Jifunze Uhusiano wa Malezi na Vilema vya Haiba (Personality Disorders)

Kizazi chetu kinakabiliwa na magonjwa mengi yasiyoonekana. Tunaumwa, na wakati mwingine taabani, lakini hatujui kuwa tunaumwa. Tunatembea, tunakutana na watu, tunapiga picha zenye nyuso zilizochangamka, tunaonekana kufurahia maisha lakini tunateseka na mahangaiko mengi tusiyoweza kuyasema. 


Tazama kiwango chetu cha ukatili. Haiwezi kuwa kawaida, kwa mfano, kuona mwenzako anaumizwa na wala hujali. Unamuumiza mtu na bado unashangaa kwa nini analalamika. Unamtesa mwenzako kihisia na bado unamdhihaki anapougulia maumivu. Unajiuliza, tumefikaje mahali mwanadamu unaweza kumtesa mwenzako, ukamsababishia maumivu na hujisikii kujutia. 

 

Mbaya, wakati mwingine, kiwango hiki cha ukatili kinakuwa kama nyenzo ya kupata tunachokitaka. Tunataka madaraka, tunataka umaarufu, mali na kila kinachotufanya kujione tunnawazidi wengine. Tunakuwa waraibu wa ukatili dhidi ya binadamu wenzetu na hatujisikii kujutia. Tazama kiwango chetu cha ubinafsi. Kwa nini tumepoteza uwezo wa kuafikiria hisia za wengine? 

 

Tazama tusivyoridhika. Kadri unavyopata ndivyo unavyotaka zaidi. Tazama tulivyo wapweke. Tazama tunavyochezeana hisia. Tazama tusivyojua kupenda wala kupendwa. Tazama kiwango chetu cha kuumizana kwenye mahusiano. Siku hizi mtu anaingia kwenye mahusiano akiwa ameshajiandaa kuachika/kuacha. Haiwezi kuwa kawaida. Tazama tunavyoteswa na sonona. Tuna vingi walivyokosa wazazi wengi lakini hatuna amani. Tunabobea kwenye kila aina ya uraibu—pombe, ngono, umaarufu, madaraka, kamari na kadhalika. Tunaonekana kuwa kizazi kinachobobea kwenye uhalifu wa wazi wazi na kificho. 


Kwenye makala haya, ninakuletea mukhtasari wa vilema 10 vya haiba (personality disorders) vinavyoweza kuathiri pakubwa ustawi wetu kama jamii. Natumia maelezo ya kitalaam na unaweza kurejea ukurasa wa 733-778, 881-902 wa Mwongozo wa Dalili za Magonjwa ya Akili(DSM-5) kujifunza zaidi vilema hivi vya haiba vinavyoweza kuwa hatari kwa mtu mmoja moja, familia, taasisi, jamii na hata taifa kwa ujumla wake. Karibu tujifunze zaidi. 

 

Msingi wa Haiba Njema

 

Kishunuzi (kisaikolojia) unakuwa mwanadamu mwenye nafsi iliyotulia, nafsi yenye afya njema, na hivyo kuwa na haiba isiyokuingiza kwenye matatizo kimahusiano, unapokuwa vizuri kwenye maeneo manne makubwa:

 

  • Unavyojitazama na kujichukulia (identity)— wewe ni nani? Nini kinakutofautisha na wenzako? Una uwezo wa kuyajua na kuyakabili mapungufu yako? Unazielewa hisia zako na madhara yake kwa watu? 
  • Unavyojiongoza (self-direction) —una uwezo wa kujiongoza na kujisimamia? Unajua unakoelekea? Kwa kiwango gani unatumia nyenzo zako kufanikisha malengo yako?
  • Unavyojali hisia za wengine (empathy) —ni kwa kiwango gani una uwezo wa kuelewa anachopitia mwenzako? Una uwezo wa kuvumilia tofauti za mitazamo? Unaelewa madhara ya tabia zako kwa mtu mwingine?
  • Unavyoweza kupenda na kupendwa (intimacy)—kina cha imani na ukaribu unaoweza kuwa nao na mtu umpendaye na uwezo wako wa kuendeleza ukaribu huo bila kukinai, kuchoka na kutumia vibaya imani ya mwenzako kwako.

