Jinsi ya Kumsaidia Mtoto Aweze Kushirikiana na Wenzake
Kushirikiana ni uwezo wa mtoto
kuelewa watu wengine wanatarajia nini kwake. Mtoto mwenye ushirikiano na watu,
ni mwepesi kutoa alichonacho, ni msikivu, hufanya kazi na wenzake, hucheza kwa
ushirikiano na wenzake na huwa na uwezo wa kutafuta suluhu pale anapojikuta
katika mazingira ya ugomvi.
Kushirikiana na wengine ni tofauti
na nidhamu. Nidhamu ni kufanya kile unachojua kinatarajiwa na wengine hata kama
moyoni unaamini vinginevyo. Mfano, mtoto anapokwenda kulala kwa sababu anajua
ni lazima afanye hivyo, hiyo ni nidhamu na si lazima iwe ushirikiano. Makala
haya yanapendekeza njia nne za kumsaidia mtoto kushirikiana na wengine.
Onekana ukishirikiana na watu
Ikiwa unataka mwanao awe na tabia ya
kushirikiana na watu, ni muhimu uanze wewe kuwa mfano wa namna tunavyoweza kushirikiana
na wengine.
Kwa mfano, wape watu vitu mbele
yake, shiriki kazi za ndani pale inapowezekana na onesha kuwapenda watu wengine
wakiwemo rafiki zake. Kufanya hivyo kutakuza imani ndani ya mtoto kuwa katika
maisha si rahisi mtu mmoja kufanya kila kitu bila msaada wa wengine.
Kadhalika, unapoongea nae tumia
lugha inayoonesha kuelewa ‘dunia’ yake. Mtoto anayejisikia kueleweka, ni rahisi
kuwa na ushirikiano. Kwa hiyo badala ya kupambana nae kwa ugomvi, jifunze kuwa
mtulivu hata pale unapokuwa na hasira. Mtoto atajifunza kushirikiana na wewe.
Aone faida za kushirikiana
Weka mazingira ya mtoto kuona faida
za kushirikiana na wengine kwa kushiriki michezo yake. Kwa mfano, anapokuwa na
changamoto ya kutatu kitu fulani, msaidie ili atumie muda mfupi zaidi. Tafsiri
atakayoipata ni kuwa unapofanya kazi na watu wengine, unaokoa muda na unaweza
kufanya vizuri zaidi.
Pia mshirikishe kazi zako
ukihakikisha kuwa atapata faida ya moja kwa moja. Kwa mfano, anaweza kutegemea
kuwa ifikapo saa fulani utamsomea kitabu. Lakini wewe unayo kazi ya kufanya
usafi kabla ya muda huo. Mkaribishe akusaidie ili mmalize kwa wakati mpate muda
wa kufanya kile anachokitarajia.
Mpe nafasi ya kuchagua, mwelekeze
Jizoeze kutoa maelezo rafiki badala
ya amri. Kwa mfano, kama unataka akalale mapema ili awahi shule kesho asubuhi,
kumwambia, ‘Zima TV nenda kalale!’ ni kumwamuru. Lakini unaweza kutumia lugha ya
kirafiki, ‘Saa zimeenda na kesho utahitaji kuamka saa 12 ili uwahi gari ya
shule. Unaonaje ukalale?’ Lugha ya pili inakaribisha ushirikiano kuliko ya
kwanza.
Sambamba na hilo, mpe fursa ya
kuchangua. Mtoto anapokuwa na fursa ya kuchagua kipi afanye inamfanya ajisikie
kuheshimika zaidi na hivyo anakuwa tayari kutoa ushirikiano. Mwekee mazingira
ya kuchagua kipi anachopendelea zaidi na anapochagua kisicho bora mpe maelezo
mepesi kumsaidia kutafakari maamuzi yake.
Msifie anaposhirikiana na wengine
Watoto wadogo wanapenda kusifiwa. Sifa zina uwezo wa kujenga tabia kuliko adhabu. Mtoto anapoonesha ushirikiano na wengine, onesha kutambua jitihada zake. Anapowapa wenzake vitu, usijifanye hujaona. Tambua tabia hiyo na ipongeze. Unapomsifia maana yake unamfanya ajitahidi kuendelea kushirikiana na wenzake ili atambuliwe.
Usisubiri afanye kinyume ili uadhibu
kosa lake. Msaidie kuelewa kinachotakiwa kufanywa badala ya kisichotakiwa
kufanyika. Panda mbegu ya ushirikiano kwa kumtambua pale anaposhirikiana.
Adhabu zisizo za lazima zinaotesha tabia ya misuguano ya ndani kwa ndani
inayoweza kufichwa kwa nidhamu ya muda.
Fuatilia gazeti la Mtanzania kwenye safu ya Uwanja wa Wazazi kila Alhamisi kwa makala kama hizi.
Maoni
Chapisha Maoni