Kumsaidia Mtoto Kujifunza na Kumudu Lugha
Lugha
ni nyenzo muhimu sana tunayoihitaji katika maisha. Hatuwezi kufikiri vizuri, kuongea
kwa ufasaha, kusikiliza, kueleza mambo tuliyokutana nayo na hata tunayoyatarajia
siku zijazo bila kuhitaji lugha. Ni wazi tunalazimika kutumia maneno au ishara
kuwasiliana na wanaotuzunguka.
Mjadala
wa namna gani mtoto hujifunza lugha ya mama una historia ndefu. Kwamba mtoto
huzaliwa na asili ya lugha inayoongoza namna anavyojifunza lugha au ni
mazingira anayokulia ndiyo yanayomwezesha kujifunza, ni vigumu kuhitimisha kwa
hakika.
Hata
hivyo, kuna ukweli kwamba ili mtoto ajifunze lugha ipasavyo anahitaji kuwa na
uwezo fulani anaozaliwa nao unaomwezesha kuelewa kanuni muhimu za lugha bila
msaada mkubwa. Lakini pia mazingira, anayokulia mtoto, nayo yana nafasi kubwa
ya kumwezesha kujifunza na kumudu lugha ya kwanza kirahisi.
Hatua za mtoto kujifunza lugha
Tangu
mtoto anazaliwa hujaribu kuwasiliana na wanaomzunguka. Kulia ni lugha ya kwanza
anayoitumia mtoto kuwasiliana na wengine. Hulia kuonesha kutokuridhishwa,
wasiwasi, maumivu au hata kutafuta kusikilizwa. Lakini kadri mtoto anavyozidi
kukua, mbinu ya kulia kama namna ya kuwasiliana hupungua na mtoto huanza kujifunza
kuwasilisha hisia zake kwa kutumia sauti zisizoeleweka.
Ni kawaida kwa watoto wa miezi miwili hadi sita kucheza kwa
kutoa sauti kama Brrrr-brrrrr! Da-da-da-da! zinazoonesha furaha na
sisi wazazi wakati mwingine huziigiza sauti hizo kama namna ya kuonesha furaha
yetu tunapokuwa nao.
Mpaka
anapofikia umri wa miezi sita, mtoto huanza kujifunza lugha ya mama yake hatua
kwa hatua. Kwa mazingira yetu kuna maneno ya awali kama
‘mama’, ‘dada’ ambayo kwa kawaida mtoto huanza kuyatamka kama ishara ya kuanza kuongea.
Kadri anavyoendelea kusikia maneno kwa watu wanaomzunguka, ndiyo anavyoongeza maneno anayoweza kuyatamka siku kwa siku. Katika umri wa miaka mitatu na minne mtoto huiga maneno mengi zaidi hasa yale anayoyasikia yakitamkwa mara kwa mara katika mazingira yake.
Wakati
mwingine neno moja kwa mtoto humaanisha zaidi ya jambo moja. Mfano neno ‘mma’ laweza
kuwa na maana ya ‘mama’, ‘maji’, ‘njaa’ na kadhalika. Ni kama vile mtoto
huonekana kuelewa vitu vingi zaidi ya vile anavyoweza kuvitamka kwa maneno yake.
Katika
umri wa miaka mitano na sita mtoto huanza kumudu lugha na huwa mwongeaji.
Hupenda kusimulia yale anayokutana nayo na kuuliza maswali mengi. Kadri
anavyopata msaada kwa wanaomzunguka, mtoto hujifunza msamiati zaidi. Baada ya
miaka sita, mtoto huwa bingwa wa lugha na huweza kuitumia kwa ufasaha katika kufikiri
asiyoyaona.
Kumsaidia mtoto kujifunza kuongea
Njia
ya kwanza iliyozoeleka ni kuongea na mtoto mchanga kwa lugha ya kitoto. Hii ni
lugha yenye kutumia maneno rahisi yanayotamkwa kwa sauti ya juu kuliko kawaida.
Lengo la lugha hii ni kumhamasisha mtoto kuvutiwa kuongea. Kadri
tunavyojibidiisha kuongea naye kitoto tunampa hamasa ya kujifunza.
Kadhalika,
kurudia kutamka kwa usahihi maneno na sentensi anazojaribu kuzitamka mtoto humsaidia
kuiga utamkaji bora zaidi wa maneno. Mfano, anaposema, ‘mma’ tunaweza kurudia
kwa marekebisho, ‘Unataka maji? Chukua m-to-to!’ Kurudia maneno yake hukuza
uwezo wake wa kuongea bila kuchelewa.
Vile
vile, kuongezea maana ya kile anachokisema mtoto humsaidia kujifunza matumizi
sahihi ya lugha. Kwa mfano, anaposema, ‘baba kuja’, tunaweza kumsaidia
kutengeneza sentensi fupi na sahihi zaidi kama, ‘Ndio! Baba anakuja!’ Kufanya
hivi humharakishia mtoto kuelewa namna ya kujieleza kwa kutumia sentensi rahisi.
Sambamba
na hiyo, tunaweza kumsaidia mtoto kuoanisha majina ya vitu anavyovitumia mara
kwa mara na maneno husika. Mfano, anapokuwa ameshika gauni lake tunaweza kumsaidia
kutamka neno ‘gauni’ ili aweze kuhusisha neno ‘gauni’ na kile anachokiona. Kwa
kufanya hivyo, tunamwekea mazingira ya kuongeza zaidi msamiati wake.
Pamoja
na ukweli kwamba si kila anachokifahamu mtoto anakuwa amefundishwa, bado kuna
uwezekano mkubwa kuwa mtoto anayeishi kwenye mazingira yanayomtia moyo
kujifunza lugha anaweza kumudu lugha kirahisi zaidi.
Inaendelea
Fuatilia safu ya Uwanja wa Wazazi
katika gazeti ya Mtanzania kila Alhamisi kwa mada kama hizi.
Kazi njema
JibuFuta