Mambo Yanayoweza Kumvutia Mwanamume kwa Mwenzi Wake -2

Tuliona katika makala yaliyopita kuwa mwanaume anahitaji sana kutambuliwa uwezo wake. Huna sababu ya kumwambia mwanaume unampenda. Lugha ya upendo anayoielewa zaidi ni kusifiwa uwezo wake. Sambamba na hili la kwanza, tuliona mwanaume anayo njaa ya heshima. Heshima ni kumtii na kumstahi hata pale anapokuwa mkosaji kwa lugha, maneno na tabia. 


PICHA: Citifmonline.com
Katika makala haya, tunamalizia sifa nyingine nne anazozihitaji mwanaume kwa mwezi wake ambazo kimsingi ni mahitaji yake anayoyatarajia kwa mwezi.

Anahitaji uhuru, faragha

Uhuru na faragha kwa hakika ni kinyume kabisa na kile ambacho wanawake wanakihitaji kama tutakavyoona mbeleni. Lakini kwa mwanaume, ukweli ni kuwa anahitaji kujiona ni mtu mwenye uhuru wa kufanya mambo anayoyafurahia bila kuambiwa kingine cha tofauti anapaswa kukifanya.

Kwa mfano, kama mume wako anapenda mpira, ukweli ni kuwa anatamani umpe ushirikino. Ukiweza kujitahidi kufurahia mpira utagusa moyo wake kwa namna ya tofauti. Chochote anachopenda kukifanya mume wako wakati wa muda wake wa ziada, mpe nafasi ya kuwa yeye bila kumwingilia isipokuwa inapokuwa ni lazima.

Kama anayo mambo anayoyapenda na hayaharibu maisha yenu, jiunge nae. Isipowezekana, mpe uhuru wa kupenda mambo yake. Huna sababu, kwa mfano, ya kumfanya aachane na marafiki zake kama hawaathiri uhusiano wenu. Huna sababu ya kumfanya aache kwenda maeneo anayoyapenda ikiwa kufanya hivyo hakuleti madhara. Mpe nafasi ya kuwa huru.

Kadhalika, uhuru unakwenda sambamba na kuhitaji faragha. Kimsingi, kama mwanamke, saa nyingine unatamani ufahamu kila anachokifanya mume wako. Unahitaji kujua mawasiliano yake, ameongea na nani, ameandikiana na nani, anafahamiana na nani na ikiwezekana ujue kila nukta ya mawazo yake. Pengine unaweza hata kushawishika kumchunguza kwa siri.

Hata hivyo, kwa wanaume wengi, jambo hili halipendezi. Wanaume wanatamani kuwa na nafasi ya kufanya mambo yao bila kupelelezwa. Hawapendi kuona wakinyang’anywa haki ya kuwa na faragha.


Ikiwa unatamani kuwa na uhusiano uliojengwa katika msingi wa kuaminiana, mfanye akuamini ili kwa utashi wake akuruhusu kuingilia maisha yake ya faragha kwa hiari yake. Kadri anavyokuamini ndivyo anavyoweza kukukabidhi uhuru unaoutaka wewe bila kuleta mtafaruku.



Mbinafsi anayevutiwa na mwili

Ingawa binadamu wanao ubinafsi kwa asili, lakini ubinafsi wa mwanaume unazidi ule wa mwanamke. Mwanaume wa kawaida hujifikiria zaidi yeye na mahitaji yake. Wakati mwingine hata katika nyakati ambazo aileti maana kujifikiria mwenyewe, ni rahisi mwanaume kujitanguliza yeye.

Hali hii ya kujitanguliza mwenyewe kwanza, inao uhusiano na maumbile yake. Mungu ameweka tamaa ya mwanaume katika macho yake. Tamaa inapotawala ufahamu wa mwanaume, kwa kawaida, ubinafsi huzaliwa.

Isipokuwa katika mazingira ambayo mwanaume amebadilishwa nafsi yake, anaposema anakupenda mara nyingi anafikiria mahitaji yake ya kimwili. Anafikiria sifa zako za kimwili zinazoweza kukidhi tamaa zake. Hali hii ni tofauti kwa wanawake. 

Ikiwa unataka kumwutia mwanaume, hakikisha unaendelea kumvutia kimwili. Fahamu kinachomvutia na jitahidi kujiweka katika namna anayoitarajia. Kosa kubwa wanalolifanya wanawake wengi ni kujisahau mara wanapoolewa. Unaposahau kuendelea kuwa vile ulivyokuwa kabla ya ndoa, unachochea ubinafsi wa mwanaume.

Mfanye ajione anahitajika

Kama mwendelezo wa mamlaka tuliyoona kuwa ni kiini cha uanaume, mwanaume wa kawaida anatamani kujisikia kuwa bado anahitajika. Mwanaume anatamani kujiona kuwa mambo hayaendi bila yeye.

Wanaume wanakua wakiaminishwa na jamii, marafiki rika na wakati mwingine kupitia matendo ya baba zao wenyewe kwamba wao ndio watatuzi wa matatizo. Na kwa jinsi imani hii ilivyojikita mizizi kwenye akili ya mwanaume, tukisema mwanaume anaamini ni mtatuzi wa matatizo hatufiki kwenye uhalisi. Mwanaume anapenda awe jibu la mambo yote.

Jaribio lolote la kumwonesha mwanaume kuwa hata asipokuwepo, hata asipofanya chochote, hata asipotoa wazo lolote, hakuna kitakachoharibika linaweza kumfanya 'akahujumu' mahusiano. Kumfanya ajione hahitajiki, kunaathiri kiburi chake cha uanaume (ego) na inaweza kuwa mwanzo wa matatizo.

Hata kama ni kweli unamzidi kipato, unamzidi hekima, unamzidi uelewa, jifunze kuwa chini yake na mwaminishe kuwa anahitajika. Mwanaume anapojua anahitajika huhamasika kupenda. Usifanye kosa la kumfanya ajione amekataliwa.

Hapendi kubadilishwa

Kila mwanadamu hapendi kujisikia kuna mtu mahali ana mpango wa kubadilisha. Mara nyingi tunapojisikia tunabadilishwa, tunajisikia kudhalilika. Kama jitihada za kujihami, mara nyingi uhusiano na huyo anayejaribu kutubadilisha huathirika.

Kwa mwanaume, hali ya kujisikia kudhalilika pale anapohisi mwenzi wake anataka kumbadilika ni kubwa zaidi. Kwa mwanaume ni kosa la jinai anapogundua kuna vitabia vyake unakazana kuvibadilisha. Mwanaume anapofahamu unambadilisha, anajiona kama mtu aliyepoteza mamlaka yake. Hawezi kukubali kirahisi.


Ni kweli yapo mambo unayohisi ni muhimu ayabadilishe. Mfano, marafiki wanaompetezea muda wake ambao angeweza kuutumia na familia, labda hana hamasa na mambo ya kiimani, labda ni kazi anayofanya au tabia fulani zinazokukera. Usijaribu kuonesha nia ya kubadilisha.

Ukitaka mwanaume afuate yale unayotaka ayafanye, mkubali vile alivyo na ajue umempokea bila masharti. Kukubaliwa ni motisha ya kubadilika. Hiyo ndio kanuni. Mume wako anapojua pamoja na mapungufu yake bado umemkubali alivyo, kubadilika ni suala la muda.


Twitter: @bwaya

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Kama sio utumwa ni nini hiki?