Mbinu Sita za Kukumbuka Maarifa Unayojifunza
Mafanikio
ya kitaaluma, kwa kiasi kikubwa, yanategemea namna unavyoweza kusoma na
kukumbuka kile ulichokisoma. Kusoma kwa bidii na kuelewa unayoyasoma ni muhimu.
Lakini kama huwezi kukumbuka ulichokielewa, itakuwa vigumu kufanikiwa.
Mitihani,
kwa mfano, hupima uwezo wako wa kukumbuka kile unachokijua. Hiyo, hata hivyo,
haimaanishi uishie kukumbuka. Unahitaji kuelewa unayojifunza kwa kina lakini
pia uwe na uwezo wa kukumbuka.
Kwa
kawaida, akili ya mwanadamu haikumbuki kila taarifa. Huchagua kipi cha
kusahaulika na kipi cha kukumbuka. Ndio maana tunaona mengi lakini tunakumbuka
yale machache ambayo akili inayapa uzito.
Ingawa
kusahau kuna faida zake, wewe kama mwanafunzi ungependa kukumbuka mambo
unayoyasoma. Uzoefu unaonesha kuwa hata
kama tunapenda kukumbuka, wakati mwingine tunasahau yale tunayotamani
kuyakumbuka.
Makala
haya, kwa kutumia uchambuzi wa tafiti mbalimbali za elimu ya kujifunza,
yanapendekeza mbinu sita kukuwezesha kukumbuka.
Furahia
unachotaka kukikumbuka
Maya
Angelou aliwahi kusema, watu huweza kusahau yale uliyowaambia, lakini hawawezi
kusahau ulivyowafanya wajisikie. Kisayansi jambo hili ni kweli. Tunakumbuka kwa
urahisi zaidi mambo yanayogusa mioyo yetu kuliko fahamu zetu.
Unapoudhiwa
na mtu, kwa mfano, ni rahisi kukumbuka. Unapofurahishwa na jambo, hulazimiki
kukariri ili ukumbuke. Ndio kusema, hisia zako zinapokuwa zimeguswa moja kwa
moja ni rahisi kukumbuka kilichokugusa. Tumia kanuni hiyo unaposoma.
Jitahidi
kufurahia kile unachojifunza. Penda masomo yako. Kama unasoma Hisabati, anza
kwa kuipenda. Unapopenda kile unachokisoma, unaongeza uwezekano wa kukikumbuka.
Usipopenda masomo, itakuwa rahisi kusahau.
Fahamu wazo kuu kabla ya undani
Kwa
kawaida, akili haipendi kuhangaika. Hutafuta namna rahisi ya kuelewa jambo. Kama
unataka kuiongezea uwezo wa kukumbuka jambo unalokusudia kulikumbuka, isaidie
akili yako kuingiza vitu kichwani hatua kwa hatua. Usisome kwa mkupuko. Soma
kwa awamu.
Anza
kwa kuelewa wazo kuu la kile unachojifunza kabla hujaweka nguvu kuelewa undani
wake. Unapoelewa maarifa ya jumla kwanza, unajenga msingi wa hatua ya pili ya
kuingiza taarifa za kina kujazia kile ambacho tayari akili yako inakijua.
Ndio
kusema, unahitaji kusoma kwa utaratibu bila papara. Soma mara ya kwanza kupata
wazo kuu linalobeba uelewa wa jumla kwanza. Ukishaelewa, tafuta muda wa
kuongeza taarifa za undani wa kile unachokijua.
Tafuta
mfanano na utofauti wa dhana
Kuelewa
unachokisoma kunategemea ni kwa kiasi gani hicho unachokisoma kinaoana na kile
unachokifahamu. Akili ina kawaida ya kupangilia maarifa kwa kuhusianisha kile kinachoingia
akili na kile kilichopo tayari.
Unapoingiza
taarifa isiyofanana na kile unachofahamu, utatumia nguvu nyingi bila sababu. Kwa
hivyo unashauriwa kusoma kidogo kidogo kwa kuhusianisha kile unachokisoma na
kile unachokifahamu ili kurahisisha kazi ya akili kupangilia mambo kukuwezesha
kuelewa.
Hata
hivyo, ili uweze kukumbuka baadae, lazima ujue namna gani hicho unachokiingiza
akili kinatofautiana na kile unachokijua tayari. Ni vizuri unaposoma ujiulize,
‘hiki ninachokisoma kinatofautianaje na ninachokifahamu?’
Oanisha unachokisoma na maisha
halisi
Akili,
kama tulivyoona, ina kawaida ya kukumbuka mambo inayoyachukulia kuwa ya muhimu.
Mambo yasiyo na umuhimu akili huachana nayo na kuyasahau. Sambamba na hilo, ni
rahisi kukumbuka maarifa yanayoendana na maisha halisi kuliko maarifa yasiyo na
uhusiano na maisha yetu.
Unapopita
barabarani, kwa mfano, unakutana na watu wengi ambao kimsingi huwezi
kuwakumbuka. Lakini unapokutana na mtu anayehusiana na maisha yako, ni rahisi
kumkumbuka.
Jaribu
kuhusianisha maarifa unayojifunza na maisha yako ya kila siku. Kama huwezi
kuona namna gani hayo unayoyasoma yanahusiana na maisha yako ya kila siku,
lazima utasahau.
Tumia maarifa unayojifunza
Wataalamu
wa elimu wanasema hatua ya juu kabisa ya kujifunza ni kutumia kile unachokijua.
Uelewa usiotumika hakuna maana. Ndio maana walimu wazuri husisitiza mwanafunzi
afanye kitu kama matokeo ya kujifunza.
Mwalimu
atakupa kazi ya kusoma mwenyewe, atakufanya ujadili na wenzako, lengo likiwa kukushughulisha
utumie maarifa unayojaribu kujifunza kwa wakati huo kwa kuyaongelea, kuyaandika
na namna nyingine za kuyatumia.
Jenga
tabia ya kutumia maarifa yako. Andika kila unaposoma. Fundisha wenzako. Jadili
na wenzako. Fanya maswali mara kwa mara. Kufanya hivyo, kunakusaidia kuyamiliki
maarifa uliyonayo na hivyo kurahisisha kazi ya kukumbuka.
Inapobidi, kariri
Pamoja
na umuhimu wa kuelewa taarifa tunazojaribu kuzikumbuka, bado wakati mwingine
tunakutana na taarifa zisizohusiana na yale tunayoyafahamu. Tunapotaka
kukumbuka namba za simu, kwa mfano, tunalazimika kukariri. Hatuwezi kusema
tunazielewa tarakimu kumi zinazotambulisha namba ya simu.
Katika
mazingira kama haya unahitaji kukariri. Ingawa watu wengi hubeza neno
‘kukariri’ na kulihusianisha na kutokuelewa, lakini ukweli ni kwamba kukariri
ni sehemu ya maarifa tuliyonayo.
Jifunze
mbinu za kukariri kwa urahisi. Rudia rudia kile unachotaka kukikumbuka.
Unaporudia rudia jambo hata kama hulielewi, unaongeza nafasi ya kulikumbuka. Unaweza
pia kutumia herufi za mwanzo za orodha ya hoja unazotaka kuzikumbuka
kutengeneza maneno unayoweza kuyakumbuka kirahisi.
Fuatilia Jarida la Maarifa ndani ya gazeti la Mwananchi kwa makala kama hizi.
Nmependa na ningependa npate ushauli mwingi wa namna ya kukalili na kufulah kile ktu. Unachokikalili
JibuFuta