Machapisho

Inaonyesha machapisho yenye lebo ya Lugha

Kumsaidia Mtoto Kujifunza na Kumudu Lugha

Picha
Lugha ni nyenzo muhimu sana tunayoihitaji katika maisha. Hatuwezi kufikiri vizuri, kuongea kwa ufasaha, kusikiliza, kueleza mambo tuliyokutana nayo na hata tunayoyatarajia siku zijazo bila kuhitaji lugha. Ni wazi tunalazimika kutumia maneno au ishara kuwasiliana na wanaotuzunguka. Mjadala wa namna gani mtoto hujifunza lugha ya mama una historia ndefu. Kwamba mtoto huzaliwa na asili ya lugha inayoongoza namna anavyojifunza lugha au ni mazingira anayokulia ndiyo yanayomwezesha kujifunza, ni vigumu kuhitimisha kwa hakika. Hata hivyo, kuna ukweli kwamba ili mtoto ajifunze lugha ipasavyo anahitaji kuwa na uwezo fulani anaozaliwa nao unaomwezesha kuelewa kanuni muhimu za lugha bila msaada mkubwa. Lakini pia mazingira, anayokulia mtoto, nayo yana nafasi kubwa ya kumwezesha kujifunza na kumudu lugha ya kwanza kirahisi.

Je, ni kweli lugha huathiri namna tunavyofikiri?

Picha
MJADALA wa nafasi ya lugha katika namna tunavyofikiri na kuyaelewa mazingira yetu una historia ndefu. Kwa ujumla kumekuwepo na pande mbili kuu. Upande wa kwanza unashikilia kuwa lugha, ama mawasiliano ayafanyayo mtu na wengine, iwe kwa maneno, ishara, alama au vitendo haina uhusiano wowote na namna mtu anavyofikiri. Ushahidi wa madai haya ni namna watoto wadogo wanavyoweza kufikiri uzuri bila hata kujua lugha. Na ni kweli pia kwamba kwa mtoto fikra au uelewa hutangulia uwezo wa lugha. Kwamba hawezi kusema wala kuonyesha kusikia kinachosemwa, hiyo haimaanishi kuwa mtoto hafikiri. Na ndio maana wakati anajifunza lugha, mtoto huweza kutumia neno moja kumaanisha mambo mengi. Anaelewa kuliko anavyotumia lugha. Vile vile, inasemekana, watu wenye ulemavu wa kutumia maneno kuwasiliana na wenzao, bubu kama tunavyowaita, wana uwezo mzuri wa kufikiri kama watu wengine. Kwamba watu hawa hawana tatizo la kuyatambua na kuyaelewa mazingira yao kwa ufanisi ule ule tunaouona kwa watu wasio na ulemavu...

Cheka na utafakari kwa bidii!

Hii ni kauli mbiu ya mdau mmoja kwenye jukwaa la majadiliano pale Jamiiforums . Yeye anasema: Usifanye kosa kuchagua RAIS MGONJWA tukaingia hasara ya kurudia uchaguzi! Nimecheka kwa sababu nilihitaji kucheka asubuhi hii. Ila nimeikopi nikitafakari. Jumamosi njema wadau!

Msaada wa msamiati...

Baada ya kimya cha ukumbi huu kwa muda mrefu na mwendo wa 'kuibuka na kuzama' kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu, sasa nimerejea rasmi. Tutaendelea kujadili, kuhoji, kuelimishana na hata kupotoshana inapotulazimu. Kumbuka huwezi kuelimika pasipo kupotosha mtazamo ulionao. Sasa nitangulie kuwaomba misamiati ya maneno haya kwa kiswahili fasaha: ethics, ethos, morality na morals. Nayafahamu maneno haya vizuri lakini sina maneno husika kwa kiswahili fasaha. Sipendi ule mtindo wa kutumia sentensi nzima kuelezea neno moja. Naomba mnisaidie kuongeza msamiati. Nitafurahi kupata majibu hayo hata kwa barua pepe kwa watakaopenda kutumia njia hiyo. Natanguliza shukrani za dhati!

Je, tunafikiri kwa kutumia lugha?

Kuna changamoto zimejitokeza kwenye ule mjadala wa tasnifu ya msomi wetu ambayo kwa maoni yaliyotolewa huenda ingekuwa bora kama ingekuwa katika kiswahili. Changamoto kubwa zaidi ni ile iliyoletwa na msomaji Godwin Habib Meghji akihoji ikiwa mwanadamu hufikiri kwa kutumia lugha. Hapa anasema: "Mimi sina uhakika kama binadamu anafikiria kwa kutumia lugha fulani. Viziwi na bubu pia hufikiri". Hii ni changamoto nyingine. Una maoni gani katika hili? Je, tunawezaje kufikiri? Fikra zinauhusiano wowote na lugha? Je, bubu ama kiziwi hana lugha kwa sababu tu hawezi kutamka ama kusikia?

Tembelea Website mpya

Pole na shuguli za kutupasha habari mbali mbali zinazotokea ndani na nje ya Tanzania. Naomba nafasi katika blog yako ili niwajulishe ndugu zangu watanzania kwamba nimetengeneza website www.rusumo.com ambapo wataweza kusikiliza nyimbo mbali mbali za Tanzania kama vile taarab,segere,dance,bongo flava,gospel na nyimbo za kigeni kama vile raggae,za kihindi,pop na nyengine nyingi tu. Pia kuna dictionary ya kisasa kabisa ambayo ina lugha zote za Ulaya na baadhi ya lugha za Asia,katika dictionary hii baada ya kupata tafsiri ya neno pia unaweza kuona picha za neno hilo kwa kubofya upande wa pili wa Ukurasa. Kadhalika wadau wataweza kuona hali ya hewa na wakati wa sehem mbali mbali za dunia. Karibuni sana wadau, ni mimi MSAFIRI ISMAIL RUSUMO. www.rusumo.com

Soma 'tasnifu' ya msomi wa Chuo Kikuu

Mjadala wa lugha gani itumike katika mfumo wetu wa elimu, ni suala la kutia aibu kuliko hata aibu yenyewe. Inadhalilisha sana unaposikia watu wazima hajui tutumie lugha gani kufundishia. Eti tunabishana kipi bora Kiswahili ama Kiingereza, kweli? Fedheha hii inatokana na ukweli kwamba lugha ya kiingereza inayolazimishiwa hivi sasa ni miongoni mwa maajabu saba ya dunia kwa wanafunzi wengi. Leo nimekuja na ushahidi wa karibu kabisa unaonyesha sura halisi ya tatizo. Nimepata bahati ya kupata karabrasha la 'utafiti' uliofanywa na mwanafunzi mmoja wa Chuo Kikuu aliyekuwa anajiandaa kuitetea Digrii yake kwa kuandika 'tasnifu'. Baada ya kusoma vipande vichache vya karabrasha hili naomba uamue mwenyewe kuwa Digrii iliyomwezesha kuandika andiko hili ni halali ama ni feki. Halafu fikiri nani wa kumlaumu: yeye mwenyewe asiyejua lugha ambayo ni ya wakoloni na haitumii kuwasiliana na jamii yake au ni serikali yake isiyoelewa makosa ya kugenisha hadi lugha? Inawezekana kabisa ku...

Viziwi wanaosikia tusivyovisikia...

Singida kwema. Nimekuwa na wakati mzuri na marafiki tulioachana kwa kipindi kirefu. Nimekuwa kiguu na njia utadhani kuku mfungwa aliyeachiwa kwa makosa. Jana nilipata fursa ya kutembelea shule ya viziwi na wasioona, Huruma. Nilikutana na walimu waliojitoa kuwasaidia watu hawa kwa moyo. Ilisisimua kuona viziwi wakipiga soga kwa lugha ya ishara. Walikuwa wenye furaha, kiasi kwamba hakuna kilichoonekana kuwapungukia. Nikajifunza. Kumbe furaha ni vile unavyoamua uwe. Huna haja ya kuwa na vyote ili kuipata. Nilimwona kijana asiyeona wala kusikia, lakini mwenye kusema! Ili kuwasiliana nae, unaandika mkononi mwake, anaelewa, halafu anajibu kwa mdomo! Naye huwezi amini kwa jinsi alivyojaa furaha! Nikaonana na wasioona wenye matumaini. Wasioona, wenye kuona tusivyoviona. Wenye furaha bila kutegemea vionekanavyo. Nikaondoka nikiwa na mawazo tele. Upofu na uziwi ni zaidi ya huu wa mwilini!

