Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke -2

Katika makala iliyopita, tuliona kuwa mwanamke anahitaji kujua anavyopendwa na mwenzi wake kwa maneno na vitendo. Kadhalika, tuliona mwanamke anatamani kuwa na uhakika wa nafasi ya kwanza kwa mwenzi wake. Hatamani kuona akishindana kwa umuhimu na chochote kile kinachoweza kuchukua nafasi yake kwa mwenzi wake.

Hapa tunajadili mahitaji mengine manne ya mwanamke unayohitaji kujifunza kuyaelewa na kuyafanyia kazi kama kweli unayo nia ya kugusa moyo wa mwenzi wako.
PICHA: verastic.com

Kueleweka kwa hisia zake
Tumekwisha kuona kuwa mwanaume, kwa kawaida, hutamani kupewa hadhi ya kuwa na sauti ya mwisho kwa kusikilizwa. Kwa mwanamke, hadhi yake hutegemea vile hisia zake zinavyoeleweka kwa mwenzi wake. Jambo hili ni gumu kidogo kueleweka kwa wanaume wengi kwa sababu nitakayoieleza.
Kwa kawaida, wanaume hutamani kutoa majibu kwa matatizo. Uwezo wa kuwa na majibu ni sehemu muhimu ya heshima ya mwanamume. Ndio maana mwanamke anapomfuata mume wake pengine ili kusikilizwa na kueleweka, mara moja akili ya mwanamume hufanya kazi ya kuchakata majibu haraka na kuyakabidhi kwa mwanamke. Uharaka wa majibu humjengea mwanaume hali ya kujiamini.
Hata hivyo, si wakati wote mwanamke anapokuwa na neno la kusema, basi hutamani kupata majibu kama ambavyo akili ya mwanaume inaweza kufikiri. Mara nyingi mwanamke anapolalamika, lengo lake kuwa ni kutafuta utulivu wa kihisia tu basi. 
Mwanamke anatamani awepo mtu anayemwamini, anayeweza kusikiliza hisia zake kwa dhati bila kujaribu kuhukumu, kupuuza au kuelekeza vile anavyopaswa kujisikia. Anatamani liwepo sikio linaloaminika kwa mwenzi wake linaloweza kusikia na kuelewa kile hasa kinachomsibu nafsini mwake.
Mwanamke anapokutana na changamoto kazini, kwa mfano, anapoudhiwa na watu wengine, anapohitafiana na majirani, anatamani mwenzi wake awe mtu wa kwanza kusimama upande wake na kuonesha kumwelewa. Ukiweza kuwa msikivu wa hisia za mwanamke unamfanya akuamini kwa alama nyingi kwa sababu umemwongezea hali ya kujiamini kuwa anaye mtu wa karibu anayemwelewa.
Uwazi wa mambo na kuambiwa ukweli
Tofauti nyingine ya mwanamke na mwanamume ni namna wawili hawa wanavyouchukulia uwazi. Tulishaona kuwa mwanamume anapenda faragha na usiri. Mara nyingi usiri huwa ni njia ya kulinda hadhi yake. Kwamba kutokutabirika wala kujulikana anafanya nini hasa ni namna ya kujihakikishia mamlaka yasiyohojiwa na mwanamke.
Lakini katika macho ya mwanamke, usiri na faragha ni dalili ya kutokuwa mwaminifu. Sababu ni kuwa mwanamke anatamani zisiwepo siri zozote asizozijua katika kila kila kona ya maisha ya mume wake. Kujua mambo ya muhimu anayoyafanya mume wake kunamhakikisha kuwa ni kweli mume wake amempa nafasi ya kwanza.
Ikiwa unataka kuugusa moyo wa mke wako, jitahidi kuaminika kwa kufanya mambo yako kwa uwazi kadri unavyoweza. Mwambie unakokwenda, mwambie uliko, mshirikishe mipango yako, mshirikishe siri zako uzizoweza kumwambia mtu mwingine. Ukifanya hivyo, atakuamini na hatakuwa na sababu ya kukupeleleza.
Sambamba na uwazi, kuwa mkweli. Jenga mazoea ya kusema mambo vile yalivyo bila kulazimika kutumia uongo kuficha mambo usiyopenda yafahamike. Mwanamke anapogundua kuwa unayo tabia ya kusema uongo, ujumbe anaoupata ni kuwa wewe si mtu anayeaminika. Asipokuamini, mwanamke hawezi kukuheshimu kama unavyotamani.
Najua wanaume wengi hujitetea kuwa uwazi na ukweli kwa mwanamke ni jambo lisilowezekana. Sababu wanayoitoa ni kuwa wanawake wenyewe hawaaminiki. Ingawa upo ukweli kuwa wapo wanawake wanaoweka wenyewe mazingira ya kufichwa mambo ya muhimu na wenzi wao, hiyo haiondoi ukweli mwingine kuwa mahusiano ya karibu, kama ya ndoa, hayawezi kukamilika bila kuheshimiwa kwa misingi ya ukweli na uwazi.
Kusifiwa kwa ‘uanamke’ wake
Yapo masuala ambayo kwa mwanamke yanabeba wajihi (utambulisho) wake. Kwa wengi, ‘uanamke’ ni pamoja na vile anavyovutia kimwonekano na kimaumbile, namna anavyotekeleza majukumu ya ndani  kama mwanamke na haiba yake kwa ujumla. Mwanaume anayetaka kugusa moyo wa mke wake ana wajibu wa kutambua na kuyasifia maeneo hayo.
Kwa mfano, mwanamke hutumia muda mwingi kujiweka katika mwonekano unaovutia. Anakwenda salon kwa masaa kadhaa tofauti na mwanaume. Mara nyingi anapojipamba lengo ni kumvutia mume wake. Msifie. 

Jitahidi kugundua mabadiliko anayoyafanya katika mwonekano wake na msifie kwa dhati. Unapofanya hivyo, unaongeza hali ya kujiamini kwake na anapojiamini atakuwa na nguvu ya kukupa heshima unayoihitaji kutoka kwake.
Wakati mwingine, ni kweli umbile la wanawake hubadilika kwa sababu nyingi ikiwemo uzazi. Mwanaume asiyefikiri vizuri huweza kuonesha kutokuvutiwa na mwonekano wake. Hali hiyo inamwuumiza mwanamke hata asiposema. Sababu ni kwamba anatamani awe na mvuto kwa mumewe. 

Hivyo, badala ya kukosoa vile anavyoonekana, mwanaume unayejitambua, utatafuta namna ya kujenga mwonekano uutakao kwa namna isiyojeruhi kujiamini kwa mwenzi wako.
Kwa mfano, kama kuna umbile la mwili unahitaji awe nalo, shirikiana naye kufanya mazoezi. Kama hupendi kitambi alichonacho, kwa nini usihakikishe umeondoa cha kwako ili uwe na haki ya kutokuridhishwa na cha kwake? Si sahihi kutamani wengine wawe vile tusivyo. Ndio kanuni ya maisha.
Kadhalika, sambamba na kumhakikishia kuwa mwenzi wako anavutia, fanya jitihada za kutambua vile anavyofanya majukumu yake kama mwanamke. Ikiwezekana msaidie kazi za ndani kuonesha kwa kiasi gani unatambua kazi kubwa anayofanya kama mwanamke hapo nyumbani. 

Ni ukweli uliowazi kuwa wanawake wanafanya kazi nyingi za ndani kwa moyo. Kazi hizo zinawachosha mwili na nafsi wakati mwingine. Hawafanyi kazi hizo zote kwa lengo la kupata sifa za wenzi wao. Lakini wanapofahamu kuwa wajibu wao huo unatambuliwa inawapa nguvu ya kujituma zaidi.
Uhakika wa kiuchumi

Hili linaweza kuwa na sura ya kiutamaduni zaidi kuliko kimaumbile. Lakini katika mazingira yetu ya ki-Afrika, tafiti zinaonesha kuwa mwanamke [wa ki-Afrika] anatarajia kuwa majukumu mazito ya kifamilia hubebwa na mwanamume. Huo ndio ukweli. Mume wa ki-Afrika ndiye anayetarajiwa kujua wapi fedha zinakopatikana ili kukidhi mahitaji muhimu ya kifamilia.
Tambua kuwa ingawa ni kweli mwanamke anaweza kuwa na kipato chake kinachotokana na kazi halali, bado hapaswi ‘kulazimika’ kufanya kazi kuilisha familia. Mwanamke wa ki-Afrika amekuzwa kuamini kuwa kinachomhusu yeye moja kwa moja ni majukumu ya ndani ya familia na mume ndiye mwenye heshima (wajibu?) ya kushughulika kuhakikisha kuwa familia inapata mahitaji yake.
Heshima hii aliyopewa mwanamume wa ki-Afrika hufanya mwanamke [wa ki-Afrika] ahitaji kupata mume anayeweza kumpa uhakika wa kiuchumi. Mwanamume hohe hahe, mvivu na asiyeonekana kuwa na dalili za mikakati inayoweza kuleta uhakika wa maisha anapunguza uwezekano wa kuaminiwa na mwanamke.

Mwanamke anatamani kuwa na uhusiano na mwanaume anayejua kupambana kwa lengo la kuilisha familia. Mwanaume mwenye bidii ya kazi, mwenye ndoto na malengo makubwa, mwenye uwezekano wa mafanikio, kwa hakika, anaweza kugusa moyo wa mwanamke. 

Tahadhari hata hivyo, ni kuwa, wakati mwingine bidii ya kazi kuenda sambamba na kusahau majukumu mengine kama tulivyoyajadili hapo juu. Mwanaume mwenye busara hujua namna ya kupangilia mambo yake vyema ili kimoja kisifanye kingine kisahaulike. 

Ni ukweli ulio dhahiri kuwa uhakika wa kiuchumi hauwezi kukuhakikishia upendo wa  bure mwanamke. Lakini, hata hivyo, upendo usioambatana na mipango na bidii ya kazi inayoweza kuleta uhakika wa kiuchumi, unaweza kukaribisha changamoto zisizo za lazima katika mahusiano.
Ndio kusema, ikiwa unataka kugusa moyo wa mwanamke, jambo la sita ni akili inayofikiri vizuri namna gani mwanamke unayempenda atapata uhakika wa mahitaji yake ya kila siku. 
Fuatilia gazeti la Mtanzania, safu ya Saikolojia kila Alhamisi, kwa makala kama hizi.

Maoni

  1. Bonge la soma nimefurahia sana kusoma...Ahsante sana.

    JibuFuta
  2. Asante sana Yasinta kwa kusoma :)

    JibuFuta
  3. Daah! Nmekuelewa sana kaka. Thanks a lot kwa somo lako

    JibuFuta
  4. Daah! Nmekuelewa sana kaka. Thanks a lot kwa somo lako

    JibuFuta
  5. nyumba baraka21/11/16 12:21 AM

    ahsante sana mwl wang sitapitwa hata juma moja


    JibuFuta
  6. asante sana kwa kutufunza bro!

    JibuFuta
  7. Asante e ndugu elimu tosha kwangu mwenyewe!

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?