Mambo ya Kuzingatia Unapojiandaa na Usaili wa Kazi

Kuitwa kwenye usaili wa kazi ni hatua ya mwisho kuelekea kupata ajira uipendayo. Mara nyingi, kazi inapotangazwa waombaji wa kazi hiyo huwa ni wengi. Baada ya kupokea maombi ya kazi, shughuli inayofuata ni kufanya uchambuzi wa kuwatambua waombaji wanaokaribia vigezo vinavyohitajika. Matokeo ya uchambuzi ni kupatikana kwa orodha ya watu wachache wanaoitwa kwa hatua ya mwisho ya uombaji wa kazi.

Kwa kuwa si watu wengi hufikia hatua hii, unapopata taarifa rasmi kuwa umeitwa kwenye usaili wa kazi uliyoiomba, ni jambo la kujivunia. Kuweza kushindana na kundi la watu wengi waliohitaji kazi hiyo na hawakuitwa si jambo dogo.

Hata hivyo, ni vizuri kutambua kuwa usaili wa kazi sio kupata kazi. Wapo watu waliowahi kuitwa kwenye usaili mara nyingi lakini hawakupata kazi. Makala haya yanakupa dondoo chache za kukusaidia kufanya usaili kwa mafanikio. Lengo la makala haya si kujadili makosa wanayofanya watu kwenye usaili. Tutajitahidi kujadili mambo halisi ya kukuwezesha kushinda usaili na kupata kazi.
 
PICHA: brightlinkprep.com
Elewa malengo ya usaili

Huwezi kujiandaa vizuri na usaili bila kuelewa malengo ya usaili. Kwa kawaida, usaili ni mahojiano kati ya mwombaji wa kazi na mwajiri kwa lengo la kutathmini uwezo wa kikazi alionao mwombaji. Mahojiano haya aghalabu hufanyika kwa mazungumzo au maandishi katika chumba au eneo lolote linaloteuliwa na mwajiri kwa kazi hiyo.

Hata hivyo, si lazima mwajiri awepo kwenye usaili. Wakati mwingine mwajiri hukasimu mamlaka yake kwa watu anaowaamini kwa kazi hiyo. Jopo hilo hufanya kazi ya kukusanya taarifa zinazotumika kufanya maamuzi ya ikiwa mwombaji wa kazi anaweza kuajiriwa ama la. Kwa muktadha huu, kinachoamuliwa na jopo hilo halali, kinawakilisha matakwa halisi ya mwajiri.

Jambo la msingi kuzingatia ni kuwa unapokwenda kwenye usaili wa kazi, una wajibu wa kuthibitisha kuwa unafaa kwa nafasi unayoomba. Hilo litawezekana ikiwa utaonesha namna uwezo wako, maarifa yako, na ujuzi ulionao yanavyowazidi watu wengine wanaoshindana kupata nafasi hiyo unayoiomba.

Fanya utafiti wa taasisi

Maandalizi yanaanza kwa kufanya utafiti wa taasisi unayotarajia ikupe kazi. Uelewa wa taasisi ni muhimu kwa sababu maswali mengi utakayokabiliana nayo siku ya usaili, kwa kiasi kikubwa, yanategemea namna unavyoielewa taasisi unayotaka ikuajiri.

Katika kufanya utafiti, unahitaji kuelewa historia ya taasisi, dira na malengo yake, mfumo wa utendaji wake, uongozi wake, walengwa katika huduma zake na mambo kama hayo. Uelewa wa kina maeneo hayo utakusaidia kujibu kwa ufasaha maswali yanayoweza kujitokeza siku ya usaili.

Ili uweze kufanya utafiti, unahitaji kufuatilia tovuti ya taasisi hiyo, kurasa za taasisi katika mitandao ya kijamii na machapisho mbalimbali yanayopatikana mtandaoni. Kadhalika, unaweza kuwasiliana na watu wanaoifahamu taasisi husika na kujaribu kupata taarifa zitakazokusaidia.

Jiandae kisaikolojia

Sambamba na kufanya utafiti wa taasisi husika, unahitaji kuiandaa akili yako kwa ajili ya siku ya usaili. Amini kuwa upo uwezekano mkubwa wa kupata kazi uliyoitiwa. Unapokuwa na mawazo chanya, ni rahisi kujenga hali ya kujiamini itakaokusaidia kufanya vizuri zaidi kwenye usaili.

Ni makosa kwenda kwenye usaili hali ukiamini hutapata kazi. Hisia kuwa unatimiza mradi tu, zitakuondolea nguvu za kufanya vizuri.

Hata kama ni kweli  mara nyingi umeitwa kwenye usaili wa kazi na hukufanikiwa, amini kuwa safari hii utapata kazi. Imani inajenga kujiamini. Kujiamini kunajenga ujasiri.

Kama una wasiwasi na kujiamini kwako, tafuta watu wenye maneno ya kuinua moyo wakusaidie. Soma maandiko yanayokuinua moyo. Kwa kusikia na kusoma maneno yanayokujenga, utaimarika kisaikolojia na kuwa jasiri zaidi.

Sambamba na hilo, epuka kuongea na watu wanaokukatisha tamaa wanaokuonesha kuwa hutapata kazi. Ukijiruhusu kukutana na watu wa namna hii, utaishia kuvunjika moyo na utashindwa kufanya vizuri.

Hakiki muda na mahali pa usaili

Kosa kubwa unaloweza kufanya siku ya usaili ni kuchelewa. Unaweza kuchelewa kwa sababu nyingi. Mosi, kutokukumbuka muda halisi wa kuanza kwa usaili. Ni rahisi kuchelewa unapokuwa huna hakika na muda halisi wa kuanza usaili.

Pili, unaweza kuchelewa kwa sababu ni huna uhakika na mahali patakapofanyikia usaili. Kubahatisha namna ya kufika eneo la usaili siku ya usaili, unajiweka kwenye hatari ya kuchelewa, na wakati mwingine, hata kushindwa kufika.

Tafuta ramani ya eneo mapema, jiridhishe na namna utakavyoweza kufika. Hiyo itakusaidia sana kukadiria muda wa kuondoka nyumbani au mahali ulikofikia ili uweze kuwahi usaili.

Ikiwa unahitaji kusafiri umbali mrefu, usisubiri siku ya mwisho kuanza safari. Fika mapema kwenye eneo lililo karibu na mahali patakapofanyikia usaili ili upate muda wa kupumzika na kutulia kifikra.

Maandalizi ya mwisho

Unahitaji kuonekana nadhifu siku ya usaili. Ingawa hulazimiki kuvaa mavazi ya gharama na ya namna fulani, hata hivyo unahitaji kuandaa nguo za heshima. Epuka kuvaa nguo zitakazotoa picha ya mtu asiye rasmi. Mavazi mafupi, yanayobana, milegezo, mitindo inayozidi kiasi na mavazi yenye maandishi hayawezi kuwa chaguo sahihi.


Kadhalika, andaa nyaraka muhimu  kama vyeti halisi, cheti cha kuzaliwa, kitambulisho, barua ya kuitwa kwenye usaili kama umepewa na nyaraka nyingine kama ulivyoelekezw. Ingawa nyaraka hizi zinaweza zisihitajike, lakini unapokuwa nazo unakuwa na utulivu wa nafsi na akili.

Inaendelea

Maoni

  1. Chapisho hili limeondolewa na msimamizi wa blogu.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia