Kumfundisha Mtoto Kuwajibika, Kufanya Kazi
Kumjengea
mtoto uwezo wa kuwajibika ni wajibu muhimu sana wa wazazi. Bila kuweka mkazo mapema
katika kukuza uwezo huu, mtoto anaweza kuwa mtu mzima asiyefahamu kufanya majukumu
mengi ya msingi na ya kawaida. Mtoto aliyefundishwa kuwajibika hujiona ana
wajibu wa kushiriki shughuli za ndani bila kujali jinsia yake.
Katika makala
haya, tunaangalia namna unavyoweza kumsaidia mtoto wako kujifunza kuwajibika
angali mdogo na hivyo kujenga uwezo wa kumudu majukumu ya msingi kadri
anavyoendelea kukua.
Umuhimu wa kujimudu na kuwajibika
Kujimudu
ni uwezo wa mtoto kufanya kitu bila msaada mkubwa wa watu wengine. Kwa mfano,
mtoto anayejimudu ni yule anayeweza kutembea mwenyewe, kulala bila kukojoa
kitandani, kula mwenyewe, kuoga, kunawa, kupiga mswaki, kupaka mafuta, kuvaa
nguo na kadhalika.
Kuwajibika,
hali kadhalika, ni kuwa tayari kufanya majukumu bila kuwasubiri wengine. Ni
kinyume cha uvivu na kutegea. Kadri mtoto anavyokua kimwili na kiakili, uwezo
wa kujimudu huongezeka na ndio unaomfanya aweze kukabiliana na mazingira yake
bila utegemezi. Kujimudu kunaenda sambamba na uwezo wa kujiamini.
Amudu mwili wake
Ingawa
uwezo wa mtoto kumudu mwili ni wa kuzaliwa nao, kuna mambo yanayohitaji uongozi
wa mzazi ili kujifunza. Kumudu haja ndogo, kwa mfano, kunahitaji msaada kama kumkumbusha
mtoto kujisaidia kabla hajalala, kuweka muda maalum wa kumwamsha akajisaidie
nyakati za usiku, hatua ambazo humsaidia mtoto kupunguza mkojo unaosababisha
aloweshe kitanda awapo usingizini
Afanye usafi wake mwenyewe
Ni
vizuri mtoto akaanza kujifunza kujisafisha mwenyewe tangu akiwa mdogo. Kwa
mfano, tangu akiwa na umri wa mwaka mmoja, mtoto anaweza kuzoeshwa kutumia
mswaki kusafisha meno kwa lengo la kumfanya ajenge mazoea ya kupiga mswaki.
Kadhalika,
kadri anavyokua, anaweza kuanza kujifunza kujisafisha baada ya kujisaidia. Unapomfundisha
kujisaidia kwenye sehemu maalum na kwa muda maalum, kwa mfano, msaidie ajue
kujitawaza kadri anavyoendelea kukomaa kiakili.
Anapofikia
umri wa miaka minne, mtoto anaweza kuanza kujifunza kufua nguo zake za ndani,
soksi na leso kwa msaada wa watu wazima. Pia anaweza kuanza kujifunza kutandika
kitanda chache, hata kama hataweza kufanya kwa ustadi. Lengo kubwa la
kumshirikisha kazi hizi ni kumjengea ari ya kuwajibika mapema.
Kumpa mtoto nafasi ya kufanya kazi za nyumbani ni kumfundisha kuwajibika. PICHA: Sayuni |
Kushiriki kazi za mikono
Shauku
ya watoto kushiriki kazi za mikono huanza tangu wakiwa wadogo. Kwa mfano, mtoto
wa miaka miwili au mitatu anaweza kabisa kutaka kudeki, kuosha vyombo na kushiriki
kazi za jikoni hata kama haziwezi. Tunahitaji kuwapa fursa ya kujiona wanaweza
kusaidia majukumu ya nyumbani kwa uangalizi wetu.
Hata
wanapokuwepo watu wanaoweza kufanya kazi nyingi katika familia, ni vizuri
kuwapa nafasi watoto kushiriki kazi ndogo ndogo nyumbani kuwajengea utamaduni
wa kufanya kazi. Wapangie ratiba ya kufagia, kuosha vyombo, kumwangilia maua,
wafundishe kufua nguo zao wenyewe. Kufanya hivi kamwe si kuwatesa wala ‘kuishi
maisha ya kimasikini’ bali kuwafundisha kuwajibika pasipokuwategemea kupita
kiasi watu wengine.
Tunapowasaidia
watoto kujimudu na kujitegemea, kwa hakika tunawajenga kuwa watu watakaowajibika
ipasavyo katika familia zao na jamii kwa ujumla. Uwepo wa watu wengine
wanaoweza kufanya majukumu ya watoto katika familia, usifatufanye tuwanyime
fursa watoto kujifunza maisha halisi watakayoyaishi kama watu wazima.
Niandikie: bwaya@mwecau.ac.tz, 0754 870 815
Maoni
Chapisha Maoni