Global Voices: Dunia inaongea, unasikiliza?

Picha
Nimeamua kukata shauri na kujiunga na Jamii ya wanablogu wa Global Voices katika ukurasa wa Kiswahili . Ninajitolea kuusogeza ujumbe karibu na wasomaji wa kiswahili kwa kutafsiri makala zinazoandikwa na wanablogu wengine. Global Voices kimsingi ni jamii ya wanablogu kama 200 waliopo duniani kote ambao wanafanya kazi kwa pamoja kukuletea tafsiri na ripoti za yanayojiri kwenye ulimwengu wa blogu na uandishi wa kiraia. Global voices inapaza sauti ambazo kwa kawaida huwa hazisikiki katika vyombo vya habari vya kimataifa. Bonyeza hapa kusoma zaidi kuhusu jamii hiyo, halafu ukaribie kuchangia maoni kwenye ukurasa huo wa Kiswahili na kubadilishana mawazo na wanablogu wengine. Ndesanjo Macha , mtu aliyefanya kazi kubwa kutangaza teknolojia ya blogu kwa lugha ya kiswahili nchini na mmoja wa wahariri waandamizi wa Jamii hiyo, alikuwa na na haya ya kusema.

Naomba msaada wa lugha

Blogu zetu zinatusaidia kukuza lugha yetu ya kiswahili. Lazima tuwe wazi kuwa mara nyingine tunalazimika kutumia sentensi nzima kufafanua neno moja. Hapa nina maneno kadhaa ninayohitaji kiswahili chake. Conscious, sub-conscious, compulsion na obsession. Naomba mwenye msaada wa karibu anisaidie kupata maneno fasaha ya kiswahili. Natanguliza shukrani.

Haki ni nini?

SIKU hizi haipiti dakika hujasikia haki zikidaiwa mahali. Kuna haki za watoto. Haki za akina mama. Haki za wafanyakazi wa ndani(Koero analizungumzia hili vizuri). Haki za masikini. Haki za vyangudoa. Haki za maalbino. Haki za wasomaji. Haki za mafisadi (hata fisadi naye ana haki ya kusikilizwa/natural justice). Haki. Haki. Haki. Orodha ni ndefu. Jambo moja. Inapodaiwa haki, ikumbukwe kuwa upo upande ambao utalazimika kunyang'anywa haki zake ili haki ile ya kwanza inayodaiwa ipatikane. Kwa maneno mengine, unajikuta ili kutetea haki, inabidi unyang'anye haki. Na upande huu wa pili unaolazimika kupoteza haki ili kufidia haki inayodaiwa, nao ukiamka, inabidi zoezi liwe mduara. Yaani poteza haki, kuleta haki. Kwa mfano. Mtoto anapodai haki, maana yake inamlazimu mzazi kupoteza haki zake ili kumpatia mwanae haki. Kwa maneno mengine, haki ya mtoto inakuwa utumwa kwa mzazi. Unapoteza haki kuleta haki. Mwanafunzi wa kike anapodai haki ya kusoma kwa upendeleo, inabidi mamlaka zinaz...

Kama sio utumwa ni nini hiki?