 

Haya manne kwa pamoja ndio msingi wa utulivu wa nafsi ya mtu unaotafsirika kwenye tabia njema unayokuwa nayo sirini na mbele za watu. Kasoro yoyote katika hayo manne ndiyo inayoitwa ugonjwa (kilema) cha haiba—personality disorder.

 

Ushahidi wa kisayansi unaonesha kuwa haya manne ni zao la malezi zaidi kuliko vinasaba. Namna unavyomlea mtoto ndivyo unavyoacha template inayoamua hayo manne yaathiri vipi tabia zake. Malezi hapa yana maana ya kujali hisia za mtoto, kumfanya aamini anaonekana, anaheshimika, anaaminika, anaeleweka na kuthaminika kama binadamu anayestahili heshima. Unapokuwa na tabia zinazotuma ujumbe wa moja kwa moja kuwa unampenda, unaelewa anachopitia, unathamini utu wake, unachangia kuimarisha afya yake kwenye hayo manne—1) unamfanya anajione/ajichukulie kwa mtazamo chanya, 2) ajimudu na kujiongoza, 3) aheshimu hisia za wenzake na awe na uwezo wa 4) kupenda na kuamini watu wanaomzunguka.

 

PARANOID 

 

Hiki ni kilema cha kumwamini mtu. Ukikutana na mtu, ukimsikiliza, unakuwa kama unajua hata asichokisema. Unamwekea maneno mdomoni aseme jambo hasi asilolisema. Muda wote una mawazo hasi hata kama huna ushahidi. Unahisi mtu anakuzunguka, ana hila anapokuja kwako, ana nia ovu na wewe na kuna kitu lazima anakitaka kwako. Una tabia ya kuharibu uhusiano mzuri unaoanza kwa kosa la kurukia mambo na kumtuhumu mwenzako kwa ubaya asiokuwa nao. Mara nyingi, unateswa na wivu, hujioni mtu salama kwenye mahusiano, muda wote una wasiwasi na anachokifanya mpenzi wako, unataka kumdhibiti mpaka unaharibu ladha ya mahusiano. 

 

Ukikosewa una kawaida ya kukuza mambo. Hata mnapozunguza, inakuwa vigumu kupata ufumbuzi kwa sababu unashutumu, unatuhumu, unaumiza kwa maneno, na aghalabu unapenda kufukua makaburi ili kuonesha ukubwa wa kosa. Unaishi na visasi, gubu na hasira zisizoisha. Kukosa imani na watu ni kasoro kubwa inayoathiri mahusiano yako na watu. Unahisi hisi watu kwa vile ufahamu wako umekuzwa kujihami na hatari kwa watu. 

 

Unatamani kuwa karibu na watu lakini unatishwa wanapojaribu kukuamini, hii ikiwa na maana umelelewa kwenye mazingira ya watu wasioaminika. Tatizo linaanzia ndani yako. Utupu unaojisikia ndani yako, hali ya kukosa upendo, unauhamishia kwa watu kama namna ya kujilinda. Huna uwezo wa kuelewa hisia za watu kwa vile hukulelewa kwenye mazingira yanayojali hisia zako. Hofu ya kusalitiwa na kuachika inaharibu uwezekano wa kuwa na mahusiano yenye kina na ya kuaminiana.




 

Uhusiano na Malezi

 

Kutokutabirika kwa mzazi, mtoto kutokujua unataka nini, kumkosoa kupindukia, kumdhalilisha, kumtisha, kumfanya awe na wasiwasi muda wote hali inayomfanya asiwe na imani na usalama wake katika mazingira ya nyumbani. Kumbuka nyumbani ndiko mahali pa kwanza kumfanya mtoto ajisikie salama. Unapomtisha na kumwogopesha unapanda mbegu ya mtoto kujisikia hayuko salama na watu hawaaminiki.

 

SCHIZOID 

 

Unapata shida kusema hisia zako. Unaweza kuumia na huwezi kusema umeumia. Unaweza kupenda na huwezi kumwambia unayempenda. Huna muunganiko wa kihisia na watu, unajichukulia kama mtu asiyehitaji ukaribu na watu. Una uwezo wa kujiongoza vizuri, huangilii watu wanasema nini, unapenda kuwa huru kujipangia mambo yako, hali inayoweza kukuingiza kwenye tuhuma za usaliti na kutokujali hususani unapolazimika kuwa sehemu ya utambulisho na mipango ya kundi. Shida yako ni kutanguliza unachokitaka na huoni namna unavyoweza kubadilika ufanane na kundi. 

 

Linapokuja suala la hisia, hapa unajikuta kwenye mtanziko. Ingawa unaweza kuelewa mwenzako anamaanisha nini bado huwezi kuelewa hisia zake. Matokeo yake uhusiano wako na watu unakuwa wa juu juu, maana huna uwezo wa kuwa na kina cha mahusiano ya watu wanaoaminiana. Ili kuwa salama, mara nyingi unakwepa mahusiano ya karibu na watu. Huendi mbele ya kufahamiana na stori za juu juu zisizoshibisha mahusiano.

 

Uhusiano na Malezi

 

Mzazi hapatikani kihisia au pengine hajali. Unaweza kuwa unapatikana kimwili lakini hufanyi juhudi za mtoto kuona unamjali, unamuona, unamuelewa na kumthamini. Dakika chache unazokuwa na mtoto unafanya nini kumfanya aone yeye ni thamani, kuna mtu anajali, anaelewa, anasikiliza? Usipofanya hivyo, mtoto anajifunza kukimbia mahusiano na anajisikia salama zaidi kuwa mwenyewe.

 

SCHIZOTYPAL 

 

Unaishi kwenye dunia unayoijua wewe, ya kufikirika, isiyohalisi, ukijichukulia kuwa vile usivyo. Hudanganywi. Unajidanganya mwenyewe. Unaamini vitu visivyo na uhalisia na hakuna mtu anaweza kukugeuza. Hupendi kuwajibikia tabia zako, una  uvivu usiotaka kuushughulikia, na muda mwingi unatafuta sababu za nje kuelezea matatizo yako. Unapata shida kujua unaelekea wapi maana hata hujui unataka nini. Muda mwingi unaongozwa na dhana za kufikirika zisizoeleweka. Mwepesi sana kuamini ‘miujiza’ na ‘bahati’, ‘zali’ na ushirikiana kukusaidia kuficha tabia yako ya kutokuwajibika. 

 

Unapata ugumu kuelewa hisia za watu. Ujumbe usio wa moja kwa moja, kwako ni hadithi zisizoeleweka. Kila mara unataka uambiwe moja kwa moja na lugha ya hisia huielewi kirahisi. Matokeo yake unapata tabu sana na mapenzi maana kila anachotaka mwenzako bila kukuambia hukielewi na hata ukiambiwa masikio yako yanakitafsiri kama malalamiko na makelele.

 


Uhusiano na Malezi

 

Mzazi anajali lakini haeleweki hali inayomfanya mtoto achanganyikiwe kufahamu aamini nini. Imani zinazopitiliza uhalisia zina uwezekano wa kumfanya mtoto akaamini anaweza kuamini kisichotekelezeka na maisha yakaenda hata kama hawajibiki. Pia, kuwa na tabia zinazomchanganya mtoto inaweza kuwa sehemu ya tatizo. Unaishi usichokisema na unakisema usichokiishi.

 

ANTISOCIAL 

 

Unasumbuliwa na ubinafsi uliopindukia kiasi cha kutokujali, na kwa kweli, ukipuuza haki za wenzako. Huoni sababu ya kuelewa jamii imejiwekea taratibu zipi, na muda mwingi, unapenda kuonekana wa tofauti kwa kufanya vitu vinavyokwenda kinyume na matarajio ya watu. Unaona sifa kujitambulisha na matendo ya kihalifu na unapenda kuwa kinyume cha taratibu zilizopo, kuvunja sheria kwa makusudi, kuchokoza haki za wenzako kwako hayo ndio maisha. Uwezekano ni mkubwa ukaingia kwenye migogoro ya kisheria na ukaishia kifungoni. 

 

Huna uwezo wa kuelewa hisia za mwenzako, na kwa kawaida, hujali mwenzako anajisikiaje. Wewe ni aina ya watu wanaofurahia maumivu ya wengine, hasa kama yanakuletea manufaa binafsi. Mahusiano kwako ni mchezo wa kucheza na hisia za watu. ‘Unampenda’ usiyempenda ili kuonesha una nguvu za kuumiza. Una tabia za ulaghai na ubazazi na hata ukikosea hujutii na usivyo na haya utatetea upuuzi wa wazi.

