Mpe Mtoto Wako Fursa ya Kujifunza Maisha Halisi
Katika
mazingira yetu, si wazazi wengi wanaweza kuwa tayari kuona watoto hawawezi kufanya
kazi za nyumbani kama kupika, kufua nguo, kusafisha vyombo na kutandika
kitanda.
Lakini
kutokuweza kufanya kazi hizi, wakati mwingine kunatokana na mitazamo ya wazazi
kuwa kazi za ndani hufanywa na mama peke yake au msichana/kijana wa kazi na
hivyo watoto hawaruhusiwi kushiriki kazi ‘zisizo zao’.
Utaratibu
huu, hata hivyo, unaweza kuwa na athari kwa maisha ya mtoto pale atakapoondoka
nyumbani na kuanza kuishi na watu wengine. Hata kama mtoto anaweza kuwa mwerevu
na mchangamfu, bado huweza kuonekana kama mtu mvivu, tegemezi na asiyejua
maisha.
Ni
kwa sababu hiyo, wazazi wanao wajibu muhimu wa kumfundisha mtoto kuwajibika na
kufanya kazi za mikono kungali mapema.
Malezi ni kukuza uwezo wa kujimudu
Mbali
na kutengeneza mazingira ya mtoto kukua kiakili, kimwili, kihisia na
kimahusiano, lipo eneo muhimu la kimakuzi linalosahaulika. Nalo ni uwezo wa
mtoto kufanya vitu bila msaada mkubwa wa watu wazima.
Uwezo
huu humsaidia mtoto kukabiliana na changamoto za maisha na huimarika kadri
mtoto anavyokuwa kiakili na kimwili. Mifano rahisi ya uwezo wa kujimudu
anaozaliwa nao mtoto ni kukaa bila msaada, kusimama, kutembea mwenyewe na hata kutumia
vifaa mbalimbali bila kuleta uharibifu.
Pia
yapo maeneo ya kujimudu ambayo mtoto huhitaji kujifunza kama vile kulala bila
kukojoa kitandani, kula mwenyewe, kujiogesha, kupiga mswaki, kufua nguo zake na
kuvaa nguo.
Kadhalika,
kujimudu huenda sambamba na kuwajibika, yaani kuwa tayari kufanya majukumu bila
kuwasubiri wengine wafanye. Ni kinyume cha uvivu na kutegea. Faida yake ni
kumwongezea mtoto uwezo wa kujiamini.
Tuangalie
maeneo matatu muhimu yanayohitaji mkazo katika kukuza uwezo wa mtoto kujimudu
na kujitegemea.
Kujimudu
kimwili
Kama
tulivyodokeza awali, mtoto huzaliwa na uwezo wa kujitegemea kimwili wakati
mwingine bila msaada. Kwa mfano, mpaka anapotimiza miezi sita, mtoto humudu kiwiliwili
chake na kuweza kunyanyua shingo na kichwa hata anapokuwa amelala kifudifudi.
Kati
ya mwezi wa 8 na 9, huanza kusimama kwa msaada wa vitu, na hutembea mwenyewe
ifikapo mwezi 10 hadi 15 tangu azaliwe.
Baada
ya miezi 18, mengi anayoyafanya mtoto yanahitaji uongozi wa karibu wa mzazi.
Mfano ili aweze kujua kushika vitu, kujilisha, kujisaidia kwa usafi, kufungua
vifungo vya nguo na kuvaa nguo, ni lazima afundishwe.
Mzazi
anahitaji kujua nini afanye ili mtoto aweze kujimudu kulingana na umri wake.
Tuchukulie mfano wa kufundisha mtoto kujisaidia haja ndogo kwa muda maalum. Kwa
mtoto asiye na matatizo ya kiafya, mzazi anahitaji kumzoeza mtoto kujisaidia
kwa muda wa maalum.
Mbinu
nyingine ni pamoja na kumpunguzia vimiminika nyakati za kulala pamoja na
kutengeneza muda maalum wa kumwamsha kujisaidia nyakati za usiku ili aache
mazoea ya kulowanisha kitanda anapokuwa usingizini.
Kumfundisha
kujisafisha mwenyewe
Usafi
ni eneo muhimu la kujimudu ambalo mzazi anahitaji kulikazia mapema. Kwa mfano, katika
umri wa kati ya miezi 10 na 15 mtoto tayari ameota meno na anaweza kushika kitu
vizuri kwa mikono yake hivyo unaweza kumfundisha kutumia mswaki.
Usafi
ni pamoja na kujitawadha baada ya kujisaidia. Lazima mzazi ujenga ulazima wa
mtoto kujisafisha mwenyewe hasa anapofikisha miaka mitatu. Mazoea haya yasipoanza
mapema, mtoto anaweza kuwa mtu mzima asiyejua kama ni lazima kujisafisha.
Vile
vile, kati ya miaka minne na mitano, anza kumtaka alazimike kutandika kitanda na
kusafisha chumba chake, kuoga, kufua nguo za ndani na soksi. Unaweza kumpa
msaada pale unapohitajika lakini ikae akili mwake kuwa hakuna mtu anayewajibika
kumfanyia kazi hizo. Kufanya hivi sio kumtesa mtoto, bali ni kumjengea tabia ya
uwajibikaji.
Kumshirikisha
majukumu ya ndani
Siku
hizi wazazi wenye uwezo wanawategemea akina dada wa kazi kufanya kazi zote za
ndani. Katika mazingira haya, mtoto anajikuta hajui kufanya chochote isipokuwa,
kama ana bahati, kufanya usafi wake binafsi.
Mshirikishe mtoto kufanya kazi za usafi tangu akiwa mdogo |
Hata
hivyo, kwa kawaida, watoto huwa na shauku ya kushiriki kazi za ndani ikiwa
watawekewa mazingira mazuri. Kwa nini basi mzazi usimpe nafasi mwanao kushiriki
kuosha vyombo, kufagia, kudeki, kumwagilia maua?
Mpangie
ratiba maalum ya kufanya kazi za nyumbani akishirikiana na watu wazima waliopo
nyumbani. Kama mazingira yanaruhusu, mtume aende sokoni na dukani akifuatana na
watu wazima. Lengo si kuishi maisha ya kimasikini bali kumpa nafasi ya
kujifunza majukumu ya kila siku hapo nyumbani.
Kwa
kufanya haya yote, tutakuwa tunawasaidia watoto kuwa watu wenye utimamu wa
tabia wanaoweza kuishi na watu wengine pasipokuwa mzigo. Usimnyime mtoto fursa
ya kujifunza maisha halisi.
Fuatilia jarida la Maarifa ndani ya gazeti la Mwananchi kila Jumanne kwa makala kama hizi.
AHSANTE SANA KWA DARASA HAKIKA NIMEAMINI ELIMU SIO KUNYIMANA INGAWA TAYARI NIMEKWISHA YAPITIA HAYO ....
JibuFutaAsante sana dada Yasitha! Tuendelee kujadiliana :)
JibuFuta