Jinsi ya Kukuza Umahiri wa Lugha kwa Mtoto

Tunahitaji lugha katika maisha yetu ya kila siku. Tunapofikiri mambo yaliyopita, yaliyopo na yajayo, tunatumia lugha. Tunapowasiliana na wengine, tunahitaji lugha. Lugha, katika mukhtadha huu, ni nyezo muhimu inayotuunganisha na watu wanaotuzunguka.

Ingawa wataalam wa namna mtoto anavyojifunza lugha hawana jibu moja, ni wazi zipo kanuni za matumizi ya lugha ambazo mtoto huzaliwa nazo. Lakini pia mazingira anayokulia mtoto, nayo yana nafasi kubwa ya kujenga uwezo wake wa kutumia lugha.

Ndio kusema, kama mzazi unahitaji kuelewa kuwa unao wajibu mkubwa wa kumsaidia mwanao kuwa mahiri katika lugha. Kujifunza lugha kunafuata hatua kadhaa.



Hatua ya kwanza ni kulia

Mtoto hulia ‘kuwaambia’ wanaomzunguka kuwa haridhishwi na jambo, ana njaa, maumivu, ana wasiwasi, hasira au basi tu anahitaji kusikilizwa.

Lakini kadri anavyozidi kukua kimwili, lugha ya kulia hupungua na mtoto huanza kujifunza kuwasilisha hisia zake kwa kutumia sauti zisizoeleweka.

Kujifunza maneno ya kwanza

Mtoto wa miezi miwili hadi sita huanza kujifunza kutumia sauti zinazotuma ujumbe kwa wengine. Mfano, katika umri huu mtoto huwa na tabia ya kurudia rudia sauti kama ‘Brrrr-brrrrr!’ ‘La-la-la!’ ‘m-mmo-mo’ kuonesha hisia zake.

Lakini anapofikia umri wa miezi sita mtoto huanza kujifunza lugha ya mama yake hatua kwa hatua kwa kutumia maneno rahisi. Kwa kawaidia, maneno ya kwanza kabisa ni majina ya watu waliokaribu naye kama, ‘mama’, ‘dada’.

Kuongeza msamiati

Mtoto husikiliza mazungumzo ya watu wanaomzunguka ili aongeze msamiati wake. Mpaka anapofikia umri wa miaka mitatu na minne mtoto huwa tayari amejifunza maneno mengi yanayomwezesha kuelezea mambo mengi anayoyajua.

Hata hivyo, ni kawaida kwa neno moja kuwa na maana zaidi ya moja. Mfano anaposema ‘mma’ anaweza kuwa na maana ya ‘mama’, ‘maji’ na ‘njaa’ kwa sababu uelewa wake huzidi idadi ya maneno aliyonayo.

Umahiri wa lugha

Mtoto huwa mahiri wa lugha anapofikia umri wa miaka mitano na sita. Katika hatua hii mtoto huwa na uwezo wa kujieleza vizuri na kuuliza maswali kwa lugha inayoeleweka. Uwezo huu hutegemea, kwa kiasi kikubwa,msaada anaoupata kutoka kwa wanaomzunguka.  
Ili kufikia hatua ya umahiri wa lugha, watafiti wanashauri njia kadhaa zinazoweza kumsaidia mtoto kujifunza lugha.

Ongea naye kwa lugha ya kitoto

Hii ni lugha ya mtu mzima yenye kutumia maneno rahisi yaliyotiwa chumvi kidogo, yanayotamkwa kwa sauti ya juu. Lengo la lugha hii ni kumhamasisha mtoto kuvutiwa kuongea. Kadri tunavyojibidiisha kuongea naye kitoto tunampa hamasa ya kujifunza.

Sahihisha lugha yake

Rudia kutamka kwa usahihi maneno anayojaribu kuyatumia. Mfano, anaposema, ‘mma’ rudia kwa usahihi, ‘Unataka maji? Chukua m-to-to!’ Kurudia maneno yake humsaidia kuiga utamkaji sahihi.

Unapomsahihisha, wakati mwingine ni vizuri kuongezea maana ya kile anachokisema. Kwa mfano, anaposema, ‘baba kuja’, unaweza kumsaidia kutengeneza sentensi fupi na sahihi zaidi kama, ‘Ndio! Baba anakuja!’ ili kumfundisha kilichosahihi.

Oanisha maneno na vitu anavyoviona

Jitahidi kutamka maneno kwa kuyaoanisha na vitu anavyoviona. Mfano, tamka neno ‘viatu’ akijua unaongelea viatu anavyoviona ili iwe rahisi kukumbuka na kuhusianisha anachokikumbuka na neno hasika.

Mpe vifaa, mruhusu kucheza

Kucheza ni fursa nzuri ya mtoto kuwasiliana na kujadiliana na wengine aina ya mchezo wanaoutaka, kanuni zinazohusika, mjadala pale sheria zinapovunjwa, mambo ambayo hukuza uwezo wake wa kujieleza.

Kadhalika, mtafutie CD za katuni, nyimbo na masimulizi, vitabu vyenye picha na ikibidi mruhusu kutazama vipindi vya televisheni vyenye maudhui yanayomfaa. Haya yote yanamwongezea uelewa wa maneno asiyoyasikia katika mazungumzo hapo nyumbani.

Zungumza naye

Mazungumzo ya kirafiki na mtoto pia yanamhamasisha kujifunza matumizi sahihi ya lugha. Kuongea naye, kunampa nafasi ya kuiga na kujifunza maneno yanayobeba mawazo mapana zaidi ambayo kwa hali ya kawaida pengine asingeyasikia kwa watoto wa umri wake.
Unapoongea nae, hata hivyo, ni muhimu kuhakikisha lugha inakuwa rahisi, wazi na ya moja kwa moja. Lugha ngumu isiyoeleweka kirahisi haimsaidii kujifunza.

Mwulize maswali yanayofikirisha

Maswali yanayohitaji kufiria kwa kina yanamsaidia kukuza umahiri wake wa lugha. Badala ya kumwuliza maswali yenye majibu ya ndio na hapana, au yale yenye majibu mafupi, mwuulize maswali yanayoitaji maelezo marefu kidogo.

Kwa mfano, maswali yanayoanza na ‘kwa nini’, ‘kivipi’, ‘namna gani’ yanamfanya afikirie zaidi na yanamsaidia kutafuta maneno sahihi ya kukuambia kile alichonacho kichwani.  

Mpe nafasi ya kukusimulia

Imethibitika kuwa watoto wanaopata fursa ya kusimuliza mambo yao kwa wengine, wanakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuijua lugha zaidi ya wale wasiopata fursa hiyo.

Anapokusimulia mambo anayokutana nae siku nzima, analazimika kutafuta maneno yake mwenyewe yatakayoelezea jambo analotaka kulieleza kwa usahihi. Kufanya hivyo humsaidia kujifunza kuelewa namna ya kuelezea hisia zake kwa kutumia maneno sahihi na kwa wakati sahihi.


Kwa mhutasari, msingi wa umahiri wa lugha kwa mtoto ni wewe mzazi. Jitahidi kumpa mtoto usaidizi wa karibu ili ajifunze namna gani atumie lugha katika kujieleza na kuwaelewa wanaowasiliana naye. 

Fuatilia jarida la Maarifa ndani ya gazeti la Mwananchi kila Jumanne kwa makala kama hizi.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia