Vipi kuhusu mahausigeli?

Hapa nchini, hivi sasa karibu kila nyumba inamiliki mtumishi wa ndani anayejulikana kama hausigeli. Mahausigeli wamekuwa fasheni manyumbani mwetu. Bila hausigeli inaonekana kama vile haijatulia. Mwidimi Ndosi anawaona watumishi hawa kama watumwa.

Mahausigeli wengi ni wasichana waliokata tamaa ya maisha. Ni mabinti walioonja machungu ya makali ya maisha vijijini kwao na hivyo kuuzwa utumwani na wazazi wao wenyewe. Wengine ni wasichana walioikosa shule, japo waliipenda shule. Kisa? Kuna wanaume wakora waliutumia umasikini wa wazazi wao kuwadanganya na kulazimisha mahusiano nao, mahusiano ambayo huhitimika ghalfa pale inapoonekana kwamba yametengenza kiumbe tumboni mwa binti. Matokeo yake, binti ndiye hufukuzwa nyumbani eti kwa kosa la kuiaibisha familia. Shule inakuwa ndio basi. Mwenye mimba anakana mashitaka ya kuhusika na kiumbe hicho. Nyumbani inakuwa polisi. Binti anakosa kimbilio kati ya watu wake mwenyewe isipokuwa kupotelea mjini.
Matukio kama haya ya kinyama ndiyo hasa yamesababisha wimbi la akina dada-watumwa wanaotafuta kuendesha maisha kwa kugeuka walezi wa watoto wa binadamu wengi wanaozaa kwa shangwe pasipokutafakari yatakayojiri mara baada ya kiumbe husika kuzaliwa.

*******************
Zamani hizo, wanawake wengi walikuwa hawapati fursa za masomo. Hivyo waliishia kuolewa na kuwa akina mama wa nyumbani. Mgawanyo wa kazi ulionyesha kwamba kazi ya kutafuta kipato cha familia, ilikuwa ni ya muoaji ambaye mpaka tunapoyaandika haya, ni mwanaume. Mwanamke, mama wa familia alikuwa na majukumu ya kutunza nyumba na kulea watoto. Hivyo katika siku hizo, nasikia wimbi hili la mahausigeli halikuwa hivi lilivyo hivi sasa. Na kama ililazimu sana familia kuwa na mtumishi wa aina hii, basi kazi yake ya msingi ilikuwa ni kuosha vyombo na kufagia nyumba na labda kazi nyingine ndogondogo.

Siku hizi mambo yamebadilika sana. Waswahili tumeendelea kupundukia. Maendeleo haya ambayo yanahusisha jinsia zote, yameleta tofauti kubwa na hivyo ilivyokuwa zamani hizo. Kwanza wanawake wengi siku hizi, wamepata fursa ya kupata elimu. Na kwa sababu hiyo, uwezekano wa kuoa mama wa nyumbani siku hizi, pia umepungua sana kiasi cha kufikia mahali tunaweza kusema lazima uoe mwanamke aliyeenda shule. Kwenda shule kuna maana ya yeye pia kuwa bize na shughuli za kuajiriwa ama kujiajiri. Hapo ndipo panapotokezea hitaji la dada-mtumwa anayeitwa hausigeli.

Hausigeli huyu kazi yake kubwa ni kufanya kazi zote za mama mwenye nyumba. Kazi hizo nyingi, ni pamoja na kulea watoto wa bosi na mkewe ambao kusema kweli hawana muda wa kukaa nyumbani na watoto waliokubaliana kuwazaa wao wenyewe tena kwa hiari. Utakuta mtoto anaamka asubuhi wazazi (soma wazaaji) walishakwenda makazini saa nyingi, anakutana na sura ya dada-mtumwa kila aamkapo. Atakaye mwosha uso, na kumpatia kifungua kinywa, tena mara nyingi akikifaidi yeye, ni hausigeli . Ndio huyo huyo dada-mtumwa atayekaa nae kutwa nzima mpaka wenye mtoto watakaporudi usiku saa mbili kasoro ama na madakika.

Basi, wenye mtoto watadumu na mwanao kwa dakika kiduchu mno, kwani wamechoka sana kama unavyojua kutafuta hela kunavyochosha, we acha tu. Mtoto naye kazurura mchana kutwa akipigizana kelele na dada-mtumwa, kwa hiyo ndiye atakayeanza kusinzia na kupelekwa kitandani na hausigeli. Ikiwa mtoto anayo mahitaji fulani yanayohitaji fedha, hausigeli ndiye msemaji, mwenye jukumu la kutaarifu wazazi. Na kwa sababu wazazi wote wanafanya kazi na fedha “wanazo”, hapo hakuna wasi, fedha zitaachwa kwa hausigeli na nyongeza yake. Wenye mtoto wakipongezana kwamba wao kama “wazazi” wanatimiza wajibu wao wa kumpatia mwanao kila anachohitaji kwa wakati. Asubuhi yake hausigeli anamaliza matatizo yote kama mama.

Wazazi wengine wameendelea. Wao wanaona afadhali basi mtoto apelekwe kwenye shule zinazomilikiwa na walanguzi mabeberu wanaowaibia watu kwa madai kuwa wanao “walimu bigwa” wa kutunza watoto. Shule hizo ndio hizi za “Mtakatifu Dei-kea”. Kwa hiyo, mtoto atakabidhiwa huko kila siku asubuhi na kurudishwa nyumbani kwa gari baada ya saa za masomo. Wazazi wengine waliopiga hatua za kimaendeleo zaidi, wanawapeleka katika Intenesheno za kulala. Hii ikimaanisha kuwa mtoto huyo ataishi na watu asiowafahamu waonaitwa walimu, kwa miezi kadhaa, akiachwa ajifunze kila aina ya mfumo wa maisha pasipo maelekezo yanayoeleweka. Baadae mtoto huungana na familia yake kwa kifupi sana, kabla ya “kuwahi masomo” muhula unaofuata na kuendelea.

Huu ndio mtindo ambao wa-Tanzania wenye hela zao wanaufuata. Swali la kujiuliza: Je, mtindo huu wa malezi ni wa lazima? Je, ni wa kuendelezwa? Ikiwa ni lazima kuufuata tutauboreshaje? Mtoto kulelewa na wasichana-watumwa waliokata tamaa ya maisha, tena wanaolipwa hela za bamia, hauna athari katika makuzi ya mtoto? Tafakari.

Maoni

  1. kwkweli msitutatanishe kwani kuwa mfanyakazi wa ndani sio kazi??? we can't all be managers so someone has to do something else.Ila tu waajiri msiwabeze na kuwapiga hawa wafanyakazi wa ndani.Maana waajiri wengine huwa wanapenda utumwa.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?