 

Uhusiano na Malezi

 

Inawezekana kilema hiki kikawa matokeo ya kuishi bila uangalizi wa karibu wa wazazi, mzazi kujali mambo mengine kuliko malezi, inawezekana pia ni mazingira ya kimalezi yanayomfanya mtoto aamini anaweza kuvunja sheria, taratibu na matarajio ya jamii bila kujali hisia za watu. Inaweza pia ikawa ni matokeo ya ubabe na udhalilishaji usiojali utu, heshima na hisia za mtoto.

 

BORDERLINE 

 

Ukiulizwa, ‘wewe ni nani?’ ni vigumu kujua kwa hakika. Utambulisho wako unategemea uko na nani, wakati gani, unatekeleza mkakati gani, na nani ananufaika na jibu la swali hilo. Unaonekana ni mtu usiyeeleweka kwa vile hata mwenyewe huna hakika kwa sasa wewe ni nani hasa. Unapata shida kujisimamia, na tabia zako nyingi zinategemea mihemuko na huwa hufikiri sana kwa nini unafanya hicho unachofanya. Una uraibu mkubwa wa kutumia usichonacho, unapenda ngono kuliko mahusiano, mlevi, na huwezi kujizuia kufanya kitu unachojua kinakuweka kwenye mazingira ya hatari. 

 

Ingawa una uwezo wa kuelewa hisia za mtu, tena kuna wakati unajali sana hisia za mtu, tatizo lako hutabiriki. Hata unapoambiwa kitu saa nyingine huwezi kuelewa kinachosemwa hasa kama hakigusi maslahi yako kwa wakati huo. Mahusiano kwako ni kitendawili maana hata hujui unataka nini. Nguvu nyingi unaweka kwenye vitu visivyokuza kina cha mahusiano, ukiamini vitu ambavyo mwenzako hana uwezo wa kuvitekeleza na hivyo unakuwa mwepesi sana kukata tamaa dhahania zako zisipotekelezwa.

 


Uhusiano na Malezi

 

Kilema hiki kina uhusiano na malezi yanayopuuza uhalisia wa mtoto. Inawezekana ikawa ni sheria ngumu, zinazolazimisha matarajio ya mzazi kwa gharama ya utashi wa mtoto, unyanyasaji wa mtoto kihisia na wakati mwingine inaweza kuwa matokeo ya kudekezwa kupindukia —kulelewa kama yai lisilohitaji kufikiri wala kujishughulisha.

 

HISTRIONIC 

 

Unapenda sana attention—kuonekana hata kwa mambo ambayo huhitaji kuonekana. Umejenga utambulisho wako kwenye maisha ya maigizo na maonesho ya vitu ulivyonavyo badala ya utu wako. Ukiangalia msukumo mkubwa nyuma ya mengi unayoyafanya ni ‘kuwaonesha’, ‘wakutambue,’ ‘wakukubali.’ Ukiangalia mipango yako mingi unaona lengo kubwa ni kuonekana na wewe upo na unabamiza mjini hapa. Unataka mambo makubwa yanayokuzidi kwa mbali, na saa nyingine, unafanya vitu huna uwezo navyo, ili tu watu wakuheshimu. 

 

Huna uwezo wa kuelewa na kuheshimu hisia za mtu mwingine, na hata ukielewa unazitumia uelewa huo kujionesha zaidi kuliko kujali kweli hisia za mwenzako. Unaweza kujali kimaigizo ili uonekane unajali. Unakuza kitu usichojisikia ili upate ushahidi kuwa wewe ni mtu anayejali. Tabia hii, bahati mbaya, huwa inakera watu wakigundua unatenda wema kwa agenda ya siri. Unaishia kukorofishana na watu unaowahitaji. 

 

Kwenye mahusiano, mwenzetu, unapenda sana drama. Maisha yako ya kimapenzi kwa hakika ni pasua kichwa. Huna uwezo wa kuyatafutia mahusiano yako kina bali maigizo ya kuwaonesha watu. Hata mpenzi unayemchagua, lengo ni ‘waone’, ‘wanikubali’, ‘wajue na mimi naweza kumpata mtoto mzuri.’ Unaweza hata kuanika mambo ya faragha na mpenzi wako ili tu tuone ulivyojipata. Si watu wengi huvumilia maigizo haya. Uwezekano ni mkubwa mpenzi wako huchoka hizi drama za attention anazojua hazimsaidia kujisikia kupendwa kweli. Kuacha na kuachana na kuacha ndio inakuwa maisha.

 


Uhusiano na Malezi

 

Mtoto ana hitaji la kuonekana na wazazi. Bahati mbaya, huenda wazazi hawakuwa na muda wa kumfanya mtoto ajione anaonekana, anathaminika na anaeleweka. Upande mwingine, inawezekana kabisa tatizo ni wazazi kuendekeza tabia ya mtoto kujionesha na kuonekana. Unapomfanya mtoto aone kujionesha onesha ni utaratibu wa kawaida, anakua akipenda drama na kuzidisha maigizo yanayomfanya aonekane. Kuna tafiti pia zinapendekeza kuwa watu wanaopenda kuonekana (maigizo) sana huwa wamekulia kwenye mazingira ya kupuuzwa walipokuwa wadogo. Ukubwani wanataka kuthibitisha kuwa hawapuuziki.

 

NARCISSITIC 

 

Unapenda kujikweza, kujitutumua uonekane bora kuliko wenzako. Ukiangalia mengi unayoyafanya ni kama unataka uwazidi wenzako uonekane una akili, una uwezo, una hekima, una pesa kuliko wengine wote. Unashindana hata na watu ambao hawana haja na mashindano na wewe. Una kiburi kinachoenda sambamba na dharau, unapenda kujisema sema, kujisifia, kujiona mtu maalum mwenye akili, uliyefanikiwa, unayestahili kusifiwa, kutumikiwa, kuheshimika kuliko wenzako. 

 

Unapenda mno sifa, hadhi, madaraka na nafasi zinazokuweka juu ya wengine na hivyo kujitambulisha na watu wenye heshima zao, wenye madaraka makubwa, elimu kubwa ndio kunakupa furaha. Dharau inakufanya ushindwe kabisa kuheshimu hisia za wengine. Unapenda kubishana hata kwa mambo yasiyo na maana, unataka usikilizwe muda wote, na huvumilii kabisa mtazamo tofauti na unavyoona mambo. Kwenye mijadala unapenda uwe na sauti ya mwisho, uwe na hadhi ya kuhitimisha jambo maana unajiona ndiye mwenye uelewa, hekima na uzoefu ambao wengine hawana. 

 

Uhusiano wa karibu na mtu kwako ni changamoto. Una dharau, unakinai, unachoka wajibu unaokufanya uwe na usawa kwenye mahusiano. Shida ni vile unafurahia kumtumia mwenzio kukidhi matakwa yako, unamgeuza kuwa mtumwa wa unachokitaka na hivyo hapati nafasi ya kujiona kama mtu mwenye hadhi sawa na wewe kwenye mahusiano. Mara nyingi mahusiano yako hayawezi kuwa na utoshelevu wa dhati labda kama mwenzako ataamua kuwa mtumwa wako.

 

Uhusiano na Malezi

 

Kupenda sifa na utukufu na kuwazidi wenzako tatizo linaweza kuwa wazazi kuwa na matarajio makubwa mno yanamyofanya mtoto aone namna pekee ya kuwaridhidha wazazi ni kupambana, kushindana na kuwazidi wengine. Pia, inawezekana tabia ya kumfanya ajione ni ‘special’, kumlinganisha na kumpambanisha na wengine sambamba na kumsifia mno mtoto kwa mafanikio anayopata inaweza kuwa tatizo. Unapomfanya mtoto akajiona ana haki ya kusifiwa na kutetemekewa akifanya vizuri unamgeuza kuwa mtumwa wa sifa, mashindano na ujuaji usio na tija. Kadri unavyomjaza upepo ndivyo unavyomfanya kuwa tegemezi wa sifa na mashindano na asiposifiwa ataanza kuona kama hajafanya kitu. 

 


 

AVOIDANT 

 

Unahisi unyonge ndani yako unaokufanya muda wote uwe na mashaka na vile watu wanakuona. Uko makini sana na maoni ya watu, jambo dogo lisilokwenda sawa na matarajio yako linaweza kukusumbua kwa muda mrefu. Unaogopa kukataliwa, kutengwa na kudharauliwa. Unajihisi watu hawakutathmini, hawakuelewi, hawakupendi na unaogopa kukosolewa hasa mbele za watu. Unaogopa mno kujisimamia, kupanga mipango na kufuatilia ndoto zako, kwa hofu ya kufanya makosa, kuharibu, kukosolewa na kuonekana kweli huwezi. Kama kuna kitu unakiogopa ni aibu na fedheha ya kushindwa. Umeachana na mipango mingi ambayo ingekusaidia kupiga hatua kwa hofu tu ya kufanya makosa yatakayowapa watu ushahidi kuwa kweli huna uwezo. 

 

Unaogopa mahusiano na watu hasa usiowafahamu vizuri. Una uwezo wa kuelewa hisia za watu lakini uwezo huo unamezwa na hofu uliyonayo na kuonekana dhaifu, mnyonge na huwezi. Unatamani sana ukaribu na mtu lakini wakati huo huo unakwepa mazingira yanayokuza kina cha mahusiano. Unaogopa aibu ya kuonekana unajipendekeza, unapenda sana, na huna kazi maalumu. Inawezekana umeharibu mahusiano yako mengi kwa hofu tu ya ‘atanionaje?’

 

Uhusiano na Malezi

 

Tunazaliwa na hitaji la mahusiano. Ukiyakosa unajifunza kujihami kwa kukwepa watu. Inawezekana tatizo likawa malezi yasiyojenga mahusiano na mtoto, yanayomfanya ajione hana thamani, hatoshi na hafai. Sababu mojawapo ni kumkosoa mtoto kupindukia. Unapomkosoa mtoto kupindukia unamfanya aishi na hofu ya kukosea, kutokufikia matarajio na hivyo aogope mazingira yoyote yanayoweza kumfanya akosolewe, abezwe na kurekebishwa. Huyu atageuka kuwa mtoto anayekwepa mazingira yenye risk ya kukosea na siku zote atakuwa mtu wa kusubiri wengine waanze ndio ajaribu na yeye.

 

DEPENDENT 

 

Una utegemezi kupindukia, hujisikii salama bila kuwa karibu na mtu anayekuzidi maarifa na sifa nyingine usizonazo. Huamini unaweza kujisimamia mwenyewe bila msaada mkubwa kutoka watu wanaokuzidi. Unapenda mno mtu anaoneshe anakujali, anakuhurumia, anakutunza na tabia hii, aghalabu, hukufanya uwe mhanga wa watu walaghai wanaotumia vibaya utegemezi wako. Unapenda mno ushauri hata kwa mambo ambayo ungeweza kuyaamua mwenyewe. Ukipewa fursa ya kuamua unaona ni adhabu. Umezoea kufanyiwa maamuzi na wewe unabaki kuwa mtekelezaji. Ingawa unaweza kuonekana kuwa na furaha unapokuwa mtiifu kwa mwenzako anayeziba ombwe na kutokujua ufanye nini, baadae huwa unakuja kugundua umejiingiza kwenye kitanzi cha mtu anayekunyanyasa na kutweza utu wako. 

 

Una uwezo wa kujua hisia za mwingine maana huna namna ya kujitegemea bila msaada wake. Tatizo kujua hisia hizo kunakudhulumu hisia zako mwenyewe. Ingawa mahusiano ndio usalama wako, tabia ya kumganda mwenzako, kumfuatilia kupindukia (ukiogopa kuachwa) inamfanya akuchoke mapema akuone mzigo unaomnyima kufurahia maisha yake. Kwa hivyo, unaweza kujikuta na visa vingi vya kuachika hata kama ulimpenda sana.

 


Uhusiano na Malezi

 

Utegemezi sio asili ya mwanadamu. Unakuwa tegemezi baada ya kuaminishwa ukijitegemea unakuwa tatizo kwa wazazi. Kwa hivyo hapa shida ni malezi dekezi, kumchukulia mtoto kama mtu asiyeweza kujitegemea, yanayoogopa kumjengea mtoto uwezo wa kujaribu, kufanya vitu mwenyewe, bila kusubiri maelekezo kupitiliza. Hawa mara nyingi ni wale wazazi wanaowalinda watoto kupindulia, kuwadhibiti utashi wao na kuwatumia kama nyenzo ya kutekeleza matakwa yao.

 

OBSESSIVE-COMPULSIVE 

 

Unajiona mkamilifu kupitiliza, makini, mwenye msimamo mkalo usiovumilia makosa mpaka unasahau kuna maisha nje ya ‘dunia ya ukamilifu’ unayoishi peke yako. Utaratibu wa maisha yako umetawaliwa na viwango vya juu kupindukia, unapenda ratiba na muda na ukishapanga kitu hakuna kitu kitakubalisha. Ukiwa kiongozi ukiweka makataa hukubali maelezo yanayoweza kufafanua kwa nini jambo halijaenda kama ilivyotarajiwa — mpaka unaonekana mbabe, jeuri usiye na hisia wala hujali utu wa watu. Unayachukulia maisha kama mkusanyiko wa sheria na kanuni ngumu zenye kazi ya kumdhibiti mwanadamu asiyepaswa kuwa na utashi wala uhuru wa kufikiri. Pamoja na kuheshimu taratibu zilizopo, unasahau uhalisia unaoweza kuacha nafasi fulani ya kuzingatia mazingira yaliyopo. 

 

Mipango yako mingi inaongozwa na vigezo vya juu mno na ni vigumu kufanya kazi na watu wanaamini kuna kukosea, kutokufikia malengo na hata kurekebisha mipango iendane na hali halisi. Unashindwa kuheshimu hisia za watu na ukiambia uchague kazi na mahusiano mema na watu utachagua kazi hata kama itakugombanisha na kila mtu. Unapenda kutumia muda mwingi kazini na hiyo inakugharimu kwenye mahusiano mengine nje ya kazi, na aghalabu, familia yako itakulalamikia kwa kutokupatikana, kuwadhibiti kupindukia na kutokujali hisia zao kama binadamu.

 

Uhusiano na Malezi

 

Hakuna maisha yenye ukamilifu. Unajikuta unataka ukamilifu kwa vile ulikulia malezi yanayoamini katika ukamilifu, yenye matarajio yasiyo na uhalisia kwa mtoto, yanayokuweka kwenye mazingira ya kufuata amri kupindukia, kutokuruhusiwa kushiriki kwenye utungaji wa taratibu hizo, yanayokufanya uamini utaratibu ukishawekwa na mzazi, hakuna swali unaweza kuuliza zaidi ya kufuata na kutii. Ukiwa mtu wa taratibu na ukamilifu kupindukia unakuwa na amani hata kama unaumiza watu.

 

HITIMISHO

 

Kuelewa vilema hivi inatusaidia kujua namna ya kuishi na watu kwenye maeneo yetu ya kazi, kutathmini mustakabili wa mahusiano yanayoanza, kuelewa wanayopitia wapenzi tulionao tayari na hivyo kujifunza namna ya kupunguza matatizo kwa njia chanya isiyozalisha migogoro zaidi. Pili, inasaidia kujua tunafanya nini kwenye malezi ya watoto wetu. 

 

Ingawa ni kweli magonjwa haya ya hisia, haiba na tabia kama tulivyoyaona yana sababu nyingi, mchango wa malezi na makuzi haukwepeki—hata kama wakati mwingine mchango huo si mkubwa kivile. Nimechagua mwelekeo wa malezi maana ndiyo jambo linalotekelezeka zaidi na liko kwenye uwezo wetu kutusaidia kupunguza tatizo tunapowalea watoto wetu.

Maoni

  1. Makala nzuri sana, nimejifunza kitu kikubwa sana

    JibuFuta
  2. Ahsante, lakini mi nahitaji unisaidie kutoka kwenye shida moja ya kisaikolojia kama inawezekana

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

UmahiriHisia (Emotional Intelligence) ni Nini?

Kutumia UmahiriHisia (Emotional Intelligence) Kuelewa Unavyojisikia

Kutumia UmahiriHisia (Emotional Intelligence) Kuimarisha Mahusiano

UmahiriHisia (Emotional Intelligence) Unavyosaidia Kurekebu na Kumudu Hisia

UmahiriHisia (Emotional Intelligence) Unavyochochea Motisha na Kujituma