Self-Esteem: Ni muhimu kwa mwanao

Ninaanza na kukupa hitimisho: Mzazi anayo nafasi muhimu sana ya kumfanya mwanae ajenge fikra-chanya kuhusu maisha yake mwenyewe zitakazomfanya ajiamini. Na mzazi huyohuyo asipokuwa mwangalifu, anaweza kumsababishia mwanae fikra-hasi na hivyo kumfanya ajione duni.

Kujenga fikra chanya kwa mwanao si kazi rahisi sana. Ni kazi ngumu inayodai muda wa kutosha wa mahusiano ya karibu kati ya mzazi na mwanae. Kazi hii haifanywi na wazazi wengi ambao huzaa pasipo kuhesabu gharama za uzazi husika. Hii ni kwa sababu kitendo kinachosababisha uzazi huwa hakihesabiki kama kazi. Kitendo hicho hufanyika katika mazingira ya starehe ya tamaa ya mwili kiasi kwamba wapenzi wengi huwa hawafikiri zaidi ya tamaa hiyo.

Kwa maana nyingine, inaweza kukubalika nikisema kuzaa si kazi. Ndio maana hata wahenga walilonga: Kuzaa si kazi, kazi ni kulea. Kila mmoja wetu anaweza kuzaa akipenda. Ndio maana unawafahamu wasichana wadogo walioshika mimba bila kupenda. Hii ina maana kwamba kila binadamu asiye na hitilafu ya mfumo wa uzazi wake, hawezi kushindwa kuzaa.

Kuzaa kunaweza kuchukuliwa kama suala gumu (sana), iwapo anayefikiri atajaribu kwenda zaidi ya tukio la kumpa mimba mwanamke. Hapo ndipo ugumu ulipo. Kulea mtoto. Si kila aliyezaa ni mzazi. Wengi wa waliozaa ni wazaaji, na hata kidogo si walezi. Kulea ni shughuli ngumu ambayo inafanywa kwa ukamilifu na wazaaji wachache. Kulea si kukuza mwili wa mtoto pekeyake. Wala si kumpeleka mtoto shule za “Watakatifu”. Wala si tu kule kuwa na uwezo wa kumpatia mwanao mahitaji yote ya kifedha. Kulea ni pamoja na kumjengea mwanao fikra sahihi kuhusu nafsi yake mwenyewe na namna anavyoonekana na wengine.
Hivyo nina hakika kwamba kama binadamu tungekuwa tunafikiri kuhusu mahitaji halisi ya kiumbe kitakachozaliwa, basi tungekuwa na idadi ndogo sana ya watoto wanaoitwa jina la hovyo, eti watoto wa mitaani.

Mtoto akishazaliwa, pamoja na mambo mengine chungu nzima, anahitaji sana kujengewa mazingira ya kuweza kukabiliana na changamoto za kila siku. Mtoto kujisikia vizuri kuhusu yeye mwenyewe ili awe na fursa nzuri ya kukabiliana na migogoro kwa njia sahihi pamoja na kukupambana na shinikizo lisilofaa. Mtoto wa namna hii huonekana wenye uso angavu, akifurahia maisha yake na kule kuwa nyumbani kwao.

Kwa upande mwingine, wapo watoto ambao wanao uwezo mdogo sana wa kukabiliana na changamoto za kila siku, wakichanganyikiwa na mambo madogo. Wapo watoto ambao hawajifurahii walivyo, wakijihesabu kuwa watu fulani duni hivi na hivyo kuwa na wakati mgumu katika kupata utatuzi wa masuala mengi wanayokabiliana nayo.

Huwaza mawazo dhaifu kama vile: “Mie bwege…!”, “…Sina ninachoweza kukifanya” “Sina mawazo ya kusikilizwa na mtu…Nina bahati mbaya kuwa hivi nilivyo!” Hali ikiwa mbaya, huweza kuwa wakimya, wasiotengeneza marafiki, na wenye mawazo na hata shinikizo la mawazo. Huwa rahisi kukata tamaa wakikutana na jambo linalohitaji utatuzi wao. Ni wepesi kutoa majibu “Siwezi mimi”.

Self-Esteem ni nini vile?

Ni jumla ya imani ama hisia tunazokuwanazo kuhusu nafsi zetu, ama kule kujielewa kibinafsi. Namna tunavyojielewa, huathiri kwa kiasi kikubwa dhamira ama mitizamo tuliyonayo ama tabia zetu na hivyo huathiri namna tunavyoweza kukabiliana na hisia mbalimbali.

Kujielewa na kujikubali huku, huanza kujengeka tangia tukiwa vichanga. Kwa mfano mtoto mdogo anapojaribu kukifikia kimdoli chake kilicho mbali kidogo na pale alipo, akafanikiwa, basi hujisikia kufanikiwa kunakoongeza kujiamini kwake. Akifanya mara ya pili, ya tatu na kuendelea, na akafanikiwa katika mazingira tofauti tofauti, basi mtoto huyo hufundishwa na mafanikio hayo kuwa “naweza”. Kule kujiona unaweza ukafanya kitu hakuanzii ukubwani. Huanzia nyakati hizi.

Mtoto anapojaribu, akashindwa, akajaribu tena akashindwa. Akaribu, hatimaye akafanikiwa, basi huyo huanza kujenga hisia-chanya kuhusu uwezo wake. Vilevile, pamoja na kujifunza kutokana na matukio yake mwenyewe, bado hujifunza kutokana na uhusiano wake yeye na wazazi wake na wengine wanaohusiana naye. Ndio maana mzazi anashauriwa sana kujihusisha kikamilifu katika suala zima la “uhandisi” wa kujiamini kwa mtoto.

Self-Esteem (fikra-chanya) pia huweza kufafanuliwa kama muunganiko wa uwezo binafsi pamoja na zile hisia za kujisikia kupendwa anazokuwanazo mtu. Kwa hiyo, mtoto anayefurahia mafanikio yake lakini hajisikii kupendwa huweza kuishia kushindwa kujiamini (low self-esteemed). Vivyo hivyo, mtoto anayejisikia kupendwa lakini bado ana mashaka na uwezo wake katika kufanya mambo fulani fulani , naye hali kadhalika huishia kuwa kama yule wa kwanza. Hatojiamini.

Kwa hivo, ili binadamu aweze kufikia kujiamini kikamilifu, panahitajika msawazo katika hayo mawili. Kimoja kikiwa juu, na kingine kikawa chini basi matokeo yake ni bila-bila.

Ishara kwamba mwanao hajiamini:

Self- Esteem hutofatiana na kukua kwa kadiri mwanao anavyokua. Na mara nyingi, self- esteem huweza kuboreshwa kwa sababu ya ukweli kwamba inahusiana sana na mambo ambayo mtoto anakutana nayo yanayomwongezea mtazamo mpya katika masuala anuai. Kwa sababu hiyo basi, ni muhimu sana kwako wewe mzazi kujua namna ya kubaini ikiwa mwanao anajiamini ama kinyume chake.

Mtoto anayejifikiria duni (low self-esteem), huwa anajiona hafai, hajiamini. Haishii kwenye kutokujiamini mwenyewe, bali pia hawaamini wanaomzunguka
Kwa ujumla mtoto mwenye low self-esteem huwatuhumu watu kimoyomoyo kwamba hawampendi, wanamtambua alivyo duni na hivyo hudhani wanamdharau kama anavyojidharau yeye. Kwa hivyo, huona haya/aibu anapokuwa nao. Ni mwoga wa macho ya watu (hasa wageni) akihisi kuwa “wanamchora”. Huwa hapendi kujaribu kufanya mambo mapya. Anapenda kufanya “zilipendwa” akiogopa kukosea. Kwa sababu ni mtu wa kujifikiria duni na dhaifu, mara nyingi huwa ni mtu wa kujisemea udhaifu, kwa sentensi kama vile, “Mie mjinga kweli,” “Sura yangu mbaya kama ya baba’ngu,” “Siwezi kujifunza jambo hili,” ama “Nifanyeje wakati hakuna mtu ananijali?”.

Mtoto huyu huwa hawezi kuvumilia anapoudhiwa na mtu, analia kirahisi kwa masuala madogo madogo, mwepesi wa kukata tamaa anapofanya jambo fulani, na mara nyingi husubiri wengine wafanye badala yake. . Kwa mtoto wa miaka chini ya miwili ni rahisi kumjaribu kama ana low self esteem: Hulia mama yake anapoondoka ama mtu mgeni anapotaka kumpakata. Maana yake ni kwamba hawaamini binadamu anaoishi nao kiasi cha kuhisi wanafikiri kumwadhibu ama kumdhuru kabisa.
Mtoto asiyejiamini, ni mgomvi, mlalamishi na hujikatia tamaa kirahisi. Anapokutana na ugumu wa muda, basi kwake yeye hali hiyo ina maana ya kudumu.

Kwa upande mwingine, mtoto mwenye kujifikiria vizuri (high self-esteemed) huwa anatambua na kuukubali udhaifu wake na uzuri wake mwenyewe. Hujikubali alivyo. Hivyo ni mtu anayejiamini na hakatishwi tamaa na matukio wala watu wanaomzunguka. Kwa sababu hiyo, hufurahia kuchangamana na wengine. Hupenda kufanya kazi kwa kushirikiana na wenzake ingawa huweza pia kuzifanya peke yake na kwa ufanisi. Anapokumbana na changamoto, ni mwepesi wa kufikiri kuhusu ufumbuzi. Anapokwama mahali huwa hajisemei vibaya wala kuwalaumu wengine kama anavyofanya huyo wa awali. Badala ya kusema “Mie bwege” mtoto anayejifiria vizuri husema “Mbona sielewi imekuwaje hivi?”

Wazazi wanawezaje kusaidia
Je, mzazi anawezaje kumsaidia mwanae ajifikirie vizuri? Mambo yafuatayo yanaweza kusaidia:

Chunga unachosema
Watoto wako makini sana kwa maneno ya wazazi wao. Ukiwa mlopokaji, ujue mwanao anakutizama tegemea kuvuna yayo hayo.
Hebu kumbuka kumsifia mwanao si tu kwa kazi nzuri anazofanya, bali hata jitihada anayojaribu kuionyosha. Jitahidi sana kuwa mwangalifu mwanao asibaini kuwa sifa zako haziaminiki. Kuwa mkweli unaposifia kitu. Kwa mfano mwanao amefagia nyumba, na unaona wazi kuwa hajafagia kama ulivyopenda, kamwe usimshutumu kwa kusema, “ Utajifunza lini kufagia wewe…!” - hata kama unatania. Haifai kusema, “Hujaweza kufagia vizuri, rudia mpaka uweze.” Badala yake mwambie, “Umejitahidi sana kufagia nadhani kesho utafagia vizuuuri zaidi” au “Nimependa unavyojitahidi kufanya usafi, ninafurahi kuwa na mtoto anayependa kujituma kama wewe”. Pengine mwanao amekuletea taarifa mbaya ya matokeo ya mtihani. Kama mzazi huwezi kufurahi kuona matokeo ya namna hiyo wakati unateketeza fedha kwenye hiyo shule ya intanesheno anakosoma mwanao. Lazima utajaa ghadhabu. Pamoja na hayo jitahidi sana usimshutumu kwa maneno kama, “Nina hasara sana kupoteza hela zangu kwa jitu lisilojua maana ya shule…” Ukisema hivyo utamuumiza hasa kama atakuwa amejitahidi kwa kadiri ya uwezo wake na kumbe hujajua kilimfelisha. Badala yake, mwonyeshe kwamba hujafurahia alama hizo kwa sababu UNAAMINI anao uwezo wa kufanya vizuri.
Katika jambo lolote analofanya mwanao, usisubiri matokeo ndipo usifie ama kuonyesha kufurahia, badala yake sifia/furahia jitihada zozote anazoonyesha mwanao.

