Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Kama tulivyoona katika makala yajuma lililopita, usaili ni hatua ya mwisho kuelekea kupata kazi. Sehemu kubwa ya usaili ni maswali na majibu yanayolenga kupima uwezo wako wa kukabiliana na changamoto halisi za kazi.

Ingawa yapo maswali yanayoweza kukupa wasiwasi wa nia ya mwuulizaji, fahamu kuwa hakuna swali linaulizwa kwa nia mbaya au kwa bahati mbaya. Kila swali linaloulizwa linalenga kutafuta uthibitisho kuwa wewe ni mtu sahihi kwa kazi unayoomba.

Vijana wengi wenye ufaulu mzuri wanaoomba kazi, hujikuta pasipokujua, wakifanya makosa madogo yanayowagharimu. Kwa kuwa umetumia muda wako kuandika barua, kuandika wasifu wako wa kazi, wakati mwingine kusafiri kwenda kuhudhuria usaili, ni muhimu kufanya maandalizi yatakayokuongezea nafasi ya kufanikiwa.

Katika makala haya, tutaangazia baadhi ya maswali yanayoulizwa kwenye usaili wa kazi na namna unavyoweza kuyajibu.


Mapokezi

Unapokaribishwa kwenye usaili, jambo la kwanza ni kuhakikisha kuwa unatengeneza taswira ya mtu anayejitambua, mkomavu na mwenye nidhamu. Salimia jopo linalokupokea kwa tabasamu na salamu ya adabu yenye kuonesha kujiamini. Ikiwa ni lazima kushikana mikono na wanajopo, fanya hivyo kwa kujiamini.

Kisha, kuwa mtulivu uelekezwe mahali pa kukaa. Hakuna sababu ya kuwa na papara kukaa mahali hata kama unahisi ndiyo sehemu iliyoandaliwa kwa ajili yako. Unapokaa, kaa mkao unaoashiria mtu mnyenyekevu asiye na makuu. Mara nyingi kukaa wima ni vizuri na kuambatane na hali inayoonesha kuwa unayo motisha ya kupata kazi unayoomba.

Kunja miguu yako kistaarabu, ukikutanisha mikono yako juu ya mapaja kutuma ujumbe wa mtu mtulivu. Egemea mbele badala ya nyuma, watazame wana jopo machoni. Kwa haraka, wazoee wana jopo kwa kuwaona ni watu wa kawaida, lakini wanaostahili heshima.

Unapojibu maswali, epuka kutikisa kichwa. Kukunja nne, kuegemea nyuma, au kuweka mikono kwa namna inayoonesha mamlaka, ni kutuma ujumbe hasi usiokusudiwa.

Utambulisho

Kumbuka kuwa usaili wako ulianza tangu jopo la usaili lilipopokea nyaraka zako. Kwa kiasi fulani, tayari wanayo taswira fulani kukuhusu. Una kazi muhimu ya kuwathibitishia kuwa hayo uliyoyaandika yana ukweli.
Mara nyingi unapokaribishwa kwenye usaili, kiongozi wa jopo la usaili, atawatambulisha kwa wenzake. Anapofanya hivyo, ana lengo la kukufanya uwazoee wanajopo, utulie na usiwe na wasiwasi. Shukuru kwa utambulisho wao.

Kiongozi huyo anaweza kukutambulisha wewe kwa jina lako na kukaribisha maswali. Mara nyingi swali linaloanza ni, ‘Tuambiwe wewe ni nani?’ ‘Karibu ujitambulishe…’

Swali kama hili halihitaji utaje majina yako bali kufahamu mhutasari wako kikazi. Ingawa utakayoyasema yatatokana na uliyoyaandika kwenye wasifu wako wa kazi, mara nyingi hautarajiwi kurudia maelezo hayo.

Jipambanue wajihi wako kikazi na kiutendaji. Jopo linatarajia uwambie mambo ya msingi unayoyaamini yanayoweza kuwasaidia kuelewa mtazamo wako kikazi. Ongelea majukumu ya kikazi uliyowahi kuyafanya ukiyaonanisha na kazi unayoiomba. Anza na kazi ya nyuma zaidi ukimalizia na kazi unayoifanya sasa hivi au ya hivi karibuni zaidi.

Ari na uwezo wako wa kazi

Unaweza kuulizwa, ‘Kwa nini  unafikiri tukuchukue kwa nafasi hii?’, ‘Kwa nini unataka kufanya kazi na sisi?’ Watu wengi wanapoulizwa swali hili hufikiri wanachohitaji ni kujilinganisha na wengine kwa majina. Huna sababu ya kuwataja wengine kama namna ya kuonesha unavyofaa zaidi.

Kwa swali kama hilo, kimsingi wanataka kuona kama unaielewa taasisi yao. Thibitisha kuwa umeitafiti taasisi kwa kina, na una uelewa wa huduma wanazotoa. Onesha unavyojisikia kuwa sehemu ya malengo mapana ya taasisi yao.

Kadhalika, ni fursa kwako kuonesha namna gani vipaji na ujuzi ulivyonavyo vinaweza kumsaidia mwajiri wako mtarajiwa. Lijibu kwa ujasiri, bila kusita. Ukionesha wasiwasi katika majibu yako, wanaokusaili nao watakuwa na wasiwasi na uwezo wao. Onesha namna gani unafaa kuajiriwa kwa sababu ya uwezo wako.

Katika eneo la ari na uwezo wako wa kazi, unaweza kuulizwa, ‘Unafikiri utaongeza tija gani katika taasisi yetu?’

Hapa ongelea ujuzi na uzoefu wa kazi unaofikiri unaweza kumsaidia mwajiri wako kutatua changamoto alizonazo. Jitahidi kuonesha namna ujuzi na vipaji ulivyonavyo vinavyoweza kutumika katika maeneo mengine zaidi ya nafasi unayoomba. Kwa kawaida, mwajiri huvutiwa na mtu anayeweza kutumika katika eneo zaidi ya moja.

‘Unaweza kuniambia mapungufu uliyonayo?’ Usiwarahisishie kazi ya kuyaelewa mapungufu yako waziwazi. Waache wao wenyewe wayajue. Badala yake zungumzia ‘mapungufu’ ambayo mtu akiyatafakari anaona ni tija.

Mfano, ‘napenda kufanya kazi muda mrefu’, ‘Nina tabia ya kufanya mambo kwa ukamilifu kiasi cha kujikuta sina muda wa kutosha kukamilisha kazi kwa wakati ninaotaka’

Uzoefu wako huko ulikotoka

Unaweza kuulizwa maswali mengi kuhusu uzoefu wako kazini. Ikiwa kwenye wasifu wako wa kazi ulionesha kuwa uliwahi kufanya kazi mahali na ukaiacha, unaweza kuulizwa swali, ‘Kwa nini uliacha kazi yako?’ au ‘Kwa nini unataka kuacha kazi uliyonayo?’

Hili ni swali gumu. Mwuulizaji analenga kupima uaminifu wako na anataka kujua mambo gani hasa yanakuridhisha kazini. Kimsingi lengo sio kujua yaliyofanyika huko uliko (kuwa) bali kujua unavyoweza kumfaa. Hutakiwi kuzunguka kwa kutafuta sababu zisizo za kweli. Jibu kwa urahisi na uwazi lakini ukiwa makini.

Inaendelea

Shukrani kwa Fr Aldalbert Donge, Mkurugenzi wa Raslimali Watu, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, kwa kuchangia uzoefu wake katika maandalizi ya makala haya.

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Pay $900? I quit blogging

Haiba ni nini?

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Heri ya mwezi mpya!