Habari za siku ndugu msomaji. Binafsi sijambo. Nafurahi kurejea kibarazani baada ya heka heka za huko na huko. Itoshe kuhusu mimi, nikukaribishe tena humu ndani. Leo ningependa kukusimulia kisa kimoja. Nikuase kwanza, kwamba usilazimike kunielewa vibaya. Sijawa na tabia ya kuona makosa zaidi niwapo mahali ama nikutanapo na watu. Maana siamini kwamba binadamu ana kazi ya kushabikia makosa kuliko jema moja. Nisijitetee sana. Jumapili hii nilipata fursa ya kuhudhuria ibada kwenye kanisa la 'kisomi'. Washirika wa kanisa hili, wengi wao ni wale ambao umande haukuwazuia kuhudhuria shule. Wamesoma. Pamoja na ukweli kwamba wote walikuwa weusi kama mimi, lakini ilikuwa bayana kwamba kiingereza kilikuwa 'nguzo' ya ibada hiyo. Hilo halikuwa tatizo kwangu. Maana inaeleweka kwa wengi wetu kwamba, kusoma kunathibitishwa na umahiri wa kusema kiingereza. Nshazoea hili. Pamoja na ukweli kwamba kiuhalisia kiswahili ndicho kinachotawala madarasani lakini watu hatutaki kuukubali ukweli...

Uhuru huu ni kwa ajili ya nani?

Ninaomba msamaha kama hutanielewa. Ila ninadhani jambo hili ni muhimu ukalitafakari kwa kina wakati ukisherehekea “uhuru” wa nchi yako iliyo masikini kuliko zote kusini mwa jangwa la Sahara. Hivi kweli nchi yetu ina haki ya kusherehekea hicho kilichopewa jina la “uhuru”? Uhuru maana yake ni nini? Ni kwa kiasi gani twaweza kujikagua kuona ikiwa tu huru kweli? Kama uhuru una maana ya mambo kuwa hivi yalivyo, vipi utumwa? Ni kwa kiasi gani uchumi wa nchi hii unathibitisha kuwa kweli tu “huru”? Ni kwa kiasi gani utamaduni wetu unathibitisha hicho kinachoitwa “uhuru”? Ni kwa kiasi gani? Ni kwa vipi tunaweza kujiridhisha kwamba elimu yetu inakubaliana na kelele zetu za “uhuru”? Hivi mababu zetu walipokuwa wakiusaka uhuru lengo hasa lilikuwa nini? Leo hii tunasoma Vyuo Vikuu kwa vitisho kutoka kwa wenzetu wanaofafana na sisi. Haturuhusiwi kufikiri. Elimu yenyewe imekaa mkao wa kitumwa. Tunafundishwa akademia ituondoayo katika wigo wa kuyaelewa matatizo yetu ya kila siku. Inatuondoa k...

Matokeo ya utafiti wa Mwaipopo

Mwaipopo, mwanablogu wa Sauti ya baragumu ameonyesha mfano wa namna wanablogu tunavyoweza kuyachunguza mambo na kisha kupata michango yenye uzito unaovutia. Mfano huu ni wa kuigwa na kila mpenda mijadala. Nataraji kwamba wasomaji watakumbuka lile swali la lugha nililokuwa nimeliuliza kuonyesha ugumu uliopo katika kulitafsiri kwenda kwenye kiingereza ambacho hakitapoteza maana. Tulipata majibu mengi. Ndipo Mwaipopo kwa msukumo wa kupenda utafiti, akafanya uchunguzi na haya ndiyo majibu yake: " Jamani sikuishia hapo. Nilikuwa nafanya kautafiti kadogo ili nije tena...Swali hili liliponitoa jasho nikaona nimuulize rafiki yangu mzungu. Nae kaiona shida. Bahati njema anajuajua kidogo Kiswahili cha kuendea kariakoo. Kama mjuavyo mimi ni linguist. Niliwahi kusoma translation course. Hili ni tatizo miongoni mwa matatizo ya fasili - maneno ama miundo yenye kuegemea katika utamaduni wa lugha husika. hata hivyo panapo nia ya kutafsiri lazima njia itafutwe. hasa ni kwa nia ya kujif...

Kwa mabingwa wa Tafsiri fasaha

Kwa wanaopenda kiingereza.Tafadhali naomba tafsiri ya maneno haya kwa kiingereza ambacho hakitabadili maana iliyopo katika kiswahili hiki: "MAMA, HIVI MIMI NI MWANAO WA NGAPI KUZALIWA?" Ukipata tushirikishane.