Kuwa mfano mzuri Ni maajabu ya mwaka kutaka mwanao awe usivyo wewe. Utakuwa kituko mbele ya mwanao kama unamdai awe na mtazamo mzuri ambao ni wazi anajua haunao. Kwa mfano mzazi anayesikia hovyo kuwa mwafrika kwa kujichubua, sauti yake haiwezi kusikika anapomshauri mwanae ajipende na kujikubali vile alivyo. Ataonekana mnafiki. Atavuna dharau za bure. Kwa hivyo kama unataka matokeo mazuri, jitahidi na wewe uwe hivyo utakavyo yeye awe. Usijihisie vibaya. Jiamini mwenyewe kwanza. Halafu onyesha kwamba wewe unajiamini. Bila shaka hutapata shida sana kumjengea mwanao self-esteem.

Tambua dhana potofu alizonazo mwanao na zishughulikie Ni jambo la maana sana kutambua dhana mbaya alizonazo mwanao. Anaweza kuwa amezisikia mtaani ama kwa marafiki zake. Ni vyema ukazibomoa kwa busara. Labda aliumizwa na kauli ya mwenzake iliyomzomea kuwa ana sura mbaya ama hana akili kabisa. Una wajibu wa kumweleza mbadala wa dhana hizo ambazo zinaweza kumwingia akilini na zikaharibu kabisa mtazamo wake. Ieleweke wazi kwamba hisia mbaya zinaweza kuota mizizi na baadae zikawa mbovu zitakazokugharimu kuziondosha. Kwa mfano mtoto asiyeisha kulalamika kwamba hawezi mahesabu kabisa kwa maneno kama “Mie hesabu siziwezi. Ninaona kama sina akili.” Hapa si tu kwamba huyu mtoto kafanya hitimisho-jumla lisilosahihi (false generalization) lakini pia huo ndio mwanzo wa kufeli kimojaaa hata katika masomo mengine. Jaribu kujua kwa nini anawaza hivyo. Pengine ni mwalimu wa Sitta amemwambia hivyo darasani. Mwonyeshe tofauti kwa dhati halafu mtie moyo mwanao alichukulie tatizo katika ukweli wake na si kwa jicho la wanafunzi wenzake. Ungeweza kumwambia: “Unazo akili ndio maana unafaulu masomo mengine. Hesabu ni somo kama masomo mengine, ingawa linakuhitaji kutumia muda mwingi kulisoma.”

Kuwa rafiki yake Wazazi wengi hawapendi kuzoeleka kwa watoto. Wanadhani hiyo itawapotezea heshima.Matokeo yake heshima hiyo inayotafutwa kwa nguvu, inawafanya watoto wajisikie kuwa mbali na wazazi wao. Usiwe hivyo. Tafuta urafiki wa karibu na mwanao. Kuwa karibu nae kadiri iwezekanavyo hata kama unabanwa na kazi. Ulipomzaa si ulijua kuwa una kazi nyingi? Mpende na awe na hakika kuwa unampenda. Ukifanya hivyo, utamfanya ajifikirie vizuri zaidi, na ajiamini. Mkumbatie mwanao. Mwambie alivyo fahari yako. Andika ujumbe kuelezea unavyomchukulia na uweke mahali atakapouona ghafla akiwa mwenyewe kama vile kwenye mfuko/begi lake la shule, kitandani kwake na kwingineko. Atafurahi. Hata kama wengine wanamponda kwamba si lolote si chochote, atawapuuza na kukuamini wewe. Msifie kila inapobidi ila kwa uangalifu usijekuta unalitia maji.

Mwelekeze kwa upole Kumwambia mwanao, “Sijui likoje....lione. Kila siku linagombana na dada’ake kwa mambo ya kipumbavu…mjinga kweli wewe…mwone alivyo mps****yyy(sonya)…” kutamwathiri. Atajiona kuwa unamwona kinyago na kikaragosi fulani. Ataugulia maumivu kwa kujua kuwa hutambui hisia zake na jitihada anazofanya kutatua migogoro. Matokeo yake yanaweza kuwa ni kukata tamaa. Kwa nini usimwambie, “Dada’ako kakuudhi sana. Lakini nafurahi kwamba leo hujamfokea wala kumpiga…!” Inaweza kuonekana sentesi ya kipole isiyoweza kufanya kitu kwenye akili ya mwanao, lakini ukweli ni kwamba atajifunza kwamba umetambua hisia na hali yake ya kuudhiwa na uamuzi aliouchukua. Kwa sababu atataka kukupendeza wewe, kwa namna unavyompenda, basi tarajia kuona mabadiliko zaidi siku nyingine.

Jenga mazingira safi ya malezi Mtoto asiyejisikia salama au yule anayejiona kuwa ananyanyaswa nyumbani anaweza kuugua ugonjwa wa “low self-esteem(Kujifikiria uduni)”. Mtoto anayelelewa na wazazi wasiomaliza siku bila kutoana ngeu na kukoromeana mbele ya watoto, hukata tamaa na mwenendo wa maisha. Huweza kupoteza hamu ya kuwa nyumbani kiasi kwamba hujiona mtu mwenye balaa kuzaliwa na wazazi kama nivyi. Anaweza kujenga chuki zisizotawalika na akawa mgomvi na mbishi dalili za kujifikiria-dhaifu. Jaribu kuchunguza ikiwa mwanao ameudhiwa huko alikokuwa, kama vile shuleni ama na marafiki zake, mwulize maswali yatakayokupa picha ikiwa yeye ndiye tatizo ama ni mhanga wa makosa ya wengine. Halafu mpe ushauri nasaha kwa zingatio hilo. Siku zote kumbuka kumpa heshima mwanao, utavuna uthubutu.

Msaidie mwanao ajifunze kujaribu Ni busara mzazi kujishughulisha sana katika kumsaidia mtoto awe na tabia ya kujaribu mambo. Shughuli zinazosisitiza ushirikiano wake na wenzake ni nzuri zaidi ya zile zilizokaa kimashindano shindano. Kwa hiyo kama unao watoto zaidi ya mmoja, ni vyema ukawapangia majukumu yenye kuwataka kushirikiana. Kwa mfano, unaweza kumshauri aliye mkubwa asaidie kumfundisha mdogo wake kusoma ama hesabu. Ukiwapa kazi zenye mkao wa kimashindano utaharibu. Yule ashindaye atajenga kiburi, majigambo na dharau, na yule ashindwaye atajiona hawezi hasa ikiwa imetokea mara kadhaa.

Ukifanya hivyo, bila shaka mwanao atajenga fikra-sahihi kwa nafsi yake na hivyo atajiamini. Kama utabaini kwamba mwanao anajidharau ama kwa lugha nyingine ana low self-esteem, ni vizuri kumwona mtaalam wa tiba ya ushauri nasaha (psychotherapy). Ingawa jamii yetu hapa nyumbani haitilii maanani suala la ushauri wa elimu-nafsi katika kutatua matatizo ya mawazo-nafsi, lakini hatuwezi kupuuza kamwe tiba hiyo ambayo inaweza kabisa kubadili kabisa mtazamo wa mwanao wake yeye binafsi na kwa wanaomzunguka. Hii itamsaidia kujitazama yeyekwa jicho lake kwanza na sio kwa jicho la mwingine linaloweza kumdanganya na kumpa dhana isiyosahihi. Hapo atajenga fikra mpya katika akili yake na atajikubali alivyo, na hivyo kuwa mtoto mwenye furaha na afya njema. Jaribu utaona matokeo.

Maoni

  1. Kazi kama hii uliyoandika hapa ingefaa sana kuchapishwa kwenye vi pamfleti fulani na kusambazwa kuwafikia hasa wazazi wapiya kila kona.Mambo unayoyazungumzia ni muhimu sana.Baadhi ya jambo ambalo JUMUWATA itabidi ifanye , ni kujaribu kupata njia ya kufikisha ujumbe kama huu hapa kwenye atiko yako katika kila kona zihusikazo. Malezi ya mtoto ni muhimu ingawa watu huchukulia eti, kila mtoto na riziki yake.

    JibuFuta
  2. Bwaya,nimekutag.
    Tujulishe vitu nane tusivyojua kuhusu wewe.

    JibuFuta
  3. I like this! hii ni nzuri sana.. nice job.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?