuuzia malezi. Ndio kusema, ni kumtelekeza mtoto na kumfanya alipe gharama ya shauku ya mzazi kutafuta mambo mengine. Namna nyingine ya kumtelekeza mtoto ni kushughulika na mahitaji ya mtoto wakati ule tu tunapokuwa na nafasi ya kufanya hivyo, na si wakati mtoto anapohitaji. Hali hii yaweza kuathiri mahusiano ya mzazi na mtoto kama tutakavyoona kadri tunavyoendelea.

Matokeo kwa mtoto
Malezi anayoyapata mtoto yana athari kubwa mbili. Kwanza, yanaathiri namna anavyojiona yeye mwenyewe na pili, yanaathiri namna anavyowaona na kuhusiana na watu wengine. Mchanganyiko wa haiba nne za kimalezi kama tulivyoona hapo juu, unaweza kuzaa haiba kuu nne kwa mtoto.

Kwanza, ni mtoto kujiona anafaa/kujiamini na kadhalika kuwaona wengine kama watu wanaofaa na kuaminika. Huyu huwa na uwezo wa kuishi vizuri na watu. Vile vile,  yaweza kusababisha mtoto kujiona bora na mwenye uwezo lakini akidharau wengine kwa kuwaona si lolote na hawamsaidii. Huyu hatakuwa na muda na watu na anaweza kuwa aina ya watu wanaowatumia watu wengine kwa manufaa yao. 

Kadhalika, uwezekano wa tatu ni kujenga haiba ya mtoto anayejiona hafai na mwenye kujidharau, ingawa akiwaona wengine kama watu wenye thamani na kufaa kuliko yeye. Huyu atakuwa na matatizo ya kutojiamini na anaweza kuwa mhanga wa marafiki matapeli watakaotumia udhaifu wake kumlaghai.

Haiba ya nne, ni mtoto kutokujielewa na kujiona asiye na maana na kuwaona wengine kama watu wasio na maana kama yeye kwa maana ya  kutokuaminika na kuhitajika. Huyu ataathirika sana na misukuko suko ya dunia.

Katika makala inayofuata tutaanza kutazama watoto wenye umri wa katika ya miaka 0 – 3 ili kuona namna haiba kuu nne za mtoto tulizogusia hapa zinavyoumbika.

Inaendelea

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia