Miaka miwili ya Kuwa 'Mama' Ina Mafunzo Makubwa Kwangu...

Nilipoamua kuchukua uamuzi wa kubadilishana majukumu na mke wangu sikujua ni kwa jinsi gani uamuzi huo ungenibadilisha mimi na kunipa mtazamo mpya kabisa katika maisha. Baada ya kuzaliwa Baraka siku kama ya leo mwaka 2012 tuliamua kubadilishana majukumu ya familia; mimi nibaki na kuangalia watoto na kutunza nyumba na mahitaji yake yote na mke wangu aendelee kufanya kazi na kusaidia wakati wowote anaoweza.

Nimesema ‘kubadilisha’ na siyo kusaidia nikimaanisha kuwa yale ambayo katika jamii nyingi yanaonekana ni majukumu ya mama niliamua kuyafanya mimi. Mtoto wetu mkubwa Tony tayari alikuwa ameanza darasa la kwanza wakati huo na hivyo nilikuwa pia na jukumu la kumuandaa asubuhi, kumpeleka na kumchukua toka shuleni, kusimamia kazi zake za nyumbani, na kuhakikisha kuwa anakuwa tayari kwa siku nyingine ya shule. Mke wangu ni Muuguzi na anafanya kazi zamu ya usiku masaa kumi na mbili kwa siku, siku tatu za wiki.


Uamuzi huo ulikuwa mgumu na rahisi kwa wakati mmoja. Ulikuwa mgumu kwa sababu ilibidi niachane na kiburi na mitazamo yangu yote niliyolelewa nayo na kuchukua mitazamo ambayo hata hapa Marekani siyo ya kawaida sana kuiona. Niliamua kuwa Mr. Mom; mtoaji wa huduma zote za msingi kwa watoto yaani primary care giver.



Tangu anazaliwa hadi leo miaka miwili baadaye nimefanya majukumu yote ambayo kiasili (traditionally) yanachukuliwa ni ya kina mama. Kulala naye, kumwogesha, kumsafisha, kumlisha, n.k Na pia majukumu ya kusafisha nyumba, kupika, kulipa ankara mbalimbali n.k Wakati huo huo pia kuendelea na majukumu mengine ya kawaida ya ‘mwanamme’ kama kuhakikisha magari yetu yako katika hali nzuri yakifanyiwa matengenezo kwa wakati, kufanya matengenezo madogomadogo ndani.


Pamoja na hayo majukumu ya kawaida ya kusimamia nidhamu vile vile yameendelea kuwa ni ya kwangu. Mama watoto ukiondoa majukumu ya kazi na kuendelea kuingiza kipato kuweza kulisha watu wanne naye amekuwa na kazi ngumu vile vile. Wakati mwingine imempasa kufanya kazi kwa ziada (overtime) na kuchukua majukumu ya ndani wakati wowote ambapo nimejikuta niko hoi bin taabani kwa uchovu.


Miaka hii miwili basi imenifundisha mambo mengi sana ambayo hata nikiamua kuyaandika naweza kujaza kitabu. Nitaje machache tu.

Kwanza kabisa imenipa heshima na adabu ya pekee kabisa kwa kina mama. Wakati mwingine kama wanaume tunapoona mama anaweza kumnyamazisha mtoto akilia, kumsafisha, kuamka usiku kumhudumia, kupika na kusafisha bila hata kulalamika tunaweza kufikiria ni mambo yaliyo katika asili (nature) yao kama wanawake. Inawezekana hilo ni kweli, lakini kwa jinsi nilivyoona kwa mang’amuzi yangu mwenyewe yanafanywa haya yote kutokana na mapenzi kwa familia na watoto, kujali maslahi yao zaidi ya kitu kingine chochote na kujitolea hadi upeo.


Mtoto akilia kwa baba ni rahisi kusema “nenda kwa mamako” au kuita tu “mama fulani embu mchukue huyu”. Mtoto anakuwa amekasirika huku Analia, hataki kunyamaza na anafanya kila aina ya vurugu kiasi kwamba kama mwanamme unaona hii sasa kasheshe; unaamua kutafuta msaada kwa “mamaa”. Na kweli bila kujali mama atakuja atamchukua mtoto, atambembeleza, mtoto atatulia na mwanamme atakuja kumchukua na kucheza naye. Mwanamme anakwepa gharika za machozi na vurugu (tantrums) za watoto. Hili nimeliona hata juzi tu kanisani ambapo baba alibaki kucheza na mtoto aliyetulia huku mama akihangaika kumbembeleza mtoto aliyekuwa Analia. Ilichukua muda lakini mama aliweza na baadaye baba akamchukua mtoto yule. Kwangu ni kinyume cha hapo.


Sijakwepa kadhia wala gharika za Baraka; pamoja naye nimepita mawimbi yale ya uchanga hadi sasa miaka miwili anapoweza kusema “nooo” na kusema “I don’t want to”! Nimeona jinsi gani mama zetu wana uvumilivu wa kimungu (divine patience). Ni uvumilivu usiojali muda, mahali au hata hali. Wakati mwingine mtoto anaweza kufanya vurugu sokoni, kanisani, barabarani, kwenye gari n.k Kote huku mama zetu kama wameumbwa toka udongo tofauti wanahimili haya yote na taratibu wanalea watoto wanakua.


Katika haya yote mtoto anachukua jina la baba! Ukifikiria sana unaweza hata kujiuliza kama kweli kina baba tuna haki ya kuwapa watoto majina yetu ati kwa sababu tu tumetoa mbegu! Wengi wetu tunaposhiriki kulea ni pale tunaposaidia. Siyo kazi sana kuamua kumwogesha mtoto, kumbeba, kumbembeleza au hata kucheza naye. Kazi ipo kwenye kumlea na kuchukua majukumu ya mama. Hili limenipa funzo kubwa sana.

Jambo la pili kubwa nililojifunza na hili limenishangaza sana ni kuwa ukaribu wa mama na mtoto ambao kwa kiasi kikubwa niliamini unatokana na kile kinachoitwa “maternal instincts” yaani hulka za kimama kwa kweli unaweza kuwepo baina ya baba mtoa huduma mkuu na mtoto. Baraka amekuwa karibu na mimi zaidi kwa sababu zile zile ambazo watoto wengine wanakuwa karibu sana na mama zao; kuwa nao muda mwingine wa malezi na huduma mbalimbali.


Baraka akilia anamlilia Baba, akiamka usingizini anaita “Papa” na akiona hajibiwi anaenda deep na kuita “Baba”. Hata nikimwacha na mama yake labda kwenda kufanya shughuli nyingine haachi kuulizia nipo wapi. Ni ukaribu wa ajabu na unaotisha sana na matokeo yake ni hata kinyume chake ni kweli. Nikiwa mbali au hata nikiwa nafanya jambo jingine mawazo yangu yote ni kuwahi kurudi nyumbani. Hivyo nimejifunza pia kuwa hiyo hisia ya umama inaweza kabisa kuwa ni hisia ya ubaba pia ukiipa nafasi.
Picha: Mimi mwanakijiji

Ukaribu huu pia umekuwepo kwa Tony na mimi zaidi pia kwani akiwa mdogo na mimi nafanya kazi pia basi alikuwa ni wa kuangaliwa na daycare au marafiki kiasi kwamba miaka ile ya mwanzo sidhani kama ilikuwa ni mizuri sana kwake kimalezi. Miaka hii miwili hata hivyo naamini imemjenga vizuri zaidi na kujaribu kulipia ya kwake iliyopotea.


Jambo a mwisho na kuu zaidi na ambalo limenibadilisha hata kiroho ni kuelewa ukuu wa Mungu. Hili naweza siku moja kuliandika zaidi. NInaelewa vizuri zaidi sasa kuhusu upendo wa Mungu kama Baba na jinsi gani Mungu ana uvumulivu mkubwa wa kumsubiri mwanadamu ajengeke asipotee. Ninaelewa zaidi na naweza kusema nimekua kitheolojia katika kuelewa jinsi gani mwanadamu anaweza kumtegemea Mungu kama mtoto amtegemeavyo mamake. Ninaelewa zaidi dhana ya kuwa Mungu ana sifa ya Umama (Feminine nature).


Ninaposoma mstari huu kutoka Biblia ninaamini unamaana kubwa sana ambayo labda imepotea katika nyakati (lost over ages); Mungu akaumba mtu kwa mfano wake; kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamme na mwanamke aliwaumba Mwanzo 1:27 Kwa muda mrefu inaonekana mfano wa Mungu ni mwanamme hasa kwa vile katika baadhi ya lugha nyingi zenye jinsia Mungu anatajwa kama “he” au “him” kama kwenye Kiingereza. Bahati nzuri Kiswahili hakina hili la jinsi hivyo huwezi kuona anayezungumzwa ni mwanamme au mwanamke isipokuwa kama inatajwa hivyo kwa jina au utambulisho mwingine. Ninaelewa upole, huruma, msamaha, uvumilivu, kujali, n.k ambavyo vinahusishwa na uanamke. Kumba mfano huu wa Mungu uko ndani yetu sote – wanaume na wanawake.


Ni kwa sababu hiyo basi niliwaahidi baadhi ya marafiki zangu kuwa mwisho wa mwaka nitaandika kidogo kuhusu hili kwani natarajia InShaaAllah kurudi kazini mapema mwakani na majukumu haya mengi tutayabadilisha. Nimejifunza mengi na ninaendelea kujifunza pamoja na changamoto zake zote siwezi kubadili kitu chochote kwa kweli. Miaka hii miwili imekuwa kwangu ni ya Baraka kweli kweli!


Ni kwa sababu hiyo tunapoingia mwaka mpya natoa changamoto kwa kina baba wenzangu ambao wana watoto wachanga au wanatarajia kupata watoto wachanga au watoto wao bado wadogo wajipe muda kubadilishana majukumu na wake zao. Hata kama haiwezekani kutoa miaka miwili au hata miezi naamini inawezekana kutoa angalau wiki moja au mbili au hata mwezi kufanya majukumu ya kina mama. Nafahamu siyo wote ambao pia wanaweza kupika – namshukuru Mamangu kwa hili kwani hata kabla ya hapa upishi kwangu sina tatizo.. iwe pilau, chapatti au maandazi!


Changamoto kubwa kwa kina mama ni kuweza kuwaamini kina baba wakiamua kuchukua jukumu hilo. Mke wangu alipata shida kidogo mwanzoni maana alikuwa kama kiranja kuhakikisha sijisahau kuwa nina mtoto nikazama kwenye facebook na jamiiforums! Lakini pole pole aliweza kuniamini kuwa naweza kufanya nilichoweza na ikabidi nibadili mambo yangu mengi na wengine labda wameona hata uwepo wangu kwenye mitandao umekuwa wa haraka haraka, wakati mwingine hata muda kwa marafiki zangu sikuwa nao tena kama ilivyokuwa huko nyuma. Lakini kubwa ni kina mama na dada zetu kuwatia moyo wanaume wanapochukua majukumu haya na siyo kukimbilia kuwaokoa kutoka kwa watoto au kujaribu kuwaokoa watoto mikononi mwa baba zao.


Hili ni kweli na ni muhimu watambue kuwa hawako kama wanawake. Hatushiki kama wanawake, na hivyo wakati mwingine tunajifunza kutoka katika makosa. Nilijifunza mwenyewe siku za mwanzo kabisa kuwa nguvu kubwa haiitajiki kumshika mtoto na pole pole niliweza kuadjust kumshika mtoto bila kuwa na hofu ya kumwumiza au kumwangusha. Kubwa ni kujiamini kuwa kama wanawake wanaweza na sisi tunaweza; mbona wao husema wakiwezeshwa wanaweza? Na sisi tukiwezeshwa – kuachiwa watoto – tunaweza.


Nimalize kwa kutoa heshima ya pekee kwa wanaume wengine wote ambao wamejikuta kama mimi kwa sababu mbalimbali. Ama kwa kuachana na wenza wao, kuachiwa watoto au kuondokewa na wenzao na kujikuta wamebakia ndio wanatoa huduma ya msingi. Wengine ni rahisi kuajiri “msichana wa kazi” au kukimbilia mahusiano mengine ili kumpata “mama mwingine”. Lakini naamini hakuna kubwa zaidi na linalodumu kama baba akiamua kuwa Mr. Mom hata kwa muda kidogo. Faida yake huwezi kuiweka na kuipima kwani inadumu milele.

Makala haya yameandikwa na Mzee Mwanakijiji, mwanablogu na mwandishi maarufu katika mitandao ya kijamii nchini Tanzania. Imetumiwa kwa idhini yake.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Pay $900? I quit blogging