Msingi wa mahusiano si matarajio bali kutambua na 'kushibisha' mahitaji ya kihisia ya mwenzi wako

NI VIGUMU kwa kijana aliye kwenye kilele cha msisimko wa mapenzi hii leo kudhania bashasha hiyo inaweza kabisa kugeuka kuwa hasira, uchungu, na kushuhudia ile shauku ya kuongea, kusikiliza, kutaniana na mpenzi wake huweza kupotea so naturally kwa jinsi hiyo hiyo mapenzi yalivyoanza. Aliyewahi kusema upo mstari mwembamba mno unaotenga mapenzi na chuki, alilitambua hili.

Kwa jinsi msisimko wa mwanzo wa kimapenzi unavyokuwa-ga mkubwa, huwa haingii akili kwa kijana anaposikia kwamba wapo wanandoa huweza kuchelewa kurudi nyumbani katika jitihada za kujaribu kuyakimbia matatizo na wenzi wao.

Kijana anashindwa kuelewa inakuwaje watu wawili wanaopendana kwa dhati, wanaweza kufikia mahali pa kutamani kuzungumzia matatizo yao kwa uwazi, lakini wasiweze, wakatamani kuwa karibu kihisia, wasiweze. Haya yote pamoja na kuwa mabaya kuyasikia, huweza kumpata mtu yeyote, tena mwenye mapenzi mazito, hatua kwa hatua.

Mahusiano ni suala zito lakini linalowezekana

Tunapoyasema haya, hatukusudii kumtisha wala kumkatisha tamaa kijana anayefurahia mapenzi ya ujana. Bali, kwa hakika, tunakusudia kumwambia kwamba wanaoachana, wanaochokana, kama tulivyoona kwenye takwimu, walikuwa kama yeye, na huenda walipendana kuliko yeye, lakini yapo mambo yalitokea hapo katikati na kusababisha hali ya hewa ikachafuka kabisa. Achukue tahadhari.

Kwako wewe uliye mhanga wa 'kuchafuka kwa hali ya hewa ya mapenzi', hakuna asiyechafukiwa na hali ya hewa kwenye mahusiano. Hili ni janga kamili la taifa. Hata hao unaowaona wakishindana kuposti picha za wapenzi wao Facebook na Instagram huwaga na nyakati zao rough wasizozisema hadharani. Pengine, wamejifunza namna ya kushughulikia matatizo ya kimapenzi na hivyo kurudisha upendo wa mwanzo kila siku. Wengine, pengine, wameweza kujifunza namna bora ya kuishi vizuri la hilo unaloliona wewe kuwa ni tatizo. Ni namna tunavyoyachukulia mambo.

Kwa ujumla matatizo ya kimahusiano, si mambo ya kubeza na hakuna bingwa. Ni mada nzito yenye unyeti wa hali ya juu. Sacred topic. We fikiria kuishi na mtu aliyekulia kwingine, akalelewa na wazazi wenye mitazamo mingine, imani nyingine, utamaduni mwingine na hata mazoea mengine. Kuishi na mtu huyo, ambaye ni tofauti kabisa na wewe, tena kila siku, si jambo jepesi hata kidogo.

Ni bahati mbaya kuwa msisimko wa mapenzi ya awali hutufanya wengi kusahau kujiandaa ipasavyo katika kukabiliana na uwezekano wa tufani huko mbele ya safari. Badala ya kujifunza kwa kina masuala haya, badala yake tunatumia muda mwingi kudai michango ya kufanya harusi ya 'kufa mtu', ambayo furaha yake hubakia ukumbini. Matokeo yake, tufani zijapo hutukuta hatujajiandaa na hivyo tunajikuta tukiongeza zile takwimu za mitafakaruku tulizozioana hapa.

Kitu gani huwafanya watu wapendane?

Msisimko wa kimapenzi baina ya watu wawili huchangizwa na sababu nyingi, zikiongozwa na moja iliyo kubwa: uwezo wa kushibishana mahitaji ya ndani ya kihisia. Emotional need, ni hitaji kuu linaloratibu mwenendo wa mahusiano ya watu wawili wanaotaka kupendana kwa maana ya mioyo yao kuendelea kuwa pamoja kimawasiliano. Tunaweza kusema kwamba, mwanaume na mwanamke, wote wawili wanayo mahitaji yao ya kihisia, ambayo ingawa hayafanani, yanakuwa kama urimbo wa kuunganisha mioyo yao iwasiliane. Nitaeleza.

Kwa nini wapenzi wapya hupendana? Picha: kongsky / FreeDigitalPhotos.net
 Wataalamu wa mahusiano wanakubaliana kwamba, kwa asili njaa ya mwanamke ni kuwa admired,  kwa vitendo na uthibitisho wa maneno kiasi cha kujiona ni malkia wa ufalme wa mwanaume huyo anayedai kumpenda.

Mwanaume, kwa nafasi yake, anapofanya jitihada za kumwambia maneno na kumfanyia vitendo vya kimapenzi vinavyomfanya ajikie mtu wa maana, aliye salama, anayethaminika kwa mwonekano na tabia, humshibisha mwanamke huyo, na kumfanya ajisikie kuridhika. Hapa tunasema mwanamke anajisikia kupendwa.

Mwanamke naye shauri ya kuridhika kihisia, hurudisha 'chenchi' kwa mwanaume, ambaye naye kiasili anayo njaa kali ya kuaminiwa kuwa anaweza, mwenye mamlaka na nguvu zinazotambuliwa na kukubaliwa na mwanamke. Akijiona mfalme kwa kiasi hicho, hapa tunasema mwanamme anajisikia kupendwa.

Kwa hivyo, kinachowafanya watu wawili wenye mahitaji tofauti ya kihisia wapendane, ni namna wawili hao wanavyotambua na kuyajibu mahitaji ya kila mmoja wao ipasavyo. Mwanamke aweze kujisikia wa maana na salama, anayethaminika kwa mumewe, ili naye aweze kushibisha njaa ya mwanaume kujisikia mtu mwenye uwezo, anayejiamini kuwa na mamlaka. Ni uhusiano wa nipe, nikupe yaani: sina, ninachokihitaji kwako, ingawa ninacho unachokihitaji.

Tutumie mfano rahisi. Kijana wa kiume amemwona kijana wa kike na angependa awe mpenzi wake na hatimaye mke. Mara nyingi, katika utamaduni wetu ambao ndio kwanza tunashindana nao siku hizi, shughuli hii ya kutengeneza mahusiano huanzishwa na mwanaume kwa ku-admire uzuri, tabia na thamani ya mwanamke anayedhani anamtaka. Kwa wanawake wengi, jitihada hizo huwa hazifui dafu kirahisi kwa sababu ya mashaka ya kuamini usalama wa kujikabidhi kwa mwanaume huyo.

Mwanaume aliye serious na kuanzisha mahusiano hayo, huendeleza jitihada za kuhakikisha mwanamke huyo anajiona malaika, kwa kutumia maneno matamu sambamba na matendo ya kimapenzi, lengo likiwa ajisikie salama mikononi mwake. Hilo likifanikiwa, mwanamke huyo huitikia kwa kuanza kushindwa kuyafikiri maisha yake bila mwanaume huyo. Watoto wa mjini wanasema, 'anaanza kukolea'. Kisha ataanza kumwamini mwanaume huyo na kuanza kuonyesha wazi kutambua nafasi ya mwanaume huyo katika maisha yake, na hivyo ku-admire uwezo na thamani ya mwanaume huyo maishani mwake, hali inayotarajiwa kumshibisha ipasavyo mwanaume husika.

Mambo haya yakifanyika, huwa ni mithili ya sumaku kali inayogundisha mioyo ya wawili hawa pamoja na hivyo kuendeleza duara la mahusiano. Mwanaume akimfanya mwanamke kujisikia malkia, na malkia naye akionyesha kumwamini na kumhitaji mwanaume huo katika maisha yake. Katika mazingira haya, ya mioyo ya wawili hawa kuwa pamoja kiasi hicho, ni rahisi watu hawa kuwasiliana kwa kiwango cha juu sana, kwa maana ya kufungua mioyo yao ili kuzungumza mambo yanayogusa hisia zao, matumaini yao na hata wakati mwingine, hofu zao.

Hapa ndipo sisi watazamaji tunapoanza kuhisi lazima kuna 'kitu' kinaendelea kati yao, kwa sababu kwanza, wote wataanza kupunguza mahusiano ya karibu na watu wengine wakati huo huo wakiendelea kukaribiana siku kwa siku kwa sababu hujikuta wakiamini kuwa ni wao tu ndio wenye uwezo wa kushibishana njaa walizo nazo kihisia, kwa kujua au kutokujua.

Kwa hiyo tunaweza kusema, kinachoratibu ukaribu huu wa 'kiroho' na 'kimwili'  ni uwezo wa mwanaume ku-admire uzuri wa mwanamke na kumhakikishia usalama wa kihisia, hali ambayo humfanya mwanamke naye ajikute aki-admire uwezo, thamani na nafasi ya mwanaume katika maisha yake na kuonyesha kwamba maisha hayawezekani bila yeye. Hali hii ndiyo inayofahamika kwa jina la mapenzi. Tutazungumzia dhana kamili ya mapenzi katika makala zinazofuata.

Mambo huanza kuharibikia wapi?

Wawili hawa wamekwisha kukutana. Wanapendana. Kila mmoja ni shibe ya njaa ya mwenzake. Mioyo yao inao uwezo wa kuwasiliana vizuri. Wamefunguka. Lakini, kadri siku na maisha yanavyoendelea, hasa baada ya kuoana, wawili hawa huzoeana. Mwanaume, ambaye mara nyingi hujikuta akikabiliwa na mihangaiko ya kutafuta maisha, huanza kugeuza vipaumbele na kumchukulia mwanamke huyo kama mtu wa kawaida tu. Ile hali ya kumfanya mke ajione mzuri, salama na wa muhimu, huanza kupungua.

Kujifunza mahitaji ya mwezi wako kunasaidia. Picha: @bwaya
Matokeo yake uhusiano wa kimapenzi hugeuka kuwa 'mahusiano ya kikazi' ambapo mke sasa hugeuka kuwa mpishi, mlezi, mama watoto, mtunzaji wa nyumba, na kadhalika. Mke huanza kujisikia si salama. Hujiona si malaika kama alivyokuwa enzi za uchumba. Ile njaa ya kuwa admired hukosa mlishaji na ule uwezo wa kuonyesha kuhitaji uwezo, mamlaka ya mwanaume kwake huzorota. Yakitokea hayo, mwanaume naye, hujikuta akiwa na njaa ya kutambuliwa, ambayo nayo humfanya asielewe inakuwaje anajisikia utupu. Mambo yanaanza kuharibika. Hasira na uchungu huanza kumea. Tutarejea hapa baadae.

Hata hivyo, si mara zote 'chokochoko cha muungano' huanzia kwa mwanaume. Wakati mwingine,  mwanamke akishakuwa na uhakika wa mahusiano, ukijumlisha na masuala ya usawa wa jinsia yanayotiliwa mkazo siku hizi, hujikuta akishindwa kumfanya mwanaume aendelee kujisikia kuwa mfalme kwenye mahusiano hayo. Huanza kuonyesha hali ya kuwa maisha yanaweza kuendelea hata bila huyo mwanaume. Hamhitaji kivile.

Kufuatia hali hiyo, mwanaume hujikuta anajisikia njaa ya kutambuliwa uwezo na mamlaka yake, na hivyo hujikuta akikosa nguvu zinazotosha kumfanya mkewe aendelee kujisikia malkia. Ikifikia hapo, ukaribu ule wa 'kiroho' ambao ndio msingi wa mahusiano huanza kuzorota, na hatimaye milango ya mawasiliano kati yao hujifunga taratibu na uchungu wa kujisikia kupuuzwa huchipuka kama tutakavyoona huko mbeleni.

Ndio kusema kwamba msingi wa matatizo ya kimahusiano ni hitaji la kihisia la wenzi. Mwenzi mmoja, kwa kutambua au kutokutambua, anaposhindwa kushibisha njaa ya kihisia ya mwenzake, ambayo kama tulivyoona inatofautiana kijinsia, humfanya mwenzi wake asukumwe kutafuta utoshelevu wa njaa hiyo nje na mahusiano. Ndio kusema, unapoanza kuhisi dalili kuwa njaa yako ya kihisia kushibishwa na kitu/mtu mwingine zaidi ya mpenzi wako, ndio wakati wa kuelewa kwamba, wawili nyie mshaanza kuparaganyika. Tutalieleza hili huko mbeleni.

Nini kinakusukuma kuingia kwenye mahusiano?

Katika kuhitimisha utangulizi huu wa pili, ningependa kusisitiza masuala mawili makuu. Kwanza, ni kwamba uwezo wa kushibisha 'njaa ya hisia' ya mwenzi wako, unategemeana kwa kiasi kikubwa na namna nafsi yako mwenyewe ilivyoshiba. Hiyo ni kusema, unapofikiria kuingia kwenye mahusiano na mtu mwingine, ni vizuri kujiridhisha kama ni kweli nafsi yako imeshiba vya kutosha, au basi tu unatafuta kushibishwa na mtu ambaye hutakuwa na kitakachoishibisha njaa yake. Tafuta msaada.

Aidha, ni vyema, na kwa kweli ni lazima, kuhakikisha kwamba pamoja na njaa yako ya kihisia, kwa upande mwingine umeshiba vya kutosha kuweza kumlisha mpenzi wako mwenye njaa usiyonayo wewe. Vinginevyo, kama kinachokusukuma kuingia kwenye mahusiano ni njaa yako tu, tafadhali, uwe na subira kijana, hujakua kiasi cha kuingia kwenye mahusiano.

Ndefu kweli makala ya leo. Ijayo itakuwa fupi, na ndiko tutakakoanza kusaili, kidogo kidogo, mahitaji ya kihisia anayoyatafuta mwanamke kwa mwenzi wake.

Twitter: @bwaya

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Kama sio utumwa ni nini hiki?